Infantino adai kuungwa mkono na idadi kubwa ya wadau wa soka duniani
Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amesisitiza kuwa anaungwa mkono na idadi kubwa ya wadau wa soka duniani, huku akipuuza kwa kicheko maswali kuhusu iwapo aliwahi kufikiria kujiuzulu kufuatia utata ulioibuka kuhusu mpango wa kuuza haki za kibiashara za mashindano ya Kombe la Dunia.
Katika mahojiano na BBC Sport, Infantino alionyesha msimamo wa kutoyumbishwa kuhusu nafasi yake, kufuatia malalamiko yaliyoibuliwa na pendekezo lenye utata la Fifa Forward Enterprise (FFE). Amesema si rahisi kila wakati kuwakutanisha watu wenye mitazamo tofauti na kuwafanya wakubaliane.
“Hakuna ubaya kutokubaliana,” amesema. “Tunaona hilo kila siku katika nchi nyingi duniani. Ni sawa kutokubaliana na kuwa na mitazamo tofauti, lakini baadaye tunapaswa kuweza kusonga mbele.”
Miezi miwili iliyopita, Infantino alikuwa akikabiliwa na shinikizo lililoongezeka la kutaka ajiuzulu kutoka nafasi ya urais wa FIFA, taasisi ambayo ameiongoza tangu mwaka 2016.
Viongozi wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), Shirikisho la Soka Asia (AFC) na Concacaf, linalosimamia soka Amerika Kaskazini na Amerika ya Kati, walitia saini barua wakimtuhumu Infantino kwa kuvunja imani yao kupitia kile walichokitaja kuwa ni udanganyifu.
Wiki iliyopita, UEFA iliitaka FIFA kutoa nyaraka zote muhimu zinazohusiana na mpango wa FFE kabla ya Novemba 2. Katibu Mkuu wa UEFA, Theodore Theodoridis, alisema FIFA ilikuwa imeshindwa kujibu “maswali kadhaa ya msingi”.
Chini ya mpango wa FFE, ambao Infantino aliufuta ndani ya siku chache baada ya kuwasilishwa, sehemu ya haki za kibiashara za mashindano yanayoendeshwa na FIFA ingeuziwa kampuni binafsi ya uwekezaji.
Tangu kuwasilishwa kwa barua hiyo, Infantino amekuwa akisafiri katika mataifa mbalimbali, akiwemo Morocco, Jamhuri ya Dominika, Cape Verde na Japan, katika juhudi za kuimarisha uungwaji mkono wake.
Hali hiyo imeimarisha nafasi yake kiasi kwamba kuchaguliwa kwake tena kwa muhula wa nne katika uchaguzi wa urais wa FIFA mwaka ujao kunaonekana kuwa na uwezekano mkubwa.
Infantino pia amependekeza kuongeza kwa dola bilioni 3.4 za Marekani kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya kuendeleza soka duniani kote.
“Ninatoka Tokyo, ambako Shirikisho la Soka Asia limenipa uungwaji mkono kamili. Nilikuwa Cape Verde, ambako nchi zote wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zimeunga mkono azma yangu. Ninaendelea kuzungumza na vyama vya soka kila mahali duniani,” amesema Infantino.
Tarehe ya mwisho kwa wagombea kuthibitisha nia yao ya kuwania urais dhidi ya Infantino katika uchaguzi wa Machi ni Novemba 18. Hata hivyo, hadi sasa hakuna mgombea mwingine aliyewasilisha jina lake, hivyo Infantino anaweza kuwania nafasi hiyo bila mpinzani.
Soma Pia: