Je, mpango wa "Bahari 4" wa Syria kuwa mbadala wa Hormuz?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Wakati Mashariki ya Kati inapambana na mzozo wa vita vya Iran na kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, mawazo tofauti yanajitokeza nchini Syria yanayoiweka nchi hiyo kama ukanda wa kati wa nishati na mtiririko wa biashara duniani.

Mnamo Aprili 17, katika mkutano wa Jumuiya ya Diplomasia ya Antalya nchini Uturuki na siku chache baadaye katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya huko Cyprus, Rais wa Syria Ahmed al-Sharaa alisema anatumai nchi yake itatumia eneo lake la kimkakati kuwa njia mbadala ya kuhamisha nishati na bidhaa, na kutoa ufikiaji salama kwa Bahari ya Mediterania kwa kuunganisha Ghuba ya Uajemi na Uturuki.

Ili kuendeleza dira hii, serikali ya Syria imezingatia mipango miwili mikuu: mradi wa "Bahari Nne" na mpango wa "4+1".

Hatahivyo licha ya matumaini yanayozunguka mipango hii miwili, miradi hii inakabiliwa na changamoto kubwa.

Mpango wa "Bahari Nne" ni upi?

Mpango wa "Bahari Nne", unaojulikana pia kama "Mpango wa 9 ," unatoa taswira ya mtandao jumuishi wa usafiri na nishati unaounganisha Ghuba ya Uajemi, Mediterania, Bahari ya Caspian na Bahari Nyeusi.

Lengo lake kubwa ni kuweka Syria na Uturuki kama vitovu vya biashara ya kikanda na mtiririko wa nishati.

Ahmed Sharia aliutambulisha mpango huo katika mkutano wa Cyprus Aprili 24, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Asad Shaibani, wakati wa ziara yake mjini Ankara, akiuelezea kuwa ni mwanzo wa awamu mpya ya ushirikiano wa kimkakati wa pande mbili.

Waraka uliochapishwa na Al-Majla, chombo cha habari cha Kiarabu kinachomilikiwa na Saudia, na kuhusishwa na Tom Barak, mwakilishi maalum wa Marekani kwa Syria, unaeleza pendekezo la Marekani la kuibadilisha Syria kuwa kitovu kikuu cha usafirishaji wa nishati duniani.

Kwa mujibu wa jarida hilo, mpango huo unalenga katika kukarabati na kupanua mtandao mkubwa wa mabomba yaliyopo na yanayopendekezwa yanayounganisha maeneo ya mafuta ya Ghuba ya Uajemi na Iraq na bandari za Bahari ya Mediterania na kisha Ulaya.

Chapisho hilo linasema kuwa ujenzi wa bomba la mafuta la Kirkuk-Banias utagharimu takriban dola bilioni 4.5, na kwamba Syria inatarajia kupata takriban dola milioni 200 kila mwaka kutokana na ada za usafiri.

Chombo hicho pia kilitaja mipango ya kupanua Bomba la Gesi la Kiarabu kutoka Misri, kupitia Syria hadi Uturuki, pamoja na njia inayopendekezwa ya gesi ya Qatar-Uturuki, ambayo itasafirisha gesi ya Qatar kupitia Jordan na Syria hadi Uturuki na kisha Ulaya.

Mpango wa "4+1" ni nini?

Kama sehemu ya juhudi za Syria kujiweka kama kitovu cha nishati kikanda, serikali ilianzisha mpango wa "4+1" mnamo Machi 2026.

Mpango huo unalenga kuunda njia za nishati zilizounganishwa na salama kupitia njia za nchi kavu ambazo hupunguza utegemezi wa njia za jadi za baharini.

Osama Ghazi, mshauri wa Wizara ya Uchumi ya Syria, aliiambia tovuti ya Al-Arabi Al-Jadeed kwamba wakati Mradi wa 'Bahari Nne' unaunganisha njia za maji za kikanda, mpango wa "4+1" unaunganisha uchumi wa kikanda na kuiweka Syria katikati ya mtandao wa bahari, ardhi na njia za reli.

Aliitaja miradi hiyo miwili kuwa ni ya nyongeza, akisema kila moja unaimarisha malengo ya mwingine kwa utulivu na maendeleo ya kikanda.

Mpango huu unakusudiwa kuunda mfumo jumuishi wenye njia mbalimbali.

Makadirio yenye matumaini, ikiwa ni pamoja na takwimu zilizotajwa na Osama Ghazi, zinaweka gharama ya jumla ya miradi ya "4+1" kuwa chini ya dola bilioni 50.

Changamoto kuu ni zipi?

Miradi hii, licha ya mvuto na matumaini yao, inakabiliwa na hali ngumu.

Uwezekano wao unategemea kushinda udhaifu wa kisiasa na kitaasisi wa Syria, kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na vita vya miaka mingi, na kukabiliana na vikwazo vya kifedha, usalama na kijiografia.

Sarkis Kasarjian, mwandishi wa habari aliyebobea Uturuki na Mashariki ya Kati, aliiambia Euronews kwamba mapendekezo hayo si mapya na kwamba Syria haina miundombinu, utulivu na manufaa ya kijiografia ya nchi kama vile Saudi Arabia, Israel na Uturuki.

Alisema dosari za kiusalama na kiutawala zimesalia kuwa vikwazo vikubwa, na udhaifu wa kisiasa na kitaasisi wa Syria ndio vikwazo vikuu vya ujenzi na maendeleo.

Mhandisi wa mafuta wa Syria Ghassan Raei aliiambia Euronews kwamba baadhi ya sehemu za mtandao wa mabomba ya Syria, ambazo zilikuwa zikifanya kazi kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza mwaka 2011, zinaweza kukarabatiwa au kupanuliwa.

Lakini aliongeza kuwa ujenzi wowote wa njia hizo utategemea upatikanaji wa rasilimali za kifedha na hali ya usalama, akibainisha uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi baada ya miaka ya vita.

Mpango wa ushindani

Mipango hii ya Syria inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mipango mingine inayopendekeza njia mbadala za biashara ambazo zinaweza kupita nchi nzima. Maarufu zaidi kati ya haya ni Ukanda wa Kiuchumi wa India-Mashariki ya Kati-Ulaya unaopendekezwa.

Mpango huo uliozinduliwa katika mkutano wa kilele wa G20 mnamo Septemba 2023, unalenga kuunganisha India, Mashariki ya Kati na Ulaya kwa kuboresha miundombinu ya usafiri, dijitali na nishati.

Mpango huo ambao unaungwa mkono na India, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Marekani na washirika wakuu wa Ulaya, umewasilishwa kama njia mbadala ya Mpango wa China Belt and Road Initiative.

Ukanda unaopendekezwa unajumuisha njia ya baharini kutoka India hadi Umoja wa Falme za Kiarabu, iliyounganishwa na njia ya reli kupitia Saudi Arabia na Jordan hadi bandari ya Haifa nchini Israel, ambapo bidhaa zingesafirishwa hadi Ulaya.