Umoja wa Mataifa wasema wapiganaji wa kigeni wanachochea vita nchini Sudan
Umoja wa Mataifa unasema wapiganaji wa kigeni, silaha na teknolojia ya kijeshi kutoka nje zinaendelea kuchochea vita nchini Sudan, huku nchi kama Somalia zikitajwa katika mtandao unaodaiwa kusaidia pande zinazopigana.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaochunguza ukweli kuhusu mzozo huo umesema msaada huo umeongeza uwezo wa jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya raia yaliyo mbali na uwanja wa vita.
Vita vilianza Aprili 2023 kutokana na mzozo wa kugombea madaraka kati ya jeshi na RSF, na hadi sasa vimewalazimisha zaidi ya watu milioni 14 kuyahama makazi yao.
Ripoti hiyo imesema zaidi ya watu 1,000 waliuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika miezi mitano ya kwanza ya 2026, huku pande zote mbili zikishutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.
Umoja wa Mataifa unasema baadhi ya vitendo hivyo vinaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita.
Wachunguzi pia wanaamini kuwa mtandao unaohusisha watu na taasisi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Chad, Libya na Somalia umeipa RSF silaha, vifaa, msaada wa vifaa na usafirishaji, mafunzo pamoja na wapiganaji wa kigeni.
Umoja wa Mataifa pia unasema hadi wakandarasi 2,000 kutoka Colombia walisaidia kuendesha na kutunza mifumo ya ndege zisizo na rubani na silaha nyingine za kisasa zinazotumiwa na RSF.
Baadhi yao walikuwepo wakati wa operesheni karibu na Al-Fashir, Darfur, mji ambao RSF iliuteka Oktoba 2025.
Umoja wa Mataifa umesema mauaji yaliyofanyika huko yalikuwa na viashiria vya mauaji ya kimbari.
UAE imekanusha mara kwa mara kutoa msaada wa kijeshi kwa RSF, huku Colombia ikisema inapinga shughuli za mamluki na imechukua hatua kukabiliana na ushiriki wa raia wake katika migogoro ya nje.
Somalia imesema inachukulia kwa uzito tuhuma hizo, na kwamba haitaruhusu ardhi, anga au bandari zake kutumiwa kwa madhumuni ya kijeshi na pande zinazohusika katika vita vya Sudan.
Hata hivyo, serikali hiyo imekiri kuwepo kwa mapengo katika ushirikishwaji wa taarifa kati ya serikali ya shirikisho na tawala za kikanda.
Chad, kupitia balozi wake mjini Geneva, imekanusha tuhuma hizo na kusisitiza kuwa haina upande wowote katika mzozo huo.
Katika kile kinachoelezwa kama vita vya ndege zisizo na rubani, Umoja wa Mataifa unasema silaha hizo zilizoingizwa kutoka nje zimeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa jeshi la Sudan na RSF kufanya mashambulizi ya masafa marefu.
Unaweza kusoma;