Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump asema Marekani itaudhibiti kijeshi Mlango-Bahari wa Hormuz

Rais Trump amesema Jeshi la Marekani litaudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz baada ya mazungumzo ya kutafuta muafaka kati ya Marekani na Iran yaliyofanyika Islamabad, Pakistan, kushindwa kufikia makubaliano.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Trump asema Marekani itaudhibiti kijeshi Mlango-Bahari wa Hormuz

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani itaweka “kizuizi cha kijeshi” na kuudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, kufuatia kushindwa kwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran.

    Trump amesema kupitia ujumbe wake katika mtandao wa Truth Social kuwa Jeshi la Wanamaji la Marekani litachukua hatua hiyo baada ya mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika Islamabad, Pakistan, kushindwa kufikia makubaliano pamoja na mambo mengine, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Ameongeza kuwa mazungumzo hayo yalivunjika kwa sababu Iran “haiko tayari kuachana na malengo yake ya nyuklia,” akisisitiza kuwa Washington ilihudhuria mazungumzo hayo kwa nia ya kutafuta suluhu ya kudumu.

    Hatua hiyo inakuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, huku juhudi za kidiplomasia za muda mrefu zikishindwa mara kadhaa kufanikisha makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

    Mlango Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ya kimkakati inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta ya dunia kutoka Mashariki ya Kati, na hatua ya Marekani inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa masoko ya nishati na usafirishaji wa kimataifa.

  2. Israel na Lebanon nao kukutana Jumanne kujadili kusitisha mapigano

    Viongozi wa Israel na Lebanon wamekubaliana kukutana Jumanne mjini Washington kujadili uwezekano wa kusitisha mapigano na kuweka msingi wa mazungumzo ya moja kwa moja.

    Mabalozi wa nchi hizo nzhini Marekani watakutana katika juhudi za kusitisha mapigano, ikiwa ni muda mfupi tangu mazungumzo ya Iran na Marekani kukosa suluhu.

    Ubalozi wa Lebanon nchini Marekani umesema mkutano huo unaweza kufanyika tu iwapo kutakuwa na utulivu wa kutosha, huku ukisisitiza kuwa hali ya usalama ni sharti muhimu kabla ya mazungumzo kuendelea.

    Kwa upande wake, Israel imethibitisha nia ya kuanza “mazungumzo ya wazi ya amani,” lakini ikieleza kuwa haitakuwa tayari kujadili makubaliano yanayohusisha kundi la Hezbollah linalofanya kazi nchini Lebanon.

    Mazungumzo hayo yanakuja wakati kukiwa na tofauti za tafsiri kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano, huku Marekani, Israel, Iran na Pakistan zikiwa na mitazamo tofauti kuhusu iwapo Lebanon inajumuishwa katika makubaliano hayo.

    Mazungumzo ya Jumanne yanatarajiwa kuwa hatua ya awali kuelekea mazungumzo mapana zaidi iwapo pande zote zitakubaliana na masharti ya awali ya utulivu.

    Wakati huo huo, Israel imeendelea na mashambulizi ya anga nchini Lebanon, ambapo Wizara ya Afya ya Lebanon inasema watu 357 wameuawa na zaidi ya 1,200 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni.

    Kwa ujumla zaidi ya watu 2000 wameuawa na wengine zaidi ya 6,400 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa mashambulizi ya hivi karibuni, tarehe 02 Machi, 2026.

    Jeshi la Israel limesema mashambulizi yake yamewaua angalau wapiganaji 180 wa Hezbollah, likidai kuwa yanawalenga wanamgambo hao.

  3. Marekani na Iran zatupiana lawama baada ya mazungumzo yao kugonga mwamba

    Marekani na Iran zinatupiana lawama kufuatia kushindwa kwa mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu mzozo unaoendelea wa Mashariki ya Kati.

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf aliyeongoza ujumbe wa Iran, amesema kuwa Marekani imeshindwa kuaminika na Tehran katika mazungumzo marefu yaliyofanyika Islamabad, Pakistan, huku akieleza jinsi mazungumzo hayo yalivyokwenda.

    Kiongozi alisema kuwa Iran iliwasilisha “mapendekezo yenye mtazamo wa mbele,” lakini mazungumzo hayo hatimaye hayakufikia makubaliano.

    Awali, Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema Iran ndiyo iliyosababisha kukwama kwa mazungumzo hayo baada ya kushindwa kukubali masharti ya Washington, akisisitiza kuwa Marekani ilijitokeza kwa nia njema ya kufikia makubaliano.

    Kwa upande wake, Iran imejibu kwa kuishutumu Marekani kwa kutoa masharti magumu na “yasiyo ya haki,” ikisema msimamo wa Washington haukuwa na nafasi ya kufanikisha makubaliano.

    Kila upande sasa unamlaumu mwenzake kwa kuvunjika kwa mazungumzo hayo, hatua inayoendelea kuongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya pande hizo mbili.

    Baadhi ya masuala yaliyobishaniwa katika mazungumzo hayo ni pamoja na Mlango wa Hormuz, Lebabon na washirika wengine wa Iran, na mpango wa nyuklia wa Iran.

  4. Watu 30 wahofiwa kufariki dunia kwa kukanyagana Haiti

    Watu wasiopungua 30 wanahofiwa kufariki dunia kwa kukanyagana katika eneo maarufu la utalii nchini Haiti siku ya Jumamosi.

    Tukio hilo lilitokea wakati wa mkusanyiko wa kila mwaka wa Pasaka katika sehemu inayoitwa Citadel ya Laferrière, eneo la urithi wa dunia linalotambulika na UNESCO. Jean Henri Petit, mkuu wa ulinzi wa kiraia katika idara ya Nord nchini Haiti, alisema idadi ya vifo huenda ikaongezeka zaidi.

    Waziri Mkuu Alix Didier Fils-Aimé alisema tukio hilo lilitokea “wakati wa tukio la utalii lililohudhuriwa na vijana wengi” katika eneo hilo, katika mji wa kaskazini wa Milot.

    Alisema uchunguzi umeanzishwa na “mamlaka zote husika” zimehamasishwa kusaidia walioathirika.

    “Serikali inatoa pole za dhati kwa familia zilizoathirika,” Fils-Aimé alisema katika taarifa.

    Eneo hilo lilikuwa limejaa wanafunzi na wageni baada ya tukio hilo la uzinduzi wa ngome hiyo ya karne ya 19.

    Inaelezwa kuwa mkanyagano huo ulianza karibu na lango la kuingilia eneo hilo na ukachangiwa zaidi na kuanza kwa mvua kubwa.

  5. Hali ya afya ya kiongozi mpya wa Iran Mojtaba yatia shaka baada ya taarifa za majeraha makubwa

    Kiongozi mpya wa juu wa Iran, Mojtaba Khamenei, mtoto wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa zamani Ayatollah Ali Khamenei, anaripotiwa kuendelea kuuguza majeraha makubwa usoni na kwenye mguu aliyoyapata kufuatia shambulio la anga lililotokea mwanzoni mwa vita, na kumuua baba yake, inaripoti Reuters.

    Kwa mujibu wa watu watatu wa karibu na mazingira yake, shambulio hilo lililolenga makazi ya uongozi wa juu wa Iran katikati ya Tehran lilisababisha uso wake kuharibika vibaya pamoja na majeraha makubwa kwenye mguu mmoja au yote mawili.

    Licha ya majeraha hayo, Khamenei mwenye umri wa miaka 56 anaendelea kupona na anadaiwa kuwa bado yuko imara kiakili.

    Anashiriki mikutano ya viongozi waandamizi kupitia mawasiliano ya sauti na anahusika katika maamuzi muhimu ya serikali, ikiwemo masuala ya vita na mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani.

    Hata hivyo, hali yake halisi ya kiafya na uwezo wake wa kuongoza bado haijathibitishwa hadharani, kwani hakuna picha, video au sauti yake iliyotolewa tangu shambulio hilo na baada ya kuchukua nafasi ya uongozi.

    Serikali ya Iran haijatoa taarifa rasmi kuhusu kiwango cha majeraha yake, huku hali ya usiri ikiendelea kuzunguka uongozi wake.

  6. Mazungumzo yaligubikwa na “kutoaminiana, mashaka na wasiwasi" - Iran

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mazungumzo ya amani yaliyofanyika Islamabad, Pakistan, yalifanyika katika mazingira yaliyojaa mashaka, kutoaminiana na tahadhari kubwa kati ya pande zilizohusika.

    Msemaji wa wizara hiyo, Esmaeil Baghaei, amesema haikutarajiwa kwamba Iran na Marekani zingefikia makubaliano ya haraka katika kikao kimoja tu cha mazungumzo.

    Ameeleza kuwa kutokana na historia ya mvutano na kile alichokiita “vita vilivyowekwa kwa muda wa zaidi ya siku 40”, hali ya mazungumzo ilikuwa tayari imeathiriwa na ukosefu wa uaminifu kati ya pande hizo mbili.

    Baghaei amesisitiza kuwa hakuna mtu aliyekuwa na matarajio ya kufikia makubaliano ya haraka, akibainisha kuwa mchakato wa mazungumzo ya aina hiyo huhitaji muda na hatua nyingi.

    Hata hivyo, ameongeza kuwa diplomasia bado haijafungwa mlango wake, akisisitiza kuwa mazungumzo yanaweza kuendelea licha ya changamoto zilizopo.

  7. Pakistan yataka Marekani na Iran kuheshimu usitishaji mapigano baada ya kushindwa kukubaliana

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetoa wito kwa Marekani na Iran kuendelea kuheshimu makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kufuatia mazungumzo ya amani yaliyofanyika Islamabad.

    Katika taarifa iliyotolewa, Pakistan imesisitiza kuwa ni “muhimu sana” kwa pande zote mbili kuendelea kusimamia ahadi yao ya kusitisha mapigano, licha ya kushindwa kufikia makubaliano ya mazungumzo kuhusu mzozo wao.

    Taarifa hiyo imeeleza matumaini kuwa Marekani na Iran wataendeleza mazungumzo kwa nia njema ili kufikia amani ya kudumu na ustawi si tu katika eneo la Mashariki ya Kati bali pia kimataifa.

    Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi mkuu wa mazungumzo hayo, imesema itaendelea kuwezesha mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika siku zijazo, ikilenga kusaidia kupunguza mvutano na kusaka suluhisho la kudumu.

    Nchi hizo zilikaa kwa saa 21 usiku wa kuamkia leo kwa saa za Afrika Mashariki, lakini zilishindwa kufikia makubaliano ya kusitisha vita kutokana na kila upande kusema masharti ya mwezie hayakuwa yanakubalika.

  8. Marekani na Iran zashindwa kufikia makubaliano baada ya mazungumzo ya kihistoria Pakistan

    Marekani na Iran zimeshindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita baada ya mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika Islamabad, Pakistan.

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema licha ya mazungumzo marefu yaliyodumu kwa saa 21, pande hizo mbili hazikuweza kukubaliana juu ya masharti ya mwisho.

    Amesema Iran “haikukubali masharti ya Marekani”, huku akisisitiza kuwa Washington inahitaji kuona dhamira ya wazi kutoka Tehran ya kuacha kabisa mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

    Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mazungumzo hayo yalikuwa “ya kina”, lakini ikaishutumu Marekani kwa kutoa “matakwa makubwa na yasiyo halali”.

    Mazungumzo hayo yalikuwa yakisimamiwa na Pakistan, huku Waziri Mkuu wake, Shehbaz Sharif akitajwa kupongezwa kwa juhudi za upatanishi.

    Licha ya kushindwa kufikia makubaliano, Donald Trump amesema matokeo hayo “hayajaleta tofauti” kwa Marekani, akisisitiza kuwa nchi yake bado ipo katika nafasi ya ushindi.

    Mazungumzo hayo yalikuwa yakilenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita vinavyoendelea huko Mashariki ya Kati, lakini hadi sasa hatma ya mgogoro huo bado haijulikani.

  9. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo April 12, 2026