Moja kwa moja , Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amwita Putin ‘muuaji’ baada ya Trump kumtaja kuwa ‘rafiki’ yake

Rais wa Ukraine, amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ni "muuaji", akijibu matamshi ya Donald Trump aliyemtaja kiongozi huyo wa Urusi kuwa "rafiki" yake.

Muhtasari

Rais wa Ukraine amtaja Rais wa Urusi kuwa 'muuaji'

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Zelensky amwita Putin kuwa ‘muuaji’ baada ya Trump kumtaja kuwa ‘rafiki’

    .
    Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemtaja Rais wa Urusi Vladimir Putin, kuwa ni "muuaji", akijibu matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump aliyemtaja kiongozi huyo wa Urusi kuwa "rafiki" yake alipokuwa China wiki hii.

    Akizungumza na kituo cha televisheni cha CNN, Zelensky alisema kuwa "kwetu sisi,Putin ni adui kwetu sisi, yeye ni muuaji".

    Pembeni mwa mkutano wa kihistoria wa pande tatu kati ya Trump, kiongozi wa China Xi Jinping na Putin siku ya Alhamisi, Trump alimtaja Putin kuwa "rafiki" yake na kusema viongozi hao wawili wamekuwa na "uhusiano mzuri kwa miaka mingi".

    Zelensky alielezea mashambulizi ya hivi karibuni ya Urusi dhidi ya Ukraine kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea mwaka huu. Alisema mashambulizi hayo yalisababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia, baada ya Urusi kurusha makombora 110, yakiwemo 27 ya masafa mafupi ya balistiki, pamoja na zaidi ya droni 400.

    Saa chache baada ya mashambulizi hayo nchini Ukraine, Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kwamba Putin "angependa kumaliza vita".

    "Wote wawili Zelensky na Putin wanataka vita vikome, na ni jambo zuri sana kwamba nina uhusiano nao," alisema Trump siku ya Ijumaa.

    Takriban watu tisa waliuawa katika mashambulizi ya Urusi yaliyolenga madaraja mjini Kyiv na vituo vya reli siku ya Ijumaa, siku chache baada ya Ukraine kuharibu vibaya Daraja la Crimea.

    Hata hivyo, Zelensky alisema licha ya msimamo wa Trump, yeye anamwona Putin kuwa "muuaji".

    "Nadhani watu wengi duniani wanamwona kuwa muuaji kwa sababu anaua watu kila siku na kila usiku," alisema.

    Mabadilishano hayo ya matamshi makali yalijiri wakati Poland, nchi jirani ya Ukraine, ilipotangaza kuwa kombora la Urusi aina ya cruise lilikuwa miongoni mwa vitu vitatu vilivyoingia katika anga yake katika eneo la kusini-mashariki mwa nchi hiyo mapema siku ya Ijumaa.

  2. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja