IRGC: Hatua dhidi ya meli zinazokiuka sheria hazitazuiliwa Lango la Hormuz pekee
Iran imeonya kuwa operesheni dhidi ya meli zinazokiuka sheria haitajikita katika Lango la Hormuz pekee, ikisisitiza kuwa vyombo vitakavyotumia njia ambazo hazijadhinishwa vitafuatiliwa na kuchukuliwa hatua popote katika eneo hilo.
Katika taarifa, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji la Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) imesema meli yoyote itakayopita katika njia ambayo haijaidhinishwa na Iran itafuatiliwa na kuchukuliwa hatua bila kusita.
Iran inasisitiza kuwa meli zote zinapaswa kutumia njia maalumu za usafiri wa majini zilizowekwa ili kupitia Lango la Hormuz.
Kauli hiyo imekuja huku ripoti zikieleza kuwa baadhi ya meli za mizigo na meli za kubeba mafuta zimeanza kutumia njia mbadala zilizobuniwa katika wiki za karibuni ili kuepuka vikwazo vilivyowekwa na Tehran.
Wakati huo huo, Iran imesema haitafungua Lango la Hormuz kwa muda wote ambao inadai Marekani inaendelea na kile ilichokiita kizuizi cha majini dhidi yake.
Hata hivyo, Marekani imesisitiza kuwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani iko wazi na salama, ikibainisha kuwa kiwango cha mafuta kinachopita katika lango hilo kimeongezeka ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia mzozo wa Iran.
Soma zaidi: