Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran, Marekani zaripoti wimbi jipya la mashambulizi ya anga Ghuba

Washington na Tehran walishambulia vituo vya kijeshi vya kila mmoja karibu na Mlango wa Hormuz

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Uingereza yashinda kesi kuhusu mkataba wa wahamiaji wa Rwanda uliovunjika

    Mahakama imeamua Uingereza haitailipa Rwanda mamilioni ya pauni kufuatia kusitishwa kwa mkataba wa wahamiaji.

    Mahakama ya kimataifa imeamua kwamba Uingereza haitalazimika kuilipa Rwanda mamilioni ya pauni kufuatia kusitishwa kwa makubaliano ya kuwahamishia waomba hifadhi nchini Rwanda, mpango uliositishwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, muda mfupi baada ya kuingia madarakani.

    Serikali ya Rwanda ilikuwa imewasilisha madai ya zaidi ya pauni milioni 100 dhidi ya Uingereza, ikidai kuwa ilikiuka masharti ya makubaliano hayo.

    Makubaliano hayo, yaliyosainiwa na serikali ya awali ya Chama cha Conservative, yalilenga kuifanya Rwanda iwe mwenyeji wa waomba hifadhi waliowasili Uingereza kwa njia zisizo halali, huku Uingereza ikigharamia mpango huo.

    Katika usikilizwaji wa kesi uliofanyika kwa siku tatu nchini Uholanzi, mawakili wa Uingereza walieleza kuwa ilikuwa jambo la kawaida kabisa kwa mpango huo kufutwa baada ya chama cha Labour kuingia madarakani, na kwamba hakukuwa na sababu ya kufanya malipo zaidi baada ya kusitishwa kwa mpango huo.

    Pia walikanusha madai kwamba Uingereza ilikiuka sehemu yoyote ya makubaliano hayo.

    Wakili wa Uingereza aliiambia mahakama mjini The Hague kwamba Rwanda haikuwa na haki ya kupata fidia yoyote iliyokuwa ikiidai.

    Kwa upande mwingine, Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Rwanda, Emmanuel Ugirashebuja, aliieleza mahakama kuwa Rwanda ilikuwa tayari imetumia fedha nyingi kujiandaa kwa utekelezaji wa ushirikiano huo, lakini Uingereza ilijiondoa katika wajibu wake wa kisheria.

    Pia alisema kuwa Uingereza haikuipa Rwanda taarifa ya awali kuhusu uamuzi wa kusitisha makubaliano hayo, na kwamba viongozi wa Rwanda walilazimika kupata habari hiyo kupitia vyombo vya habari.

    Uamuzi huo wa mahakama unaondoa madai ya fidia ambayo Rwanda ilikuwa ikitaka kutoka Uingereza kutokana na kusitishwa kwa mpango huo wa wahamiaji.

    Unaweza kusoma;

  2. Waziri Mkuu wa Israel aamuru mashambulizi katika vitongoji vya Beirut wakati mzozo na Hezbollah ukiongezeka

    Waziri Mkuu wa Israel aagiza mashambulizi Beirut wakati mvutano na Hezbollah ukiendelea kuongezeka

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameagiza mashambulizi kufanywa katika vitongoji vya kusini mwa mji mkuu wa Beirut, huku mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran yakiendelea kuongezeka.

    Netanyahu alisema kuwa maeneo aliyoyataja kama "maeneo ya kigaidi" katika eneo la Dahieh, ambalo ni ngome ya Hezbollah, yatalengwa kwa mashambulizi.

    Alidai hatua hiyo ni jibu kwa mashambulizi dhidi ya raia wa Israel na ukiukwaji mwingine wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani mwezi Aprili, lakini ambayo yameshindwa kumaliza mapigano.

    Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Lebanon aliliambia shirika la habari la BBC kuwa serikali yake inategemea juhudi za upatanishi za Marekani kushinikiza Israel kusitisha ukiukwaji wake wa makubaliano hayo na kuzuia vifo zaidi vya raia.

    Siku ya Jumapili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alizungumza kwa simu na Netanyahu pamoja na Rais wa Lebanon, Joseph Aoun.

    Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani, Rubio alisema kuwa kama hatua ya kwanza, viongozi wa Lebanon waishinikize Hezbollah kusitisha mashambulizi yake dhidi ya Israel. Kwa upande mwingine, Israel itaepuka kuongeza mashambulizi Beirut.

    Afisa huyo alisema hatua hiyo inaweza kutoa nafasi ya kupunguza mvutano hatua kwa hatua na kufanikisha kusitishwa kwa mapigano.

    Wakati huo huo, wanajeshi wa Israel walioko kusini mwa Lebanon walivuka Mto Litani na kuteka Beaufort Castle, ngome yenye historia ya zaidi ya miaka 900 iliyopo kwenye eneo lenye umuhimu mkubwa wa kijeshi.

    Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema operesheni yao "bado haijaisha" na kwamba wana azma ya kudhoofisha na kuvunja nguvu za Hezbollah.

    Unaweza kusoma;

  3. Wagonjwa watano wapona Ebola DRC

    Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zina sababu ya kusherehekea baada ya wagonjwa watano waliokuwa wameambukizwa virusi vya Ebola kupona na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

    Mlipuko wa sasa wa Ebola unashukiwa kusababisha vifo vya karibu watu 250. Hata hivyo, watu wanaoambukizwa wanaweza kupona, na maafisa wa afya wanasisitiza kwamba yeyote anayeshuku ameambukizwa anapaswa kutafuta matibabu haraka.

    Siku ya Jumapili, hafla maalum ilifanyika kwa ajili ya wauguzi wanne waliopona na kuruhusiwa kutoka hospitali moja mjini Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, ambalo ndilo kitovu cha mlipuko huo.

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliwaambia wauguzi hao wakati wa ziara yake mjini Bunia:

    “Ninyi ni ushahidi hai kwamba mlipuko huu unaweza kudhibitiwa na kusimamishwa.”

    Mmoja wa wauguzi hao, Etienne Ezo, aliliambia shirika la habari la Reuters kuhusu hali aliyopitia:

    “Tulikuwa tumekata tamaa kabisa kwa sababu tulijua kwamba wakati fulani tungekufa. Hiyo ndiyo ilikuwa hali halisi. Ninawaambia, kama hujawahi kuwekwa kwenye karantini, huwezi kujua jinsi ilivyo ngumu.”

    Mtu wa kwanza kupona katika mlipuko huu, ambaye alikuwa mfanyakazi wa maabara, aliruhusiwa kutoka hospitalini wiki iliyopita.

    Wahudumu wa afya wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya kuenea kwa Ebola, na mara nyingi ndio walio katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa virusi hivyo.

    Unaweza kusoma;

  4. CCTV yafichua moto ulivyoanza katika shule ya wasichana Kenya

    Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya, imetoa video kutoka kwa CCTV ya shule ikionyesha kile kilichojiri muda mfupi kabla ya tukio la moto kuanza kwenye bweni la shule ya wasichana ambapo wanafunzi 16 wa Utumishi Academy walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.

    Uchunguzi wa CCTV kwa ushirikiano na waalimu, timu ya uchunguzi imebaini wanafunzi saba waliohusika kwenye kitendo hicho kabla ya kutoka nje ya bweni.

    Wakati uchunguzi unaendelea kubaini hasa kilichojiri, video kutoka kwa CCTV imeonyesha kuwa karibu saa 12:10 usiku, wanafunzi kadhaa walitembea kimya kimya ndani ya bweni wakati wengine wamelala fofofo.

    Video iliyotolewa inaonyesha wanafunzi hao wakiingia kwenye chumba 11 kwa muda mfupi sana kabla ya kuendelea kutembea eneo lingine la bweni.

    Wanafunzi wanaonekana wakifanya mienendo yao kimya kimya huku mmoja akiwa amejifunika uso.

    Dakika chache baadaye, wanafunzi watatu wameonekana wakitembea kwa haraka kutoka nje ya bweni huku wawili wakisalia nyuma.

    Wachunguzi wanasema wanafunzi hao walielekea sehemu nyingine ya bweni ambako magodoro yalikuwa yamepangwa na kuwasha moto wa pili.

    Picha za CCTV zinaripotiwa kuwanasa wawili hao wakiwasha kibiri kabla ya kuelekea eneo la mlango wa kutoka kwenye bweni.

    Wakati huu, moto ulienea kwa kasi zaidi.

    Baada ya kuthibitisha kuwa moto huo umeshika kasi, wanafunzi hao wanaonekana wakitoka nje ya bweni hilo bila kuzua taharuki.

    Na ndani ya dakika chache, moshi na miali ya moto vilianza kuenea katika jengo hilo.

    Kufikia saa 12:13 usiku, hofu ilikuwa imezuka ndani ya bweni hilo huku wanafunzi wakiamka kutokana na moshi mwingi na miale ya moto inayozidi kuongezeka.

    Wengine wanaonekana wakijaribu kuelewa kilichokuwa kikitendeka huku wengine wakihangaika kutafuta njia ya kutokea.

    Na ndani ya dakika tano moto huo ulikuwa umeteketeza sehemu kubwa ya bweni huku wanafunzi waliojawa na hofu wakitafuta njia ya kutoroka.

    Kati ya wanafunzi wanane waliokuwa wamezuiliwa awali, sita wamethibitishwa kupitia picha za CCTV, wa saba ni miongoni mwa walioruhusiwa kuondoka na wazazi wao hapo awali, ambaye kwa sasa hayuko kituoni lakini juhudi zinaendelea kuhakikisha amepatikana na kukamatwa.

    Wakati huo huo, vipimo vya DNA vya wanafunzi 16 walioaga dunia kwenye mkasa huo mbaya wa moto shuleni, matokeo yameonyesha kuwa walifariki dunia kutokana na majeraha ya moto kupita kiasi.

    Soma zaidi:

  5. Maambukizi 282 yarekodiwa ya Ebola – DR Congo

    Mamlaka katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zimesema watu 19 wamepatikana na virusi vya Ebola hivi karibuni, na kufanya idadi ya walioambukizwa kufikia 282, ikiwa ni pamoja na vifo 42.

    Katika taarifa yake Jumapili, Wizara ya Mawasiliano ilisema 264 kati ya maambukizi hayo ni kutoka mkoa wa Ituri, kitovu cha virusi hivyo, huku majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini yakirekodi maambukizi 15 na 3 mtawalia.

    Kwa jumla, zaidi ya maambukizi 1,100 yanayoshukiwa bado yanaendelea kuchunguzwa nchini DRC na Uganda, Dk. Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa CDC Afrika alisema katika gazeti la The Financial Times siku ya Jumapili.

    Alikubali hatari iliyopo ya kuenea kwa virusi vya kikanda, akisema "lazima tuende kwa kasi ya janga hilo."

    Pia alisisitiza haja ya msaada wa kimataifa ili kuendana na mikakati iliyowekwa na nchi za Afrika.

    Soma zaidi:

  6. Iran na Marekani zaripoti wimbi jipya la mashambulizi katika anga ya Ghuba

    Mashambulizi ya anga yameanza tena kati ya Marekani na Iran mwishoni mwa juma huku kila upande ukidai kushambulia maeneo ya kijeshi karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema ilifanya "mashambulizi ya kujilinda kwenye rada za Iran na maeneo ya kutoa amri na udhibiti wa ndege zisizo na rubani huko Goruk, Iran na Kisiwa cha Qeshm wikendi hii".

    Wakati huo huo, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) kilisema kimelenga kambi ya anga inayotumiwa na vikosi vya Marekani kulipiza kisasi, lakini hakikusema ni wapi.

    Hapo awali vyombo vya habari vya Marekani viliripoti kwamba Rais Donald Trump alikuwa ameomba kufanyika kwa "marekebisho" katika pendekezo la hivi karibuni ambalo lingeweza kuwa msingi wa makubaliano ya amani, ingawa hakukuwa na dalili yoyote ya mafanikio.

    Marekani ilisema mashambulizi yake siku ya Jumamosi na Jumapili yalikuwa ni kujibu "vitendo vya uchokozi vya Iran vilivyojumuisha kupigwa risasi kwa ndege isiyo na rubani ya Marekani ya MQ-1 iliyokuwa ikifanya kazi juu ya maji ya kimataifa".

    Katika chapisho kwenye mtandao wa X, Centcom ilisema wapiganaji wa Marekani walishambulia ulinzi wa anga wa jeshi la Iran, kituo cha udhibiti wa ardhini na ndege mbili zisizo na rubani ambao ulisema "zilikuwa tishio dhahiri kwa meli zinazopita katika maji ya kikanda". Hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyejeruhiwa katika mashambulizi hayo, jeshi lilisema.

    Jeshi la IRGC lilisema lilishambulia kambi ya jeshi la anga ambayo Marekani iliitumia kutekeleza mashambulizi kwenye mnara wake wa mawasiliano kwenye Kisiwa cha Sirri katika Ghuba, karibu maili 40 (kilomita 65) kutoka pwani ya kusini mwa Iran.

    Jeshi la Iran liliongeza kuwa jibu lake litakuwa "tofauti kabisa" ikiwa uchokozi wa Marekani "utarudiwa", kulingana na matamshi ya IRGC yaliyoripotiwa na shirika la habari la Fars la Iran ambalo si rasmi.

    Soma zaidi:

  7. Ethiopia inafanya uchaguzi wake wa saba tangu 1990

    Uchaguzi mkuu nchini Ethiopia unafanyika leo Jumatatu huku mzozo ukiendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo hatua ambayo inaweza kuwa changamoto ya wengi kuweza kupiga kura.

    Serikali imekanusha ukosoaji wa mchakato wa uchaguzi na kusema zaidi ya watu milioni 50 wamejiandikisha kupiga kura.

    Eneo lote la Kaskazini la Tigray, ambalo limekuwa likijaribu kujikwamua kutoka kwa vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mnamo 2022, limetengwa kabisa kwenye uchaguzi huu.

    Ni uchaguzi wa saba tangu kuanguka kwa utawala wa kijeshi mwaka 1991, msukosuko ambao ulisababisha kujitenga kwa Eritrea miaka miwili baadaye, na unafanyika wakati uhusiano wa Ethiopia na jirani yake wa kaskazini ukiwa sio mzuri.

    Vyombo vya habari vimedhibitiwa vikali na mashirika mengi, ikiwa ni pamoja na BBC, hayajapewa kibali cha kushiriki kwenye uchaguzi huo.

  8. Brazil inawafuatilia wagonjwa wawili kwa uwezekano wa kuambukizwa Ebola

    Maafisa wa afya nchini Brazil wamesema wanachunguza kisa cha pili kinachoshukiwa kuwa cha Ebola mjini Rio de Janeiro ambapo raia wa Ubelgiji hivi karibuni aliwasili kutoka Uganda.

    Raia huyo alionyesha"dalili za virusi kama vile kikohozi, baridi na kuhara".

    Kisa kingine kinachoshukiwa kiligunduliwa Jumamosi katika jimbo la São Paulo. Matokeo ya vipimo kwa wagonjwa wote wawili yanatarajiwa kupatikana wiki ijayo.

    Iwapo yatathibitishwa, hii itakuwa mara ya kwanza kwa maambukizi hayo kuripotiwa nje ya Afrika tangu mlipuko ulipoanza nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Mlipuko wa sasa kuna zaidi ya maambukizi 1,000 yenye kushukiwa kuwa Ebola nchini DR Congo, huku vifo vikishukiwa kuwa takriban 246. Uganda imeripoti maambukizi tisa yaliothibitishwa na kifo kimoja.

    Mlipuko wa sasa umesababishwa na aina adimu ya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo haina chanjo iliyothibitishwa.

    Awali, mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus aliwataka watu nchini DRC kutafuta matibabu haraka iwapo watahisi dalili za ugonjwa huo.

    Soma zaidi:

  9. Mlipuko mkubwa waua makumi ya watu katika kijiji kinachoshikiliwa na waasi Myanmar

    Mlipuko mkubwa umewaua watu wasiopungua 55 na kuwajeruhi wengine kadhaa katika kijiji kimoja katika eneo la Myanmar lililo chini ya udhibiti wa waasi, BBC imeambiwa.

    Chanzo kinachofahamu hali iliyopo eneo la Kaung Tat, kijiji kilichopo katika Mji wa Namkham katika Jimbo la Shan, karibu na mpaka wa China, kilisema wanawake 25 na wanaume 30 wamefariki. Ripoti zingine zilitoa takwimu tofauti kidogo.

    Wingu kubwa la moshi lilionekana likitanda juu ya kijiji muda mfupi baada ya mlipuko kutokea Jumapili.

    Jeshi la Kitaifa la Ta'ang Liberation ambalo linadhibiti eneo hilo na limekuwa likipigana na utawala wa kijeshi, lilisema vilipuzi vinavyotumika katika uchimbaji madini na uchimbaji mawe vimelipuka.

    Soma zaidi:

  10. Polisi Nigeria waonya mashambulizi dhidi ya raia wa Afrika Kusini

    Polisi nchini Nigeria wamewataka wananchi kutojihusisha na “mashambulizi ya kulipiza kisasi” dhidi ya raia au biashara za raia wa Afrika Kusini kufuatia “taarifa za mashambulizi ya chuki dhidi ya raia wa wageni yaliyowalenga raia wa Nigeria nchini Afrika Kusini.

    Katika taarifa, msemaji wa polisi, Anthony Okon Placid, amesema vyombo vya usalama vilifanya tathmini ya hali hiyo baada ya mkutano ulioongozwa na mshauri wa usalama wa taifa, na kuwahakikishia raia wa Nigeria kwamba “hakuna sababu ya kuwa na hofu”.

    Amesema serikali inaendelea kushirikiana na mamlaka za Afrika Kusini pamoja na wadau wengine kupitia njia za kidiplomasia na kiusalama ili kushughulikia hali hiyo na kuhakikisha usalama wa raia wa Nigeria.

    “Ingawa wasiwasi kuhusu mashambulizi dhidi ya Wanigeria nchini Afrika Kusini unaeleweka, wananchi wanashauriwa kutokuchukua sheria mkononi mwao. Mashambulizi ya kulipiza kisasi, vurugu, vitisho, uharibifu wa mali, matamshi ya chuki au vitendo vyovyote vinavyotishia amani ya umma na usalama wa taifa ni kinyume cha sheria na havitavumiliwa,” Bwana Placid amesema.

    Polisi wamesema hatua za ziada za kiusalama zimewekwa katika balozi na misheni za kigeni, miundombinu muhimu pamoja na maeneo mengine nyeti.

    Onyo hilo linatolewa wakati mvutano ukiendelea kuongezeka nchini Afrika Kusini kufuatia maandamano dhidi ya wahamiaji.

    Waandamanaji wamewashutumu wahamiaji wasiokuwa na stakabadhi halali kwa kuongeza shinikizo kwenye huduma za umma na wametoa wito kwa serikali kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji.

    Soma zaidi:

  11. Wagonjwa 5 wapona virusi vya Ebola nchini DR Congo - WHO

    Maafisa wa afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamefurahia kupona kwa wagonjwa watano walioambukizwa aina ya nadra ya virusi vya Ebola.

    Wanasema hatua hii ni matokeo chanya katika kukabiliana na mlipuko ambao umesababisha vifo vya takriban watu mia mbili arobaini na sita mashariki mwa nchi.

    Hakuna chanjo au matibabu yaliyokubaliwa kwa spishi ya Ebola ya Bundibugyo inayosababisha mlipuko wa sasa.

    Wagonjwa wanne wameruhusiwa kurejea makwao huko Bunia, mji mkuu wa mkoa wa Ituri, na kufanya jumla ya waliopona kufikia watano.

    Wagonjwa hao -- wauguzi -- walitoka katika kituo cha matibabu huko Bunia jana. Waliambukizwa walipokuwa wakiwahudumia wagonjwa wa Ebola na walisema kwamba wanashukuru kuwa hai.

    Mtu mwingine aliyenusurika, mfanyakazi wa maabara, alienda nyumbani siku ya Ijumaa. Dk Mwamba Kazadi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Umma amewaita waliopona kuwa ni ushindi unaostahili kusherehekewa.

    Amesema ugunduzi wa mapema na utunzaji thabiti ulikuwa msingi wa mafanikio hayo.

    Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye anazuru mkoa wa Ituri, kitovu cha mlipuko huo, amesema uaminifu ni hatua muhimu.

    Amezitaka jamii kushirikiana na wafanyikazi wa matibabu baada ya wakaazi wengine kushambulia vituo vya afya juu ya sheria kali za mazishi ambazo zinakinzana na mila za wenyeji.

    Mbali na Ituri, maambukizi ya Ebola pia yameripotiwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa DRC, pamoja na nchini Uganda.

    Takribani watu 246 wamefariki dunia kutokana na Ebola, huku wengine zaidi ya 1,000 wakishukiwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo.

    Nchi jirani ya Uganda imeripoti kifo kimoja na kuthibitisha watu tisa mpaka sasa wameambukizwa Ebola.

    Soma zaidi:

  12. Trump ataka marekebisho yafanywe katika mkataba kati ya Marekani na Iran

    Rais Donald Trump wa Marekani ameomba marekebisho yafanywe kwenye makubaliano kati ya Marekani na Iran yanayolenga kukomesha mapigano yaliyoanza mapema mwaka huu, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti.

    Mabadiliko hayo yanahusiana na Mlango-Bahari wa Hormuz na kuondolewa kwa madini ya urani, CBS News, mshirika wa habari wa BBC nchini Marekani, iliripoti. Ikulu ya White House haikujibu ombi la kutoa maoni.

    Mohammad Bagher Ghalibaf, mpatanishi mkuu wa Iran, alisema Jumapili kwamba Tehran haitakubali makubaliano yoyote isipokuwa haki za Iran zipatikane kikamilifu.

    Rais na wasaidizi wake wakuu walikutana Ijumaa kufanya "uamuzi wa mwisho" juu ya mfumo wa kuongeza muda katika suala la kusitisha mapigano na Iran, lakini mkutano huo ulimalizika bila ufafanuzi kuhusu hatua zinazofuata.

    Makubaliano hayo yaliyoripotiwa kwa mara ya kwanza na Axios siku ya Jumamosi, yanajumuisha kusitishwa kwa vurugu kwa siku 60, wito wa kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na mfumo wa kufungua tena na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, kulingana na CBS.

    Ikiwa diplomasia itaendelea, makubaliano hayo pia yanaripotiwa kuhusisha uwezekano wa kupunguzwa vikwazo kwa Iran ambavyo vinaweza kuiruhusu kupata mabilioni ya dola katika mali zilizozuiliwa, CBS ilisema.

    Ripoti za Jumapili za marekebisho zaidi ni hatua ya hivi karibuni katika mazungumzo ya siku nyingi kati ya Ikulu ya White House na Iran kuhusu mfumo wa makubaliano yanayolenga kukomesha vita vya miezi kadhaa.

    Siku ya Alhamisi, maafisa wa Marekani walisema nchi hizo mbili zimekubaliana kuhusu mfumo - unaojulikana kama mkataba wa makubaliano - unaosubiri idhini ya Trump na uongozi wa Iran.

    Soma zaidi:

  13. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara ya Tarehe 01/06/2026.