Matukio kutoka mkasa wa moto shuleni nchini Kenya

Kundi la wachunguzi limetumwa katika Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha, polisi wanasema, baada ya moto uliotokea jana usiku katika shule hiyo.

Muhtasari

  • Watoto 70 'bado hawajulikani walipo' - Naibu Rais Kenya
  • Mwanaharakati wa Marekani auawa kwa kupigwa risasi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa
  • Mtu aliyechoma moto hoteli ya watafuta hifadhi ahukumiwa kifungo kirefu zaidi Uingereza
  • Kenya: Mwongozo wa usalama wa shule mwaka wa 2008
  • Kenya: Picha zinazosambazwa za matukio ya moto ya kitambo
  • Wachunguzi watumwa kutathmini chanzo cha moto - Kenya
  • Tunawaunganisha wanafunzi na wazazi wao – Shirika la Msalaba Mwekundu
  • Barabara zenye matope zimechelewesha uokoaji
  • Majirani walikimbia shuleni kusaidia kuzima moto
  • Zaidi ya wanafunzi 150 walikuwa katika bweni - polisi
  • Rais wa Kenya aagiza uchunguzi ufanyike kuhusu vifo vya wanafunzi 17
  • Vifo vya wanafunzi 17 Kenya: Tunachojua kufikia sasa
  • Mkurugenzi wa Telegram Durov anasema kukamatwa kwake 'kumepotoshwa'
  • Wanafunzi 17 wateketea kwa moto nchini Kenya
  • Ukraine ilifanikiwa kutokana na mashambulizi ya Kursk - Katibu Mkuu wa NATO
  • Wapalestina watano wauawa kwa shambulizi Ukingo wa Magharibi, wizara ya afya yasema

Moja kwa moja

Na, Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri.

  2. Naibu Rais wa Kenya asema 70 'bado hawajulikani walipo' baada ya shule kuchomeka kwa moto

    Naibu Rais wa Kenya asema 70 'bado hawajulikani walipo' baada ya shule kuchomeka kwa moto

    Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua amewaambia waandishi wa habari kwamba watu 70 bado hawajulikani walipo kufuatia moto wa shule katika eneo la katikati mwa Kenya.

    Alitoa wito kwa wazazi waliowachukua watoto wao baada ya moto uliotokea usiku kucha katika bweni la wavulana, pamoja na majirani waliowasaidia waliotoroka kuripoti kwa mamlaka.

    Rigathi Gachagua amekuwa akizungumza nje ya shule, baada ya kukutana na wazazi.

    Amesema wachunguzi watatoa ripoti ambayo itawekwa wazi itakapokamilika.

  3. Mwanaharakati wa Marekani auawa kwa kupigwa risasi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa

    TH

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamke wa Marekani mwenye umri wa miaka 26 ameuawa kwa kupigwa risasi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa wakati wa maandamano.

    Aysenur Ezgi Eygi, ambaye ana asili ya Uturuki, anaripotiwa kushiriki katika maandamano ya kupinga upanuzi wa makazi ya Wayahudi katika mji wa Beita karibu na Nablus.

    Bi Ezgi Eygi alidaiwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani. Jeshi la Israel (IDF) linasema wanafahamu tukio hilo na wanalichunguza.

    Mwanaharakati huyo wa Marekani alikimbizwa katika hospitali ya Nablus akiwa na risasi kichwani na baadaye akatangazwa kuwa amefariki, shirika la habari la AFP liliripoti.

    Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Palestina, kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 alikuwa amehusika katika kampeni ya kuwalinda wakulima dhidi ya ghasia za walowezi wa Israel.

    Hili linawadia baada ya vikosi vya Israel kuondoka katika mji wa Jenin na kambi yake ya wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kufuatia operesheni kubwa ya siku tisa huko.

  4. Vikosi vya Israel vimeondoka Jenin baada ya operesheni kubwa

    .

    Wanajeshi wa Israel wameondoka katika mji wa Jenin na kambi yake ya wakimbizi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu baada ya operesheni kubwa ya siku tisa.

    Eneo hilo - ngome ya wanamgambo na lenye wakazi wapatao 60,000 - lililengwa katika mojawapo ya hatua kubwa zaidi za Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) katika Ukingo wa Magharibi.

    IDF ilisema ilikuwa ikikabiliana na ugaidi.

    Takriban Wapalestina 36 waliuawa - 21 kutoka mkoa wa Jenin - wizara ya afya ya Palestina inasema.

    Makundi yenye silaha wamedai idadi kubwa ya waliofariki ni wanachama wake, lakini wizara inasema watoto pia ni miongoni mwa waliouawa.

    Mwanajeshi wa Israel pia aliuawa wakati wa mapigano huko Jenin.

    Mji wa Tubas na kambi ya wakimbizi ya al-Faraa pia ilivamiwa wakati wa operesheni hiyo katika Ukingo wa Magharibi wa Kaskazini – shambulizi baya zaidi tangu kuanza kwa vita huko Gaza Oktoba iliyopita kuliko sababishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israeli.

    Wakazi wa kambi ya Jenin magharibi mwa jiji wanajitokeza mitaani kwa mara ya kwanza tangu IDF ilipoanza mashambulizi tarehe 27 Agosti.

    Soma zaidi:

  5. Mtu aliyechoma moto hoteli ya watafuta hifadhi ahukumiwa kifungo kirefu zaidi Uingereza

    .

    Chanzo cha picha, Polisi ya Yorkshire Kusini

    Thomas Birley, 27, wa Rowms Lane, Swinton, ambaye anatuhumiwa kushiriki katika ghasia nje ya hoteli iliyotumiwa kuwahifadhi wanaotafuta hifadhi huko Rotherham, amehukumiwa kifungo kirefu zaidi ikilinganishwa na wengine wenye kuhusishwa na ghasia hizo.

    Kwa kifupi tu, yale yaliyotokeamahakamani:

    • Birley alihusika katika ghasia nje ya Holiday Inn Express huko Manvers, Rotherham mnamo tarehe 4 Agosti, ambapo waomba hifadhi walikuwa wakihifadhiwa wakati huo
    • Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 27 alikuwa sehemu ya kundi lililovunja madirisha ya hoteli hiyo na kuongeza moto dhidi ya jengo hilo
    • Hapo awali, alikiri shitaka la uchomaji moto kwa nia ya kuhatarisha maisha, kuzua ghasia, na kuwa na silaha ya kushambulia
    • Alihukumiwa katika Mahakama ya Sheffield Crown kifungo cha miaka tisa jela, na kuongezewa miaka mitano kwa leseni.
    • Mwandishi wa rekodi za Sheffield Jaji Jeremy Richardson KC alisema maisha ya takriban watu 50 yalikuwa hatarini na wale waliokuwa ndani walidhani wangeuawa
    • Birley na watu kama yeye "walikuwa na nia ya kueneza ujumbe wa chuki wa ghasia na ubaguzi wa rangi", hakimu alisema.
    • Ilikuwa ni moja ya kesi mbaya zaidi ambayo mahakama ilisikiliza kuhusiana na tukio hilo, jaji aliongeza
  6. Kenya: Mwongozo wa usalama wa shule mwaka wa 2008

    Serikali ya Kenya ilitoa mwongozo mpya mwaka wa 2008 kuhusu usalama shuleni, kufuatia ghasia zilizotokea nchini humo karibu na uchaguzi wa 2007.

    Ilijumuisha itifaki za usalama wa mabweni, ikiwa ni pamoja na sheria zinazosema kwamba kila bweni linapaswa kuwa na mlango kila eneo la mwisho na njia ya dharura ya ziada katikati.

    Sheria hiyo ni pamoja na kwamba madirisha ya mabweni yanapaswa kuwa bila vyuma na "lazima iwe rahisi kufungua nje". Pia inasema kuwa vifaa vya kuzima moto "vinapaswa kufanya kazi na kuwekwa katika kila njia ya kutoka na ving'ora vya moto vilivyowekwa kwenye sehemu zinazofikika kwa urahisi".

  7. Katika Picha: Hali ilivyo kwenye shuleni iliyochomeka usiku

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Watu wamekusanyika nje ya shule huku wakisubiri taarifa zaidi kuhusu moto huo na watoto wao.

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Shirika la Msalaba Mwekundu na mashirika mengine yako kwenye eneo la tukio kusaidia familia kupata watoto wao na kutoa msaada mwingine
    ,

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Moto huo ulianza mwendo wa saa sita usiku, katika bweni la wavulana, eneo la tukio limezingirwa huku polisi wakichunguza moto huo.
    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais aliamuru uchunguzi kuhusu moto huo huku wizara na mashirika mbali mbali yakijitokeza kutoa msaada tofauti tofauti
  8. Kenya: Picha zinazosambazwa za matukio ya moto ya kitambo

    Moto katika shule ya bweni nchini Kenya ukiwa umetokea usiku, kuna ukosefu wa picha za kuonyesha moto wa shule hiyo wa wakati halisi jinsi ulivyokuwa.

    Katika ombwe hili, watu wamekuwa wakishiriki picha za zamani kwenye mitandao ya kijamii kana kwamba ni moto huo.

    Kwa mfano, picha iliyo hapa chini imeshirikishwa na akaunti kadhaa mtandaoni, wakiwemo waandishi wa habari.

    .

    Ukweli ni kwamba, moto huo ulitokea katika shule moja nchini Kenya, lakini ni Shule ya St Patrick's huko Iten mnamo Julai 2016 - mji ulio umbali wa kilomita 200 kutoka Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha huko Nyeri.

    Hata hivyo, inaonekana kuwa inatumika kama picha ya kielelezo, wala sio kwamba inashirikishwa kwa nia mbaya.

    Tumeona ilitumika kwenye vyombo vya habari vya ndani mnamo mwaka 2021, 2022 na 2023, lakini haipaswi kuchukuliwa kuwa ni moto huu wa shule uliotokea usiku.

    Pia kuna picha nyingine inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya maiti zilizochomwa moto kwenye chumba kilichoungua, huku watu wakichungulia madirishani kwenye eneo la tukio. Pia nayo, sio ya jana usiku.

    Imekuwa ikitumika tangu mwaka wa 2008, kuhusu ghasia katika mji wa Naivasha – kilomita 64 kutoka Nyeri.

    Hadi jana, ilikuwa inashirikishwa kama ya tukio jingine, lisilo na uhusiano na vurugu zilizotokea nchini Kenya, wakati huu, umbali wa kilomita 82 katika eneo la Kiambaa.

  9. Wachunguzi watumwa kutathmini chanzo cha moto - Kenya

    .

    Wizara ya mambo ya ndani nchini Kenya, imesema maafisa wa polisi - ikiwa ni pamoja na wataalam wa mahakama - kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wametumwa kuchunguza chanzo cha moto huo.

    Pia imethibitisha kuwa eneo hilo limezingirwa na maafisa ambao tayari wako kwenye eneo la tukio.

    Taarifa ya wizara pia imethibitisha kuwa wataalam wa kukabiliana na maafa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya tayari wako kwenye eneo la tukio na "linaratibu utoaji wa usaidizi kwa wazazi na jumuiya ya shule, kutoa misaada na huduma za ushauri".

    Inasema maafisa wa wizara ya elimu na wafanyikazi wa afya pia wako kwenye eneo hilo kutoa "huduma na usaidizi maalum".

    "Tunawatakia afueni ya haraka waliojeruhiwa katika kisa hiki cha kusikitisha wakati ambapo pia tunapitia tena usimamizi wa usalama wa shule," wizara hiyo inaongeza.

  10. Tunawaunganisha wanafunzi na wazazi wao – Shirika la Msalaba Mwekundu

    .

    Chanzo cha picha, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya

    Kama sehemu ya juhudi zinazoendelea kukabiliana na mkasa wa moto katika bweni la wanafunzi lililochomeka usiku wa manane, Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema linafanya kazi kuwaunganisha wanafunzi na wazazi wao, ikiwa ni pamoja na wale walio hospitalini.

    Pia inaendelea kutoa msaada wa kisaikolojia na kutathmini ustawi wa watoto.

    "Hili linafanywa kwa ushirikiano na timu yenye kuhusisha mashirika mbalimbali."

  11. Barabara zenye matope zimechelewesha uokoaji

    Iliwachukua wazima moto muda kufika shuleni kutokana na barabara zenye matope kufuatia mvua za asubuhi.

    Licha ya changamoto hizo, hatimaye moto huo ulizimwa, kwa msaada wa wakazi wa eneo hilo ambao walikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio.

    "Serikali ya kaunti imefanya yote iwezayo kuokoa hali hiyo," Gavana wa kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga amesema.

    Alitaja moto huo kuwa "hasara kubwa", kwani "umechukua maisha ya vijana wenye waliojawa na matumaini siku zijazo".

    Wachunguzi wanafanya kazi kubaini chanzo cha moto huo.

    Soma zaidi:

  12. Majirani walikimbia shuleni kusaidia kuzima moto

    Moto huo ulianza mwendo wa saa sita usiku katika bweni moja lenye wavulana 156, Mwandishi wa BBC Afrika Anne Soy amesema.

    Akiongea kwenye BBC News asubuhi ya leo, amesema baada ya kuona moto huo, "majirani walikimbilia shuleni" kusaidia kuuzima.

    Akiongea kwenye BBC News asubuhi ya leo, amesema baada ya kuona moto huo, "majirani walikimbilia shuleni" kusaidia kuuzima.

    Kwa sasa wazazi wameenda shuleni kuangalia hali ya watoto wao na watu wengi wamejua kuhusu moto huo kupitia vyombo vya habari.

    Na jinsi ulivyoanza, Soy anaongeza kuwa bado hakuna taarifa za moja kwa moja. Baadhi ya walioshuhudia wamesema wakati walipoamka, bweni lao lilikuwa tayari "limezingirwa na moto".

    Soma zaidi:

  13. Zaidi ya wanafunzi 150 walikuwa katika bweni - polisi

    .

    Chanzo cha picha, Ephantus Maina

    Zaidi ya wanafunzi 150 walikuwa kwenye bweni ambalo lilishika moto mwendo wa saa sita usiku, mkuu wa polisi wa eneo hilo Pius Murugu alisema.

    Moto huo ulisambaa kwa kasi sana kwani majengo mengi shuleni humo yamejengwa kwa mbao kulingana na mwanahabari kutoka runinga ya Citizen.

    Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 824, wengi wao wakiwa na umri wa kati ya miaka mitano na 12.

    Wachunguzi wa mauaji tayari wako shuleni.

    Soma zaidi:

  14. Rais wa Kenya aagiza uchunguzi ufanyike kuhusu vifo vya wanafunzi 17

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais William Ruto

    Rais wa Kenya William Ruto anasema habari za moto huo ni mbaya sana na ameagiza uchunguzi ufanyike kuhusu chanzo chake.

    "Tunawaombea manusura wapone haraka," amesema kwenye mitandao ya kijamii.“Naagiza mamlaka husika kuchunguza kwa kina tukio hili la kutisha, waliohusika watachukuliwa hatua.

    "Serikali chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa inakusanya rasilimali zote muhimu kusaidia familia zilizoathiriwa."

  15. Habari za hivi punde, Vifo vya wanafunzi 17 Kenya: Tunachojua kufikia sasa

    Kundi la wachunguzi limetumwa katika Shule ya Msingi ya Hillside Endarasha, polisi wanasema, baada ya moto uliotokea jana usiku katika shule hiyo.

    Kama tulivyoripoti, chanzo cha moto ulioua wanafunzi 17 bado hakijajulikana.Rais William Ruto aliutaja moto huo kuwa "wa kutisha" na "wa kuangamiza", na ameagiza uchunguzi ufanyike.

    "Waliohusika watachukuliwa hatua," aliandika kwenye mtandao wa kijamii.

    Msemaji wa polisi Resila Onyango ameliambia shirika la habari la AFP kwamba miili iliyookotwa "ilichomwa kiasi cha kutoweza kutambulika".

    "Miili zaidi ina uwezekano wa kupatikana iwapo eneo litachunguzwa kikamilifu," aliongeza.

  16. Mkurugenzi wa Telegram Durov anasema kukamatwa kwake 'kumepotoshwa'

    Pavel Durov, pichani mnamo 2016

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Telegram Pavel Durov amewashambulia viongozi wa Ufaransa, akitaja kukamatwa kwake wiki iliyopita kuhusiana na madai ya kutosimamia vyema programu ya utumaji ujumbe "kulipotoshwa".

    Katika taarifa yake ya kwanza kwa umma tangu azuiliwe, alikanusha madai kwamba Telegram ni "aina fulani ya paradiso ya machafuko" kama "isiyo ya kweli kabisa".

    Bw Durov alikamatwa tarehe 25 Agosti katika uwanja wa ndege kaskazini mwa Paris na tangu wakati huo ameshtakiwa kwa tuhuma za kushiriki katika kuruhusu miamala haramu, ulanguzi wa dawa za kulevya, ulaghai na kuenea kwa picha za unyanyasaji wa watoto kushamiri kwenye tovuti yake.

    Katika taarifa ya Bw Durov, ambayo aliichapisha kwenye Telegram, alisema kumshikilia kuwajibika kwa uhalifu uliofanywa na watu watatu kwenye jukwaa ni "mtazamo wa kushangaza" na "upotovu". "Ikiwa nchi haijafurahishwa na huduma ya mtandao, utaratibu uliowekwa ni kuanza hatua za kisheria dhidi ya huduma yenyewe," bilionea huyo mzaliwa wa Urusi, ambaye pia ni raia wa Ufaransa, alisema.

    "Kutumia sheria za enzi za kabla ya simu mahiri kumshtaki Mkurugenzi Mtendaji kwa uhalifu uliofanywa na wahusika wengine kwenye jukwaa analosimamia ni mbinu potofu."

    "Kuunda Teknolojia ni ngumu vya kutosha kama ilivyo. Hakuna mvumbuzi atakayewahi kuunda zana mpya ikiwa anajua anaweza kuwajibika binafsi kwa matumizi mabaya ya zana hizo," aliongeza.

    Ingawa alikubali kwamba Telegram haikuwa kamili, alisema mamlaka ya Ufaransa ilikuwa na njia kadhaa za kuwasiliana naye na Telegram, na kwamba programu ina mwakilishi rasmi katika EU.

    "Madai katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba Telegram ni aina fulani ya paradiso isiyo ya kweli si ya kweli kabisa. Tunaondoa mamilioni ya machapisho na chaneli zenye madhara kila siku," alisisitiza.

    Telegramu huruhusu vikundi vya hadi wanachama 200,000, jambo ambalo wakosoaji wamebishana hurahisisha habari potofu kuenea, na kwa watumiaji kushiriki maudhui ya njama, Nazi-mamboleo, watoto, au yanayohusiana na ugaidi.

    Telegram iliondoa baadhi ya makundi, hata hivyo wataalam wa usalama wa mtandao wanasema kwa ujumla mfumo wake wa kudhibiti maudhui yenye itikadi kali na haramu ni dhaifu sana kuliko ule wa makampuni mengine ya mitandao ya kijamii na programu za messenger.

    Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Bw Durov alikiri kwamba "ongezeko la ghafla" la idadi ya watumiaji kwenye programu ya kutuma ujumbe ikikadiriwa kuwa milioni 950, "imesababisha maumivu ambayo yamerahisisha wahalifu kutumia vibaya jukwaa letu." Alisema atalenga "kuboresha kwa kiasi kikubwa mambo katika suala hili".

    Hatua hiyo inakuja baada ya BBC kufahamu wiki jana kwamba Telegram imekataa kujiunga na programu za kimataifa zinazolenga kugundua na kuondoa nyenzo za unyanyasaji wa watoto mtandaoni.

  17. Habari za hivi punde, Wanafunzi 17 wateketea kwa moto nchini Kenya

    Moto

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wanafunzi kumi na saba wateketea kwa moto hadi kutoweza kutambulika katika ajali ya moto iliyotokea kwenye shule ya Hillside Endarasha iliyopo kaunti ya Nyeri nchini Kenya.

    Akithibitisha kisa hicho, msemaji wa polisi nchini Kenya Dr. Resila Onyango amesema kwamba maafisa wa polisi wa kuchunguza jinai wamefika katika shule hiyo kuanza uchunguzi wa kilichochangia moto huo.

    14 wanapata matibabu katika hospitali mbali mbali katika kaunti hiyo ya Nyeri iliyopo katika eneo la kati mwa nchi hiyo.

    Kwa sasa shule imefungwa huku polisi wakichunguza bweni ambapo moto huo ulianza.

    Rais wa Kenya William Ruto ametoa salamu za pole kwa Wakenya.

    Amesema Serikali inakusanya rasilimali zote muhimu ili kusaidia familia zilizoathiriwa.

  18. Ukraine ilifanikiwa kutokana na mashambulizi ya Kursk - Katibu Mkuu wa NATO

    Ukraine imepata mafanikio mengi wakati wa mashambulizi yake katika eneo la Kursk

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ukraine imepata mafanikio mengi wakati wa mashambulizi yake katika eneo la Kursk, lakini ni vigumu kusema jinsi hali itakavyoendelea zaidi, Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema wakati wa ziara ya Oslo.

    "Waukraine pekee ndio wanaweza kufanya maamuzi magumu ambayo ni muhimu, kama vile wapi pa kupeleka majeshi yao na aina gani ya vita inafaa katika hali hii," alisema.

    Ukraine ina haki ya kujilinda, ikiwa ni pamoja na msaada wa makombora ya masafa marefu ambayo yanaweza kufikia malengo ya kijeshi kwenye ardhi ya Urusi, Katibu Mkuu wa NATO alisisitiza.

    "Nina furaha kwamba nchi nyingi za NATO zimetoa fursa hii, na zile ambazo bado zina vikwazo zimezipunguza ili Ukraine iweze kujilinda," Stoltenberg alinukuliwa akisema.

    Unaweza kusoma;

  19. Wapalestina watano wauawa kwa shambulizi Ukingo wa Magharibi, wizara ya afya yasema

    Athari za mashambulizi

    Chanzo cha picha, EPA

    Wapalestina watano wameuawa katika shambulizi la anga la Israel kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, wizara ya afya ya Palestina imesema.

    Wengine wawili walijeruhiwa wakati gari lilipopigwa huko Tubas mapema Alhamisi. Jeshi la Israel lilisema lilishambulia "kikundi cha kigaidi kilichokuwa na silaha" na makundi yenye silaha yalidai waliuawa kama wapiganaji.

    Vyombo vya habari vya Palestina pia vilisema mvulana mwenye umri wa miaka 16 aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel katika kambi ya karibu ya wakimbizi ya al-Faraa.

    Jeshi lilisema vikosi vilimuua "gaidi ambaye alikuwa na kilipuzi" katika majibizano ya risasi na kwamba shambulio lililenga wengine.

    Kwa muda wa siku tisa, wanajeshi wa Israel wamekuwa wakivamia miji ya kaskazini ikiwa ni sehemu ya kile wanachosema ni operesheni kubwa ya kukabiliana na ugaidi.

    Kufikia sasa, takribani Wapalestina 36 wameuawa, wakiwemo 21 kutoka mkoa wa Jenin, wanane kutoka Tubas, kulingana na wizara ya afya.

    Wengi wa waliofariki wamedaiwa na makundi yenye silaha kama wanachama, lakini wizara hiyo inasema watoto kadhaa pia ni miongoni mwao, akiwemo msichana mwenye umri wa miaka 16 ambaye alipigwa risasi nyumbani kwake karibu na Jenin siku ya Jumanne.

    Mwanajeshi mmoja wa Israel ameuawa wakati wa mapigano huko Jenin.

    Taarifa kutoka kwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) ilisema wanajeshi na jeshi la Magereza la Israel walianza operesheni katika kambi ya Tubas na al-Faraa Jumatano usiku.

    Ilimtaja mmoja wa watu watano waliouawa katika shambulio la anga huko Tubas kuwa ni Mohammed Zakaria Zubeidi, 21, na kusema alikuwa "gaidi mkubwa kutoka eneo la Jenin".

    Alikuwa pia mtoto wa Zakaria Zubeidi, kamanda wa zamani aliyefungwa huko Jenin wa mrengo wenye silaha wa harakati ya Fatah, Brigedi za Mashahidi wa Al-Aqsa, na anayedaiwa kuwa ndiye mpangaji mkuu wa uvunjaji wa gereza mnamo 2021.

    Unaweza kusoma;

  20. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu