Jinsi ya kujua kama mwili wako unatoa harufu inayowasumbua wengine

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

"Uchovu wa kunusa (nose blindness au olfactory fatigue) unaweza kukufanya usitambue harufu ya mwili wako mwenyewe. Hata hivyo, kuna njia kadhaa zinazoweza kukusaidia kubaini kama harufu hiyo inawasumbua wengine."

Sote wakati fulani huwa na harufu ya mwili, wakati bakteria wanapojikusanya kwenye jasho linalozalishwa na tezi za apocrine.

Tatizo ni kwamba hisi zetu za kunusa zinaweza kuzoea harufu tunazozipata mara kwa mara, hata zile zisizopendeza. Hali hii huitwa uchovu wa kunusa au kutokuwa na uwezo wa kutambua harufu uliyoizoea.

Hii ndiyo sababu, kwa mfano, huenda usitambue harufu ya mbwa wako ndani ya nyumba, lakini wageni wakaweza kuinusa.

Kuna njia zinazopendekezwa za kukabiliana na hali hii, ingawa hazijafanyiwa utafiti wa kutosha. Njia moja ni kupitisha vidole vilivyo safi kwenye ngozi ya kichwa au chini ya kwapa, kisha kunusa vidole hivyo kwa tahadhari.

Harufu ya mwili

Harufu ya mwili hutokea pale jasho linapochanganyika na bakteria waliopo kwenye ngozi.

Harufu ya mwili inaweza kubadilika kutokana na homoni, vyakula unavyokula, maambukizi, dawa au magonjwa yaliyopo mwilini kama vile kisukari. Dawa za kuzuia jasho zenye nguvu maalumu au dawa nyingine zinaweza kusaidia.

Harufu ya mwili ni nini?

Harufu ya mwili ni ile unayonusa wakati jasho linapokutana na bakteria walio kwenye ngozi. Jasho lenyewe halina harufu, lakini linapochanganyika na bakteria kwenye ngozi, husababisha harufu.

Harufu ya mwili inaweza kuwa tamu, chachu, kali au kufanana na vitunguu. Kiasi cha jasho unalotoa si lazima kiwe na uhusiano na harufu ya mwili. Ndiyo maana mtu anaweza kuwa na harufu mbaya ya mwili bila kutokwa na jasho nyingi. Vivyo hivyo, mtu anaweza kutokwa na jasho jingi lakini asiwe na harufu.

Hii ni kwa sababu harufu ya mwili hutokana na aina ya bakteria walio kwenye ngozi na jinsi bakteria hao wanavyoingiliana na jasho, si jasho lenyewe.

Kutokwa na jasho ni utoaji wa majimaji kupitia tezi za jasho hadi kwenye uso wa ngozi. Kuna aina mbili za tezi za jasho: eccrine na apocrine. Tezi za apocrine ndizo zinazohusika zaidi na uzalishaji wa harufu ya mwili.

Tezi za eccrine

Tezi za eccrine hutoa jasho moja kwa moja kwenye uso wa ngozi. Jasho linapovukiza, husaidia kuupoza mwili na kudhibiti joto la mwili. Tezi hizi hazizalishi harufu.

Joto la mwili linapoongezeka kutokana na kufanya shughuli za mwili au kuwa katika mazingira ya joto, uvukizaji wa jasho kutoka kwenye ngozi husaidia kuupoza mwili. Tezi za eccrine hupatikana sehemu kubwa ya mwili, ikiwemo kwenye viganja vya mikono na nyayo za miguu.

Tezi za apocrine

Tezi za apocrine hufunguka kwenye vinyweleo. Vinyweleo ni miundo inayofanana na mirija inayoshikilia nywele ndani ya ngozi. Tezi hizi hupatikana kwenye sehemu za siri na kwapani.

Tezi za apocrine huzalisha jasho ambalo linaweza kuwa na harufu linapokutana na bakteria kwenye ngozi. Tezi hizi huanza kufanya kazi mtu anapofikia balehe, ndiyo maana watoto wadogo kwa kawaida hawana harufu ya mwili.

Kutokwa na jasho ni mchakato wa kawaida wa mwili, lakini kutokana na baadhi ya vyakula tunavyokula, kanuni za usafi au vinasaba, jasho linaweza kuwa na harufu mbaya linapogusana na ngozi.

Mabadiliko katika kiasi cha jasho unalotoa au harufu ya mwili wako yanaweza kuwa ishara ya hali fulani ya kiafya.

Nani yuko katika hatari zaidi ya kuwa na harufu kali ya mwili?

Wanaume huathirika zaidi na harufu ya mwili kwa sababu kwa kawaida huwa na shughuli kubwa zaidi za tezi za apocrine na nywele nyingi zaidi mwilini.

Tezi za apocrine huanza kufanya kazi mtu anapofikia balehe, hivyo harufu ya mwili huanza kujitokeza wakati wa ujana.

Nini husababisha harufu ya mwili?

Harufu ya mwili hutokea bakteria walio kwenye ngozi wanapokutana na jasho. Ngozi yetu kwa kawaida huwa na bakteria. Tunapotokwa na jasho, maji, chumvi na mafuta huchanganyika na bakteria hao na kusababisha harufu.

Harufu hiyo inaweza kuwa mbaya, nzuri au isiwe na harufu kabisa. Mambo kama vyakula unavyokula, homoni au dawa yanaweza kuathiri harufu ya mwili.

Hali inayoitwa hyperhidrosis husababisha mtu kutokwa na jasho kupita kiasi. Watu wenye hali hii wanaweza kuwa katika uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na harufu ya mwili kwa sababu wanatokwa na jasho jingi. Hata hivyo, mara nyingi ni tezi za eccrine zinazohusika zaidi na usumbufu wa kutokwa na jasho kwenye viganja na nyayo.

Kila unapotoa jasho, kuna uwezekano wa kupata harufu ya mwili isiyopendeza. Baadhi ya watu wako katika uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na harufu kali ya mwili kuliko wengine.

Mambo mengine yanayoweza kuathiri harufu ya mwili ni:

  • Mazoezi.
  • Msongo wa mawazo au wasiwasi.
  • Hali ya hewa ya joto.
  • Kuwa na uzito mkubwa au unene kupita kiasi.
  • Vinasaba.

Kwa nini jasho langu linanuka?

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kufanya jasho lako linuke. Kwa mfano, baadhi ya dawa, virutubisho au vyakula vinaweza kufanya jasho lako linuke.

Kumbuka kwamba jasho lenyewe si chanzo cha harufu; ni bakteria walio kwenye ngozi wanapochanganyika na jasho.

Magonjwa na hali kadhaa za kiafya zinahusishwa na mabadiliko katika harufu ya kawaida ya mwili, ikiwa ni pamoja na:

  • Kisukari.
  • Gauti.
  • Kukoma hedhi.
  • Tezi ya thyroid kufanya kazi kupita kiasi.
  • Ugonjwa wa ini.
  • Ugonjwa wa figo.
  • Magonjwa ya kuambukiza.

Ikiwa una kisukari, mabadiliko katika harufu ya mwili yanaweza kuwa ishara ya ketoasidosisi inayohusiana na kisukari (diabetes-related ketoacidosis).

Kiwango kikubwa cha ketoni husababisha damu kuwa na tindikali, na harufu ya mwili inaweza kuwa kama ya matunda. Kwa mtu mwenye ugonjwa wa ini au figo, harufu ya mwili inaweza kufanana na dawa ya kuua viini au bleach kutokana na mkusanyiko wa sumu mwilini.

Je, mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha harufu ya mwili?

Ndiyo. Mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha harufu ya mwili kubadilika.

Vipindi vya joto mwilini, kutokwa na jasho wakati wa usiku na mabadiliko ya homoni yanayotokea wakati wa kukoma hedhi husababisha kutokwa na jasho kupita kiasi, jambo linaloweza kubadilisha harufu ya mwili.

Baadhi ya watu wanaamini kuwa harufu ya mwili hubadilika wakati wa ujauzito au hedhi. Utafiti unaonyesha kuwa harufu ya mwili inaweza kubadilika wakati wa ovulation, kipindi katika mzunguko wa hedhi ambapo mtu anaweza kushika mimba, ili kuvutia mwenza.

Je, baadhi ya vyakula vinaweza kusababisha harufu ya mwili?

Methali inayosema "wewe ni kile unachokula" inaweza pia kuhusishwa na harufu ya mwili.

Ukitumia vyakula vyenye kiwango kikubwa cha salfa, unaweza kupata harufu ya mwili. Salfa inanuka kama mayai yaliyooza. Mwili unapotoa salfa hiyo kupitia jasho, inaweza kusababisha harufu isiyopendeza.

Vyakula vyenye salfa kwa wingi ni pamoja na:

  • Vitunguu.
  • Kitunguu saumu.
  • Kabichi.
  • Broccoli.
  • Cauliflower.
  • Nyama nyekundu.

Baadhi ya vyakula vinaweza pia kukufanya utoe jasho zaidi. Jasho hili la ziada linaweza kusababisha harufu kali zaidi ya mwili.

Vyakula hivyo havisababishi harufu ya mwili moja kwa moja, lakini vinaweza kuathiri jinsi unavyonuka kwa sababu vinaongeza kiasi cha jasho. Vyakula na vinywaji hivyo ni pamoja na:

  • Monosodium glutamate (MSG).
  • Kafeini.
  • Viungo kama unga wa curry au cumin.
  • Pilipili na vyakula vingine vyenye ukali.
  • Pombe.

Kupunguza au kuacha vitu hivi vinavyochochea hali hiyo kunaweza kusaidia kuboresha harufu ya mwili.

Unawezaje kuondoa harufu ya mwili kwa njia za asili?

Ikiwa unataka njia ya asili ya kukabiliana na harufu ya kwapa, kuna baadhi ya njia zinazoweza kusaidia. Zungumza na mtoa huduma wako wa afya kuhusu:

  • Baking soda: Tengeneza mchanganyiko mzito kwa kutumia baking soda na maji. Paka kwenye kwapa na uache ikauke. Baking soda husaidia kusawazisha kiwango cha asidi kwenye ngozi na kupunguza harufu.
  • Chai ya kijani: Loweka mifuko ya chai ya kijani kwenye maji ya uvuguvugu. Weka mifuko hiyo iliyolowekwa chini ya kwapa kwa dakika kadhaa kila siku. Chai ya kijani inaweza kusaidia kuziba vinyweleo na kupunguza kutokwa na jasho.
  • Apple cider vinegar: Changanya apple cider vinegar na kiasi kidogo cha maji kwenye chupa ya kunyunyizia. Nyunyizia mchanganyiko huo kwenye kwapa. Asidi iliyomo kwenye siki husaidia kuua bakteria.
  • Juisi ya limau: Changanya juisi ya limau na maji kwenye chupa ya kunyunyizia. Nyunyizia chini ya kwapa. Asidi ya citric iliyomo kwenye limau huua bakteria.

Ni deodorant gani bora kwa kwapa zinazonuka?

Deodorant hufanya kazi kwa kuficha harufu ya mwili kwa kutumia manukato yenye harufu nzuri zaidi.

Kwa upande mwingine, antiperspirant hupunguza kiasi cha jasho unalotoa. Hakikisha unatumia bidhaa ya kwapani iliyoandikwa "antiperspirant" kwenye kifungashio.

Kiambato kinachotumika katika antiperspirant nyingi ni aluminium.

Paka antiperspirant baada ya kuoga na kabla ya kulala. Hakikisha unapaka kwenye ngozi kavu ili kupata matokeo bora.

Ikiwa antiperspirant zinazopatikana bila cheti cha daktari hazikusaidii, mtoa huduma wako wa afya anaweza kukuandikia antiperspirant yenye nguvu zaidi.

Kwa ujumla, harufu ya mwili ni hali ya kawaida inayoweza kuathiri mtu yeyote. Kudumisha usafi wa mwili, kuchagua vyakula kwa uangalifu na kutumia bidhaa sahihi za kuzuia jasho kunaweza kusaidia kupunguza tatizo hilo. Ikiwa harufu ya mwili itabadilika ghafla au kuwa kali kupita kawaida, ni vyema kumwona mtaalamu wa afya kwa uchunguzi zaidi.