Moja kwa moja, Kulenga miundombinu ya kiraia ni uhalifu wa kivita - Balozi wa Iran katika UN

Balozi huyo wa Iran pia alionya kwamba iwapo Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama havitachukua hatua madhubuti, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki yake, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ya kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kulinda mamlaka yake.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Ujerumani yaripoti kuongezeka kwa vitisho vya kiusalama

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Waziri wa usalama wa Ndani wa Ujerumani ameonya kuhusu kuongezeka kwa vitisho vya kiusalama na kusema kuwa amepandisha kiwango cha tahadhari ya usalama nchini humo hadi cha "juu zaidi"; hali ambayo inaashiria kuwa shambulio linaweza kutokea wakati wowote.

    Katika mahojiano na gazeti la *Welt am Sonntag*, Alexander Dobrynt alisema kuwa kuna "ushahidi wa wazi" wa kuwepo kwa mipango ya kushambulia watu, miundombinu, na taasisi za serikali nchini Ujerumani.

    Aliongeza kuwa chanzo cha vitisho hivyo kiko nje ya Ujerumani, lakini hakutoa maelezo zaidi.

  2. Serikali ya Kenya yakabiliana na wadukuzi wa Tovuti rasmi ya Rais

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Kenya imesema kwamba imechukuwa hatua za dharura kupambana na udukuzi dhidi ya tovuti rasmi ya Rais William Ruto.

    Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mchana wa Jumamosi Julai 18, Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa dijitali William Kabogo amesema kwamba wataalamu wamechukuwa hatua mwafaka za kudhibiti hali na kuwazuia wadukuzi kutekeleza hasara kubwa.

    "Kwa wakati huu, hakuna ushahidi kwamba wenye kutekeleza uhalifu huo wamepata taarifa au data muhimu za serikali wala hakuna data ambayo imevuja wala kupotea. Mifumo ya serikali kwa pamoja na shughuli za kidijitali za serikali ziko salama na zinaendelea kama kawaida," alisema Waziri Kabogo.

    Mamlaka ya kusimamia mawasiliano ya teknolojia {ICT AUthority} nchini Kenya imeripotiwa kushirikiana na taasisi husika za serikali kwa pamoja na kampuni za teknolojia zinazoshirkiana na serikali ya Kenya kufanya uchunguzi wa kina kupata tathmini ya kina kuhusu kiwango cha hasara ambacho huenda kimefanywa na wadukuzi hao.

    Tovuti ya Rais wa Kenya: https://www.president.go.ke: ilidukuliwa mapema Jumamosi hii huku wadukuzi wakiitaka serikali ya Kenya kuwalipa takriban shilingi milioni 41 za Kenya sawia na shilingi milioni 890 za Tanzania kabla ya kurejesha tovuti hiyo mikononi mwa serikali.

    Hii si mara ya kwanza ya tovuti za serikali ya Kenya kudunguliwa na wahuni, mara ya mwisho, wadukuzi walilenga huduma muhimu za serikali kama vile E-citizen ambayo inatumika kwa malipo yote rasmi ya huduma za serikali.

    Soma Zaidi Hapa:

  3. Iran: Siasa ya "vita na mazungumzo kwa pamoja" imefikia mwisho

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mohsen Rezaei mshauri wa kijeshi wa kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa sera ya 'mazungumzo na vita kwa wakati mmoja' imefikia mwisho.

    Alisema: "Ikiwa Wamarekani wataendelea na mapigano katika siku mbili au tatu zijazo, tutaingia katika awamu ya operesheni kamili ya kukera na kuharibu."

    Haya yanajiri huku maeneo mengine ya kusini mwa Iran yakikumbwa na mashambulizi ya anga ya Marekani jana usiku, usiku wa saba wa mapigano kati ya Iran na Marekani. Iran ilitangaza kuwa Kuwait, Bahrain, Jordan na Saudi Arabia zimeishambulia.

    Katika upande mwingine, ofisi ya rais wa Lebanon imetangaza kuwa Rais Joseph Aoun wa nchi hiyo ameondoka leo Beirut na kuelekea Washington.

    Anatarajiwa kukutana na Donald Trump wakati wa safari hii na kujadili "kujiondoa kwa Israeli kutoka kwa maeneo yanayokaliwa kwa sasa na Israeli."

    Nchini Iran, msemaji wa idara ya mahakama ametangaza kuwa kesi imewasilishwa dhidi ya Reza Pahlavi.

    Soma Zaidi

  4. Katika Picha: Rais wa Misri akikagua Gwaride la Jeshi la Tanzania

    .

    Chanzo cha picha, IKULU

    Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi akikagua Gwaride rasmi la Mapokezi lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Julai Juni, 2026.

    .

    Chanzo cha picha, IKULU

    .

    Chanzo cha picha, IKULU

  5. Maghala ya biashara ya mtandaoni Urusi yashambuliwa na Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, social media

    Maelezo ya picha, Video imeonyesha moto mkubwa ukiwaka katika bohari la kuweka bidhaa

    Watu saba wameuawa na wengine 49 kujeruhiwa baada ya ndege zisizo na rubani za Ukraine kushambulia maghala mawili ya kuhifadhi bidhaa yanayomilikiwa na kampuni kubwa zaidi ya Urusi ya biashara ya mtandaoni, Wildberries, kulingana na maafisa wa Urusi.

    Vifo vyote na majeruhi 25 kati ya hao yalitokea katika ghala moja jijini Tambov, takriban maili 295 (kilomita 475) kusini-mashariki mwa Moscow. Majeraha mengine 24 yalitokea katika ghala jingine la Wildberries huko Elektrostal, katika eneo la Moscow.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema mashambulizi hayo yalilenga "vituo muhimu vya usafirishaji na ugavi" ambavyo vilikuwa vikitumika "kusambaza vipengele vilivyowekewa vikwazo kwa ajili ya utengenezaji wa ndege zisizo na rubani na vifaa vya urambazaji".

    Aliongeza kuwa Ukraine pia ilishambulia maeneo lengwa katika Bahari ya Azov, Bahari Nyeusi, na Crimea, eneo lililochukuliwa na Urusi.

    Zelensky alisema operesheni za Ukraine zilikuwa majibu dhidi ya "mashambulizi ya Urusi kwenye miundombinu yetu ya kiraia na kwenye miji na jamii zetu". Katika usiku wa kuamkia Jumatano, watu 14 waliuawa katika mashambulizi ya Urusi kote Ukraine.

    Wildberries mara nyingi huchukuliwa kama kampuni ya Urusi inayolingana na Amazon. Kundi la RWB lililoundwa kwa kuunganisha Wildberries na kampuni ya matangazo ya Russ, lilikadiriwa kuwa na thamani ya takriban dola bilioni 12.6 (pauni bilioni 9.3) na jarida la Forbes Russia.

    Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wildberries, Tatyana Kim, alisema ulikuwa "usiku wa kutisha" kwa Urusi na kwa kampuni hiyo.

    "Watu saba waliokuwa wakifanya kazi zamu ya usiku walifariki papo hapo," gavana wa eneo la Tambov, Evgeniy Pervyshov, aliandika kwenye Telegram, akiongeza kuwa ndege zisizo na rubani 28 pia zilidunguliwa wakati zikikaribia eneo hilo.

    Wakati huo huo, gavana wa eneo la Moscow, Andrei Vorobyov, alisema baadhi ya watu waliojeruhiwa katika mashambulizi kwenye ghala la Wildberries huko Elektrostal walikuwa katika "hali mbaya".

    Aliongeza kuwa jumla ya ndege zisizo na rubani 48 zilidunguliwa katika eneo la Moscow usiku huo, na kwamba ghala la mafuta la Urusi pia lilishambuliwa na ndege isiyo na rubani iliyoanguka, tukio ambalo alilielezea kuwa lenye "madhara makubwa zaidi".

    "Wazima-moto, huduma za dharura, na Wizara inayosimamia shughuli za udhibiti wa hali za dharura wanaendelea kufanya kazi katika eneo la tukio," aliandika kwenye Telegram.

    Hakuelezea kwa kina kiwango cha uharibifu. Zelensky alithibitisha kivyake kuwa Ukraine ilishambulia "kituo cha mafuta".

    Soma Zaidi:

  6. Tumezuia na kudungua makombora kumi ya Iran - Jordan

    Jeshi la Jordan linasema kuwa mifumo ya nchi hiyo ya ulinzi wa anga ilizuia na kutungua makombora kumi yalioingia kwenye anga ya Jordan kutoka Iran.

    Aidha Jeshi hilo pia lilisema katika taarifa kwamba hakuna vifo au majeraha wala hasara ya kifedha iliyosababishwa na mashambulizi hayo.

    Soma Zaidi:

  7. Tovuti Rasmi ya Rais Ruto yadukuliwa

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Tovuti rasmi ya Rais William Ruto imedukuliwa, na ukurasa wake wa mwanzo umeharibiwa kwa kuwekwa ujumbe unaomlenga Rais na kudai malipo ya fidia kwa njia ya Bitcoin.

    Ukaguzi uliofanywa na Kenyans.co.ke kwenye ukurasa wa mwanzo wa tovuti hiyo (president.go.ke) ulionyesha kuwa maudhui rasmi yalikuwa yameondolewa na badala yake kuwekwa ujumbe wa dharau unaomlenga Mkuu wa Nchi.

    Ukurasa huo ulionyesha madai dhidi ya Ruto, anwani ya mkoba wa sarafu ya kidijitali (cryptocurrency wallet) na agizo la malipo, huku wadukuzi hao wakitishia kutoa taarifa ambazo hazikutajwa iwapo matakwa yao hayatatimizwa.

    "Huu ni ujumbe wa tatu kwako; kabla hatujavujisha kila kitu kukuhusu. Fanya malipo ya Bitcoin 5 kwenye mkoba wa Bitcoin... Ikiwa unataka amani kabla ya saa kumi na mbili jioni hii," ujumbe huo kwenye ukurasa ulioharibiwa ulisema.

    Katika taarifa fupi kwa chapisho hili siku ya Jumamosi, Julai 18, Ikulu ya Serikali ilithibitisha kuwa ilikuwa inajua kuhusu udukuzi huo na kusema timu yake ya TEHAMA ilikuwa ikishughulikia suala hilo.

    Ikiwa Ikulu ya Serikali itaheshimu mahitaji ya fidia, hesabu zetu zinaonyesha kuwa Hazina italazimika kulipa Ksh 41,337,872.40 sawia na dola laki tatu za Marekani na shilingi 838,605,411.25 za Tanzania. Hii inatokana na kiwango cha ubadilishaji ambapo BTC 1 inafanya biashara kwa takriban Ksh 8,267,574.48.

    Wadukuzi walibadilisha bango la tovuti, wakionyesha ujumbe uliorejelea majina ya watu watatu huku chapa rasmi ya Ikulu ikiendelea kuonekana nyuma.

    Tukio hilo limeibua wasiwasi kuhusu usalama wa miundombinu ya kidijitali ya serikali, kwani bado haijulikani wazi ikiwa uvujaji huo uliwekwa kwenye ukurasa wa mbele wa tovuti au ulienea kwenye mifumo yake ya nyuma.

    Tukio la hivi karibuni si mara ya kwanza tovuti za serikali ya Kenya kulengwa katika shambulio la mtandaoni.

    Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, tovuti kadhaa zinazomilikiwa na wizara na mashirika ya serikali, ikiwa ni pamoja na Afya, Elimu, Kazi, Mazingira, TEHAMA, Utalii, Mambo ya Ndani na Ikulu, ziliathiriwa katika shambulio lililoratibiwa.

    Washambuliaji waliharibu tovuti zilizoathiriwa kwa kubadilisha maudhui rasmi na jumbe zisizoidhinishwa na kufanya milango kadhaa ya serikali isipatikane.

    Usumbufu huo uliathiri huduma muhimu za mtandaoni zinazotegemewa na umma, huku baadhi ya tovuti zikionyesha kauli mbiu kali na maudhui mengine yasiyoidhinishwa.

    Hata hivyo, Wizara ya Ulinzi na Hazina ya Kitaifa zilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoripotiwa kutoathiriwa na shambulio hilo la mtandaoni.

    Pia Unaweza Kusoma:

  8. Shirika la ndege la Kuwait labadilisha ratiba ya safari zake nyingi za ndege

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika la ndege la Kuwait limetangaza siku ya Jumamosi kuwa limebadilisha ratiba ya safari nyingi za ndege kutokana na kusitishwa kwa muda kwa shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuwait kufuatia mashambulizi ya makombora ya Iran na ndege zisizo na rubani.

    Shirika hilo la ndege hapo awali lilikuwa limesema kuwa mabadiliko ya ratiba ya safari ya ndege hiyo yalitokana na kufungwa kwa anga ya Kuwait.

    Kuwait ilitangaza saa chache zilizopita kwamba imegundua na kunasa makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani katika anga lake.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Kituo cha kuondoa chumvi kwenye maji chaharibiwa kabisa Iran

    .

    Chanzo cha picha, Tasnim

    Maelezo ya picha, Picha ya uharibifu wa kiwanda cha kusafisha maji cha Bunji huko Jask

    Abdul Hamid Hamzapour, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka ya Mkoa wa Hormozgan, amesema kuwa kutokana na shambulio la Marekani kwenye kituo cha kusafisha maji cha Bunji magharibi mwa wilaya ya Jask, usambazaji wa maji ya kunywa kwa wakazi wapatao 10,000 wa vijiji takriban 20 umetatizika kabisa, na watu wa vijiji hivyo wamekabiliwa na uhaba wa maji.

    Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, mashambulizi hayo yaliharibu kabisa kituo cha kusukuma maji ghafi kutoka baharini, pamoja na transfoma ya umeme ya kiwanda cha kusafisha chumvi cha Bunji, kilichokuwa na uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 3,150 za maji mchana na usiku.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Argentina VS Uhispania: Ni kikosi kipi chenye safu kali ya ushambulizi kufunga mabao?

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Lionel Messi anashiriki michuano ya tatu ya kombe la dunia huku Michuano ya 2026 yakiwa ya kwanza kwa Lamine Yamal kushiriki.

    Zimesalia chini ya saa 36 kabla ya dunia kujuwa ikiwa Argentina watahifadhi taji lao au Uhispania itakuwa Bingwa wa Kombe la Dunia baada ya kushinda mwisho mwaka wa 2010 nchini Afrika Kusini.

    Na kabla ya kutinga Fainali, timu hizi mbili zilikabiliwa na kibarua kigumu.

    Kikosi cha Argentina kimejizolea jumla ya mabao 19 katika michuano ya mwaka huu, idadi kubwa ambayo wataalamu wanasema imetokana na uwezo wao mkubwa wa kushambulia goli na kufunga mabao.

    Messi na wenzake wamefunga angalau mabao mawili katika kila moja ya mechi 13 ambazo wameshiriki, tangu kupoteza mechi yao dhidi ya Saudia Arabia 2-1 kwenye mechi yao ya kwanza katika michuano yaliyoandaliwa Qatar miaka minne iliyopita.

    Na japo Uhispania imerusha makombora makali upande wa goli, safu yake ya ushambulizi imepenya na kufunga mabao sita pekee, huku wataalamu wakisema kwamba mchezo wao ni wa kadri.

    Katika mechi zao, Uhispania imekuwa na nafasi kadha nzuri za kufunga mabao ila hazikutumika vyema.

    Nao Argentina wamefunga bao moja tu ndani ya boxi ila mengine yote makali zaidi yamefungwa nje ya eneo hilo, huku wakifunga mabao matano kutoka mbali huku Uhispania ikikosa kufanya hivyo katika mechi zake.

    Uhispania imefunga mabao sita chini ya idadi ya Argentina, ila wamefungwa mabao macheche hadi sasa – katika mechi ya robo fainali ambapo walifungwa bao moja na Ubelgiji, walishinda kwa mabao mawili dhidi ya Ubelgiji.

    Argentina huenda wakijiona wamekosa kuwa na Bahati kwani wamefungwa mabao saba katika michuano ya mwaka huu, huku timu tatu pekee zikilinda goli lao dhidi ya mashambulizi na kutofungwa mabao mengi.

    Lakini hata kama safu ya ulinzi ya Argentina imewahi kufanya vyema kuliko ilivyo kwa sasa, Uhispania imejitokeza kuwa katika kiwango bora cha mchezo.

    Bila shaka, hata baada ya kucheza mechi zaidi ya 44, Uhispania bado ina kiwango kidogo cha tishio dhidi ya safu yake ya ulinzi kutokana na kufungwa hilo bao moja na Ubelgiji huku timu ya pili ambayo haikufungwa mabao mengi katika awamu ya makundi ikiwa Uruguay.

    Soma Zaidi Hapa:

  11. Balozi wa Iran katika UN: Kulenga miundombinu ya kiraia ni uhalifu wa kivita

    ,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa "amelaani vikali" mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu ya raia wa Iran katika barua kwa Baraza la Usalama.

    Amir Saeed Irwani alisema kuwa mashambulizi ya mara kwa mara kwenye maeneo ya raia, hasa barabara na mitandao muhimu ya usafiri wa reli inachukuliwa kuwa "uhalifu wa kivita."

    Balozi huyo wa Iran pia alionya kwamba iwapo Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama havitachukua hatua madhubuti, "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki yake, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ya kuchukua hatua zote zinazohitajika ili kulinda mamlaka yake, ukamilifu wa mipaka yake, watu wake na maslahi yake muhimu."

    Soma Zaidi:

  12. Matukio yakuvutia katika michuano ya Kombe la Dunia 2026

    • “Patrice Lumumba” – shabiki wa DRC alisimama kama sanamu kushabikia ‘Leopards’
    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mechi 104 zinatarajiwa kukamilika usiku wa Jumapili Julai 19 ambapo mbivu na mbichi itajulikana wazi kuhusu ni nani Bingwa wa Kombe la Dunia katika Soka mwaka huu wa 2026.

    Na huku Lamine Yamal wa Uhispania akijiandaa kukabiliana na mmoja wa wachezaji bora duniani Lionel Messi, wengi watakumbuka mengi yaliyotokea kwenye maeneo ya mashabiki kuketi, au hata nje ya uwanja lakini yalikuwa na uhusiano mkubwa na kabumbu iliyokuwa ikisakatwa.

    Haya hapa matukio yaliyowavutia wengi hasa kwenye mitandao ya kijamii:

    “Patrice Lumumba”, Shabiki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Michel Kuka Mbolandinga anayefahamika kama ‘Lumumba Vea – au sanamu iliyohai,’ alikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki waliokuwa uwanjani na hata waliomtazama kwenye mitandao ya kijamii hasa wakati ambapo timu ya taifa ya DRC ilipokuwa ikicheza mechi zao za makundi, awali kwenye michuano ya mwaka huu.

    Alipigwa picha akiwa amesimama bila kusonga kwa muda wote ambao mechi zilikuwa zikichezwa, akiwa ameinuwa mkono wake wa kulia na akiwa amevalia suti yenye rangi za bendera ya taifa hilo.

    Hatua hiyo inafanana na sanamu ya kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Patrice Lumumba ambayo ipo katika mji mkuu Kinshasa.

    2: Ndugu mdogo wa Lamine Yamal avutia wengi

    Mtangazaji wa soka wa BBC Kelly Cates alimtaja kijana huyo mdogo kama mtoto mrembo aliyewavutia wengi kwa uzuri wake. Mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu – Keyne – ni kaka yake mdogo mshambulizi wa Uhispania Lamine Yamal – mwenye umri wa miaka 19.

    Na japo ndugu yake mkubwa ni mchezaji maarufu wa Klabu ya Barcelona nchini Uhispania, Keyne amejipatia umaarufu wa aina yake aliporekodiwa akijaribu kucheza mchezo wa gofu, na kukerwa na kutokuwa na uwezo wa kuupiga mpira vyema miongoni mwa mambo mengine.

    Katika mechi kati ya Ubelgiji na Uhispania, kijana huyo mdogo alipigwa picha ya video akiwa amepakatwa huku akitabasamu kwa kuwa Uhispania ilikuwa imefuzu kuendelea mbele baada ya kuicharaza Ubelgiji.

    .

    3. Haaland na Bellingham wakijitokeza kama marafiki

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Licha ya kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England kwa misimu kadhaa, Erling Haaland anaonekana hakuwa amepata umaarufu mkubwa nchini Marekani na Canada hadi sasa.

    Hata hivyo, mambo yalibadilika kabisa msimu huu wa kiangazi baada ya mitandao ya kijamii kumuenzi mshambuliaji huyo wa Norway na Manchester City kupitia wimbi la 'meme' zilizotawala TikTok na Instagram, na kumjengea kile kilichoonekana kama ulimwengu wa kipekee mtandaoni.

    Kulikuwa na mengi ya kuvutia mashabiki, huku Haaland akionekana pamoja na mwigizaji Channing Tatum. Baadaye akafunga mabao saba, akapata maelfu ya wafuasi wapya kwenye mitandao ya kijamii.

    Erling Haaland na Jude Bellingham wakikumbatiana baada ya England kuibuka na ushindi dhidi ya Norway mjini Miami.

    IShowSpeed

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mwanamitandao maarufu IShowSpeed, anayejulikana kwa kuruka sarakasi za nyuma (backflips), kubweka kwa utani na kuvaa jezi zilizogawanywa rangi mbili, atatumbuiza kwa wimbo wake wa (World Cup) Champions katika sherehe ya kufunga mashindano kabla ya fainali ya Jumapili.

    Mshawishi huyo wa mitandao ya kijamii ambaye pia hurusha matangazo yake moja kwa moja amekuwa mmoja wa watu walionufaika zaidi na Kombe la Dunia la mwaka huu, akiongoza vipindi vya kutazama mechi mubashara mtandaoni akiwa ndani ya viwanja wakati wa michezo.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Kombe la Dunia: Marekani yatetea bango la wachezaji wa Argentina

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ikulu ya Marekani imetetea timu ya taifa ya Argentina baada ya wachezaji wake kuonyesha bango lililoandikwa "Las Malvinas son Argentinas" ("Visiwa vya Falklands ni vya Argentina") kufuatia ushindi wao dhidi ya England katika nusu fainali ya Kombe la Dunia.

    Hatua hiyo imekosolewa na Uingereza huku Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) likitatarajiwa kuchukua hatua za kinidhamu.

    Andrew Giuliani, mkuu wa kikosi kazi cha FIFA cha Ikulu ya Marekani, amesema wachezaji hao walikuwa wakitumia haki yao ya uhuru wa kujieleza chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani walipokuwa nchini humo, kwa mujibu wa BBC.

    Bango hilo linarejelea madai ya muda mrefu ya Argentina kuhusu visiwa vilivyoko kusini mwa Bahari ya Atlantiki, vinavyojulikana kwa Kiingereza kama Falkland Islands na kwa Kihispania kama Las Malvinas.

    Serikali ya Uingereza imekosoa kitendo hicho, huku Ikulu ikisisitiza kwamba Visiwa vya Falklands "kwa hakika ni" vya Uingereza na kuunga mkono wito wa FIFA kuchunguza iwapo bango hilo lilikiuka kanuni za shirikisho hilo zinazokataza kauli za kisiasa wakati wa mechi.

    Serikali ya Visiwa vya Falklands pia imeeleza kusikitishwa kwake na kuitaka FIFA kuichukulia hatua timu ya Argentina, ikisema haitaki kutumiwa kama "mpira wa kisiasa".

    Soma Zaidi:

  14. Tumelenga kituo cha Marekani na madaraja kadhaa nchini Bahrain - Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Iran limetangaza kwamba katika awamu ya kumi na tano ya Operesheni "Shine", limelenga "maeneo ya ndege pamoja na matangi ya mafuta, katika kituo cha Sheikh Issa nchini Bahrain" kwa kutumia ndege zisizo na rubani za kujilipua.

    Taarifa hiyo pia ilidai kwamba madaraja kadhaa nchini Bahrain yalilengwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani. Hata hivyo, si maafisa wa Bahrain wala Marekani hakuna ambaye ametoa maoni juu ya kiwango cha uharibifu au uwezekano wa kuwepo kwa majeruhi.

    Soma Zaidi:

  15. Mwanaharakati wa India aliyegoma kula kwa siku 20 apelekwa hospitalini kwa nguvu

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanaharakati na msomi wa India Sonam Wangchuk, ambaye alikuwa kwenye mgomo wa kula kwa siku 20 zilizopita huko Delhi, ameondolewa kwa nguvu kutoka eneo lake la maandamano.

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 59 alikuwa akiandamana kuunga mkono harakati za kejeli mtandaoni zinazoitwa Cockroach Janta Party (CJP) zinazotaka mageuzi ya kielimu. Waandamanaji walikuwa wamepanga maandamano hadi bunge la India siku ya Jumatatu.

    Wangchuk alikuwa amegoma kula chakula wakati wa kiangazi chenye joto kali, huku akila chumvi na maji tu. Alikuwa amepunguza uzito zaidi ya kilo 9 na alikuwa na maumivu makali.

    Mwanzilishi wa CJP Abhijeet Dipke sasa ameanza mfungo usiojulikana badala yake. Anasema maandamano ya kuelekea bungeni yataendelea na amemtaka Waziri Mkuu Narendra Modi ajiuzulu.

    Dipke aliambia BBC kwamba alikuwa ameenda nyumbani kwa rafiki yake asubuhi ili kupumzika wakati polisi walipofika na kukataa kumruhusu aondoke.

    Video kutoka kwenye tovuti ya maandamano siku ya Jumamosi zilionyesha machafuko yakizuka kabla tu ya saa 1:30 kwa saa za huko (02:00 GMT) wakati polisi kadhaa na wanajeshi walipoingia ghafla kwenye jukwaa ambalo mwanaharakati huyo alikuwa amelala. Waandamanaji waliojaribu kuwazuia walisukumwa mbali.

    Walimfunika kwa mapazia ya shuka kabla ya kumtoa jukwaani. Dakika chache baadaye, ambulensi ilionekana ikiondoka kwa kasi.

    Mke wa mwanaharakati huyo Gitanjali Angmo baadaye alichapisha kwenye mtandao wa X kwamba alikuwa "katika hospitali ya Safdarjung ambapo amelazwa".

    Soma Zaidi:

  16. Marekani yaishambulia Iran kwa usiku wa saba mfululizo

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi kwa usiku wa saba mfululizo dhidi ya Iran tangu Rais Donald Trump atangaze makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda "yamefutiliwa mbali".

    Katika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa X, Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) iliandika kwamba vikosi vyake "vimeshambulia maeneo ya uchunguzi, miundombinu ya vifaa vya kijeshi, maghala ya silaha yaliyopo chini ya ardhi, na uwezo wa kijeshi wa majini".

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilisema meli mbili za mafuta zililipuka katika Mlango-Bahari wa Hormuz wakati zikipita kwenye sehemu ya njia ya meli iliyokuwa na mabomu ya ardhini. Taarifa hiyo ilipuuzwa na Hata hivyo, Centcom ilisema kuwa taarifa hiyo si ya kweli.

    Vikosi vya kijeshi vya Jordan vilisema vilidungua makombora 10 ya Iran yaliyorushwa kwenye anga yake usiku huo, ingawa hakukuwa na majeruhi wala uharibifu wowote.

    Centcom ilisema kuwa ilimaliza mashambulizi yake saa 21:30 kwa saa za Marekani Mashariki (02:30 BST) baada ya kufanya mashambulizi hayo kwa muda wa saa kadhaa.

    Katika taarifa yake, Centcom ilisema: "Vikosi vya Marekani vilitumia ndege za kivita, ndege zisizo na rubani, na meli za kivita pamoja na vifaa vingine katika operesheni hiyo."

    Shirika la habari la serikali ya Iran, Fars, lilisema meli mbili za mafuta "zililipuka na kushika moto wakati zikipita kwenye njia iliyokuwa na mabomu ya ardhini kusini mwa Mlango wa Hormuz". Baadaye, Centcom iliandika kwenye X: "Kama madai mengi ya IRGC, hii si kweli."

    Usafirishaji wa meli katika Mlango muhimu wa Hormuz umesitishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kuendelea kwa mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya vikosi vya Marekani na Iran.

    Soma Zaidi:

  17. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara tarehe ni 18/07/2026.