Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Kenya na Tanzania kushirikiana kwa karibu kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ni uanaharakati unaovuruga utulivu, akihimiza hatua madhubuti dhidi ya watu aliowatuhumu kutumia demokrasia kuchochea machafuko.
Akizungumza wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais William Ruto nchini Tanzania, Suluhu amesema suala la uanaharakati wa kuvuka mipaka pamoja na maandamano yanayoongozwa na vijana imejitokeza kwa uzito katika mazungumzo yake na kiongozi huyo wa Kenya.
Amesema viongozi hao wamejadili namna ya kushughulikia kile alichokitaja kuwa tabia ya vijana wanaojiita Gen Z ambao, kwa mujibu wake, huzunguka wakidai kutetea demokrasia huku wakisababisha vurugu, kuchoma mali na kuvuruga utulivu wa serikali zao.
“Tunapaswa kusimama kidete dhidi ya watu hawa. Wakija kwangu nitashughulika nao, wakija kwako washughulikie ili wajifunze kuwa na nidhamu,” amesema, akiongeza kuwa demokrasia haipaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuvuruga serikali au kuharibu mali.
Aidha, Suluhu alisema mifumo ya kidemokrasia inapaswa kuakisi mila, desturi na mazingira ya jamii husika badala ya kuiga mifumo kutoka nje.
“Demokrasia isiharibu nchi zetu, mila zetu wala desturi zetu. Demokrasia haina mfumo mmoja wa wote,” alisema.
Kauli zake zinakuja wakati serikali za Afrika Mashariki zinaendelea kuangaliwa kwa karibu kuhusu namna zinavyoshughulikia maandamano ya vijana na sauti za upinzani.
Hivi karibuni, Kenya na Tanzania zimekumbwa na ukosoaji kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu kuhusu hatua kali dhidi ya wanaharakati.
Nchini Kenya, maandamano dhidi ya muswada wa fedha wa mwaka 2024 yaliyoongozwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa Gen Z, yalikumbana na nguvu kubwa ya polisi, hatua iliyolaaniwa na asasi za kiraia pamoja na waangalizi wa kimataifa.
Ripoti ya karibuni ya Freedom House imezidisha mjadala huo baada ya kuitaja Kenya na Tanzania miongoni mwa nchi zinazotuhumiwa kutumia ukandamizaji wa kuvuka mipaka, ikiwemo kuwafuatilia wapinzani wa kisiasa nje ya mipaka yao.
Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya walikuwa wa kwanza kujibu kauli hizo. Katibu Mkuu wa Orange Democratic Movement, Edwin Sifuna, alitetea uanaharakati akisema ni nguzo muhimu ya demokrasia. “Kama wanasema tupigwe, basi iwe hivyo. Tutaendelea kuitetea demokrasia, hata kama wanatuona kuwa ni vijana wasio na nidhamu,” Sifuna aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Ruto, ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kiserikali inayolenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika biashara, miundombinu na ushirikiano wa kikanda, hakugusia moja kwa moja matamshi ya Suluhu kuhusu wanaharakati wakati wa kuonekana kwao pamoja hadharani.