Rosana Kathure: "Ningejua anayenioa atanikata jicho, nisingeolewa"

.
Maelezo ya picha, Rosana Kathure
    • Author, Asha Juma
    • Nafasi, BBC Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Mwanamke anapotoka kwao na kuamua kuolewa huwa anajua amepata mwenza wake akiwa na matumaini ya kuishi naye kwa shida na raha hadi kifo kitakapowatenganisha.

Lakini inakuwaje pale unapogundua kuwa aliyekutoa kwenu amebadilika na kuwa mtu tofauti kabisa na badala ya kuishi pamoja kwa upendo ikageuka sio tu karaha lakini kiasi cha hata kunusurika kifo kwa tundu ya sindano.

Katika Waridi wa BBC, Asha Juma alipata fursa ya kuzungumza na Rosana Kathure kutoka eneo la Meru nchini Kenya aliyepitia ukatili katika ndoa yake.

Mwanamke anapotoka kwao na kuamua kuolewa huwa anajua amepata mwenza wake akiwa na matumaini ya kuishi naye kwa shida na raha hadi kifo kitakapowatenganisha.

Lakini inakuwaje pale unapogundua kuwa aliyekutoa kwenu amebadilika na kuwa mtu tofauti kabisa na badala ya kuishi pamoja kwa upendo ikageuka sio tu karaha lakini kiasi cha hata kunusurika kifo kwa tundu ya sindano.

Katika Waridi wa BBC, Asha Juma alipata fursa ya kuzungumza na Rosana Kathure kutoka eneo la Meru nchini Kenya aliyepitia ukatili katika ndoa yake.

Ndoa ya karaha

.

Rosana Kathure anakumbuka wakati alipokutana na baba watoto wake mtarajiwa wakati huo upendo ndio ulikuwa umetawala.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kipindi kifupi cha kuchumbiana, waliamua kwenda kwa wazazi ili kurasimisha ndoa yao.

Rosana anasema maisha kabla ya mtafaruku kati yake na mume wake, walipenda kama chanda na pete.

"Kabla ya huu mkasa kutokea, tulikuwa tunakunywa na glasi moja ya chai. Kaupendo kalikuwa kazuri sana," kwa tabasamu la aina yake Rosana anasema.

"Kuna wakati alikuwa anakuja akiwa mlevi, nilimchukua nikamtoa viatu na kumuosha miguu. Kisha nikampandisha kitandani akalala. Nilikuwa nampenda," Rosana anaongeza.

Lakini kulingana na simulizi ya Rosana, mume wake alibadilika baada ya miaka kadhaa.

"Mtu hakuonyeshi mambo mabaya wakati uko kwenu. Lakini ubaya huanza pole pole hadi inapofikia wakati hali inakuwa mbaya zaidi," anasema Rosana.

"Mtoto wa kwanza na wa pili, mume wangu alikuwa sawa. Mtoto wa tatu akiwa na miezi minne, mume wangu alianza kubadilika. Alianza kuvuta bangi na kunywa chang'aa. Alikuwa akinipiga bila sababu, vita kila wakati ndani ya nyumba hadi anamwaga chakula jikoni. Na mimi pia nikaanza kelele," Rosana anakumbuka.

Rosana anakiri kuwa baada ya kuona tabia za mume wake zimebadilika, hata yeye alianza kuwa mama mwenye kelele na kila wakati alikuwa akimwambia mume wake kwamba atarudi kwao. Ila majibu ya mume wake yalikuwa makali ingawa kwake aliyachukulia kirahisi.

"Alikuwa akiniambia kuliko nitoke hapa na kurudi kwetu, ni heri yeye aniuwe na ajiue," Rosana anakumbuka majibu ya mume wake kila walipokwazana.

Rosana alikuwa amezoea kusikia maneno hayo masikioni mwake kila wakati.

Usiku wa mateso

.
Maelezo ya picha, Rosana Kathure

Mambo yalibadilika kabisa alipofingua mtoto wake wa mwisho na alipotimiza miezi miwili, kile ambacho hakikutarajiwa kikatokea.

Rosana anasema hakujua kama siku hiyo maisha yake yangechukua mwelekeo mpya.

Hali ilikuwa kama kawaida na ratiba ya Rosana siku hiyo ilikuwa kumpeleka kliniki. Aliamka na kujitayarisha na kumuacha mume wake na watoto wengine watatu.

Siku hiyo, kliniki hakukuwa na foleni ndefu kama ilivyozoeleka. Hii ina maana kwamba mtoto alipata chanjo yake na mara moja Rosana akaanza safari ya kurejea nyumbani.

Lakini alipowasili, alikutana na kitu ambacho hakukitarajia.

"Nilimkuta mume wangu na msichana mdogo aliyekuwa kidato cha nne kwenye kitanda chetu cha ndoa. Hicho ndio chanzo cha vita ambavyo mwishowe, mume wangu alinikatakata," anasema Rosana.

Mama huyu anasema kilichomtia machungu zaidi ni kufanya kitendo hicho licha ya kujua fika kwamba ana mtoto mdogo wa miezi miwili.

Lakini punde baada ya msichana wa shule kumuona Rosana amewafumania, aliamua mguu niponye kabla ya mama mwenye nyumba kutibuka zaidi.

"Msichana alitoka mbio nikasalia na mume wangu ambaye sasa alikuwa ameketi. Na mimi nikamlaza mtoto chini," Rosana anasema.

Kilichofuata ilikuwa ni Rosana kuanza kuzungumza kwa kupaza sauti nje huku akiwa anarejelea maneno ya kuwa atarudi kwao, asijue kilichokuwa kinamsubiri.

"Alisimama mlangoni akaniambia. Wewe huwa unasema kuwa utaenda kwenu. Heri nikuharibu sura badala ya wewe kutoka hapa uende kwenu, kwa sababu unaweza kwenda na uolewe na mwanamume mwingine. Afadhali nikuue na mimi nijiue tuende pamoja," Rosana anakumbuka alichoambiwa.

"Unaona alitimiza alichosema. Aliharibu jicho langu. Si unaona sina jicho na pia alinikata kichwa. Hata tumboni alinikata utumbo ukawa nje. Mguuni pia alinikata kwa panga na kunidunga kisu," Rosana anaonyesha sehemu alizokatwa katwa na mume wake.

Lakini baada ya kugombana na Rosana kisa na mkasa ni msichana wa shule. Mume wake alijishusha na akaomba msamaha.

"Aliniambia pole, nisamehe. Maandiko yanasema tusameheane. Mimi huwa nakuona ukienda kanisani. Nisamehe kwa sababu hata Mungu anasema tusahameane," Rosana anakumbuka alichoambiwa na mume wake.

Mama huyu alichukulia msamaha ambao mume wake ameomba kuwa wa kweli na kumaanisha, lakini kumbe usichokijua ni usiku wa giza. Mume wa Rosana alikuwa na mengine tofauti anayopanga akili mwake.

"Kumbe mimi nilikuwa nasubiri kifo. Hata singeshuku kilichotokea baadaye usiku. Hili jicho langu, sikujua atalikata na panga wala mkono wangu. Sasa hivi umelemaa," Rosana anasema.

Baada ya kusameheana, mume wa Rosana aliomba apewe panga na tupa, kifaa cha kunoa panga. Pia alimuomba mke wake ampe chupa ya mafuta taa. Ni jambo la kawaida yeye kuondoka na vitu hivi.

"Aliniitisha panga na chupa ya mafuta ya taa na tochi. Nikampatia. Kumbe mimi ndiye atakayenimwilika jioni hiyo," Rosana anakumbuka.

Baada ya hapo, mume wake alimuaga kuwa anaenda kumletea unga na akamuomba kuwa asifunge mlango na ndani kwa sababu anaweza kuchelewa kurudi asijue kuwa alikuwa anampangia kumuua.

"Hakika, huwezi kuingia kwenye roho ya mtu ukajua anavyokupangia," Rosana anasema.

Kufikia saa nne usiku, mume wa Rosana alikuwa bado hajarudi na hapo ndipo alipoambia watoto walale wakati hawakuwa wamepata riziki.

Mume wa Rosana alirejea usiku mwingi wakati kila mmoja alikuwa amelala.

Rosana hakusikia wakati anapoingia lakini alishtukia mtu akimwilika kwa tochi akiwa ndani ya blanketi.

"Nakumbuka siku hiyo, nilipojilaza pale chini sikupata usingizi mara moja. Niligaragara sana lakini mwisho wa siku nililaia upande wa kulia na wa kushoto ukawa juu, mtoto wangu mdogo akiwa upande wa chini," Rosana anasema.

Kufumba na kufumbua, kabla ya Rosana kuelewa nini kinachoendelea akiwa bado yuko chini, aliuliza ni nani anayemwilika tochi. Na hivyo ndivyo Rosana alivyokumbana na jinamizi lililokuwa likimsubiri.

"Nilikuambia nitakuua na nikuue tuende pamoja. Kusikia ni yeye wakati ameenua panga na akilini kikakumbuka kweli, alibeba panga wakati anaondoka. Nikajua tu sasa leo ndio ninakufa, hakuna siku nyingine," Rosana anasema.

Rosana anaongeza kuwa mkono aliokuwa ameuenua ili kujikinga na mwanga wa tochi, ndio alioanza kuukata na panga. Hadi wa leo, mkono wa kushoto wa Rosana umelemaa.

Wakati Rosana ameanza kupiga kelele ili kuashiria kwa majirani kuwa kwake sio salama na anahitaji usaidizi. Mume wake alirusha panga sehemu nyingine ya mwili.

"Alinikata kuanzia hapa juu ya jicho hadi chini yake, Nilipogeuka, akataka kunikata na panga jicho la pili lakini likaingia upande ule ule wa kwanza, Rosana anasema.

Hivi ndivyo Rosana alivyopoteza jicho lake. Lakini uhasama wa mume wake haukuishia hapo. Aliendelea kumshambulia kwa panga kichwani na shingoni kwa nyuma. Akarusha panga jingine kwenye kiuno, mguuni na kila alipoweza kurusha silaha aliyokuwa nayo alifanya hivyo.

"Wakati nilipoanza kupiga mayowee, mtoto ambaye alikuwa chini ya ubavu wangu, alianza kunywa damu iliyokuwa inanitiririka kwa sababu nilikuwa naye sako kwa bako," Rosana anakumbuka.

Watoto wake pia nao waliamka na kuanza kupiga mayowe ili kumsaidia mama yao. Na punde si punde majirani wakaanza kumiminika.

"Wakati majirani wanaingia, mume wangu alitoroka mbio hadi kwa jirani wa mbali kidogo ambaye hakuwa amepata taarifa ya kilichotokea. Aliomba sehemu ya kulala usiku ule akidai kuwa asubuhi alitaka kurauka kwende sehemu ya mbali kidogo. Lakini asubuhi ilipofika, wenyeji walishikwa na butwaa walipomuona akiwa ananing'inia juu ya mti wa mkadamia, tayari amejitia kitanzi," Rosana anasema hivyo ndivyo mume wake alivyojitoa uhai.

Rosana alipoteza fahamu na kukimbizwa hospitali na majirani zake waliokuwa wamekuja kumuokoa.

Lakini kipindi hicho hicho, mtoto wake mdogo aliyekuwa amelala naye, pia alipelekwa hospitali kwa sababu tumbo lake lilianza kufura kutokana na damu ya mama yake aliyokuwa amekunywa wakati wa tukio.

Watoto wa Rosana walipelekwa kwa wazazi wake kipindi yeye yuko hospitali akipigania maisha yake.

Rosana anasema baadhi ya matibabu aliyopata akiwa kwenye chumba cha wangonjwa mahututi ni pamoja na kufanyiwa upasuaji wa kutolewa jicho ambalo lilikatwa na mume wake kwa sababu tayari lilikuwa limeoza na kuanza kunuka.

"Nilikuwa kwenye chumba cha wagonjwa kwa miezi mitatu bila kukaa,kula wala kuzungumza," anasema Rosana.

Rosana alikuwa anapewa vinywaji tu kwa kutumia mirija.

.

Alichojifunza

.
Maelezo ya picha, Rosana Kathure

Rosana anasema pengine pale alipokosea ni kukubali penzi la mume wake.

"Kama ningejua naolewa na mtu ambaye atanikata jicho langu na mkono wangu hivi, niwe sina mkono wa kujitafutia, nisingeolewa. Niliambiwa nakupenda na mimi nikasema nakupenda pia. Ndio maana nina alama kila sehemu mwilini mwangu," Rosana anasema.

Anatoa ushauri wake kwa mwanamke ambaye anapitia ukatili katika ndoa kama alivyopitia yeye.

"Kama unamuheshimu mume wake ambaye naye anakuja akiwa mgomvi kama wangu, uwe mpole na uondoke taratibu bila kusema chochote kwa sababu ukimwambia, utakatwa shingo. Muache mume wako hapo, na uende kwenu.

"Heri ukae bila kuolewa kuliko mtu akuoe na akukate shingo na uuawe au utiwe alama na ufanywe kiwete kama mimi," Rosana anamalizia.

Rosana alikuwa hospitalini kwa takriban miaka miwili na miaka mingine miwili hadi kuanza tena kutembea dede.

Rosana anasema angekuwa na uwezo duniani angehakikisha wasichana wanayapata masomo yao kipau mbele.

"Laiti ningejua, kile ambacho ningekifanya kwa njia bora zaidi katika maisha yangu, ningemaliza shule kwanza kabla ya kujiingiza katika mapenzi," Rosana anasema.

Ujumbe alionao kwa wanaoshambuliwa na waume zao ni upi?

"Kama ningejua, ningemuacha mume wangu taratibu badala ya kumpigia makele. Pengine hata ningeenda kwa wazazi wangu kwanza kwa ajili ya kutuliza hasira," Rozana anasema.

Lakini kwa miujiza ya Mungu, sasa Rosana amepona na la msingi zaidi alimsamehe mume wake kwa yote aliyomtendea.