Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yatoa pendekezo la kumaliza vita na Marekani huko Islamabad

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema amewasilisha “maoni na mitazamo ya Tehran” kuhusu kumaliza vita, katika mkutano na mkuu wa majeshi ya Pakistan mjini Islamabad.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Iran yatoa pendekezo la kumaliza vita na Marekani huko Islamabad

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema amewasilisha “maoni na mitazamo ya Tehran” kuhusu kumaliza vita, katika mkutano na mkuu wa majeshi ya Pakistan mjini Islamabad.

    Inaonekana kuwa Waziri huyo alifika katika mji huo mkuu wa Pakistan akiwa na pendekezo la kina ambalo analenga kulikabidhi kwa mpatanishi Pakistan, kwa mujibu na mwandishi wa BBC Persian, Jiyar Gol aliyeko Islamabad.

    Ikulu ya Marekani imethibitisha mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na mkwe wa Rais Donald Trump, Jared Kushner, pia wangekwenda Pakistan kwa mazungumzo na Iran siku ya Jumamosi, ingawa hakuna taarifa kama tayari wameondoka.

    Maafisa wa Iran wameiambia BBC kuwa mkutano na Marekani haupo katika ajenda ya Araghchi.

  2. Kinachoendelea kuhusu mazungumzo ya Iran na Marekani huko Pakistan

    Bado haijawa wazi ni kwa namna gani au kama mazungumzo kati ya Marekani na Iran yatafanyika leo.

    Marekani imesema ujumbe wake utaelekea Islamabad leo siku ya Jumamosi. Waziri wa mambo ya nje wa Iran tayari yuko huko, lakini Tehran inasema ziara hiyo ni sehemu ya safari ya kikanda ya nchi tatu.

    Tukukumbushe yaliyojitokeza hivi karibuni:

    Nchini Pakistan:

    • Tehran inasema hakuna mpango wa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran
    • Marekani ilisema Ijumaa kuwa wajumbe Steve Witkoff na Jared Kushner wataelekea Islamabad kwa mazungumzo, huku Makamu wa Rais JD Vance akiwa tayari kusaidia
    • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amekutana na mkuu wa majeshi ya Pakistan, Asim Munir, na amesema ataelekea Oman na Urusi baadaye kwa “mashauriano kuhusu maendeleo ya kikanda”

    Nchini Lebanon na Israel:

    • Jeshi la Israel (IDF) na Hezbollah wametuhumiana kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano, huku wakiendelea kushambuliana licha ya kuongezwa kwa muda wa wiki tatu wa kusitisha vita

    Nchini Iran:

    • Uwanja wa ndege wa Imam Khomeini International Airport umeanza tena baadhi ya safari za kimataifa, karibu miezi miwili baada ya safari za abiria kusimamishwa
    • Iran imesema imemnyonga mtu aliyeshiriki maandamano ya kitaifa mwezi Januari, baada ya kumtuhumu kushirikiana na ujasusi wa Israel.

    Unaweza kusoma pia:

  3. Wafahamu Kushner na Witkoff washirika wa Trump wanaoelekea Pakistan kwa mazungumzo

    Kama tulivyokuwa tukiripoti, Ikulu ya Marekani imesema kuwa Steve Witkoff na Jared Kushner wataelekea Pakistan leo kwa mazungumzo zaidi kuhusu mzozo unaohusisha Iran.

    Lakini wao ni nani, na kwa nini wanahusika? Jared Kushner ni mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, akiwa ameoa binti yake Ivanka Trump.

    Alikuwa mshauri mwandamizi wa rais wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, na ingawa kwa sasa hana cheo hicho rasmi, ameendelea kushiriki katika masuala muhimu ya kimataifa, ikiwemo mazungumzo kati ya Israel na Hamas mwaka jana.

    Kwa upande wake, Steve Witkoff ni mfanyabiashara wa sekta ya mali isiyohamishika na rafiki wa karibu wa Trump, ambaye aliteuliwa kuwa mjumbe maalum wa Mashariki ya Kati mwanzoni mwa muhula wa pili wa Trump.

    Amekuwa mmoja wa watu muhimu katika mazungumzo ya kimataifa ya utawala huo, akichukua nafasi kubwa katika juhudi za upatanishi kuhusu migogoro ya Israel na Hamas pamoja na ile ya Urusi na Ukraine.

  4. Mali yakumbwa na mashambulizi makubwa yaliyoratibiwa na makundi yenye silaha nchi nzima

    Milipuko na milio ya risasi imeripotiwa katika mji mkuu wa Mali, Bamako, huku makundi yenye silaha yakianzisha mashambulizi yanayoonekana kuratibiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

    Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, jeshi la nchi hiyo lilisema “mapigano yanaendelea,” likiongeza kuwa “vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa sasa vinapambana kuwazuia washambuliaji.”

    Kwa mujibu wa Reuters, mashuhuda wanasema kuwa milipuko na risasi zilisikika karibu na kambi ya kijeshi, kambi kubwa iliyopo nje kidogo ya mji mkuu. Wanajeshi wamepelekwa kufunga barabara katika eneo hilo.

    Pia kuna taarifa za mashambulizi katika mji wa Gao mashariki, Kidal kaskazini na Sevare katikati mwa Mali, katika kile ambacho mchambuzi mmoja amekielezea kuwa ni shambulio kubwa zaidi la wanamgambo wa jihadi kwa miaka ya hivi karibuni.

    Mkazi mmoja aliyekuwa akisafiri kurejea Bamako kutoka Ethiopia aliiambia BBC kuwa safari zote za ndege kuelekea mji huo zilifutwa mapema Jumamosi. Bado haijabainika wazi kama mashambulizi hayo yameathiri uwanja wa ndege.

    Ubalozi wa Marekani nchini Mali umewashauri raia wake kubaki walipo na kuepuka safari, ukitaja milipuko na milio ya risasi karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Modibo Keita mjini Bamako na maeneo ya kati ya nchi.

    Ulf Laessing, mkuu wa Mpango wa Sahel katika Konrad Adenauer Foundation nchini Mali, ameiambia BBC kuwa tukio hilo linaonekana kuwa “shambulio kubwa zaidi lililoratibiwa na wanamgambo wa jihadi nchini Mali kwa miaka kadhaa.”

    Jeshi la Mali limesema linapambana na “makundi ya kigaidi” ambayo hayajatambuliwa, ingawa maelezo zaidi bado hayajawekwa wazi. Video zinazosambaa mitandaoni zinaashiria uwepo wa kundi la jihadi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) pamoja na waasi wa Tuareg wa Azawad Liberation Front (FLA).

  5. Araghchi hayupo Pakistan kuzungumzia nyuklia - Iran

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, hana “jukumu lolote linalohusiana na mazungumzo ya nyuklia” katika ziara yake nchini Pakistan, kwa mujibu wa mkuu wa kamati ya usalama wa taifa ya Iran.

    Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tehran jana usiku, Ebrahim Azizi alisema waziri huyo yuko Islamabad “kwa ajili ya mazungumzo ya mahusiano ya pande mbili pekee.”

    Azizi ambaye pia ni kamanda wa zamani wa Jeshi la walinzi wa mapinduzi ya kiislamu (IRGC) alisema masuala ya shughuli za nyuklia “yanabaki kuwa moja ya mipaka mikuu ambayo Iran haiwezi kuvuka.”

    Kwa upande mwingine, Marekani imeitaka Iran kusitisha mpango wake wa nyuklia, ikisisitiza kuwa hilo linapaswa kuwa sehemu ya makubaliano yoyote ya mwisho ya amani.

  6. Marekani yazuia meli nyingine ya Iran

    Jeshi la Marekani limesema limefanikiwa kuiizuia meli nyingine iliyokuwa na bendera ya Iran ikiwa njiani kuelekea bandari ya Iran, kama sehemu ya hatua za kuimarisha mzingiro wa baharini dhidi ya nchi hiyo.

    Kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la nchi hiyo, operesheni hiyo ilifanyika Aprili 24, ikiongozwa na manowari ya kivita ya USS Rafael Peralta, ambayo ilitekeleza hatua za kudhibiti usafiri wa majini unaohusishwa na Iran.

    Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi pana za Marekani za kuzuia biashara ya mafuta ya Iran na kukata vyanzo vya mapato ya nchi hiyo, hasa kufuatia mvutano unaoendelea kati ya pande hizo mbili.

    Mvutano huo umeongezeka katika wiki za karibuni baada ya Marekani kufanya mashambulizi ya kijeshi na Iran kujibu kwa kuzuia baadhi ya njia muhimu za usafirishaji wa mafuta katika eneo la mlango bahari wa Hormuz, jambo lililoathiri usafirishaji wa nishati duniani na kuongeza bei ya mafuta.

  7. Marekani yaongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran

    Marekani imetangaza kuongeza shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran, ikisema inachukua hatua “madhubuti” kuvuruga biashara haramu ya mafuta ya nchi hiyo.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema hatua hizo zinajumuisha vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta nchini China pamoja na maeneo mengine 40.

    Kwa mujibu wa Marekani, taasisi hizo ni “mishipa muhimu ya kifedha” kwa utawala wa Iran, zikichangia kufadhili shughuli zinazoelezwa kuwa za “kuleta machafuko” katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Taarifa hiyo imeongeza kuwa vikwazo hivyo vinalenga kukata mtiririko wa fedha unaosaidia biashara hiyo ya nishati, huku Marekani ikiahidi kuimarisha zaidi kampeni yake ya shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran na mtandao wa kimataifa unaoiunga mkono.

  8. Iran yafika Pakistan kwa mazungumzo, Marekani yasubiri mapendekezo ya Tehran

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amewasili Islamabad, Pakistan kwa mazungumzo yanayolenga kufufua juhudi za amani kati ya Iran na Marekani baada ya wiki nane za mvutano mkubwa wa kijeshi.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran inatarajiwa kuwasilisha mapendekezo yanayoweza kukidhi matakwa ya Washington, ingawa hakufafanua maelezo ya mapendekezo hayo.

    Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran amesema hakuna mipango ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili, akibainisha kuwa ujumbe wa Iran utawasilishwa kupitia Pakistan.

    Wakati huo huo, wajumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, wanatarajiwa kuwasili Pakistan kwa mazungumzo hayo, huku Ikulu ya White House ikisema Washington iko tayari kutoa nafasi kwa diplomasia.

    Mvutano kati ya Iran na Marekani umeendelea kuathiri masoko ya dunia, hasa baada ya Marekani kufanya mashambulizi ya anga na Iran kuzuia njia muhimu ya usafirishaji mafuta ya Strait of Hormuz, hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

    Pande zote mbili zinaonekana kutafuta njia ya kusitisha mgogoro huo, ingawa bado kuna kauli zinazokinzana kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano.

  9. Habari na karibu katika habari zetu za moja kwa moja