Matumaini kwa Mamilioni: Sindano ya kuzuia HIV yenye ufanisi wa karibu asilimia 100 yafika Afrika
Uganda inatarajiwa kupokea shehena yake ya kwanza ya toleo nafuu la sindano ya mapinduzi ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (HIV), hatua inayotoa matumaini ya kupanua upatikanaji wa dawa hiyo barani Afrika ambako maambukizi ya HIV bado ni makubwa kuliko maeneo mengine duniani.
Shehena ya kwanza duniani ya dawa hiyo ya bei nafuu, inayojulikana kama lenacapavir, iliwasili nchini Zambia Jumatano, huku usambazaji nchini Uganda ukitarajiwa kuanza katika siku chache zijazo, kwa mujibu wa shirika la Global Fund.
Dawa hiyo hutolewa kwa njia ya sindano mara mbili tu kwa mwaka na imeonekana kuwa na ufanisi wa karibu asilimia 100 katika kuzuia maambukizi ya HIV. Inatarajiwa kugharimu takribani dola 40 za Marekani kwa mtu mmoja kwa mwaka.
Zimbabwe nayo inatarajiwa kupokea shehena yake mwanzoni mwa mwaka ujao, huku nchi nyingine kadhaa zikitarajiwa kufuata.
Kuwasili kwa dawa hiyo ya bei nafuu kunakuja mwaka mmoja tu baada ya toleo la awali lililotengenezwa na kampuni ya dawa ya Marekani ya Gilead Sciences kuanza kupatikana katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Toleo hilo la awali lilikuwa likigharimu karibu dola 28,000 kwa mwaka nchini Marekani, gharama iliyokuwa kubwa mno kwa watu wengi katika nchi zinazoendelea.
Mkataba wa kihistoria wafungua njia
Lenacapavir hufanya kazi kwa kushambulia ganda la kinga la virusi vya HIV, jambo linalovuruga uwezo wa virusi hivyo kuongezeka na kuanzisha maambukizi mwilini.
Katika utafiti mkubwa wa kimatibabu uliohusisha zaidi ya wasichana balehe na wanawake vijana 5,000 nchini Uganda na Afrika Kusini mwaka 2024, hakuna hata mshiriki mmoja aliyepokea sindano hiyo aliyeambukizwa HIV.
Wataalamu wa afya wanasema sindano hiyo ina faida kubwa ikilinganishwa na dawa za kila siku za kuzuia HIV zinazojulikana kama PrEP (Pre-Exposure Prophylaxis), ambazo zinahitaji kumezwa kila siku na wakati mwingine huambatana na unyanyapaa wa kijamii.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilipendekeza rasmi matumizi ya lenacapavir kwa ajili ya kuzuia HIV mwezi Julai 2025.
Global Fund imeeleza kuwasili kwa dawa hiyo barani Afrika kama "hatua kubwa ya mafanikio" katika mapambano dhidi ya HIV, ikisema upatikanaji wa toleo nafuu utasaidia kuwafikia mamilioni zaidi walio katika hatari ya kuambukizwa.
Katika taarifa yake, shirika hilo limesema:
"Usambazaji huu unaashiria kasi na upanuzi ambao haujawahi kushuhudiwa wa upatikanaji wa dawa bora, salama na nafuu za kuzuia HIV katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati."
Kwa mujibu wa Global Fund, zaidi ya watu 189,000 katika nchi 10 tayari wamepokea sindano yao ya kwanza ya lenacapavir.
Shirika hilo linatarajia nchi 24 zitakuwa zimepokea dawa hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kwa kushirikiana na serikali ya Marekani, lina mpango wa kuwafikia angalau watu milioni tatu ifikapo mwisho wa mwaka 2028.
Hatimaye, dawa hiyo inatarajiwa kupatikana katika nchi 120 zenye kipato cha chini na cha kati duniani.
Afrika bado inaathirika zaidi
Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zinachangia karibu theluthi mbili ya watu wote wanaoishi na HIV duniani, huku wasichana balehe na wanawake vijana wakibeba mzigo mkubwa zaidi wa maambukizi mapya.
Afrika Kusini ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaoishi na HIV duniani, ikiwa na karibu watu milioni nane wenye maambukizi ya virusi hivyo. Nchi hiyo ni miongoni mwa zinazotarajiwa kupokea sindano hiyo nafuu.
Kwa mujibu wa WHO, watu milioni 41 duniani waliishi na HIV mwaka jana, huku watu 570,000 wakifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na Ukimwi.
Hofu ya kupungua kwa misaada
Usambazaji wa lenacapavir unafanyika wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu kupunguzwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani chini ya utawala wa Rais Donald Trump.
Wataalamu wanaonya kuwa hatua hizo zinaweza kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa katika mapambano dhidi ya HIV barani Afrika, ambapo mataifa mengi bado yanategemea kwa kiasi kikubwa ufadhili wa kimataifa kwa ajili ya huduma za kinga na matibabu.
Umoja wa Mataifa umeweka lengo la kutokomeza Ukimwi kama tishio la afya ya umma duniani ifikapo mwaka 2030.
Soma Pia: