Kenya yaagiza waajiri kuwalipa wafanyakazi wa nyumbani angalau dola 140 kwa mwezi

Chanzo cha picha, Getty Images
Kanuni mpya za mishahara ya chini kwa wafanyakazi wa majumbani nchini Kenya zimeongeza kiwango cha chini cha mshahara wao wa kila mwezi hadi shilingi 18,047 za Kenya, sawa na takriban dola 140 za Marekani.
Waajiri watakaokiuka masharti hayo wanakabiliwa na kifungo cha hadi miezi mitatu jela au faini ya shilingi 50,000 pesa za Kenya.
Marekebisho hayo yanafuatia uamuzi wa hivi karibuni wa serikali wa kuongeza kiwango cha chini cha mshahara kwa asilimia 12, hatua inayolenga kuwasaidia wafanyakazi kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, viwango hivyo vipya vinawahusu maelfu ya wafanyakazi wa majumbani, wakiwemo wasaidizi wa nyumbani, walezi wa watoto, watunza bustani na wafanyakazi wengine wa huduma za nyumbani kote nchini.
Chini ya muundo huo mpya wa mishahara, wafanyakazi wa majumbani katika miji mikuu ikiwemo Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nakuru na Eldoret sasa wanastahili kulipwa angalau shilingi 18,047 kwa mwezi.
Ongezeko hilo ni sehemu ya mageuzi mapana ya sekta ya ajira yanayolenga kuboresha ustawi wa wafanyakazi na kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi nchini Kenya.
Hata hivyo, wakenya wameingia mitandaoni na kueleza kutoridhishwa kwao na agizo hilo mpya.
Pia unaweza kusoma:


