Kiongozi wa upinzani Ghana afungwa miaka 20 kwa uchimbaji haramu
Chama kikuu cha upinzani nchini Ghana, New Patriotic Party (NPP), kimeeleza hasira zake baada ya mmoja wa viongozi wake waandamizi kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kazi ngumu, kufuatia kutiwa hatiani kwa makosa ya uchimbaji madini haramu.
NPP imesema hukumu dhidi ya Bernard Antwi Boasiako, mwenyekiti wa chama hicho katika Mkoa wa Ashanti, maarufu kama Chairman Wontumi, ina msukumo wa kisiasa.
Boasiako ndiye kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu nchini Ghana kutiwa hatiani kwa makosa ya uchimbaji haramu wa madini tangu serikali ilipoanza kampeni ya kukabiliana na shughuli hizo mwaka 2017.
Mbali na kifungo hicho, Boasiako, ambaye alikana mashtaka yote, ameamriwa pia kulipa faini ya zaidi ya dola za Marekani 10,000.
Alionekana akiwa ameduwaa wakati jaji alipokuwa akisoma hukumu hiyo katika mahakama ya Accra, mji mkuu wa Ghana, Jumatatu.
Mahakama ilimpata na hatia ya kutoa vibali vya uchimbaji bila idhini halali na kuwezesha shughuli za uchimbaji madini bila kibali, kupitia kampuni yake ya Akonta Mining.
Ghana ndiyo nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika. Hata hivyo, uchimbaji haramu wa madini, unaojulikana nchini humo kama galamsey, umeendelea kuchafua mito na kuharibu mazingira kwa kiwango kikubwa.
Kwa miaka kadhaa, serikali mbalimbali za Ghana zimejaribu kudhibiti tatizo hilo, ikiwemo kutumia jeshi, lakini juhudi hizo hazijafanikiwa kulimaliza.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, Katibu Mkuu wa NPP, Justin Kodua Frimpong, aliwaambia waandishi wa habari:
"Mapambano dhidi ya uchimbaji haramu wa madini hayawezi kuwa ya kuaminika ikiwa yatalenga wapinzani wa kisiasa pekee bila ushahidi wa makosa."
Alidai kuwa jaji alipuuza "ushahidi wa wazi" ambao, kwa maoni yake, ungemwezesha Boasiako kuachiwa huru.
Waendesha mashtaka walisema Boasiako aliwaruhusu watu wawili, Henry Okum na Michael Gyedu Ayisi, kufanya shughuli za uchimbaji katika mgodi wa kampuni ya Akonta Mining bila kibali kutoka kwa Waziri wa Ardhi na Maliasili.
Makundi ya wanaharakati wa mazingira yamekaribisha hukumu hiyo, yakisema itakuwa fundisho kwa wanasiasa na wafanyabiashara wanaofadhili uchimbaji haramu wa madini nchini Ghana.
Soma Zaidi: