Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Wamarekani waanza kupiga kura katika uchaguzi muhimu kwa urais wa Trump

Kadiri vituo zaidi vinavyofunguliwa kote nchini humo, wapiga kura watakuwa wakiwachagua wagombea katika uchaguzi muhimu utakaoamua uwiano wa nguvu katika Bunge la Marekani (Congress) pamoja na nafasi za ugavana katika baadhi ya majimbo.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Asha Juma

  1. Wamarekani waanza kupiga kura katika uchaguzi muhimu kwa urais wa Trump

    Kura zaanza katika uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani utakaoamua mwelekeo wa kipindi kilichosalia cha urais wa Trump

    Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa pwani ya mashariki ya Marekani

    Saa kumi na mbili asubuhi kwa saa za pwani ya mashariki ya Marekani, vituo vya kupigia kura vimefunguliwa rasmi katika majimbo kadhaa ya eneo hilo, yakiwemo New York, New Jersey, Virginia, Maine na Kentucky.

    Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja iliyopita katika jimbo la Vermont, huku wapiga kura wa North Carolina, Ohio na West Virginia wakitarajiwa kuanza kupiga kura ndani ya nusu saa.

    Kadiri vituo zaidi vinavyofunguliwa kote nchini humo, wapiga kura watakuwa wakiwachagua wagombea katika uchaguzi muhimu utakaoamua uwiano wa nguvu katika Bunge la Marekani (Congress) pamoja na nafasi za ugavana katika baadhi ya majimbo.

    Matokeo ya uchaguzi huu yanatarajiwa kuwa na athari kubwa si tu nchini Marekani bali pia katika medani ya kimataifa.

    Endelea kufuatilia kwa taarifa zaidi kutoka kwa waandishi wetu kote nchini Marekani, pamoja na maoni ya wananchi kuhusu masuala yanayowasukuma wanapoelekea kupiga kura.

    Soma Zaidi:

  2. Israel: Hatukuhusika na mashambulizi ya jana usiku dhidi ya Iran

    Jeshi la Israel lilisema Jumanne kwamba halikuhusika katika mashambulizi yanayoripotiwa kufanywa na Marekani dhidi ya kisiwa kimoja nchini Iran.

    Taarifa hiyo imekuja wakati Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, hivi karibuni alitishia kuanzisha tena vita dhidi ya Tehran.

    Akijibu swali la AFP, msemaji wa jeshi la Israel alisema kuwa Israel haikushiriki katika mashambulizi ya Marekani ya jana usiku dhidi ya Kisiwa cha Qeshm.

  3. Mshambuliaji wa Tenerife Miguel afariki baada ya kuumia kichwa uwanjani

    Mshambuliaji wa klabu ya Hispania ya Tenerife, Jesus de Miguel, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 30 baada ya kupata majeraha makubwa wakati wa mchezo wa ligi daraja la pili nchini humo dhidi ya Andorra .

    Mshambuliaji huyo alipata majeraha kichwani na kifuani wakati wa mchezo dhidi ya Andorra siku ya Jumatatu, baada ya kugongana na kipa Jesus Owono, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kutokana na tukio hilo.

    Hali ya De Miguel ilielezwa kuwa “mbaya lakini imara” siku ya Jumatatu, lakini afya yake ilizidi kuwa mbaya zaidi Jumanne asubuhi, kabla ya kuaga dunia saa mbili asubuhi.

    “Mioyo yetu imeumia na kushindwa kuamini kuwa haya yametokea kweli, klabu ya CD Tenerife inasikitika kutangaza kifo cha Jesus de Miguel Alameda,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.

    “Hakuna maneno yanayoweza kutoa faraja; hakuna kabisa kitu kinachoweza kupunguza huzuni hii kubwa. Tuko pamoja na familia yake yenye majonzi, wapendwa wake na watu wote wa Tenerife wanaoomboleza msiba huu leo.

    Klabu ya Andorra, ambayo inamilikiwa kwa pamoja na beki wa zamani wa Barcelona, Gerard Pique, ilisema: “Tunahuzunika, tunapenda kutoa pole zetu za dhati kwa familia ya Jesus de Miguel, wachezaji wenzake, marafiki zake na klabu ya CD Tenerife.”

    Tenerife na Andorra zilikuwa sare ta mabao 2-2, dakika saba baada ya muda wa kawaida wa mchezo kuongezwa, tukio hilo lilipotokea.

    Owono alitoka lango kuuwahi mpira mrefu, kwenye purukushani za kuokoa goti lake lilimgonga De Miguel.

    Mshambuliaji huyo alipoteza fahamu huku wahudumu wa afya wakimpatia matibabu, kabla ya kuondolewa kwa gari la wagonjwa kutoka uwanja wa Estadio Heliodoro Rodriguez Lopez wa Tenerife na kupelekwa hospitalini.

    Wachezaji wa timu zote mbili walionekana kushtushwa sana na tukio hilo, huku baadhi ya wachezaji wenzake De Miguel wakitokwa na machozi.

    Mwamuzi alimwonyesha Owono kadi nyekundu ya moja kwa moja kabla ya kusimamisha mchezo.

    Vyombo vya habari vya Hispania, vikiwemo gazeti la Marca, viliripoti kuwa De Miguel alipata mshtuko wa moyo ndani ya gari la wagonjwa akikimbizwa kwenda hospitalini.

    Tenerife ilieleza Jumatatu usiku kuwa hali yake ilikuwa “mbaya lakini imara”. Hata hivyo, taarifa nyingine iliyotolewa Jumanne asubuhi ilisema hali yake ilizidi kuwa mbaya katika upande wa mfumo wa fahamu”. Kabla baadae kutangaza kifo chake

  4. Tinubu: Niliwaombea Wanigeria wote wakati wa hija yangu Saudi Arabia

    Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, amekamilisha ibada ya Umra nchini Saudi Arabia, akisema aliwaombea Wanigeria wote wapate amani, umoja na ustawi.

    Rais huyo alieleza hayo Jumatatu kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.

    “Nimekamilisha hija yangu nchini Saudi Arabia. Pamoja na wajumbe wa msafara wangu, tulipata heshima kubwa ya kuingia ndani ya Al Kaaba Tukufu, kuomba na kutekeleza ibada ya Umra,” alisema.

    Tinubu pia alieleza kuwa ziara hiyo na uzoefu alioupata ni ushahidi wa uhusiano wa kidini wa muda mrefu, urafiki na kuheshimiana kati ya Nigeria na Saudi Arabia.

    Wiki iliyopita, rais huyo alisafiri kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Umrah.

  5. DRC: Tshisekedi adai kesi dhidi ya familia yake Ubelgiji ni njama ya kumharibia sifa

    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, amesema kesi inayowakabili baadhi ya wanafamilia wake nchini Ubelgiji ni kampeni ya kumchafua inayoratibiwa na wapinzani wake, akiiita njama ya kihalifu inayolenga kuharibu sifa yake.

    Kwa mujibu wa Radio Okapi, Tshisekedi alitoa kauli hiyo alipokutana na raia wa Congo wanaoishi nchini Urusi.

    Kituo hicho cha redio kilinukuu mahojiano aliyofanya kwa lugha ya Lingala, ambayo baadaye yalichapishwa kwenye akaunti ya Ofisi ya Rais katika mtandao wa X.

    Tshisekedi amesema wapinzani wake waligeukia familia yake baada ya kuona kuwa alikuwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wananchi.

    Amesema awali walimtuhumu kutumia vibaya fedha za serikali kwa safari, lakini Benki Kuu ya Congo ilieleza kuwa fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwenye bajeti.

    Rais huyo aliwashutumu wakili aliyemtaja kuwa bandia na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, kwa kushirikiana katika kile alichokiita njama ya kumfikia kupitia familia yake.

    Alisema: “Kisha waliamua kuishambulia familia yangu. Waliungana na wakili bandia ambaye amekuwa akishirikiana na Wanyarwanda kwa miaka 30, pamoja na mtu tuliyemwondoa madarakani, ili kuihujumu familia yangu wakitarajia kuwa hilo pia litaniathiri.”

    Akizungumzia uchunguzi unaoendelea kuhusu kesi hiyo, Tshisekedi amesema hadi sasa hakuna ushahidi muhimu uliojitokeza kuhusu fedha zinazotiliwa shaka au vitu vilivyokamatwa wakati wa upekuzi.

    Amesema bado anasubiri kufahamishwa ni nini hasa kilichopatikana katika upekuzi huo.

    Tshisekedi amesema tayari ameunda timu ya mawakili ili kukabiliana na madai hayo kupitia njia za kisheria.

    “Tumeajiri timu ya mawakili. Tutawajibu wanaotushutumu,” alisema.

    Rais huyo amekanusha tuhuma zinazohusisha baadhi ya wanafamilia wake na uchimbaji haramu wa madini ya thamani katika eneo la Katanga.

    Badala yake, amedai kuwa watu waliohusika na uporaji wa rasilimali za asili katika eneo hilo wanajulikana, akiwataja aliyekuwa rais Joseph Kabila na Moïse Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga ambaye sasa ni mwanasiasa wa upinzani anayeishi uhamishoni.

    Kauli hizo zinatolewa wakati kesi dhidi ya baadhi ya wanafamilia wa Tshisekedi ikiendelea kuzua mjadala nchini DRC na kuongeza mvutano katika uhusiano kati ya Kinshasa na Brussels.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Lissu aitaka familia kumpa kaka yake mazishi ya heshima

    Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameitaka familia yake kuhakikisha kaka yake mkubwa, marehemu Alute Mughwai Lissu, anazikwa kwa heshima na staha.

    Lissu pia ameahidi kuchangia shilingi milioni 15 kugharamia maandalizi ya mazishi hayo.

    ''Mpatieni maziko ya heshima'', Lissu aliiambia familia yake baada ya kupokea taarifa za kifo cha kaka yake kilichotokea Jumapili.

    Akiwa mahakamani, Lissu alitoa maelekezo hayo kwa familia yake, akisisitiza kuwa kaka yake anapaswa kupewa mazishi yanayostahili.

    Haya yanajiri baada ya familia yake kuahirisha mazishi hadi hukumu ya. kesi ya uhaini dhidi ya Lissu itolewe Novemba 6, 2026.

    Dk. Vincent, ambaye ni mmoja wa ndugu wa familia hiyo, amesema wamekubaliana kufanya mazishi baada ya tukio hilo muhimu, akieleza kuwa wanataka kwanza kuwa pamoja wakati wa kusikiliza hukumu ya ndugu yao.

    “Tumepanga mazishi ya kaka Alute yatafanyika Singida. Tunatarajia tutasukuma mbele mazishi ili Ijumaa (Novemba 6, 2026), wanafamilia tuweze kuwepo Dar es Salaam kuhudhuria hukumu ya kesi ya ndugu yetu Tundu,” amesema.

    Alute alikuwa akiugua kwa muda mrefu. Katika siku zake za mwisho, alilazwa katika Hospitali ya Selian jijini Arusha, hali yake ilizidi kuwa mbaya kuanzia juzi kabla ya kufariki dunia Jumamosi usiku.

    Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika katika kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, baada ya familia kushiriki katika usomaji wa hukumu ya kesi ya Tundu Lissu.

    Lissu amekuwa mahabusu tangu Aprili mwaka 2025, akikabiliwa na shtaka la uhaini. Hukumu ya kesi hiyo inatarajiwa kutolewa Novemba 6, 2026.

    Unaweza kusoma;

  7. Marekani yashambulia kisiwa cha Iran kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula

    Marekani imeripotiwa kufanya mashambulizi katika kisiwa cha Qeshm nchini Iran, kilichopo katika Mlango-Bahari wa Hormuz, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Fox News na The Wall Street Journal.

    Kituo cha televisheni cha CBS, kikirejelea maafisa wa Marekani, pia kimeripoti kuwa vikosi vya Marekani vilishambulia kisiwa hicho. Taarifa hizo zimesababisha kupanda kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa.

    Maafisa wa Marekani wameelezea mashambulizi hayo kuwa operesheni yenye wigo mdogo, wakisema yalifanyika kujibu kuangushwa kwa ndege ya Marekani na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC).

    Hata hivyo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), inayosimamia operesheni za kijeshi katika Mashariki ya Kati, haijatoa tamko kuhusu taarifa hizo. BBC imesema imewasiliana na CENTCOM kutaka maelezo zaidi.

    Taarifa za mashambulizi hayo zimeibuka wakati Marekani ikifanya uchaguzi wa katikati ya muhula, ambao utaamua iwapo Chama cha Republican kitaendelea kudhibiti Congress au Democrats watapata wingi wa viti.

    Rais Donald Trump amekuwa akikabiliwa na kushuka kwa viwango vya uungwaji mkono katika siku za hivi karibuni, huku baadhi ya wanachama wa chama chake wakimtaka kusitisha vita vilivyoanza mwezi Februari baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Mapema Jumatatu, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa hana haraka ya kuongeza mashambulizi dhidi ya Iran.

    Akizungumza na chombo cha habari cha Axios, alisema: "Kwa namna moja au nyingine, tutachukua hatua, lakini hakuna haraka. Tumewadhoofisha kifedha."

    Aliongeza kuwa Iran haina fedha wala mafuta ya kutosha, na kwamba wananchi wake wameanza kuchoshwa na hali hiyo.

    Katika mahojiano na Fox News siku moja kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula, Trump pia alisema Marekani huenda ikalazimika kulenga Mlima Kalinga, eneo linalohusishwa na mpango wa nyuklia wa Iran. Alidai kuwa shambulizi hilo si jambo kubwa na linaweza kutekelezwa ndani ya saa moja.

    Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na tetesi kuwa Marekani inaweza kurejea kwenye mashambulizi makubwa dhidi ya Iran baada ya uchaguzi huo. Hata hivyo, alipoulizwa Jumatatu iwapo angeanzisha tena mashambulizi baada ya uchaguzi, Trump alijibu: "Hapana."

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameiambia shirika la habari la IRNA kuwa mazungumzo muhimu yanaendelea na maafisa wa Marekani kupitia wapatanishi, kwa lengo la kumaliza vita.

    Araqchi amesema Tehran iko tayari zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa suluhisho la kidiplomasia au hatua za kijeshi. Ameongeza kuwa uamuzi sasa uko mikononi mwa Marekani, kuchagua njia ya busara ya mazungumzo au kurudia kile alichokiita kosa la uchokozi wa kijeshi.

    Soma Pia:

  8. Korea Kaskazini yakanusha kuhusika na wizi wa dola bilioni 6.3 katika Binance

    Korea Kaskazini imekanusha madai kuwa ilihusika na wizi wa fedha za kidijitali wenye thamani ya dola bilioni 6.3 kutoka katika jukwaa la biashara ya sarafu za kidijitali la Binance, ikiyataja madai hayo kuwa ni kauli zisizo na msingi.

    Kim Yo Jong, afisa mwandamizi wa Korea Kaskazini na dada wa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un, amesema Jumanne kuwa tuhuma hizo ni jaribio jingine la Marekani la kuchafua taswira ya Pyongyang mbele ya jumuiya ya kimataifa.

    Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), Idara ya Usalama wa Taifa na wachambuzi wa masuala ya uhalifu wa kimtandao wamesema Korea Kaskazini ndiyo iliyopanga shambulizi hilo, ambalo limetajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia.

    Hili ni tukio la hivi karibuni kati ya mashambulizi kadhaa ya kimtandao yanayohusishwa na Korea Kaskazini, ambayo imekuwa ikituhumiwa kutumia uhalifu wa kimtandao kupata fedha za kufadhili uchumi wake unaokabiliwa na vikwazo vya kimataifa.

    Wachambuzi wa teknolojia ya blockchain pamoja na FBI wamesema shambulizi hilo lilitekelezwa na kundi la wadukuzi linaloungwa mkono na serikali ya Korea Kaskazini, linalojulikana kama TraderTraitor.

    FBI imezitaka kampuni na wadau wa sekta hiyo kushirikiana kuzuia miamala inayohusisha akaunti za sarafu za kidijitali zinazohusishwa na kundi hilo.

    Katika taarifa yake, Kim Yo Jong, ambaye ni mkurugenzi wa Idara ya Masuala ya Jumla ya Korea Kaskazini, amesema Marekani imeendeleza uchochezi wa kawaida kwa kuihusisha tena nchi yake na uhalifu wa kimtandao.

    Amesema ni uchochezi mkubwa wa kisiasa kwa Marekani kupotosha maoni ya jumuiya ya kimataifa kwa kuashiria kuwa uhalifu wote wa kimtandao unaotokea sehemu mbalimbali duniani unafanywa na Korea Kaskazini.

    Hata hivyo, Pyongyang imekuwa ikihusishwa na mashambulizi kadhaa makubwa ya kimtandao katika miaka ya hivi karibuni, ingawa imeendelea kukanusha tuhuma hizo.

    Kwa upande wake, Binance imesema wateja wake walitoa mali zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3.6 kutoka kwenye jukwaa hilo siku ya Jumapili, baada ya kurejesha huduma zilizokuwa zimesitishwa kufuatia shambulizi hilo.

    Kampuni hiyo imesema itagharamia hasara zote zilizotokana na wizi huo na kwamba tayari imeshughulikia takribani asilimia 95 ya mali zilizoibwa.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Wang Yi: China yaunga mkono juhudi za Iran kulinda mamlaka na usalama wake

    Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, amesema nchi yake inaiunga mkono Iran katika juhudi za kulinda mamlaka yake ya kujitawala na usalama wake.

    Akizungumza katika mkutano na Ali Bagherikani, Naibu Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Wang amesema China inazitaka pande zote zinazohusika katika mzozo wa Mashariki ya Kati kuelekeza nguvu zao katika kutafuta suluhisho la kisiasa.

    Rais wa China, Xi Jinping, pia alisema Jumatatu alipokutana na Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq Al Said, kuwa Mashariki ya Kati na eneo la Ghuba havipaswi kuwa uwanja wa mashindano ya mataifa yenye nguvu duniani.

    Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo, Oman iliunga mkono mapendekezo ya China kuhusu amani Mashariki ya Kati, huku ikieleza matumaini kuwa Beijing itachukua nafasi kubwa zaidi na inayoonekana katika juhudi za kuhakikisha utulivu wa kudumu katika eneo hilo.

    China ndiyo mnunuzi mkubwa zaidi wa mafuta kutoka Iran na ni miongoni mwa washirika wake muhimu wa kiuchumi.

    Beijing imelaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na vikwazo ilivyowekewa na Washington. Pia imekuwa ikitoa wito wa kusitishwa kwa vita, ikisisitiza umuhimu wa kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kupitia diplomasia.

    Soma pia:

  10. Trump kuiondoa Rwanda na Afrika Kusini katika mpango wa biashara wa Marekani

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameiarifu Bunge la nchi hiyo kuhusu mpango wake wa kuiondoa Rwanda na Afrika Kusini katika mpango wa upendeleo wa kibiashara, kuanzia Januari Mosi mwaka 2027.

    Mpango wa Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA) unaziwezesha nchi za Afrika zinazokidhi vigezo kuuza maelfu ya bidhaa nchini Marekani bila kutozwa ushuru wa forodha.

    Katika taarifa yake, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, amesema tathmini ya kila mwaka imebaini kuwa nchi hizo mbili zinajihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na masharti ya mpango huo.

    Ameongeza kuwa utawala wa Trump tayari umeziarifu Rwanda na Afrika Kusini kuhusu uamuzi huo.

    Utawala wa Marekani umetaja vikwazo katika biashara na uwekezaji wa Marekani, pamoja na wasiwasi kuhusu masuala ya usalama wa taifa na maslahi ya sera za kigeni katika eneo hilo.

    Kwa upande wa Rwanda, Washington pia imeibua wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu, uwepo wa vyama na mitazamo mbalimbali ya kisiasa, utawala wa sheria na haki za wafanyakazi.

    Hatua hiyo inakuja takribani wiki moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda kuwekewa vikwazo na Wizara ya Fedha ya Marekani kutokana na madai ya kuhusika kwake katika uasi wa makundi yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema Wizara ya Ulinzi ya Rwanda ilielekeza maelfu ya wanajeshi kushirikiana na waasi wa M23 katika mapigano mashariki mwa DRC, huku ikiwapatia silaha, vifaa, msaada wa usafirishaji na mahitaji ya kijeshi pamoja na mafunzo.

    Soma Pia:

  11. Tetesi za soka Jumanne: Arsenal wamnyatia Kroupi katika dirisha la usajili la Januari

    Mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Arsenal, wanataka kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi katika dirisha la usajili la Januari.

    Hata hivyio, wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa Bayern Munich na Paris Saint-Germain katika kinyang'anyiro cha kumwania mshambuliaji huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 20. (Mirror)

    Kiungo mshambuliaji wa Juventus, Kenan Yildiz, mwenye umri wa miaka 21, pia anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia Arsenal. Hata hivyo, kocha Mikel Arteta kwa sasa ameweka mkazo katika kuimarisha safu ya ushambuliaji. (Mirror)

    Manchester United imekuwa ikifuatilia kwa karibu wachezaji wanne wa Borussia Dortmund. Wachezaji hao ni mshambuliaji wa Guinea Serhou Guirassy, mwenye umri wa miaka 30, kiungo Mwingereza Jobe Bellingham, 21, kiungo Mjerumani Felix Nmecha, 26, na beki wa Sweden Daniel Svensson, 24. (Teamtalk)

    Kipa wa Brighton na timu ya taifa ya Uholanzi, Bart Verbruggen, mwenye umri wa miaka 24, yuko tayari kujiunga na Real Madrid endapo klabu hiyo itatoa nafasi ya kumsajili. (Football Insider)

    Brighton pia inamfuatilia beki chipukizi wa Estoril, Jordan Arnolin, mwenye umri wa miaka 18. Hata hivyo, klabu hiyo ya England inakabiliwa na ushindani kutoka Barcelona, ambayo pia inavutiwa na huduma ya beki huyo Mreno. (Record kupitia Sport Witness)

    Sunderland inatarajiwa kumpa kocha Regis Le Bris fedha za kufanya usajili katika dirisha la Januari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha matokeo ya klabu hiyo. (The i)

    Kocha wa Nottingham Forest, Oliver Glasner, ambaye amekuwa akikabiliwa na presha kutokana na matokeo ya timu hiyo, amepata uungwaji mkono kutoka kwa wachezaji wake baada ya kufanya nao kikao katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo. (Telegraph)

    Klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England zinafuatilia maendeleo ya beki wa Celta Vigo, Javi Rodriguez, mwenye umri wa miaka 23. (Teamtalk)

    Atletico Madrid nayo inataka kumsajili kiungo chipukizi wa Almeria, Stefan Dzodic, mwenye umri wa miaka 21, raia wa Serbia, ili kuimarisha kikosi chake kwa msimu ujao. (Marca)

    Soma pia:

  12. Watu 26 wauawa katika shambulio la Urusi nchini Ukraine

    Takribani watu 26 wameuawa baada ya mabomu ya Urusi kulenga kituo cha usambazaji wa misaada ya kibinadamu nchini Ukraine, katika shambulizi ambalo Rais Volodymyr Zelensky amelielezea kuwa la kutisha mno.

    Watu wengine watano wamejeruhiwa, huku 27 wakiripotiwa kutoweka awali baada ya angalau mabomu tisa ya angani, kila moja likiwa na uzito wa tani tatu, kuliporomoka katika kijiji cha Komyshuvakha, katika eneo la Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine.

    Mkuu wa eneo hilo, Mykhailo Semikin, amesema mashambulizi hayo yalitokea Jumatatu.

    Rais Zelensky amesema shambulizi la kwanza lililenga shule ya eneo hilo iliyokuwa ikitumika kwa shughuli za kibinadamu. Ameongeza kuwa shambulizi la pili lilifuata, likilenga eneo ambalo watu walikuwa wamejisitiri.

    Katika video aliyochapisha, Zelensky alionyesha shimo kubwa lililoachwa na mlipuko huo pamoja na waokoaji wakifanya shughuli za kutafuta manusura na miili ya watu kwenye vifusi.

    Jeshi la Urusi halijatoa tamko lolote hadharani kuhusu shambulizi hilo.

    Soma pia:

  13. Marekani yapiga kura leo kuamua udhibiti wa bunge la Congress

    Wagombea wa vyama vya Republican na Democratic nchini Marekani wamehitimisha kampeni zao za mwisho kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula, huku udhibiti wa Bunge la Congress ukiwa hatarini kwa chama cha Rais Donald Trump.

    Wamarekani wanatarajiwa kupiga kura leo Jumanne, Novemba 3, katika uchaguzi utakaohusisha viti vyote 435 vya Baraza la Wawakilishi na viti 35 kati ya 100 vya Seneti.

    Chama cha Democratic kinaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kurejesha udhibiti wa Baraza la Wawakilishi, lakini kinakabiliwa na ushindani mkali zaidi katika kinyang’anyiro cha Seneti.

    Matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa Rais Trump kutekeleza ajenda yake ya kisiasa katika miaka miwili iliyosalia ya muhula wake wa urais.

    Iwapo chama cha Republican kitapoteza udhibiti wa chumba chochote cha bunge la Marekani yaani Congress, uwezo wa Trump kupitisha sheria unaweza kudhoofika, huku Democrats wakipata nafasi ya kuchunguza utendaji wa utawala wake.

    Kudhibiti Seneti pia kungewawezesha Democrats kuzuia au kuchelewesha uteuzi wa Trump wa majaji katika mahakama za shirikisho, wakiwemo majaji wa Mahakama ya Juu.

    Mvutano umeonekana pia katika jimbo la Michigan, ambako mgombea Abdul El-Sayed anawania kuwa Mwislamu wa kwanza kuchaguliwa katika Seneti ya Marekani.

    Wakati huohuo, huko California, Mahakama ya Juu imekataa ombi la Wizara ya Sheria ya Marekani la kuingilia mchakato unaohusiana na uchaguzi huo.

    Katika siku yake ya mwisho ya kampeni, Trump alitumia hotuba yake kuu kuzungumzia ukarabati wa bwawa la maji katika eneo la Lincoln Memorial Reflecting Pool mjini Washington, mojawapo ya miradi ya miundombinu ambayo ameipa kipaumbele tangu kurejea kwake Ikulu ya White House.

    Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Reuters kwa ushirikiano na Ipsos unaonyesha kuwa wagombea wa Democratic wanaongoza kwa tofauti ya asilimia nane dhidi ya Republican, ishara ya changamoto inayokikabili chama cha Trump katika uchaguzi huo.

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 03/11/2026.