Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani yashambulia kwa siku 11 mfululizo; mifumo ya ulinzi wa anga yawashwa katika maeneo kadhaa ya Iran

Mbali na miji ya pwani ya kusini mwa Iran ambayo imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya Marekani kwa wiki kadhaa, ulinzi wa anga pia uliripotiwa kuanzishwa Tehran Jumatano asubuhi.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani: Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini Iran haina nia ya dhati

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa iwapo Iran itadhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, hali hiyo itasababisha "mwelekeo hatari" kwa usalama na biashara ya kimataifa.

    Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, Rubio alisema Marekani bado iko tayari kufanya mazungumzo ya kumaliza mgogoro na Iran, lakini alidai kuwa Tehran haijaonesha nia ya dhati ya kushiriki mazungumzo hayo.

    Kauli zake zinakuja wakati kuongezeka kwa mzozo huo kumeathiri njia mbili muhimu za usafirishaji wa nishati duniani.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, afisa mmoja mwandamizi wa Iran alisema Jumatatu kwamba Tehran imepokea pendekezo kutoka kwa wapatanishi la kusitisha mapigano kwa muda wa siku 10.

    Jana, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran alisafiri kwenda Pakistan kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Shehbaz Sharif, pamoja na Mkuu wa Jeshi, Jenerali Asim Munir. Viongozi hao wawili wamekuwa miongoni mwa wapatanishi wakuu katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani.

    Unaweza kusoma;

  2. CDC yaomba Marekani iondoe vizuizi vya safari dhidi ya Uganda kutokana na Ebola

    Shirika kuu la afya ya umma barani Afrika limesema Jumanne kuwa haliungi mkono marufuku ya safari kama hatua ya kukabiliana na mlipuko unaoongezeka wa Ebola barani humo. Citizen imeripoti

    Shirika hilo limeitaka Marekani kuondoa vizuizi vya safari ilivyoweka kwa Uganda.

    Wito huo umetolewa siku chache baada ya Washington kuongeza masharti ya usafiri yanayohusiana na mlipuko wa sasa wa Ebola, ambao ulianzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa wasafiri kutoka DRC, Uganda na Sudani Kusini.

    Akizungumza katika mkutano wa afya wa Umoja wa Afrika mjini Accra, Ghana, Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa,CDC, Jean Kaseya, alisema shirika hilo "halishauri kuwekwa kwa marufuku ya safari."

    Wataalamu wa afya ya umma wamekuwa wakisema katika milipuko ya Ebola iliyopita kwamba marufuku ya safari huathiri usafirishaji wa vifaa vya matibabu na wafanyakazi wa afya, kuvuruga biashara, na badala yake inaweza kuzuia juhudi za ufuatiliaji wa magonjwa na kutengwa kwa wagonjwa.

    Kaseya alisema amemwandikia Waziri wa Afya wa Marekani, Robert F. Kennedy, akiomba kuondolewa kwa vizuizi vya safari dhidi ya Uganda pekee. Alisema nchi hiyo imekaa kwa wiki tatu bila kuripoti kesi mpya ya Ebola na mgonjwa wake wa mwisho aliachiliwa tarehe 16 Julai.

    "Hakuna sababu kwa Marekani kuendelea na kizuizi hiki cha safari," alisema Kaseya, akiongeza kuwa nchi hazipaswi "kuadhibiwa kwa kuwa wazi kuhusu milipuko ya magonjwa."

    Hata hivyo, licha ya kupinga vizuizi vya safari, Kaseya alionya kuwa mlipuko huo unaendelea kuongezeka kwa kasi.

    "Ikiwa hatutazuia mlipuko huu leo, utakuwa mlipuko mbaya zaidi ambao dunia itakuwa ikiurekodi," alisema.

    Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kumekuwa na visa 2,344 vilivyothibitishwa vya Ebola nchini DRC, vikiwemo vifo 930, tangu mlipuko huo ulipotangazwa katikati ya Mei.

    Uganda imeripoti visa 20 na vifo viwili, wengi wao wakiwa raia wa Congo waliovuka mpaka.

    Africa CDC inakadiria kuwa inahitaji dola bilioni 1.4 za Marekani ili kudhibiti mlipuko huo, kiasi ambacho ni karibu mara tatu ya makadirio ya awali ya dola milioni 518 yaliyotolewa mwezi uliopita.

    Unaweza kusoma;

  3. Utafiti: Nyani wakubwa hubusiana na kukumbatiana ili kudumisha amani

    Wanasayansi wamegundua kuwa kugusana, kukumbatiana na hata kubusiana kabla ya matukio yenye msongo wa mawazo huenda ni tabia ya kale inayosaidia kujenga uaminifu, kulingana na utafiti wa nyani wakubwa walio karibu zaidi na binadamu.

    Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Durham walichunguza tabia za sokwe na bonobo, na kubaini kuwa hutumia mgusano wa mwili kutulizana na kupeana uhakikisho kabla ya migogoro, hasa inayohusiana na chakula.

    Moja ya matokeo yaliyowashangaza watafiti ni kwamba sokwe, licha ya kujulikana kwa tabia yao ya ukali, walionekana wakifanya mawasiliano ya karibu, ikiwemo kuweka vidole vyao midomoni mwa wenzao.

    "Kabla ya matukio yenye msongo, hukusanyika pamoja, hutulizana, hugusana na kukumbatiana," alisema Profesa Zanna Clay

    Profesa Zanna Clay alielezea tabia hiyo kuwa ni "wito wa kuunganisha nguvu" kabla ya tukio lenye msongo wa mawazo, akilinganisha na jinsi wachezaji wa mpira wa miguu hukusanyika pamoja na kutiana moyo kabla ya mechi muhimu.

    "Ni zaidi ya 'sisi' kuliko 'mimi'," alisema.

    Wataalamu hao walifanya utafiti huo kwa sokwe na nyani aina ya bonobo waliokuwa wakiishi katika vituo viwili vya kuhifadhi nyani wakubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.

    Nyani hao walifuatiliwa katika dakika tano kabla ya karanga kuletwa, wakati walipokuwa wakijua kuwa chakula kilikuwa kinakaribia kutolewa.

    Watafiti walirekodi matukio mbalimbali ya mgusano wa kuwafariji, yakiwemo kugusana, kukumbatiana na kubusiana.

    Timu ya watafiti ilibaini kuwa nyani waliokuwa wakigusana na kukumbatiana walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata chakula na kukila kwa amani pamoja na wenzao.

    Aidha, makundi yaliyokuwa na uvumilivu mkubwa yalionesha kiwango cha juu zaidi cha mgusano wa kupeana utulivu. Watafiti walielezea hali hiyo kama " kufarijiana", ambapo nyani kadhaa walikuwa wakikumbatiana mmoja baada ya mwingine kabla ya tukio lenye kuwasababishia hali ya msongo.

  4. Mhudumu wa misaada wa Uingereza yuko chini ya uangalizi kwa hofu ya Ebola katika hospitali ya London

    Mhudumu wa misaada ya kibinadamu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehamishiwa nchini Uingereza kwa uangalizi wa kitabibu baada ya uwezekano wa kuathiriwa na virusi vya Ebola akiwa kazini.

    Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza (UKHSA) limesema mtu huyo, ambaye ni mkazi wa Uingereza na jina lake halijawekwa wazi, hana dalili zozote za Ebola kwa sasa, na hatua ya kumhamisha imechukuliwa kama tahadhari.

    Kwa mujibu wa UKHSA, mhudumu huyo anaendelea kuwa katika hali nzuri kiafya lakini anafanyiwa vipimo na kufuatiliwa katika hospitali moja jijini London.

    Jina la hospitali hiyo halijatangazwa, ingawa Hospitali ya Royal Free kaskazini mwa London ina kitengo maalumu cha kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa hatari ya kuambukiza.

    Kipindi cha kujitokeza kwa dalili za Ebola ni kati ya siku mbili hadi 21, hivyo mhudumu huyo atalazimika kujitenga kwa muda wote wa kipindi hicho.

    Mhusika huyo alikuwa akifanya kazi na shirika la misaada lililokuwa likisaidia kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini DRC.

    Ebola ni ugonjwa hatari sana unaosababishwa na virusi. Tofauti na mafua au Covid-19, virusi vya Ebola haviambukizwi kwa njia ya hewa, bali huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.

    Dalili zake huanza ghafla na zinafanana na za mafua au malaria, zikiwemo homa, maumivu ya kichwa na uchovu.

    Ugonjwa unapoendelea, mgonjwa anaweza kutapika, kuharisha na kushindwa kwa baadhi ya viungo vya mwili kufanya kazi. Baadhi ya wagonjwa pia hutokwa na damu ndani na nje ya mwili.

    Richard Pebody, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Mlipuko na yanayoibuka katika Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza (UKHSA), amesema:

    "Hatari kwa umma kwa ujumla bado ni ndogo. Mtu huyu amehamishwa kama hatua ya tahadhari ya ziada, na tunafurahi kuwa anaendelea kuwa katika hali nzuri."

    UKHSA pia imesema kwa sasa hakuna kesi yoyote iliyothibitishwa ya ugonjwa wa Ebola nchini Uingereza.

    Unaweza kusoma;

  5. Rais wa Ukraine amtimua Mkuu wa Jeshi, Oleksandr Syrskyi

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemwondoa Mkuu wa Majeshi ya Ukraine, Oleksandr Syrskyi, kutoka wadhifa wake.

    Hatua hiyo imekuja siku chache tu baada ya kuondolewa kwa Waziri wa Ulinzi aliyekuwa maarufu, Mykhailo Fedorov, hatua iliyosababisha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini humo.

    Awali kulikuwa na uvumi kwamba kuondolewa kwa Fedorov kulihusiana na mgogoro kati yake na Syrskyi, na baadaye taarifa hizo zikathibitishwa.

    Fedorov, mwenye umri wa miaka 35, amekuwa akisifiwa kwa kuleta mageuzi makubwa katika Wizara ya Ulinzi, kuimarisha uwezo wa jeshi la Ukraine na kuongoza juhudi za kupambana na rushwa.

    Kwa upande mwingine, Syrskyi, mwenye umri wa miaka 60, anaonekana na wengi nchini Ukraine kama kamanda mwenye mtazamo wa kijeshi wa enzi za Umoja wa Kisovieti, ambaye hakuwa tayari kutekeleza mabadiliko makubwa ndani ya jeshi.

    Nafasi yake imechukuliwa na Jenerali Mykhailo Drapatyi, mwenye umri wa miaka 43, ambaye anajulikana kwa uzoefu wake mkubwa vitani na umaarufu miongoni mwa wanajeshi.

    "Nitafanya kazi kwa uwajibikaji, kwa umakini wa hali ya juu, na kwa heshima kwa wale wote wanaolinda nchi yetu leo," Drapatyi aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook.

    Pia alimshukuru Syrskyi "kwa kazi yake ya muda mrefu ya kuimarisha jeshi la Ukraine," akiongeza kuwa, "Nilikulia ndani ya jeshi hilo."

    Katika ujumbe wa video aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii usiku wa Jumanne, Rais Zelensky alimshukuru Syrskyi kwa mchango wake katika kampeni za kijeshi, ikiwemo nafasi yake muhimu katika kutetea kwa mafanikio mji mkuu wa Kyiv wakati wa siku za mwanzo za uvamizi kamili wa Urusi mwaka 2022.

    Unaweza kusoma;

  6. Vita vya Iran vimeigharimu Marekani dola bilioni 37.5 kufikia sasa - Waziri wa ulinzi

    Vita na Iran vimeigharimu Marekani takriban dola bilioni 37.5 (pauni bilioni 28) hadi sasa – ambalo ni ongezeko la karibu dola bilioni 8 tangu makadirio ya mwisho mwezi Mei, Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amesema.

    Hegseth aliiambia Kamati ya Matumizi ya Seneti kwamba ilikuwa muhimu kwa wabunge kuidhinisha ufadhili mwingine wa dola bilioni 87 katika bunge la Pentagon, huku dola bilioni 67 kati ya hizo zikielekezwa kwa shughuli za Mashariki ya Kati.

    Kikao hicho kilivurugwa mara kadhaa na waandamanaji wa kupinga vita na kumalizika kwa mapigano kati ya waziri wa ulinzi na seneta. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Hegseth kuonekana Capitol Hill tangu uadui kati ya Marekani na Iran uanze tena wiki iliyopita na unakuja baada ya wanajeshi watatu wa Marekani kuthibitishwa kuuawa katika eneo hilo.

    Ikulu ya White House iliiomba Bunge mwezi Aprili dola trilioni 1.5 kwa Pentagon katika mwaka ujao wa fedha, ambayo ingeongeza matumizi ya kijeshi ya Marekani hadi kiwango cha juu zaidi katika enzi ya kisasa.

  7. Marekani yatangaza kumalizika kwa awamu ya 11 ya mashambulizi yake

    Saa moja baada ya kutangaza kuanza kwa mashambulizi yake dhidi ya Iran, Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilitangaza kukamilika kwa awamu ya kumi na moja ya mashambulizi hayo.

    Siku ya Jumatano asubuhi, wakati mashambulizi hayo yakianza, kulikuwa na ripoti za milipuko kadhaa katika miji kadhaa ya kusini mwa Iran.

    Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha usiku wa kumi na moja , Tehran pia ilishuhudia kuwashwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga siku ya Jumatano asubuhi, lakini hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa hadi sasa kuhusu shambulio lolote linaloweza kuwa limeilenga mji mkuu huo wa Iran.

    Miji mingine ambayo iliripotiwa kushambuliwa ni pamoja na Sirik, Chabahar, Bushehr, Mahshahr, Konarak, Tabriz, Behbahan, na Omidieh.

  8. Natumai hujambo na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja