Kwa nini wanaume na wanawake wana sauti tofauti?

ll

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Sauti ya mwanadamu ni kifaa cha kipekee sana. Inatoa hisia, huashiria mamlaka, na hubeba utambulisho wetu. Kabla hata hatujashughulikia maneno ambayo mtu anasema, kwa kawaida tunaweza kutambua kama mzungumzaji ni mwanaume au mwanamke ndani ya sekunde moja.

Uofauti huu wa kijinsia si wa bahati mbaya; ni matokeo ya mabadiliko ya kibiolojia, muundo wa mwili, na homoni ambayo hutokea wakati wa kukuwa kwetu kama binadamu.

Ili kuelewa ni kwa nini wanaume na wanawake wana sauti tofauti, tunapaswa kuangalia kwanza injini kuu ya sauti: zoloto au kisanduku cha sauti na mikunjo inayosababisha sauti iliyo ndani yake.

Mabadilika wakati wa balehe

Wakati wa utoto, wavulana na wasichana huwa na sauti zinazofanana sana. Mifumo yao ya sauti ina ukubwa sawa, na kusababisha uzito wa sauti zao kufanana. Tofauti kubwa hutokea wakati wa kubalehe, ikisababishwa hasa na homoni.

Kwa wanaume, ongezeko la homoni za testosterone husababisha zoloto kukua kwa kiasi kikubwa. Zoloto linapopanuka, husogea mbele, na kusababisha kutokea kwenye koo linalojulikana kama koromeo. Kwa sababu sehemu ya ndani ya zoloto hukua, mikunjo yake ya ndani yake hulazimika mirefuka na kuwa minene.

Kinyume chake, ingawa wanawake pia hupitia mabadiliko ya sauti wakati wa kubalehe kutokana na homoni za estrojeni na projesteroni, ukuaji wa zoloto sio mkubwa. Koromeo la mwanamke hukua kidogo tu, na ukubwa na umbo hubaki sawa na kabla ya kubalehe.

Chukua mfano wa kamba ya gitaa

k

Chanzo cha picha, Shutterstock

Tofauti katika ya sauti ya mwanamke na mwanaume inaweza kueleweka kwa urahisi kwa kutumia mfano wa kifaa cha muziki kama vile gitaa au piano.

Nyuzi nene na ndefu hutoa sauti ya chini lakini nzito, huku nyuzi nyembamba na fupi zikitoa sauti nyembamba.

Mikunjo katika zoloto ya mwanaume, kwa kawaida hukua hadi urefu wa kati ya milimita 17 na 25. Kwa sababu ni mirefu na mizito, hutetemeka kwa masafa ya chini, kawaida karibu Hertz 100 hadi 120 (mitetemo kwa sekunde).

Mikunjo katika zoloto ya wanawake, kwa kawaida huwa kati ya milimita 12.5 na 17.5. Kwa kuwa ni mifupi na nyembamba, hutetemeka kwa kasi zaidi, wastani wa masafa ya takriban Hertz 200 hadi 220.

Tofauti hii katika kasi ya mtetemo ndiyo sababu kuu ya sauti za wanaume kusikika kuwa ni nzito zaidi na sauti za wanawake kusikika kuwa ni nyembamba.

Njia ya Sauti

Zoloto ni sehemu moja ya sababu ya tofauti ya sauti. Huku njia ya sauti ambayo inajumuisha koromeo (koo), mdomo, na pua hufanya kazi kama kipaza sauti cha asili.

Kwa sababu wanaume kwa ujumla wana fuvu kubwa, shingo ndefu, na njia pana za hewa wakati wa kubalehe, njia zao za sauti ni kubwa zaidi. Ukubwa huu wa njia huchuja sauti inayosafiri kutoka kwenye mikunjo ya sauti na kuifanya sauti ya mwanaume kuwa nzito zaidi.

Wanawake wana njia fupi za sauti, hilo hufanya sauti zao kuwa nyembamba, kali na kuifanya sauti kuwa angavu na iliyo wazi zaidi.

Sababu za kitamaduni na kijamii

km

Chanzo cha picha, getty images

Ingawa maumbile ndio sababu kuu, tabia ya binadamu pia huchangia muundo wa sauti. Wataalamu wanasema wanaume na wanawake hubadilisha mifumo yao ya usemaji bila kujua ili kuendana na matakwa ya kitamaduni ya uanaume na uwanawake.

Mara nyingi wanaume huzungumza kwa sauti nzito ili kuonesha mamlaka yao au uwanaume wao, huku wanawake hutoa sauti zao nyembamba na laini, ili kuendana na sifa za kike kama jamii itakavyo.

Uzito na wepesi wa sauti una sababu ya kimaumbile na matakwa ya kijamii, na sauti hiyo huzalishwa ya misuli yenye midogo ya milimita chache na huongezeka kutokana na mabadiliko ya homoni.