Kiongozi wa upinzani nchini Zambia ashtakiwa kwa uhaini

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kiongozi wa upinzani nchini Zambia, Brian Mundubile, ameshtakiwa kwa uhaini, kwa mujibu wa wakili wake, katika hatua inayokuja wakati wa mvutano wa kisiasa kufuatia uchaguzi wa urais uliopita.
Mundubile alikamatwa Alhamisi baada ya operesheni ya usalama iliyomlazimu kujificha kwa muda. Mwanasiasa huyo alikuwa amepinga matokeo ya uchaguzi uliompa Rais Hakainde Hichilema ushindi wa muhula wa pili.
Mamlaka zilidai kuwa chama cha Mundubile, NRPUP, kilikuwa kinapanga uasi wa kutumia silaha, madai ambayo chama hicho kimeyakanusha.
Akizungumza Jumamosi usiku, wakili wake Milner Katolo alisema mteja wake atafikishwa mahakamani kujibu shtaka la uhaini. Aliongeza kuwa watu wengine 17, wakiwemo mgombea mwenza wa Mundubile, Makebi Zulu, pia wanakabiliwa na mashtaka hayo.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Mundubile alipata asilimia 38 ya kura katika uchaguzi wa Agosti 13, huku Hichilema akishinda kwa asilimia 60.
Siku moja baada ya uchaguzi, vikosi vya usalama vilivamia jengo lililohusishwa na kiongozi huyo wa upinzani mjini Lusaka. Operesheni hiyo iliripotiwa kusababisha kifo cha waziri wa zamani na kuwakamata wanasiasa kadhaa.
Baadaye Mundubile na Zulu walikimbilia katika jengo la Umoja wa Mataifa mjini Lusaka kabla ya kutiwa mbaroni na mamlaka za Zambia.
Wakati huo huo, upinzani unasema haukuweza kuwasilisha pingamizi mahakamani dhidi ya matokeo ya uchaguzi kwa sababu mahakama zilikuwa zimefungwa siku ya mwisho wa muda wa kisheria wa kufungua kesi.
Rais Hichilema anatarajiwa kuapishwa kwa muhula wake wa pili tarehe 1 Septemba.
Waangalizi wa uchaguzi walisema upigaji kura ulikuwa wa amani kwa kiasi kikubwa, ingawa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Zambia imetoa wito wa uchunguzi kuhusu watu wanaodaiwa kutoweka baada ya operesheni za usalama zilizofanyika wakati wa uchaguzi.

























