Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi baada ya Putin: Je, mabilionea waliokuwa kimya wanajiandaa kurejesha mamlaka yao?
Saa chache baada ya kuanzisha uvamizi mkubwa dhidi ya Ukraine, Februari 24, 2022, Rais Vladimir Putin aliwakusanya baadhi ya matajiri wakubwa wa Urusi katika Ikulu ya Kremlin.
Zaidi ya mabilionea 36 walikaa upande mmoja wa ukumbi mkubwa wa Yekaterininsky, wakiwa wamevaa barakoa kutokana na janga la Covid-19. Putin alikaa upande wa pili, akiwa hana barakoa, huku nafasi kubwa ikiwatenganisha na kiongozi huyo.
Kwa lugha ya mafumbo, Putin aliwataka wafanyabiashara hao kuelewa hali iliyokuwa ikiendelea na kushirikiana na serikali kulinda uzalishaji, uchumi na ajira.
Lakini jambo lililovutia zaidi halikuwa alichokisema Putin, bali kile ambacho matajiri hao hawakukisema.
Hakuna hata mmoja aliyezungumza.
Ukimya huo unaeleza mengi kuhusu maisha ya matajiri wa Urusi chini ya utawala wa Putin. Kwa miaka mingi wamejifunza kwamba kumkosoa rais huyo kunaweza kugharimu uhuru wao, biashara zao na hata maisha yao.
Mwaka 2003, Mikhail Khodorkovsky, aliyekuwa tajiri zaidi nchini Urusi, alimkosoa Putin kwa kusimamia ufisadi na kufadhili makundi ya upinzani. Baadaye alifungwa jela kwa miaka 10 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kodi, ulaghai na ubadhirifu wa fedha. Khodorkovsky alikanusha mashtaka hayo.
Kesi yake ikawa onyo kwa matajiri wengine: nchini Urusi, utajiri haukupi uhuru wa kumpinga Putin.
Lakini sasa, licha ya ukimya huo, kuna dalili kwamba baadhi ya matajiri hao wameanza kufikiria kuhusu Urusi ya baada ya Putin.
Kutoka kuwa watawala hadi kuwa watumishi wa Putin
Baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, Urusi iliingia katika kipindi cha misukosuko ya kiuchumi na kisiasa.
Kampuni kubwa za serikali zilianza kubinafsishwa, na watu waliokuwa na uhusiano mzuri na viongozi wakapata fursa ya kujitajirisha kwa kasi. Hawa ndio waliopewa jina la oligarchs, likimaanisha kundi dogo la watu wenye mamlaka makubwa.
Katika miaka ya 1990, matajiri hao hawakuwa na fedha pekee, bali pia walikuwa na uwezo wa kushawishi serikali na maamuzi ya kisiasa.
Hata hivyo, baada ya Putin kuingia madarakani mwaka 2000, alianza kuwadhibiti. Hakutaka kushiriki mamlaka na mtu yeyote.
Bill Browder, aliyewahi kuwa mwekezaji mkubwa wa kigeni nchini Urusi, anasema aliwahi kuwaona oligarchs wakijiamini kupita kiasi katika mikutano ya kimataifa. Lakini Putin alipoingia, watu hao walibadilika na kuwa wanyenyekevu kana kwamba ni watoto wa shule wanaomwogopa mwalimu.
Tangu uvamizi wa Ukraine mwaka 2022, Putin ameendeleza mfumo wa kuwazawadia wanaomtii na kuwaadhibu wanaompinga.
Wanaokosoa vita wamekumbwa na uporaji wa mali, huku wanaoendelea kuwa waaminifu wakipata mikataba mikubwa ya serikali.
Kwa mujibu wa Forbes, Urusi sasa ina mabilionea 155, huku utajiri wao kwa pamoja ukifikia karibu dola bilioni 700.
Hata hivyo, utajiri huo haujawapa uhuru waliokuwa nao zamani.
Mabilionea wenye fedha lakini wasio na mamlaka
Tatizo kubwa kwa matajiri hao ni kwamba fedha zao haziwezi tena kununua ushawishi wa kisiasa kama ilivyokuwa miaka ya 1990.
Dmitry Nekrasov, mwanasiasa na mchambuzi anayeishi uhamishoni, anasema matajiri hao wana utajiri kwa sababu ya uhusiano wao na Putin, si kwamba Putin anawahitaji kwa sababu ya utajiri wao.
Nje ya Urusi, hali ni ngumu zaidi. Vikwazo vya nchi za Magharibi vimewafanya baadhi yao kushindwa kutumia ndege binafsi, kupeleka majahazi yao katika bandari maarufu za Ulaya au kufurahia maisha ya kifahari waliyoyazoea.
Hali hiyo imeanza kuwafanya baadhi yao kujiuliza: nini kitatokea Putin atakapoondoka madarakani?
Urusi inaweza kuwa na sura gani baada ya Putin?
Putin amekuwa madarakani kwa takribani robo karne. Ingawa hakuna dalili za wazi za kuondoka kwake hivi karibuni, siku moja hatakuwa tena rais.
Iwapo atajiuzulu au kufariki akiwa madarakani, Waziri Mkuu Mikhail Mishustin ndiye atakayechukua nafasi yake kwa mujibu wa utaratibu wa kikatiba.
Lakini wachambuzi wanaona uwezekano wa kutokea kwa hali tatu.
Kwanza, demokrasia.
Baadhi ya watu wanatumaini kwamba kuondoka kwa Putin kutafungua nafasi ya kujenga mfumo wa kidemokrasia, wenye uchaguzi huru, ushindani wa kisiasa na uhuru wa kujieleza.
Hata hivyo, Alexandra Prokopenko, mchambuzi wa Urusi aliye uhamishoni, anaona uwezekano huo kuwa mdogo. Anasema taasisi za kidemokrasia zimeharibiwa kwa kiwango kikubwa, huku jamii ikiwa imezoea ukandamizaji na matumizi ya nguvu.
Pili, kuendelea kwa utawala wa kimabavu.
Mtu mwingine anaweza kuchukua nafasi ya Putin na kuendeleza mfumo wake wa utawala.
Hata hivyo, mrithi huyo huenda asiwe na nguvu sawa na Putin mwanzoni, kwa sababu kujenga mamlaka ya aina hiyo huchukua muda.
Tatu, kurejea kwa utawala wa oligarchs.
Huu ndio mfumo ambao baadhi ya matajiri wanaupenda zaidi.
Katika mfumo huo, kundi dogo la wafanyabiashara wakubwa na familia zenye nguvu lingekuwa na ushawishi mkubwa katika serikali na maamuzi ya nchi, kama ilivyokuwa miaka ya 1990.
Kwao, hiyo ingekuwa fursa ya kurejesha mamlaka waliyopoteza chini ya Putin.
Ishara ya mabadiliko kutoka kwa mfalme wa mbolea
Dalili muhimu ya namna matajiri hao wanavyofikiria kuhusu mustakabali wa Urusi ilijitokeza kupitia Andrey Melnichenko, mmoja wa matajiri wakubwa nchini humo na anayejulikana kimataifa katika biashara ya mbolea.
Melnichenko aliwashangaza wengi alipokubali kufanya mahojiano na gazeti la The Economist, chombo cha habari kutoka nchi ambayo Kremlin inaichukulia kuwa isiyo rafiki.
Katika mahojiano hayo alirudia baadhi ya hoja za Kremlin kuhusu vita vya Ukraine na madai kwamba nchi za Magharibi zilipuuza wasiwasi wa Urusi kuhusu usalama wake.
Lakini pia alitoa hoja muhimu: Urusi inahitaji kuacha mfumo wa mtu mmoja kutawala na kushirikiana zaidi na dunia.
Hakumwita Putin aondoke madarakani, lakini alitetea mabadiliko ya mfumo wa utawala.
Mwandishi aliyemhoji, Arkady Ostrovsky, anasema walikuwa na majadiliano marefu na makali katika hoteli na mikahawa. Aliona kwamba Melnichenko alikuwa akifikiria kwa dhati kuhusu majibu yake, badala ya kutoa kauli zilizopangwa kisiasa.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini huenda mahojiano hayo yalifanyika kwa idhini ya kimyakimya ya Kremlin. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa wazi unaothibitisha hilo.
Prokopenko anaamini ujumbe wa Melnichenko ulikuwa mwito kwa matajiri wengine kuanza kuzungumza kuhusu mustakabali wa nchi.
Hofu bado inawazuia kuchukua hatua
Pamoja na dalili hizo, matajiri wa Urusi bado wanaogopa kuchukua hatua za wazi dhidi ya Putin.
Prokopenko anasema baadhi yao wamebadilisha hata namna wanavyomwita rais huyo. Zamani walitumia majina kama "Nachalnik", likimaanisha bosi, na "Perviy", likimaanisha wa kwanza.
Sasa baadhi yao humwita "Ded", yaani babu au mzee, jina linaloashiria kupungua kwa heshima waliyokuwa nayo kwake.
Wengine wanatamani kurejea kwa siasa zenye ushindani, uhuru wa kujieleza na nafasi ya wananchi kushiriki katika maamuzi ya nchi.
Lakini hofu imeendelea kuwatawala.
Prokopenko anasimulia kumhoji tajiri mmoja aliyekaa juu ya simu yake wakati wote wa mazungumzo, akiamini kwamba kufanya hivyo kungezuia vyombo vya usalama kumsikiliza kupitia teknolojia ya kidijitali.
Hali hiyo inaonyesha kiwango cha hofu kilichojengeka miongoni mwa watu wenye fedha nyingi nchini Urusi.
Nekrasov anasema matajiri wenye fedha nyingi zinazoweza kutumika kwa uhuru wanaweza kuanza kujipanga kisiasa. Lakini wale wanaotegemea mikataba ya serikali wanaogopa kupoteza kila kitu.
Bill Browder anaamini hakuna oligarch atakayethubutu kumpinga Putin waziwazi akiwa bado madarakani, kwa sababu anajua matokeo yake yanaweza kuwa mabaya.
Mike Calvey, mwekezaji wa Marekani aliyewahi kufanya biashara nchini Urusi, anaunga mkono mtazamo huo. Anasema ni rahisi kwa watu walioko nje ya Urusi kuwataka matajiri hao wampinge Putin, lakini kwa uhalisia wanaweza kuishia gerezani na kupoteza mali zao.
Swali kubwa: Nani atamiliki Urusi baada ya Putin?
Jambo moja linaonekana wazi: baadhi ya matajiri wakubwa wa Urusi hawaridhishwi na mfumo wa sasa.
Wanataka kurejesha ushawishi wao, kupata uhuru wa kufanya biashara bila hofu ya kisiasa na kuona Urusi ikishirikiana zaidi na dunia.
Lakini maslahi yao si lazima yawe sawa na maslahi ya wananchi wa kawaida wanaotamani demokrasia na uhuru.
Huenda Urusi ya baada ya Putin ikawa nchi yenye demokrasia zaidi. Huenda ikapata kiongozi mwingine wa kimabavu. Au huenda matajiri wakarejesha mfumo wa oligarchs uliowapa nguvu kubwa miaka ya 1990.
Kwa sasa, matajiri hao wanaendelea kunyamaza na kusubiri wakati mwafaka.
Lakini swali kubwa si kama Putin ataondoka siku moja. Swali ni je, atakapoondoka, Urusi itatawaliwa na wananchi, dikteta mwingine au mabilionea waliokuwa wakimwogopa kwa miaka mingi?
Imefasiriwa na Asha Juma