Moja kwa moja, Vikosi vya Marekani vyashambulia meli za mafuta za Iran; IRGC yatangaza mashambulio ya kulipiza kisasi

Masaa kadhaa baada ya meli tatu za mafuta za Iran kushambuliwa, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilithibitisha kuwa lilifyatua makombora matatu kutoka Sirik kuelekea mlango Bahari wa Hormuz yakilenga meli kubwa ya kubeba ndege na meli ya kivita ya Marekani.

Moja kwa moja

Na Sarafina Robi & Seif Abdalla

  1. Balozi wa Marekani nchini Israel akemea makazi "haramu" ya Israel katika Ukingo wa Magharibi

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mike Huckabee, balozi wa Marekani nchini Israel, alisema kuwa raia wa Marekani wanaoishi katika eneo la makazi la Termeziya walielezea katika mkutano wa baraza la eneo hilo kuhusu nyumba zilizoharibiwa, vitisho dhidi ya watoto, pamoja na vitendo vya vurugu na vitisho vingine.

    Eneo hili liko Ramallah, katika Ukingo wa Magharibi, na ni makazi ya idadi kubwa ya Wamarekani.

    "Ninaamini kuwa Waisraeli wanaoishi Judea/Samaria (jina linalotumiwa na Israel kwa ajili ya eneo la Ukingo wa Magharibi linalodhibitiwa kimabavu) wana haki ya kuishi huko, na ninaunga mkono hilo, hata hivyo, si kila anayeamini katika Biblia anaunga mkono vitendo visivyo halali,"

    Huckabee aliandika katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X. Makazi ya Waisraeli katika eneo la Ukingo wa Magharibi linalodhibitiwa kimabavu yanachukuliwa kuwa haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

  2. Israel yashambulia kusini mwa Lebanon kulipiza mashambulizi dhidi ya askari wake

    Israel yasema imelenga maeneo kusini mwa Lebanon kufuatia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya askari wake, Jeshi la Israel lilitangaza kuwa lililenga maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon Jumapili asubuhi, ikiwa ni jibu kwa hatua ya Hezbollah kurusha ndege mbili zisizo na rubani dhidi ya askari wa Israel.

    Awali, jeshi la Israel liliwataka wakazi wa maeneo yanayozunguka jengo moja katika mji wa Arab Salem, kusini mwa Lebanon, kuhama, likisema jengo hilo lingelengwa kwa sababu lilikuwa likitumiwa na Hezbollah.

    Hezbollah bado haijatoa tamko lolote kuhusu suala hili. Israel inalitaja eneo la kusini mwa Lebanon kama ukanda wa usalama na kusema haitaondoka katika maeneo hayo hadi pale Hezbollah itakapoweka chini silaha zake.

    Tangu tarehe 2 Machi, mashambulizi ya Israel nchini Lebanon yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,300.

  3. Ukraine na Urusi: Mazungumzo kati ya ujumbe wa Putin na Trump yakamilika

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na wajumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner, yalihitimishwa katika ikulu ya Kremlin baada ya mkutano wa saa tatu na dakika 10 uliolenga juhudi za kumaliza vita nchini Ukraine.

    Mshauri wa Rais wa Urusi, Yuri Ushakov, alielezea mazungumzo hayo kuwa "yenye tija, ya kujenga, mazuri kabisa na yaliyojikita katika msingi wa kuaminiana," akisema kuwa hali ya mambo nchini Ukraine pamoja na masuala mengine kati ya Moscow na Washington yalijadiliwa.

    Mwanzoni mwa mkutano huo, Putin alisema kuwa mawasiliano na mazungumzo na Marekani "huwa na tija kila mara," na kusifu juhudi za Trump za kutafuta suluhu ya kumaliza vita.

    Wakati huo huo, Witkoff alifikisha salamu kutoka kwa Rais wa Marekani na kumshukuru Putin kwa hatua alizochukua kuhakikisha usalama wa ujumbe huo.

    Putin pia aliamuru vikosi vya Urusi kutoshambulia Kyiv kwa muda wa siku tatu, kuanzia saa sita usiku wa Jumamosi, huku wajumbe hao wawili wa Marekani wakijiandaa kusafiri kwenda mji mkuu wa Ukraine.

    Wakati huohuo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alitangaza kuwa nchi yake iko tayari kujiepusha na mashambulizi dhidi ya Moscow hadi mwisho wa siku ya Jumatatu, akitoa wito kwa Urusi kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya Kyiv.

    Alisema: "Kuanzia sasa hadi mwisho wa Jumamosi, pamoja na Jumapili na Jumatatu, Ukraine iko tayari kujiepusha na kushambulia Moscow kwa makombora, na tunatarajia Urusi ifanye vivyo hivyo kwa Kyiv."

    Moscow haijatangaza kukubaliana na usitishaji wa mapigano wa siku tatu ambao ni mpana zaidi kuliko ule wa awali.

    Zelensky aliongeza kuwa alizungumza na wajumbe hao wawili wa Marekani, ambao alisema "tayari wameanza ushirikiano na upande wa Urusi," akithibitisha kuwa Kyiv iko tayari kwa "mazungumzo mazito" pindi ujumbe wa Marekani utakapowasili katika mji mkuu wa Ukraine siku ya Jumapili.

  4. Vikosi vya Marekani vyashambulia meli za mafuta za Iran; IRGC yatangaza mashambulio ya kulipiza kisasi

    .

    Chanzo cha picha, Atta Kenare / Getty Images

    Masaa kadhaa baada ya meli tatu za mafuta za Iran kushambuliwa, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilithibitisha kuwa lilifyatua makombora matatu kutoka Sirik kuelekea mlango Bahari wa Hormuz yakilenga meli kubwa ya kubeba ndege na meli ya kivita ya Marekani.

    IRGC pia ilisema kuwa, ikiwa ni jibu kwa shambulio la Marekani dhidi ya meli za mafuta za Iran, ililenga meli tatu za mafuta zilizokuwa zikipita katika "njia zisizoruhusiwa kupitia mlango Bahari wa Hormuz" na pia ilishambulia meli ya kivita ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuingia katika mlango huo.

    Marekani bado haijatoa tamko lolote kuhusu mashambulio hayo.

    Mapema Jumamosi, CENTCOM ilitangaza kuwa vikosi vya Marekani vilishambulia meli tatu za mafuta za Iran.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ililaani mashambulio hayo na kusema kuwa Marekani ndiyo inayowajibika kwa matokeo ya vitendo hivyo. CENTCOM ilisema kuwa shambulio hilo lilifanyika baada ya IRGC kufyatua makombora ya balistiki dhidi ya meli mbili za kivita za Marekani.

  5. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.