Siasa za Afrika zinavyojengwa 'kihuni'

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuibuka upya kwa kasi kwa magenge ya kukodiwa yanayojulikana kama "wahuni"-kumekuwa ni mtindo ambao umejitokeza mara kadhaa na kuonekana kuwa hatari sana katika siasa za Kenya.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, mikutano ya kisiasa, mikutano ya hadhara, maeneo ya kidini na hata basi la shule lililodhaniwa kubeba wafuasi wa mrengo fulani yameshuhudia matukio ya kuvamiwa na vijana.

Wimbi hili la wahuni limezua wasiwasi nchini na hofu kwamba Kenya huenda muda si mrefu inaweza kujikuta katika dimbwi la machafuko ya kisiasa.

Ukikumbuka vizuri hili sio geni. Wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/2008, wanasiasa waliunda makundi ya wahuni ya kikabila na vijana kama vile Mungiki kwa ajili ya masilahi ya eneo ambayo baadaye yalitikisa nchi kwa utendaji wa vitendo visivyokubalika katika jamii.

Mara kwanza tukio la wahuni kuvamia mkutano wa kisiasa huenda ilichukuliwa kama vurugu tu zinazojitokeza pengine wakati wa matukio kama maandamano lakini kadiri siku zinavyosonga mbele, imedhihirika wazi kuwa hili linatumika na wengine kama mkakati wa kumtishia adui, kumnyamazisha au kuzima kabisa mjadala ambao unaonekana kuwa kero kwa mwingine.

Baadhi ya matukio ya 'wahuni' Kenya 2026

  • Uvamizi wa Kanisa la All Saints Cathedral

Nyakati za nyuma wakati mtu au jamii ilipokumbana na machafuko pengine baadhi ya sehemu ambazo wangefikiria kwenda kujistiri ni Kanisani. Lakini mwenendo unaonekana kubadilika.

Katika shambulio la kinyama lililoshtua wengi, wavamizi waliokodiwa waliokuwa wakiendesha pikipiki walivamia kanisa la kihistoria la All Saints Cathedral jijini Nairobi. Waliingia na kuvuruga kongamano la amani la uwajibikaji baada ya kusomwa kwa bajeti lililokuwa limehudhuriwa na makundi ya kiraia, viongozi wa kidini, wanasheria na wananchi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wavamizi waliingia kwa nguvu katika ukumbu wa Kanisani na kuwaibia waliohudhuria kongamano waliokuwa wakikimbilia maeneo salama.

Viongozi wa Kidini na chama cha Wanasheria Kenya walilaani vikali uvamizi huo.

  • Shambulio dhidi ya Seneta Godfrey Osotsi

Seneta wa kaunti ya Vihiga Godfrey Osotsi alishambuliwa na kundi lililojihami katika mkahawa mmoja huko Kisumu. Wahuni walimfuata hadi sehemu aliyokuwa ameketi na kumshambulia hatua iliyodaiwa kuchochewa na msimamo wake wa kisiasa.

Mwanasiasa huyo alishambuliwa vibaya kiasi cha kulazwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu.

  • Rigathi Gachagua

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua nchini Kenya amewahi kuvamiwa mara kadhaa ikiwa ni pamoja na ndani ya Kanisa moja eneo la Nyeri. Wanaume waliovaa barakoa waliingia ndani ya kanisa na kuvuruga ibada ambayo Gachagua pia alikuwa amehudhuria.

Magari kadhaa yalitiwa moto na waumini kurushiwa vitoza machozi.

  • Kuvamiwa kwa basi la shule

Kama haitoshi, ni hivi majuzi tu ambapo basi lililokuwa limebeba wanafunzi lilionekana likiwa limevamiwa na wahuni ambao inasemekana kuwa walidhani lilikuwa limebeba wafuasi wa kisiasa.

Pengine orodha hii inaweza kuendelea na kuendelea.

Nani wa kulaumiwa?

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Matukio haya na mengine yamesababisha kutupiana lawana kutoka kila upande.

Upande wa upinzani viongozi wamekuwa wakishtumu serikali kwa kupanga au kuwezesha kimya kimya ghasia zinazotekelezwa na makundi ya wahuni na hata kudai kuwa maafisa wa usalama wanachukua muda kujibu matukio kama hayo yanapotokea.

Hata hivyo, Serikali imekanusha madai hayo huku Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen akiambia kamati ya bunge kwamba serikali inafuatilia zaidi ya magenge ya uhalifu 100. Alionya vijana serikali itawafuatilia wale wanaojihusisha na uhalifu.

"Wanasiasa hawatakuwa na wewe wakati unapofanya uhalifu," Waziri alisema.

Kwa nini "Uhuni" unaongezeka kwenye siasa za dunia?

Kuna hofu kwamba uvamizi wa wahuni unaoendelea unaweza kuwa tatizo kubwa siku zijazo.

Ukosefu wa ajira kwa vijana na mazingira magumu ya kiuchumi, huenda kunatumiwa vibaya na wanasiasa kwa sababu inakuwa rahisi kwao kushawishi vijana kutekeleza vitendo vya uhalifu kwa ahadi za kuwapa pesa kidogo.

Historia inaonyesha kwamba wanasiasa wa Kenya mara kwa mara hutengeneza mitandao ya aina hii wakati wa tofauti kali za kisiasa.

Kupitia kituo cha habari cha Citizen nchini Kenya, mmoja wa vijana aliyehojiwa alisema huwa wanatumwa na wanasiasa.

Makundi ya aina hii yanatumika kama njia ya kutishia na kuogopesha kundi pinzani ili kujijengea mazingira ya kuwa upande wenye nguvu na udhibiti.

Kwanini 'wahuni' wanaongezeka kwenye siasa za Afrika?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maandamano Nigeria

Kenya ni mfano tu wa hivi karibuni, lakini zinafanyika katika nchi kadhaa za Afrika, ikiwemo Nigeria, Msumbiji , Zimbabwe na Sierra Leone.

Mfano mkubwa ni nchini Nigeria, ambapo wahuni wa kisiasa wamefungamana pakubwa na uchaguzi. Kwa kawaida ni wanamgambo wasio rasmi, madhehebu, au magenge ya mitaani yanayokodishwa na wanasiasa ili kupata ushindi kwa njia yoyote ile.

Haya ni matukio yaliyoanza kitambo enzi za ukoloni. Wakati vyama vinaundwa vilijifungamanisha na vijana ili kulinda wanasiasa na kutatiza mikutano ya wapinzani.

Wakati wa mpito wa Kidemokrasia wa 1999 Nigeria iliporejea kwenye demokrasia, misimamo iliongezeka sana. Wasomi wa kisiasa walijiingiza katika kundi kubwa la vijana wasio na ajira, na kubadilisha udugu na "vikundi" vya vyuo vikuu kuwa makundi ya kisiasa yenye silaha. Wanasiasa waliwapa silaha na pesa taslimu ili kuiba masanduku ya kura, kutishia wapiga kura, na kuwaua wapinzani.

Matokeo yake ni kuwa baada ya uchaguzi, makundi ya wahuni sio kuwa hutokomea moja kwa moja, kwa sababu huachwa njia panda na wanasiasa wao, huwa wanabadilika na kuwa makundi ya wizi wa kimabavu,wanaoteka watu nyara na kuiba mafuta.

Mara nyingi hata wanapokamatwa, inakuwa vigumu kuadhibiwa kwa sababu wanasiasa hao hao hujitokeza kuwatetea wasikabiliwe na mkono wa sheria.

Nchi zingine duniani zenye makundi ya wahuni

Wakati makundi haya yanatekeleza kile walichoagizwa wakati huo huchukuliwa kama mkakati wa kumshinda adui ila ukweli wa mambo ni kwamba baada ya muda, makundi hayo hayo ndio hugeuka na kuwa chungu kwa aliyelibuni na kuliwezesha.

Tuangazie baadhi ya nchi ambazo zimejikuta kwenye tatizo la magenge ya wahuni ambayo awali, yalitumiwa kama njia ya kujiimarisha kisiasa.

Haiti

.

Chanzo cha picha, EPA

Haiti ni mfano hai zaidi wa nchi inayoendeshwa na makundi ya "wahuni". Kwa miongo kadhaa, wanasiasa na vikundi vya wafanya biashara wasomi vilifadhili magenge ya mitaani kama vile G9 Family kutishia upinzani wa kisiasa.

Wakati magenge hayo yalipogundua kuwa wanasiasa wanatumia nguvu yao kuendelea kusalia madarakani, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa serikali kuporomoka.

Kufuatia kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse, magenge hayo yaligundua kuwa hayahitaji tena dalali.

Walijiimarisha na kuchukua udhibiti wa mji mkuu, wakashikilia miundombinu muhimu kama bandari na vituo vya mafuta na kumuamuru Waziri Mkuu kujiuzulu.

Ecuador

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ecuador kwa sasa imekuwa yenye mfano wa kusikitisha zaidi wa nchi inayotumbukia kwenye uhalifu wa magenge. Miaka kadhaa iliyopita, ilikuwa mojawapo ya mataifa salama zaidi Amerika ya Kusini lakini leo hii, simulizi ni tofauti.

Inasimamiwa na makundi ya magenge kama vile Los Choneros na Los Lobos.

Awali, wanasiasa na wakuu wa magereza waliwachukulia viongozi wa magenge kama "magavana" wasio rasmi ndani ya magereza. Waliwapa uhuru wa kusimamia seli kwa mabadilishano ya udumishaji amani.

Wahuni walitumia njia hii kuwa na umoja wao na kutengeneza mitandao yao imara kwa ushirikiano na magenge ya Mexico na kupata hifadhi ya silaha za kijeshi.

Utawala wa makundi ya wahuni ulijitokeza kabisa wakati wa uchaguzi wa urais ambapo mgombea Fernando Villavicencio aliuawa na wahuni.

Na tangu wakati huo, wametekeleza mashambulizi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwaua waendesha mashtaka na kuacha vichwa vyao kwenye fukwe za bahari za umma, na kulazimisha serikali kutangaza "migogoro ya ndani ya makundi yenye silaha."

Mexico

.

Chanzo cha picha, EPA

Wakati Mexico inaendeleza shughuli zake kiserikali na yenye jeshi kama nchi nyingine yoyote, maeneo mengi yanasimamiwa na magenge ya wahuni kama vile la Jalisco na Sinaloa.

Miongo kadhaa iliyopita wanasiasa bila kujua, walihadaiwa na makundi haya ya wahuni yaliyokuwa yakiwahonga na kudai kuwa pamoja nao wakati wanatafuta njia za kuingia madarakani.

Baada ya muda, mzunguko wa fedha wa makundi hayo uliongezeka kwa kasi zaidi kuliko bajeti za manispaa ya mitaa.

Magenge hayo yakabadilisha mfumo wao kutoka kuhonga serikali hadi kuamuru kwa nguvu yote nani atakuwa serikalini. Walianzisha mfumo wa kiongozi akubali pesa zao na maagizo yao, au auawe kwa risasi.

Chaguzi za Mexico zimesemekana kuwa za umwagaji damu nyingi zaidi duniani kwa wanasiasa. Wasimamizi wa magenge hufyatua risasi mara kwa mara kwenye misafara ya kampeni kulenga wanasiasa na kuua wagombeaji wa umeya katikati ya mikutano.

Jinsi wahuni wanayofanya kazi ni sawa na mfumo wako wa kinga kushambulia kimakosa tishu zako za mwili. Huletwa kwa madhumini ya kuvamia wapinzani lakini hatimaye, makundi haya hukua, yanapata ujuzi na kujua jinsi serikali zinavyojiendesha pamoja na mapungufu yao. Kisha hubadilika na kuwa zimwi mla watu tuliyejitengenezea wenyewe na kumaliza wanasiasa wale wale waliowawezesha.

Na inapofikia hatua hii, kubadili tena mfumo wa taasisi hadi kuurejesha kuwa wa kidemokrasia, inakuwa kibarua kigumu kinachohitaji utayari na ushirikiano wa pande nyingi bila kusahau na mkono wa Mungu.