Baada ya ripoti ya Jaji Chande njia tatu zitakazoamua mustakabali wa Tanzania

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, chini ya Mwenyekiti Jaji Othman Chande imeibua mjadala mpana zaidi ya tukio la Oktoba 29. Badala ya kueleza tu kilichotokea, imefungua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa taifa, uwajibikaji wa taasisi za dola, na uwezo wa mfumo wa kisiasa kushughulikia migogoro ya kitaifa.

Katika mjadala huu, pande mbalimbali za kisiasa, wataalamu na wananchi wameanza kutoa mitazamo tofauti kuhusu kama ripoti hiyo ni hatua ya mbele au mwanzo wa mjadala mwingine tata zaidi. Je, itaiponya taifa ama itazidi kuleta mgawanyiko.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi anasema Serikali ina utashi na kama hakutakuwa na vitimbi, basi Tanzania itavuka salama.

Serikali kupitia CCM inaiona kama sehemu ya mchakato wa kuponya taifa, wakati upinzani hasa CHADEMA na baadhi ya wachambuzi wanaibua maswali kuhusu uhalali na uhuru wake.

Hali hii inaweka Tanzania katika kipindi cha maamuzi muhimu ya kisiasa, ambapo njia itakayochaguliwa inaweza kuamua mustakabali wa utulivu au mvutano wa baadaye.

Tanzania ya maridhiano na mageuzi

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jaji Chande akimkabidhi ripoti ya tume kwa Rais Samia

Iwapo mapendekezo ya tume ya Jaji Chande yatatekelezwa kikamilifu, hasa kuanzishwa kwa mchakato wa maridhiano ya kitaifa na Katiba mpya, Tanzania inaweza kuingia katika awamu mpya ya utulivu wa kisiasa unaotokana na makubaliano si ukimya, wala matamanio ya upande mmoja.

Katika hali hii, ushindani wa kisiasa utakuwa na kanuni zinazoeleweka na kukubalika kila upande, malalamiko ya wananchi yatapata majibu kupitia mifumo halali, na taasisi za dola zitajengewa uwezo wa kuzuia migogoro kabla haijalipuka.

Hii ndiyo Tanzania ambayo ripoti inaonekana kuielekeza, taifa linalokiri changamoto zake na kuzitatua kwa uwazi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa kufikia hatua hiyo kunahitaji zaidi ya mapendekezo pekee. Baadhi yao wanapendekeza kuwepo kwa tume huru ya ukweli, haki na maridhiano, wakitolea mfano wa Afrika Kusini ambapo mchakato wa maridhiano ulihusisha hatua kubwa za kisiasa, ikiwemo kuachiliwa kwa Nelson Mandela.

"Nadhan ni jambo la busara kwa serikali, lazima ifikirie, wamtoe Tundu Lissu gerezani, ili kuleta maridhiano ya ukweli," anasema Nicodemus Minde, mchambuzi.

Tundu Lissu, mwenyekiti wa CHADEMA, yuko gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa tuhuma za uhaini. Kwa baadhi ya wachambuzi, kumtenga kiongozi mkuu wa upinzani na hata chama chake katika mchakato wa maridhiano kunaweza kuathiri uhalali wake.

Kwa upande wa CCM, maridhiano yanaonekana kuwa njia sahihi ya kuponya taifa. Makamu mwenyekiti wake, Stephen Wasirra, anasisitiza mbele ya BBC:

"Hatuendi kwenye maridhiano kuridhiana na chama fulani, sisi tunataka kuridhiana kama nchi, tunataka kuponya nchi."

Hata hivyo, msimamo wa CHADEMA wa kutotambua baadhi ya michakato, ukiwemo uchaguzi mkuu, tume ya Chande, masuala ya katiba mpya, unaendelea kuongeza pengo la kisiasa, changamoto ambayo inaweza kuathiri utekelezaji wa njia hii inayoonekana ndiyo muafaka na bora kwa mazingira ya sasa.

Waziri kabudi anasema; " Matumaini ya kupata Katiba mpya ni makubwa, kwa sababu serikali ya Samia ina utashi wa kisiasa, pasipokuwa na vitimbi vya wale ambao hawana nia njema katiba itapatikana (mwaka 2028)".

2. Tanzania ya uwajibikaji wa kweli

Iwapo baadhi ya mapendekezo yatatekelezwa, lakini si yote hasa yale magumu kama uwajibikaji wa wahusika wakuu basi Tanzania inaweza kubaki kwenye hali ya mpito.

Katika mazingira haya, kuna uwezekano wa kuona hatua za juu juu kama fidia kwa waathirika au maboresho ya baadhi ya taasisi, lakini maswali ya msingi kuhusu haki na uwajibikaji yakaendelea kuwepo.

Wananchi wanaweza kuendelea kuwa na imani nusu na taasisi za dola, hali inayoweza kudumisha utulivu wa muda mfupi, lakini bila kuondoa mizizi ya migogoro.

Kwa mfano mauaji yametokea nani anawajibika nayo? Waziri Kabudi alipoulizwa swali hili na BBC alijibu kwamba tume ya Chande imebainisha ghasia za uchaguzi zilipangwa na kuratibiwa na wanasiasa na wanaharakati: "Ni kazi ya tume ya upelelezi kuwaita hao watu wanaotuhumiwa, ili wahojiwe, waonyeshe ushahidi na wajitetee", .

Tume imependekeza kuundwa kwa tume nyingine ya kijnai kuchunguza masuala ya kijinai ili kuruhusu uwajibikaji. Hapa ndipo uwajibikaji wa kisiasa unapohitajika zaidi kwa manufaa ya taifa kuliko hata wa kijinai unaopitia mchakato mrefu huku taifa likiendelea kupitia mgogoro.

Mchambuzi Salim Amin anaona njia hii kama ya kati, lakini inayohitaji msukumo wa jamii yenyewe: "Njia ya uwajibikaji… kila upande ukichukua nafasi yake, nchi inaweza kuvuka. Hii ni njia ambayo Watanzania wenyewe wanaweza kuichagua."

Hata hivyo, kuna mashaka kuhusu tume ya uchunguzi wa jinai wa yale yaliyotokea Oktoba 29 na uhuru wa mchakato wa uchunguzi zaidi uliopendekezwa. Mchambuzi Evance Rubara anaonya:

"Kuna malalamiko, hii tume imefanya kile ambacho rais alitaka… kama itaendelea kuundwa tume nyingine, je, hiyo itakuwa huru?" Hili tume, iliwaji kujibu kwamba iko huru, haina dalali na haiingiliwi na yoyote.

Rubara anaongeza kuwa hata taarifa zilizotolewa bado zinahitaji uthibitisho wa kina:

"Hata taarifa tulizopatiwa zinahitaji uthibitisho… njia nzuri ni tume huru inayofanywa na watu huru."

Mitazamo hii inakuonyesha changamoto si tu utekelezaji, bali pia uaminifu wa mchakato wenyewe, kufikia Tanzania inayohitajika.

Tanzania ya mvutano unaojirudia

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Iwapo ripoti ya tume ya Jaji Chande itabaki kuwa nyaraka ya kisiasa bila utekelezaji wa maana, basi dalili zilizotajwa ndani yake zinaweza kujirudia na hata kwa nguvu zaidi.

Katika hali hii, malalamiko ya muda mrefu yataendelea kujilimbikiza. Masuala kama haki, Katiba mpya, utawala bora, utekaji, ukosefu wa ajira na utendaji wa viongozi yataendelea kuwa chanzo cha mvutano.

Katika mazingira haya, wanasiasa au makundi yenye maslahi wanaweza kuendelea kutumia hasira za wananchi, kama ripoti yenyewe ilivyobainisha. Hii inaweza kulazimisha vyombo vya dola kujikuta vikikabiliana tena na hali kama ile ya Oktoba 29.

Mchambuzi Salim Amin anaonya kuwa kuchelewesha mabadiliko kuna gharama kubwa: "Huu ndio wakati muhimu kwa Watanzania kufanya mabadiliko ya kweli. Wakipoteza fursa hii, inaweza kuchukua miongo kadhaa au hata kizazi kizima kujinasua…"

Kwa tafsiri rahisi, Oktoba 29 inaweza isiwe tukio la mwisho bali mwanzo wa mzunguko wa migogoro unaoweza kujirudia.

Ripoti ya Jaji Chande imefanya jambo moja muhimu kubwa moja; imeweka wazi changamoto zilizokuwepo badala ya kuzifunika.

Sasa, Tanzania ya kesho inaonekana wazi ikiwa hakutakuwa na kufukia na kuziba masikio. Inaweza kuwa taifa lenye maridhiano, uwazi na ushindani wa haki, au taifa linaloendelea kubeba migogoro iliyofichwa chini ya utulivu wa maneno.

Tofauti kati ya njia hizi haitatokana na ripoti yenyewe, bali uamuzi wa kisiasa, taasisi na jamii kwa ujumla kuhusu kama kweli wako tayari kubadilika.

Hapa muhimu kuzingatia, sio kuhusu kama mabadiliko yanawezekana bali kama kuna utashi wa kuyafanya.