Uchunguzi waanzishwa Kenya baada ya tembo 14 kufa katika njia ya kutatanisha
Mamlaka nchini Kenya zimeanzisha uchunguzi wa dharura kuhusu vifo vya kutatanisha vya tembo 14 kusini mwa nchi hiyo, karibu na Hifadhi ya Taifa ya Amboseli.
Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) liliiambia BBC kuwa wataalamu wanachunguza mizoga hiyo na kwamba sampuli za tembo hao zimepelekwa kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini ikiwa chanzo cha vifo hivyo kilikuwa ugonjwa, sumu au sababu nyingine.
Hifadhi ya Taifa ya Amboseli na maeneo yanayoizunguka, yanayojulikana kama Mfumo wa Ikolojia wa Amboseli, yanachukua eneo kubwa kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania na yanajulikana kwa utajiri wake wa aina mbalimbali za wanyamapori.
Maafisa wanasema hii ni mara ya kwanza katika miongo kadhaa ambapo idadi kubwa kama hiyo ya vifo vya tembo imerekodiwa katika eneo hilo, ambalo limefanikiwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa uwindaji haramu wa tembo katika miaka ya hivi karibuni.
Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya limesema kuwa "kwa sasa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kuna chanzo cha vifo vya tembo hawa."