Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vyakula vya rangi tofauti: Siri ya lishe bora na afya njema
Kula vyakula vya rangi mbalimbali kunaweza kusaidia kuimarisha afya ya akili, kuboresha ustawi wa mwili na kupunguza hatari ya magonjwa mbalimbali, ikiwemo yale ya moyo.
Kila siku, watu hufanya maamuzi kuhusu aina ya chakula watakachokula kulingana na upatikanaji, gharama na mapendeleo binafsi. Hata hivyo, swali muhimu hubaki: tunawezaje kuhakikisha tunapata virutubishi vyote muhimu kutoka kwenye chakula tunachokula?
Wataalamu wa lishe wanasema njia moja rahisi ya kuhakikisha mwili unapata virutubishi vya kutosha ni kula vyakula vya rangi tofauti, vinavyowakilisha rangi mbalimbali za upinde wa mvua. Rangi za matunda na mboga mara nyingi huashiria uwepo wa virutubisho na kemikali asilia zinazotoa manufaa tofauti kwa afya.
Dhana hiyo inaonekana wazi katika lishe ya Mediterania, ambayo inajumuisha matunda mengi, mboga, nafaka zisizosindikwa na mafuta yenye afya. Lishe hii imekuwa ikitajwa mara kwa mara na watafiti kama miongoni mwa lishe zenye manufaa makubwa kwa afya.
Kwa mujibu wa Profesa Francesco Sofi wa Chuo Kikuu cha Florence nchini Italia, kufuata lishe ya Mediterania kunamaanisha kupata aina mbalimbali za virutubisho, ikiwemo phytonutrients.
"Kula mlo wa Mediterania kunamaanisha kuwa unapata virutubisho vya aina mbalimbali, pamoja na phytonutrients," anasema Sofi.
Phytonutrients ni kemikali asilia zinazopatikana kwenye mimea ambazo husaidia mwili kutumia virutubisho kwa ufanisi na kulinda seli dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na sumu au uchakavu wa mwili.
Hata hivyo, Sofi anasema lishe ya Mediterania haihusishi kila wakati rangi zote za upinde wa mvua, kwa kuwa mara nyingi hutegemea vyakula vya msimu na vinavyopatikana katika maeneo husika. Watu wanaofuata lishe hiyo pia huwa na tabia ya kula mazao yanayolimwa karibu nao au kwenye bustani zao wenyewe.
Anabainisha kuwa utofauti wa rangi katika lishe hiyo hauko mbali sana na unaopatikana kwa watu wanaofuata lishe inayojikita zaidi kwenye vyakula vya mimea.
Sababu nyingine inayofanya lishe ya Mediterania ihusishwe na afya bora ni namna chakula kinavyoandaliwa. Kwa mujibu wa Sofi, mboga nyingi huchemshwa au kupikwa kwa njia rahisi badala ya kukaangwa, jambo linalosaidia kuhifadhi virutubisho muhimu vilivyomo kwenye vyakula hivyo.
Mtu anafaa kuzingatia kula mboga na matunda mengi, kwani inasaidia kuimarisha afya ya akili na moyo, hii ni kulingana na mtaalam wa lishe Deanna Minich,kutoka chuo kikuu cha Western States, jimbo la Oregon Marekani.
Kula chakula chenye rangi nyingi humsaidia mtu kupata madini yote muhimu yanayohitajika mwilini.
"Iwapo utakosa rangi ya upinde wa mvua, basi utakuwa hauli virutubishi muhimu vya chakula hicho," anasema Minich.
Hii ni kwasababu vyakula vya mimea vina phytonutrients, carotenoids, flavonoids na uwezo wa kupunguza uvimbe mwilini. Na mimea yenye rangi tofauti huwa na manufaa tofauti.
Vyakula vyenye rangi ya samawati au zambarau ikiwemo matunda aina ya blueberry ina virutubisho asili vya mimea aina ya anthocyanin ambayo huhusishwa na kupunguza hatari ya kupata maradhi ya moyo, na ugonjwa wa kisukari.
Virutubishi vya Flavones ambavyo huipa chakula rangi ya manjano hupunguza hatari ya kupata maradhi ya moyo.
Kuna tafiti zinaonyesha kuwa virutubisho vya flavonoids huimarisha afya ya akili kwa kuzuia aina ya sumu ambayo huingia kwenye akili na kusababisha ugonjwa unaoathiri kumbukumbu wa Alzheimer's.
Tian-shin Yeh, mtafiti wa magonjwa katika idara ya afya ya uma chuo kikuu cha Havard, alibaini kuwa wale wanaokula vyakula vilivyo na virutubishi vya flavonoid, ikiwemo machungwa,pilipili, balungi, figili si rahisi kupata ugonjwa wa kupoteza ufahamu na dementia.
Ingawa kwa sasa hakuna tiba ya dementia na kupoteza ufahamu katika maisha ya uzeeni, kula chakula kilicho na flavonoid hupunguza hatari ya kupata magonjwa hayo.
Kwa hivyo mtu anaweza anza kula milo hizo wakati wowote kama bado hajaanza.
Kula chakula chenye rangi nyingi, husaidia pia kukabiliana na athari ya kula chakula kingi cha aina moja.
Hata hivyo, Minich anasema kuwa vyakula vyenye rangi ya upinde wa mvua si tu matunda na mboga, kunavyo pia vyakula vingine vya kiasili kama mitishamba, viungo, jamii ya kunde, karanga, nafaka, na hata chai.
Pia anachukulia vyakula vya rangi nyeupe kuwa sehemu ya lishe ya upinde wa mvua, ikiwemo tofu, ambayo ina aina nyingi za isoflavones zinazohusishwa na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na baadhi ya magonjwa ya saratani, pamoja na kuzuia kupoteza ufahamu.
Kula chakula chenye rangi nyingi pia huchangia ulaji wa lishe yenye afya.
Ila wakati mwingine kula chakula chenye rangi nyingi kinaweza kumchochea mtu kula chakula kisichokuwa na afya.
Chakula kama Pizza kina rangi tofauti za kuvutia ambazo zinaweza kumshinikiza mtu kula chakula hiki kwa wingi.Kwa hivyo kula matunda na mboga kwa wingi kunasemakana kuwa njia bora ya kutopotoshwa na rangi zinazoongezwa kwa chakula kuipa mvuto, kama vile keki.
Kando na rangi, ladha ya chakula pia ni muhimu kuhakikisha unapata virutubish tofauti haswa phytonutrients.
Utafiti mmoja ulibaini kuwa wale waliokula mboga zilizo na ukali kwa muda wa wiki mbili, waliweza kupunguza shinikizo la damu kutokana na chakula hizo kuwa na fiber nyingi na virutubisho tofauti vya phytonutrients.
Kulingana na utafiti huo mboga za mizizi na kabeji zina antioxidants kwa wingi kama vile flavonoids, carotenoids na phytochemicals ambazo kwa pamoja huboresha maisha ya mtu.
"Rangi ya chakula ni muhimu kwa milo yetu, ila ladha yake ni muhimu sana, haswa chakula zenye ladha ya ukali kama sukuma wiki, celery na chai," anasema Minich ambaye anakubaliana na utafiti huo.
Kingine cha kuzingatia ni sehemu ipi ya mmea unakula.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliala na kuhaririwa na Ambia Hirsi