Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asema ataharibu daraja au kituo cha umeme kwa kila shambulio la Iran dhidi ya meli

Trump asema kuwa mashambulizi hayo yanaweza kulenga miundombinu iliyo karibu au ndani ya mji mkuu wa Iran, Tehran.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Serikali ya Kenya yakiri kwa mara ya kwanza kuwaweka watu karantini kutokana na tishio la Ebola

    Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale, amekiri kwa mara ya kwanza kuwa kuna watu wengi waliowekwa kwa karantini kwa siku 21.

    ''Tumeweka watu wengi kwa karantini ikiwemo wafanyikazi wa Rais '', asema Waziri wa Afya Aden Duale.

    Alipoulizwa na wanahabari kuhusu mustakabali wa vituo vya karantini kujengwa ili kuhifadhi wamarekani ameeleza kuwa serikali imesitisha ujenzi wa kituo cha karantini ya Ebola kilichokuwa kinajengwa Laikipia, kufuatia amri ya mahakama iliyosimamisha mradi huo.

    ''Tumeheshimu Mahakama na tumesitisha ujenzi wa kituo cha karantini cha Laikipia,'' asema Duale.

    Duale alitoa kauli hiyo alipokuwa akipokea tani tano za vifaa vya matibabu kutoka India, vikiwemo vifaa vya kujikinga (PPE), vifaa vya uchunguzi, vipima joto vya miale ya infraredi na vifaa vingine vya dharura kwa ajili ya kuimarisha maandalizi ya Kenya dhidi ya Ebola.

    Waziri huyo alisema kuwa hadi sasa hakuna kisa cha Ebola kilichothibitishwa nchini Kenya, lakini serikali inaendelea kuwa katika hali ya tahadhari.

    Kauli yake inajiri wakati kukiwa na mjadala kuhusu kituo cha karantini kinachofadhiliwa na Marekani mjini Nanyuki, ambacho baadhi ya taarifa zinadai kinaendelea kufanya kazi licha ya amri ya mahakama iliyositisha ujenzi wake mwezi Mei.

    Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilithibitisha kuwa wafanyakazi saba wa misaada wa Marekani waliokuwa wakishiriki kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanajitenga katika kituo kilichopo Kenya. Hata hivyo, haijawekwa wazi iwapo wanahifadhiwa katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Laikipia kilichopo Nanyuki.

    Unaweza kusoma:

  2. Lissu na Msigwa wakutana Mahakama Kuu huku kesi ya kikatiba ikiahirishwa

    Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameendelea kujitetea katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa dhidi ya Mamlaka ya Magereza, huku Mahakama ikisikiliza ushahidi wa shahidi wa nne na wa mwisho wa upande wa wajibu maombi.

    Shahidi huyo ni Mkuu wa Gereza la Ukonga, ambaye amefika mahakamani kutoa ushahidi kuhusu madai yaliyowasilishwa katika kesi hiyo.

    Kesi hiyo ilifunguliwa na mawakili Nashon Nkungu, Paul Kisabo na Kulwa Maduhu, wakipinga vikwazo wanavyodai wamekuwa wakikumbana navyo wanapomtembelea Lissu gerezani na kufanya mashauriano ya kisheria.

    Usikilizwaji wa kesi hiyo umeendelea kwa siku nne mfululizo. Katika siku zilizopita, Lissu alimaliza kumuhoji shahidi wa tatu kabla ya Mahakama kuendelea na ushahidi wa Mkuu wa Gereza la Ukonga.

    Aidha Tundu Lissu, amekutana na aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza wawili hao kuonekana pamoja hadharani tangu Msigwa arejee Chadema.

    Wawili hao walionekana wakikumbatiana muda mfupi baada ya mahakama kuahirisha kwa muda usikilizwaji wa shauri lililowasilishwa na mawakili wawili wanaojitambulisha kuwa washauri wa kisheria wa Lissu.

    Msigwa, ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, alifika mahakamani kufuatilia mwenendo wa shauri hilo.

    Katika kesi hiyo, mawakili hao wanapinga kile wanachodai kuwa ni vikwazo vinavyowazuia kufanya mazungumzo ya siri ya kisheria na mteja wao, Tundu Lissu, ambaye anashikiliwa katika Gereza la Ukonga.

    Msigwa alihama Chadema na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, CCM, mwezi Juni mwaka 2024 kabla ya kurejea tena Chadema tarehe 23 Mei 2026.

    Kuonekana kwake katika Mahakama Kuu kunatajwa kuwa tukio la kwanza la hadhara akiwa pamoja na Lissu tangu alipojiunga tena na chama hicho cha upinzani.

    Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai, amemfananisha mwanasiasa Peter Msigwa na kiungo wa Simba SC, Clatous Chama, kufuatia uamuzi wa Msigwa kurejea Chadema baada ya kuondoka CCM.

    Akizungumza mbele ya wanachama na wafuasi wa chama hicho, Boni Yai alisema kurejea kwa Msigwa kunafanana na jinsi Clatous Chama alivyorejea Simba SC baada ya kipindi cha kuichezea klabu nyingine.

    ''Sasa subirini magoli 50'', anasema Boniface Jacob.

    Shauri hilo, linalohusu haki ya mawakili kupata fursa ya kufanya mawasiliano ya siri na mteja wao (Lissu), limeahirishwa kwa muda, huku mahakama ikitarajiwa kutoa mwelekeo wa hatua zinazofuata.

    Haya yanajiri baada ya wito kutoka Jumuiya ya Madola ikitaka Lissu aachiliwe huru ndani ya siku 28.

    Soma Pia:

  3. Trump asema ataharibu daraja au kituo cha umeme kwa kila shambulio la Iran dhidi ya meli

    Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa Marekani itajibu mashambulizi yoyote ya Iran dhidi ya meli katika Mlango wa Hormuz kwa kulenga miundombinu ya nchi hiyo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema:

    "Kuanzia sasa, kila Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakaposhambulia meli katika Mlango wa Hormuz, iwe kwa kombora, roketi, droni au silaha nyingine yoyote, Marekani itashambulia na kuharibu daraja au kituo cha kuzalisha umeme."

    Aliongeza kuwa mashambulizi hayo yanaweza kulenga miundombinu iliyo karibu au ndani ya mji mkuu wa Iran, Tehran.

  4. Rais wa La Liga amtaka Infantino ajiuzulu FIFA

    Rais wa La Liga, Javier Tebas, amemtaka Rais wa FIFA Gianni Infantino kujiuzulu, akidai uongozi wake "unaiua soka."

    Akizungumza na gazeti la Italia La Gazzetta dello Sport, Tebas alisema anaamini muda wa Infantino kuongoza shirikisho hilo umefika mwisho, ingawa alikiri kuwa anaungwa mkono na vyama vingi vya soka duniani.

    Tebas alidai mfumo wa uchaguzi wa rais wa FIFA umeharibika kiasi kwamba hakuna anayethubutu kumpinga Infantino kwa kuwa wanaamini hawawezi kushinda.

    Pia alimkosoa Infantino kwa madai ya kuingiliwa kwa uamuzi wa kusimamishwa kwa mchezaji wa Marekani, Balogun, pamoja na mapumziko ya kunywa maji wakati wa mechi, muda mrefu wa mapumziko ya fainali na pendekezo la kuongeza timu zinazoshiriki Kombe la Dunia hadi 64.

    Aidha, Tebas alisema viongozi wengi wa soka hawaridhishwi na uongozi wa Infantino lakini wamechagua kunyamaza.

    Kwa upande wake, UEFA ilikosoa uamuzi wa kumruhusu Balogun kucheza, ikiuita "usio na mfano, usioeleweka na usio na maelezo."

    Infantino anatarajiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa nne katika Kongamano la FIFA litakalofanyika Machi mwaka ujao, lakini Tebas alikiri kuwa suala la Balogun lingeweza kumgharimu nafasi hiyo.

    BBC Sport bado inaendelea kuwasiliana na FIFA ili kupata maoni yake kuhusu madai hayo dhidi ya rais wake.

  5. Video za CCTV zaonyesha Albert Ojwang akiwasili hai kituoni, mahakama yaelezwa

    Mahakama Kuu ya Kibera ya Kenya imeahirisha hadi Desemba 14 usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang.

    Siku hiyo, mkuu wa uchunguzi wa kisayansi na eneo la tukio wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi, IPOA, Joshua Mutua, anatarajiwa kurejea mahakamani kuendelea na maswali ya upande wa utetezi.

    Jaji Diana Kavedza alitoa mwelekeo huo Jumatano baada ya upande wa mashtaka kukamilisha ushahidi mkuu wa Mutua, ambapo aliwasilisha mahakamani rekodi za kamera za CCTV zilizopatikana kutoka Kituo cha Polisi cha Central na Hospitali ya Mbagathi.

    Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Ojwang alikamatwa nyumbani kwake katika Kaunti ya Homa Bay mnamo Juni 7, 2025, kufuatia tuhuma zinazohusiana na chapisho aliloweka kwenye mitandao ya kijamii. Alifikishwa kwanza katika Kituo cha Polisi cha Mawego kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi usiku huohuo.

    Mahakama Kuu ya Kibera imeonyeshwa video za kamera za usalama (CCTV) ambazo, kwa mujibu wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA), zinamuonyesha Albert Ojwang akiwasili akiwa hai katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi usiku wa Juni 7, 2025.

    Mpelelezi wa uchunguzi wa kisayansi wa IPOA, Joshua Mutua, aliiambia mahakama kuwa video zilizopatikana zinaonyesha Ojwang akiwasili kituoni saa 3:23 usiku.

    Mutua alieleza kuwa uchunguzi wa kisayansi wa mfumo wa CCTV ulibaini kuwa waya wa umeme wa mfumo huo ulikuwa umetolewa, huku diski kuu zilizohifadhi video zikifutwa taarifa zake asubuhi ya Juni 8, 2025.

    Hata hivyo, alisema wachunguzi walifanikiwa kurejesha mamia ya gigabaiti za video ambazo zilithibitishwa kuwa halisi kwa kutumia mbinu za uchunguzi wa kisayansi.

    Mahakama ilielezwa kuwa picha za kamera za usalama pamoja na ushahidi wa mashahidi zinaonyesha Ojwang aliwasili kituoni akiwa hai na bila majeraha makubwa yanayoonekana. Hata hivyo, ndani ya saa chache, alipata majeraha yaliyosababisha kifo chake akiwa rumande.

    Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilihitimisha kuwa alifariki kutokana na majeraha yanayoendana na kushambuliwa, jambo lililopingana na maelezo ya awali ya polisi yaliyodai kuwa alijijeruhi mwenyewe akiwa ndani ya seli.

    Katika ushahidi uliotolewa awali, shahidi aliyelindwa aliimtaja Konstebo Peter Kimani kuwa askari aliyekuwa akisimamia seli usiku ambao Ojwang aliwekwa rumande.

    Video zilizoonyeshwa mahakamani pia zilimuonyesha Kimani akiwa katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho, ikiwemo nje ya vizimba vya mahabusu na katika lango kuu la kituo.

    Upande wa mashtaka unatumia ushahidi huo wa CCTV kujaribu kubaini mlolongo wa matukio kabla na baada ya Ojwang kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.

    Aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, Samson Talaam, Konstebo Peter Kimani, Konstebo James Mukhwana pamoja na raia watatu wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Albert Omondi Ojwang.

    Washtakiwa wote wamekanusha mashtaka dhidi yao.

    Soma Pia:

  6. Dubai yatoa ofa maalumu kwa watakaozuru mji huo kufufua sekta ya utalii

    Dubai imetangaza mpango wa kutoa ofa na punguzo maalumu lenye thamani ya zaidi ya dola 800 kwa wakazi watakaowaalika marafiki na ndugu zao kutembelea mji huo kati ya Julai 20 na Oktoba 31.

    Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Dubai, mpango huo unalenga kufufua sekta ya utalii iliyodorora kutokana na athari za vita vya hivi karibuni katika eneo hilo.

    Walionufaika watapata ofa mbalimbali, ikiwemo malazi ya hoteli, huduma za migahawa na tiketi za vivutio vya utalii.

    Dubai hupokea takribani watalii milioni 19.5 kila mwaka, lakini msimu wa kiangazi huwa kipindi cha watalii wachache.

    Serikali ya Dubai pia imeidhinisha vifurushi vya msaada wa kiuchumi kwa biashara zilizoathiriwa na vita na usumbufu wa biashara katika Mlango wa Hormuz.

    Falme za Kiarabu ziliathirika pakubwa wakati wa vita vya siku 40 kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Katika kipindi hicho, makombora mengi ya Iran yalilenga maeneo ya Falme za Kiarabu, yakiwemo hoteli katika eneo la Palm Jumeirah na jengo maarufu la Burj Al Arab. Kwa mujibu wa Reuters, mashambulizi hayo yaliwafanya watalii wengi kuondoka nchini wakati wa msimu wa kilele wa utalii wa majira ya baridi.

    Tangu kusitishwa kwa mapigano kwa makubaliano dhaifu yaliyofikiwa Aprili 8, idadi ndogo ya watalii imeanza kurejea Dubai.

    Mwezi Mei, serikali ya Dubai iliidhinisha kifurushi cha msaada wa kiuchumi cha dola milioni 400 kusaidia biashara zilizoathiriwa na vita na vikwazo vya usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz.

    Aidha, mwishoni mwa Machi, mamlaka za Dubai zilitangaza kifurushi cha kwanza cha msaada chenye thamani ya dola milioni 270 kwa ajili ya kusaidia biashara na familia zilizoathiriwa.

    Soma Zaidi:

  7. Pakistan yaonya Wahouthi, yatishia kujilinda ikiwa meli zake zitashambuliwa

    Pakistan imelaani vitisho vya kundi la Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia na usafirishaji wa meli katika Bahari ya Shamu, ikisema inahofia juhudi za kuisukuma Saudi Arabia kuingia kwenye mzozo wa Mashariki ya Kati.

    Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imesisitiza kuwa itaendelea kuunga mkono usalama, uhuru, mipaka na ustawi wa Saudi Arabia.

    Msimamo huo unakuja baada ya Pakistan na Saudi Arabia kusaini mkataba wa ulinzi wa pamoja mwaka 2025, unaotambua kuwa shambulio dhidi ya upande mmoja ni shambulio dhidi ya wote. Pakistan pia imepeleka maelfu ya wanajeshi na ndege za kivita nchini Saudi Arabia.

    Maafisa wa Pakistan wamewahi kueleza kuwa shambulio lolote dhidi ya Saudi Arabia ni "mstari mwekundu" kwa Islamabad, huku wakionya kuwa kuongezeka kwa mashambulizi ya Wahouthi kunaweza kuilazimisha Pakistan kujiingiza kijeshi kwenye mzozo huo.

    Wasiwasi huo umeongezeka kufuatia mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran dhidi ya Saudi Arabia, pamoja na vitisho vyao vya kuvuruga usafirishaji wa meli katika Bahari ya Shamu.

    Aidha, Pakistan imezitaka pande zote kuheshimu makubaliano ya maelewano yaliyolenga kupunguza mvutano kati ya Iran na Marekani na kurejesha usalama wa njia za biashara za baharini.

    Soma Zaidi:

  8. Kijana afungwa jela kwa kujaribu kuiba gari la polisi Ghana

    Mahakama nchini Ghana imemhukumu kifungo cha mwezi mmoja jela kijana mwenye umri wa miaka 26 baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kuiba gari la polisi.

    Ebenezer Frimpong alikamatwa baada ya kuingia kwenye gari la polisi lenye ulinzi maalumu na kuondoka nalo, wakati dereva wake alipokuwa ameshuka kununua dawa katika duka la dawa mwezi Aprili mwaka huu.

    Kwa mujibu wa dereva wa gari hilo, Joshua Denkyi, tukio hilo lilitokea alipokuwa ameegesha gari njiani ili kununua dawa.

    Frimpong alikamatwa baada ya polisi kumfukuza alipokuwa akijaribu kutoroka na gari hilo.

    Kabla ya kutoa hukumu, mahakama iliamuru afanyiwe uchunguzi wa afya ya akili ili kuthibitisha kuwa alikuwa na utimamu wa akili.

    Baada ya kukiri kosa, jaji alimhukumu kifungo cha mwezi mmoja jela, akieleza kuwa adhabu hiyo imepunguzwa kwa sababu mshtakiwa alikiri kosa mapema na hakupoteza muda wa mahakama.

  9. Trump: Niko tayari kuzungumza na Hezbollah ikiwa Lebanon itataka

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na Hezbollah iwapo Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ataomba hatua hiyo ichukuliwe.

    Trump alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake wa kwanza na Aoun katika Ikulu ya White House.

    Trump amesema Lebanon imekuwa "ikitendewa vibaya sana" na kuahidi kuwa nchi hiyo "itapata heshima inayostahili", kabla ya kueleza kuwa bado kuna "tatizo la Hezbollah."

    Alipoulizwa iwapo yuko tayari kuwasiliana na Hezbollah, Trump alisema:

    "Iwapo rais wa Lebanon ataniomba nizungumze na Hezbollah, nitafanya hivyo."

    Hata hivyo, hakufafanua mazungumzo hayo yangekuwa ya aina gani wala kama kuna mipango yoyote ya kuyafanya siku zijazo.

    Katika mazungumzo hayo, Aoun aliitaka Marekani kuendelea kuunga mkono jeshi la Lebanon ili kukamilisha kuondoka kwa wanajeshi wa Israel kusini mwa nchi hiyo na kuimarisha usalama.

    Pia alionya kuwa kusitishwa kwa msaada wa Marekani kunaweza kurejesha hali ya machafuko iliyowahi kushuhudiwa kusini mwa Lebanon katika miaka ya 1970.

    Mkutano huo umefanyika wakati jeshi la Lebanon likianza kupelekwa katika baadhi ya maeneo ambayo wanajeshi wa Israel wameondoka, kufuatia makubaliano yaliyopatanishwa na Marekani kati ya Lebanon na Israel.

    Soma Zaidi:

  10. Rais wa Ufaransa aunga mkono marufuku ya mitandao ya kijamii kwa watoto chini ya miaka 15

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amepongeza uamuzi wa Bunge la nchi hiyo kupitisha sheria inayowazuia watoto wenye umri chini ya miaka 15 kutumia mitandao ya kijamii.

    Macron amesema hatua hiyo inalenga kuwalinda watoto dhidi ya athari zinazohusishwa na matumizi ya mitandao ya kijamii, ikiwemo matatizo ya afya ya akili na matatizo ya kula vizuri.

    Kwa mujibu wa sheria hiyo, kuanzia Septemba, mtu yeyote atakayefungua akaunti mpya kwenye mitandao ya kijamii atalazimika kuthibitisha umri wake, huku watoto walio chini ya miaka 15 wakikatazwa kufungua akaunti.

    Sheria hiyo pia inazitaka kampuni za mitandao ya kijamii kuweka mifumo ya kuthibitisha umri wa watumiaji, huku shule za sekondari zikitakiwa kupiga marufuku matumizi ya simu za mkononi shuleni.

    Soma zaidi:

  11. Marekani na Saudi Arabia zakubaliana kuhusu ushirikiano wa nishati ya nyuklia

    Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa utawala wa Rais Donald Trump umefikia makubaliano na Saudi Arabia kuhusu ushirikiano wa nishati ya nyuklia, huku maelezo kamili yakitarajiwa kutangazwa hivi karibuni.

    Kwa mujibu wa ripoti hizo, makubaliano hayo yanaweza kuiruhusu Saudi Arabia kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya kuzalisha nishati katika mitambo ya nyuklia.

    Hata hivyo, suala la kurutubisha urani limekuwa likizua mjadala kwa miaka kadhaa kutokana na hofu kwamba teknolojia hiyo inaweza pia kutumika kutengeneza silaha za nyuklia.

    Baadhi ya wabunge wa Marekani wameeleza wasiwasi wao wakisema hatua hiyo inaweza kuipa Saudi Arabia uwezo wa kuendeleza mpango wa silaha za nyuklia, ingawa Riyadh imekuwa ikisisitiza kuwa inalenga matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

    Iwapo makubaliano hayo yatatekelezwa, yanaweza kufungua ukurasa mpya katika uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia, ambao umeonekana kuyumba katika kipindi cha hivi karibuni, hasa baada ya mvutano wa kikanda uliotokana na vita vya Iran. Aidha, yanaweza kufungua fursa mpya za kibiashara kwa kampuni za Marekani katika sekta ya nishati ya nyuklia.

    Soma Pia

  12. Niger, Mali na Burkina Faso zataka kuandaa AFCON 2032 kwa pamoja

    Niger, Mali na Burkina Faso zimewasilisha ombi la pamoja la kuandaa michuano ya Mataifa ya Afrika, AFCON 2032.

    Pendekezo hilo liliwasilishwa kwa rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Patrice Motsepe, wakati wa mkutano uliofanyika mjini New York, Marekani.

    Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa vyama vya soka vya mataifa hayo matatu pamoja na Kanali Djibrilla Hima Hamidou wa Niger, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la FIFA.

    Shirikisho la Soka la Mali, FEMAFOOT, limesema kuwa kuandaa mashindano hayo kutasaidia kuimarisha umoja kati ya mataifa ya ukanda wa Sahel na kuchochea maendeleo ya soka barani Afrika.

    Kwa mujibu wa shirikisho hilo, Niger, Mali na Burkina Faso zitashirikiana kuandaa mpango wa pamoja wa maandalizi utakaolenga kuboresha miundombinu ya soka na kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa mafanikio.

    CAF bado haijatangaza nchi itakayopewa haki ya kuandaa AFCON 2032.

    Niger, Mali na Burkina Faso ni wanachama wa Muungano wa Nchi za Sahel, AES, ulioundwa baada ya mataifa hayo kujiondoa katika Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea katika nchi hizo. Muungano huo unalenga kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usalama, biashara na uchumi.

    Soma Zaidi:

  13. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani: Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini Iran haina nia ya dhati

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa iwapo Iran itadhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, hali hiyo itasababisha "mwelekeo hatari" kwa usalama na biashara ya kimataifa.

    Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Rubio alisema Marekani bado iko tayari kufanya mazungumzo ya kumaliza mgogoro na Iran, lakini alidai kuwa Tehran haijaonesha nia ya dhati ya kushiriki mazungumzo hayo.

    Kauli zake zinakuja wakati kuongezeka kwa mzozo huo kumeathiri njia mbili muhimu za usafirishaji wa nishati duniani.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, afisa mmoja mwandamizi wa Iran alisema Jumatatu kwamba Tehran imepokea pendekezo kutoka kwa wapatanishi la kusitisha mapigano kwa muda wa siku 10.

    Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran alisafiri kwenda Pakistan kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Shehbaz Sharif, pamoja na Mkuu wa Jeshi, Jenerali Asim Munir. Viongozi hao wawili wamekuwa miongoni mwa wapatanishi wakuu katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani.

    Unaweza kusoma;

  14. CDC yaomba Marekani iondoe vizuizi vya safari dhidi ya Uganda kutokana na Ebola

    Shirika kuu la afya ya umma barani Afrika limesema Jumanne kuwa haliungi mkono marufuku ya safari kama hatua ya kukabiliana na mlipuko unaoongezeka wa Ebola barani humo. Citizen imeripoti

    Shirika hilo limeitaka Marekani kuondoa vizuizi vya safari ilivyoweka kwa Uganda.

    Wito huo umetolewa siku chache baada ya Washington kuongeza masharti ya usafiri yanayohusiana na mlipuko wa sasa wa Ebola, ambao ulianzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa wasafiri kutoka DRC, Uganda na Sudani Kusini.

    Akizungumza katika mkutano wa afya wa Umoja wa Afrika mjini Accra, Ghana, Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa,CDC, Jean Kaseya, alisema shirika hilo "halishauri kuwekwa kwa marufuku ya safari."

    Wataalamu wa afya ya umma wamekuwa wakisema katika milipuko ya Ebola iliyopita kwamba marufuku ya safari huathiri usafirishaji wa vifaa vya matibabu na wafanyakazi wa afya, kuvuruga biashara, na badala yake inaweza kuzuia juhudi za ufuatiliaji wa magonjwa na kutengwa kwa wagonjwa.

    Kaseya alisema amemwandikia Waziri wa Afya wa Marekani, Robert F. Kennedy, akiomba kuondolewa kwa vizuizi vya safari dhidi ya Uganda pekee. Alisema nchi hiyo imekaa kwa wiki tatu bila kuripoti kesi mpya ya Ebola na mgonjwa wake wa mwisho aliachiliwa tarehe 16 Julai.

    "Hakuna sababu kwa Marekani kuendelea na kizuizi hiki cha safari," alisema Kaseya, akiongeza kuwa nchi hazipaswi "kuadhibiwa kwa kuwa wazi kuhusu milipuko ya magonjwa."

    Hata hivyo, licha ya kupinga vizuizi vya safari, Kaseya alionya kuwa mlipuko huo unaendelea kuongezeka kwa kasi.

    "Ikiwa hatutazuia mlipuko huu leo, utakuwa mlipuko mbaya zaidi ambao dunia itakuwa ikiurekodi," alisema.

    Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kumekuwa na visa 2,344 vilivyothibitishwa vya Ebola nchini DRC, vikiwemo vifo 930, tangu mlipuko huo ulipotangazwa katikati ya Mei.

    Uganda imeripoti visa 20 na vifo viwili, wengi wao wakiwa raia wa Congo waliovuka mpaka.

    Africa CDC inakadiria kuwa inahitaji dola bilioni 1.4 za Marekani ili kudhibiti mlipuko huo, kiasi ambacho ni karibu mara tatu ya makadirio ya awali ya dola milioni 518 yaliyotolewa mwezi uliopita.

    Unaweza kusoma;

  15. Utafiti: Nyani wakubwa hubusiana na kukumbatiana ili kudumisha amani

    Wanasayansi wamegundua kuwa kugusana, kukumbatiana na hata kubusiana kabla ya matukio yenye msongo wa mawazo huenda ni tabia ya kale inayosaidia kujenga uaminifu, kulingana na utafiti wa nyani wakubwa walio karibu zaidi na binadamu.

    Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Durham walichunguza tabia za sokwe na bonobo, na kubaini kuwa hutumia mgusano wa mwili kutulizana na kupeana uhakikisho kabla ya migogoro, hasa inayohusiana na chakula.

    Moja ya matokeo yaliyowashangaza watafiti ni kwamba sokwe, licha ya kujulikana kwa tabia yao ya ukali, walionekana wakifanya mawasiliano ya karibu, ikiwemo kuweka vidole vyao midomoni mwa wenzao.

    "Kabla ya matukio yenye msongo, hukusanyika pamoja, hutulizana, hugusana na kukumbatiana," alisema Profesa Zanna Clay

    Profesa Zanna Clay alielezea tabia hiyo kuwa ni "wito wa kuunganisha nguvu" kabla ya tukio lenye msongo wa mawazo, akilinganisha na jinsi wachezaji wa mpira wa miguu hukusanyika pamoja na kutiana moyo kabla ya mechi muhimu.

    "Ni zaidi ya 'sisi' kuliko 'mimi'," alisema.

    Wataalamu hao walifanya utafiti huo kwa sokwe na nyani aina ya bonobo waliokuwa wakiishi katika vituo viwili vya kuhifadhi nyani wakubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.

    Nyani hao walifuatiliwa katika dakika tano kabla ya karanga kuletwa, wakati walipokuwa wakijua kuwa chakula kilikuwa kinakaribia kutolewa.

    Watafiti walirekodi matukio mbalimbali ya mgusano wa kuwafariji, yakiwemo kugusana, kukumbatiana na kubusiana.

    Timu ya watafiti ilibaini kuwa nyani waliokuwa wakigusana na kukumbatiana walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata chakula na kukila kwa amani pamoja na wenzao.

    Aidha, makundi yaliyokuwa na uvumilivu mkubwa yalionesha kiwango cha juu zaidi cha mgusano wa kupeana utulivu. Watafiti walielezea hali hiyo kama " kufarijiana", ambapo nyani kadhaa walikuwa wakikumbatiana mmoja baada ya mwingine kabla ya tukio lenye kuwasababishia hali ya msongo.

  16. Mhudumu wa misaada wa Uingereza yuko chini ya uangalizi kwa hofu ya Ebola katika hospitali ya London

    Mhudumu wa misaada ya kibinadamu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehamishiwa nchini Uingereza kwa uangalizi wa kitabibu baada ya uwezekano wa kuathiriwa na virusi vya Ebola akiwa kazini.

    Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza (UKHSA) limesema mtu huyo, ambaye ni mkazi wa Uingereza na jina lake halijawekwa wazi, hana dalili zozote za Ebola kwa sasa, na hatua ya kumhamisha imechukuliwa kama tahadhari.

    Kwa mujibu wa UKHSA, mhudumu huyo anaendelea kuwa katika hali nzuri kiafya lakini anafanyiwa vipimo na kufuatiliwa katika hospitali moja jijini London.

    Jina la hospitali hiyo halijatangazwa, ingawa Hospitali ya Royal Free kaskazini mwa London ina kitengo maalumu cha kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa hatari ya kuambukiza.

    Kipindi cha kujitokeza kwa dalili za Ebola ni kati ya siku mbili hadi 21, hivyo mhudumu huyo atalazimika kujitenga kwa muda wote wa kipindi hicho.

    Mhusika huyo alikuwa akifanya kazi na shirika la misaada lililokuwa likisaidia kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini DRC.

    Ebola ni ugonjwa hatari sana unaosababishwa na virusi. Tofauti na mafua au Covid-19, virusi vya Ebola haviambukizwi kwa njia ya hewa, bali huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.

    Dalili zake huanza ghafla na zinafanana na za mafua au malaria, zikiwemo homa, maumivu ya kichwa na uchovu.

    Ugonjwa unapoendelea, mgonjwa anaweza kutapika, kuharisha na kushindwa kwa baadhi ya viungo vya mwili kufanya kazi. Baadhi ya wagonjwa pia hutokwa na damu ndani na nje ya mwili.

    Richard Pebody, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Mlipuko na yanayoibuka katika Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza (UKHSA), amesema:

    "Hatari kwa umma kwa ujumla bado ni ndogo. Mtu huyu amehamishwa kama hatua ya tahadhari ya ziada, na tunafurahi kuwa anaendelea kuwa katika hali nzuri."

    UKHSA pia imesema kwa sasa hakuna kesi yoyote iliyothibitishwa ya ugonjwa wa Ebola nchini Uingereza.

    Unaweza kusoma;

  17. Rais wa Ukraine amtimua Mkuu wa Jeshi, Oleksandr Syrskyi

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemwondoa Mkuu wa Majeshi ya Ukraine, Oleksandr Syrskyi, kutoka wadhifa wake.

    Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya kuondolewa kwa Waziri wa Ulinzi aliyekuwa maarufu, Mykhailo Fedorov, hatua iliyosababisha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo.

    Awali kulikuwa na uvumi kwamba kuondolewa kwa Fedorov kulihusiana na mgogoro kati yake na Syrskyi, na baadaye taarifa hizo zikathibitishwa.

    Fedorov, mwenye umri wa miaka 35, amekuwa akisifiwa kwa kuleta mageuzi makubwa katika Wizara ya Ulinzi, kuimarisha uwezo wa jeshi la Ukraine na kuongoza juhudi za kupambana na rushwa.

    Kwa upande mwingine, Syrskyi, mwenye umri wa miaka 60, anaonekana na wengi nchini Ukraine kama kamanda mwenye mtazamo wa kijeshi wa enzi za Umoja wa Kisovieti, ambaye hakuwa tayari kutekeleza mabadiliko makubwa ndani ya jeshi.

    Nafasi yake imechukuliwa na Jenerali Mykhailo Drapatyi, mwenye umri wa miaka 43, ambaye anajulikana kwa uzoefu wake mkubwa vitani na umaarufu miongoni mwa wanajeshi.

    "Nitafanya kazi kwa uwajibikaji, kwa umakini wa hali ya juu, na kwa heshima kwa wale wote wanaolinda nchi yetu leo," Drapatyi aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

    Pia alimshukuru Syrskyi "kwa kazi yake ya muda mrefu ya kuimarisha jeshi la Ukraine," akiongeza kuwa, "Nilikulia ndani ya jeshi hilo."

    Katika ujumbe wa video aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii usiku wa Jumanne, Rais Zelensky alimshukuru Syrskyi kwa mchango wake katika kampeni za kijeshi, ikiwemo nafasi yake muhimu katika kutetea kwa mafanikio mji mkuu wa Kyiv wakati wa siku za mwanzo za uvamizi kamili wa Urusi mwaka 2022.

    Unaweza kusoma;

  18. Vita vya Iran vimeigharimu Marekani dola bilioni 37.5 kufikia sasa - Waziri wa ulinzi

    Vita na Iran vimeigharimu Marekani takriban dola bilioni 37.5 (pauni bilioni 28) hadi sasa – ambalo ni ongezeko la karibu dola bilioni 8 tangu makadirio ya mwisho mwezi Mei, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema.

    Hegseth aliiambia Kamati ya Matumizi ya Seneti kwamba ilikuwa muhimu kwa wabunge kuidhinisha ufadhili mwingine wa dola bilioni 87 katika bunge la Pentagon, huku dola bilioni 67 kati ya hizo zikielekezwa kwa shughuli za Mashariki ya Kati.

    Kikao hicho kilivurugwa mara kadhaa na waandamanaji wa kupinga vita na kumalizika kwa mapigano kati ya waziri wa ulinzi na seneta. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Hegseth kuonekana Capitol Hill tangu uadui kati ya Marekani na Iran uanze tena wiki iliyopita na unakuja baada ya wanajeshi watatu wa Marekani kuthibitishwa kuuawa katika eneo hilo.

    Ikulu ya White House iliiomba Bunge mwezi Aprili dola trilioni 1.5 kwa Pentagon katika mwaka ujao wa fedha, ambayo ingeongeza matumizi ya kijeshi ya Marekani hadi kiwango cha juu zaidi katika enzi ya kisasa.

  19. Marekani yatangaza kumalizika kwa awamu ya 11 ya mashambulizi yake

    Saa moja baada ya kutangaza kuanza kwa mashambulizi yake dhidi ya Iran, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilitangaza kukamilika kwa awamu ya kumi na moja ya mashambulizi hayo.

    Siku ya Jumatano asubuhi, wakati mashambulizi hayo yakianza, kulikuwa na ripoti za milipuko kadhaa katika miji kadhaa ya kusini mwa Iran.

    Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha usiku wa kumi na moja , Tehran pia ilishuhudia kuwashwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga siku ya Jumatano asubuhi, lakini hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa hadi sasa kuhusu shambulio lolote linaloweza kuwa limeilenga mji mkuu huo wa Iran.

    Miji mingine ambayo iliripotiwa kushambuliwa ni pamoja na Sirik, Chabahar, Bushehr, Mahshahr, Konarak, Tabriz, Behbahan, na Omidieh.

  20. Natumai hujambo na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja