Mahakama Kuu ya Kibera ya Kenya imeahirisha hadi Desemba 14 usikilizwaji wa kesi ya mauaji ya mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang.
Siku hiyo, mkuu wa uchunguzi wa kisayansi na eneo la tukio wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendaji wa Polisi, IPOA, Joshua Mutua, anatarajiwa kurejea mahakamani kuendelea na maswali ya upande wa utetezi.
Jaji Diana Kavedza alitoa mwelekeo huo Jumatano baada ya upande wa mashtaka kukamilisha ushahidi mkuu wa Mutua, ambapo aliwasilisha mahakamani rekodi za kamera za CCTV zilizopatikana kutoka Kituo cha Polisi cha Central na Hospitali ya Mbagathi.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, Ojwang alikamatwa nyumbani kwake katika Kaunti ya Homa Bay mnamo Juni 7, 2025, kufuatia tuhuma zinazohusiana na chapisho aliloweka kwenye mitandao ya kijamii. Alifikishwa kwanza katika Kituo cha Polisi cha Mawego kabla ya kuhamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi usiku huohuo.
Mahakama Kuu ya Kibera imeonyeshwa video za kamera za usalama (CCTV) ambazo, kwa mujibu wa Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA), zinamuonyesha Albert Ojwang akiwasili akiwa hai katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi usiku wa Juni 7, 2025.
Mpelelezi wa uchunguzi wa kisayansi wa IPOA, Joshua Mutua, aliiambia mahakama kuwa video zilizopatikana zinaonyesha Ojwang akiwasili kituoni saa 3:23 usiku.
Mutua alieleza kuwa uchunguzi wa kisayansi wa mfumo wa CCTV ulibaini kuwa waya wa umeme wa mfumo huo ulikuwa umetolewa, huku diski kuu zilizohifadhi video zikifutwa taarifa zake asubuhi ya Juni 8, 2025.
Hata hivyo, alisema wachunguzi walifanikiwa kurejesha mamia ya gigabaiti za video ambazo zilithibitishwa kuwa halisi kwa kutumia mbinu za uchunguzi wa kisayansi.
Mahakama ilielezwa kuwa picha za kamera za usalama pamoja na ushahidi wa mashahidi zinaonyesha Ojwang aliwasili kituoni akiwa hai na bila majeraha makubwa yanayoonekana. Hata hivyo, ndani ya saa chache, alipata majeraha yaliyosababisha kifo chake akiwa rumande.
Ripoti ya uchunguzi wa maiti ilihitimisha kuwa alifariki kutokana na majeraha yanayoendana na kushambuliwa, jambo lililopingana na maelezo ya awali ya polisi yaliyodai kuwa alijijeruhi mwenyewe akiwa ndani ya seli.
Katika ushahidi uliotolewa awali, shahidi aliyelindwa aliimtaja Konstebo Peter Kimani kuwa askari aliyekuwa akisimamia seli usiku ambao Ojwang aliwekwa rumande.
Video zilizoonyeshwa mahakamani pia zilimuonyesha Kimani akiwa katika maeneo mbalimbali ya kituo hicho, ikiwemo nje ya vizimba vya mahabusu na katika lango kuu la kituo.
Upande wa mashtaka unatumia ushahidi huo wa CCTV kujaribu kubaini mlolongo wa matukio kabla na baada ya Ojwang kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, Samson Talaam, Konstebo Peter Kimani, Konstebo James Mukhwana pamoja na raia watatu wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Albert Omondi Ojwang.
Washtakiwa wote wamekanusha mashtaka dhidi yao.