Hapa chini ni muhtasari wa namna tukio la risasi lililoripotiwa katika Hoteli ya Washington Hilton, Marekani lilivyotokea, ukionyesha muda kwa saa za Afrika Mashariki (EAT) na kwenye mabano kwa saa za Mashariki ya Marekani (ET – Eastern Time. Rais Donald Trump, mkewe na viongozi wengine wa Marekani akiwemo Makamu wa rais, JD Vance. walinusurikia kwa kuondolewa na walinzi haraka.
Lilitokea alfajiri kuanzia saa 03:35 kwa saa za Afrika Mashariki ambayo ilikuwa saa 20:35 usiku kwa saa za Washington D.C., Marekani).
03:35 EAT (20:35 ET – Washington D.C., Marekani)
Milio ya risasi inasikika katika Hoteli ya Washington Hilton iliyopo Washington D.C. Wageni wanajificha kchini ya meza wa hofu. Maafisa wa usalama wanamfikia haraka Donald Trump na watu wake wa karibu na kuwatoa eneo la tukio kwa ulinzi mkali.
04:17 EAT (21:17 ET – Washington D.C., Marekani)
Donald Trump anatoa taarifa yake ya kwanza kupitia mtandao wa Truth Social, akisema mshukiwa wa tukio hilo “amekamatwa”.
04:36 EAT (21:36 ET – Washington D.C., Marekani)
Trump anasema anaondoka katika hoteli hiyo kwa maelekezo ya vyombo vya usalama na sheria.
05:29 EAT (22:29 ET – Washington D.C., Marekani)
Trump anachapisha video inayoonekana kuonyesha mwanzo wa tukio la risasi. Baadaye anachapisha pia picha ya mshukiwa.
05:30 EAT (22:30 ET – Washington D.C., Marekani)
Anazungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa Ikulu ya White House, akiwa na maafisa wakuu wa serikali. Anasema kuna uwezekano mshukiwa alikuwa akifanya kazi peke yake (“lone wolf”).
05:50 EAT (takriban 22:50 ET – Marekani)
Vyombo vya habari vya Marekani, ikiwemo CBS, vinamtaja mshukiwa kuwa ni Cole Tomas Allen, mwenye umri wa miaka 31, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya uchunguzi.
06:10 EAT (takriban 23:10 ET – Torrance, California, Marekani)
Picha za moja kwa moja zinaonyesha polisi wakifanya msako katika nyumba moja mjini Torrance, California, kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea.
06:15 EAT (takriban 23:15 ET – Washington D.C., Marekani)
Mwanasheria wa Marekani wa huko eneo la Columbia anasema mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu kwa mashtaka rasmi.