Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani inaendelea na Mazungumzo na Iran huku mashambulizi yakisitishwa - Trump

Hata hivyo, ameonya kuwa iwapo mazungumzo hayo hayatakuwa na mafanikio, Marekani "itarejea kufanya kile tulichokuwa tukifanya" kabla ya kusitishwa kwa mashambulizi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Haiti kufanya uchaguzi wa kwanza baada ya muongo mmoja

    Baraza la uchaguzi la Haiti (CEP) limetangaza Jumatatu kuwa uchaguzi wa kwanza wa urais baada ya miaka kumi utafanyika mnamo mwezi Desemba, huku duru ya pili ya uchaguzi ikipangwa kufanyika mwezi Februari.

    Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwezi Agosti na duru ya pili mwezi Desemba, lakini uliahirishwa kutokana na wasiwasi kuhusu hali ya usalama.

    Haiti haijafanya uchaguzi tangu mwaka 2016.

    Rais wake wa mwisho, Jovenel Moise, aliuawa mwaka 2021 baada ya kuchelewesha kufanyika kwa uchaguzi. Serikali zilizofuata zilipewa jukumu la kuandaa uchaguzi, lakini zilisema hali ya ukosefu wa usalama kutokana na mapigano na magenge yenye silaha yenye nguvu imefanya hilo lisiwezekane.

    Siku ya Jumatatu, baraza hilo la uchaguzi lilitoa ratiba inayoonyesha kuwa awamu ya kwanza ya uchaguzi wa rais na wabunge nchini Haiti itafanyika tarehe 13 Desemba, huku duru ya pili ya uchaguzi ikifanyika tarehe 21 Februari. Pia limetangaza kuwa matokeo ya mwisho yatachapishwa tarehe 7 Machi.

    Wananchi pia wanatarajiwa kupiga kura kuhusu mabadiliko ya katiba pamoja na kuwachagua viongozi wa maeneo ya serikali za mitaa, kulingana na ratiba hiyo.

    Baraza hilo lilisisitiza kuwa utekelezaji wa ratiba hiyo unategemea "kuwepo kwa hali ya usalama inayokubalika na kupatikana kwa fedha zinazohitajika kuendesha shughuli za uchaguzi."

    Mapema mwezi huu, baraza hilo lilisema limeanza kusajili wapiga kura na kutoa mafunzo kwa maafisa wa usalama wa uchaguzi. Pia lilichapisha orodha rasmi ya zaidi ya vyama 300 vya kisiasa vilivyoidhinishwa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi unaokuja.

    Pia Unaweza Hapa:

  2. CHAD yatangaza kujitoa ICC

    Chad imekuwa nchi ya hivi karibuni kutangaza mipango ya kujitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huku nchi hiyo ikidai kwamba kati ya mashauri 13 yaliyochunguzwa tangu mahakama hiyo kuanza kufanya kazi mwaka 2002, tisa yanahusu mataifa ya Afrika.

    Chad inajiunga na orodha inayokua ya mataifa mengi ambayo yanayoituhumu mahakama hiyo ya ICC kwa ubaguzi, huku ikizitaka nchi za Afrika kuimarisha mifumo yao ya sheria ya ndani badala ya kutegemea mahakama za Magharibi.

    Kwa mujibu wa serikali ya Chad ni kwamba mahakama hiyo ina ubaguzi dhidi ya mataifa ya Afrika. Burkina Faso, Mali na Niger nazo pia zimeanza mchakato wa kujitoa kutoka Mahakama ya ICC, ambayo inawashtaki watu binafsi kwa makosa ya hatia za kivita na makosa dhidi ya binadamu.

    Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema uamuzi wa Venezuela kujitoa kutoka Mahakama ya ICC wiki iliyopita unatia wasiwasi mkubwa na utazidisha utamaduni wa kutoadhibiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Maafisa wa Venezuela walitangaza kujitoa ICC huku wakidai mahakama hiyo ina ubaguzi wa kijiografia.

    Soma Zaidi:

  3. Marekani itamaliza fedha za msaada kwa Ukraine Trump atakapoondoka madarakani

    Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umeeleza wajumbe wa Bunge kwamba hautamaliza kutumia dola milioni 400 ambazo Bunge liliidhinisha kwa ajili ya msaada kwa Ukraine hadi mwaka wa fedha wa 2029. Haya yanajiri wakati Ukraine ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa silaha muhimu za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora kutoka Urusi.

    Mnamo mwezi Mei, Wizara ya Ulinzi ya Marekani iliwatumia wabunge barua ikieleza mpango wake wa matumizi ya fedha hizo, kwa mujibu wa chanzo kinachoufahamu waraka huo.

    Wanademocrats pamoja na baadhi ya Wabunge wa Chama cha Republican, ambao pia ni washirika wa Trump, wamekuwa wakiikosoa Wizara ya Ulinzi kwa kuchelewesha kutoa msaada huo kwa Ukraine, licha ya kwamba ulipitishwa na wabunge kutoka vyama vyote viwili mwaka uliopita.

    Chanzo hicho kilisema kuwa miezi miwili baada ya barua hiyo kutumwa, fedha hizo bado hazijatolewa wala kutengwa rasmi kupitia mikataba ya matumizi.

    Bunge la Marekani limekuwa likilalamika mara kwa mara juu ya kasi ya chini ya matumizi ya fedha hizo. Barua hiyo haikuwa imewahi kuzungumziwa hadharani kabla.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, anatarajiwa kukutana na Trump katika Ikulu ya White House siku ya Jumanne, ambapo ataendelea kusisitiza ombi la Ukraine la kupata mifumo ya ulinzi wa anga inayohitajika kwa haraka, pamoja na kukamilisha makubaliano ya ushirikiano wa ndege zisizo na rubani (drones) kati ya Ukraine na Marekani, kwa mujibu wa chanzo kinachofahamu mipango hiyo.

    Baada ya mkutano huo, Zelensky, anatarajiwa kuelekea Bunge la Marekani (Capitol), ambako atakutana na maseneta wote. Hata hivyo, Baraza la Wawakilishi liko likizo ya mapumziko ya kiangazi.

    Soma Zaidi:

  4. Mwimbaji wa Marekani D4vd kujibu tuhuma za mauaji ya msichana (14)

    Jaji wa mahakama moja huko Marekani ameamua kuwa mwanamuziki wa nchini humo, D4vd, atashtakiwa kwa mauaji kuhusiana na kifo cha msichana kijana.

    Uamuzi huo ulitolewa baada ya shauri kusikilizwa katika hatua za awali kwa siku tano, ambapo waendesha mashtaka wa Los Angeles waliwahoji mashahidi kadhaa na kuonesha ushahidi wa picha huku familia ya Celeste Rivas Hernandez, mwenye umri wa miaka 14, ikishuhudia.

    Nyota huyo, ambaye jina lake halisi ni David Anthony Burke, anatuhumiwa kumuua msichana huyo, ambaye mabaki ya mwili wake yalikutwa Septemba 2025 ndani ya gari aina ya Tesla lililosajiliwa kwa anwani yake.

    Burke, mwenye umri wa miaka 21, ameyakana mashtaka ya mauaji na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya binti huyo.

    Kusomewa mashtaka rasmi kwa Burke kumepangwa kufanyika Agosti 31. Kesi hiyo inatarajiwa kuanza ndani ya siku 90 kuanzia tarehe hiyo.

    Waendesha mashtaka wanadai kuwa Burke alimchoma kisu msichana huyo na kisha kuukata mwili wake vipande vipande baada ya miaka kadhaa ya madai ya unyanyasaji wa kijinsia.

    Wanadai alimuua kwa sababu msichana huyo alitishia kufichua uhusiano wake na mtu aliye chini ya umri wa utu uzima na kuharibu taaluma yake ya muziki yenye thamani ya mamilioni ya dola.

    Ushahidi uliowasilishwa mahakamani jana Jumatatu ulionesha vitisho ambavyo Hernandez alimtumia Burke Aprili 22, 2025, kutokana na mabishano kuhusu urafiki wake na msichana mwingine.

    "Naapa kwa MUNGU nitakuua," ujumbe mmoja wenye lugha chafu ulisema, ukifuatiwa na tishio la kumnyonga na kumwambia baba yake uongo kumhusu. "Nitaharibu taaluma yako na maisha yako, nitaharibu kila kitu," ujumbe mmoja ulisema.

    Siku iliyofuata, Hernandez alikwenda nyumbani kwa Burke huko Hollywood kwa kutumia gari la Uber ambalo Burke alilituma kumchukua. Waendesha mashtaka walidai kuwa Burke alimchoma kisu mara tu alipowasili.

    Wakati wa kuhojiwa katika kikao cha mahakama jana Jumatatu, Mpelelezi Corey Farrell wa Idara ya Polisi ya Los Angeles aliiambia mahakama kuwa msichana huyo alikuwa amempa mshtakiwa taarifa zisizo sahihi kuhusu umri wake, kwamba ana umri wa miaka 16 na 18 kwa nyakati tofauti.

    Mawakili wa utetezi wa Burke walidai kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa alitenda uhalifu huo.

  5. Twiga Stars yaandika historia kwa kuifunga Afrika Kusini WAFCON 2026

    Tanzania imeandika historia kwa kupata ushindi wake wa kwanza kabisa katika Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) baada ya kuifunga mabingwa wa mwaka 2022, Afrika Kusini, mabao 2 kwa 1 katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi B.

    Twiga Stars ilitoa moja ya matokeo ya kushangaza zaidi katika mashindano hayo baada ya kuonyesha mchezo wa nidhamu na ujasiri dhidi ya Banyana Banyana, huku Hasnath Ubamba akifunga bao la ushindi dakika ya 87.

    Diana Msewa aliitanguliza Tanzania mbele dakika ya 37 baada ya Twiga Stars kuanza mchezo kwa kasi na kulisukuma lango la Afrika Kusini mara kwa mara.

    Hata hivyo, Bambanani Mbane aliisawazishia Afrika Kusini katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza, na kuifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1 kwa 1.

    Kipindi cha pili kilikuwa na ushindani mkubwa huku Afrika Kusini ikitafuta bao la ushindi, lakini Twiga Stars iliendelea kujilinda kwa umakini na kutumia mashambulizi ya kushtukiza.

    Dakika ya 87, Hasnath Ubamba aliyeingia akitokea benchi aliifungia Tanzania bao la ushindi, lililozua shangwe kubwa miongoni mwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki.

    Ushindi huo ni hatua muhimu kwa soka la wanawake Tanzania. Kabla ya mchezo huo, Twiga Stars ilikuwa imecheza mechi sita za WAFCON bila kushinda, ikipata sare moja na kupoteza tano.

    Matokeo hayo pia yanaongeza matumaini ya Tanzania kutinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.

    Kwa upande wa Afrika Kusini, mabingwa wa mwaka 2022 wameanza vibaya kampeni yao ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingine, na sasa watakuwa chini ya shinikizo la kupata matokeo mazuri katika mechi zao zilizosalia za Kundi B ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata.

    Kwa Twiga Stars, ushindi huo dhidi ya moja ya timu zenye nguvu zaidi barani Afrika unaweza kuwa chachu ya kujiamini katika harakati za kuandika historia nyingine kwenye WAFCON 2026.

    Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, kwa kuanza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 nchini Morocco.

    “Ninaungana na Watanzania wote kuitakia kila la kheri Twiga Stars inapoendelea kupeperusha bendera ya Taifa letu katika michezo inayofuata. Endeleeni kupambana kwa moyo huo huo, mkionyesha uzalendo, nidhamu na ari ya ushindani inayolitangaza vyema Taifa letu,” amesema Rais Samia Suluhu Hassan.

    Fuatilia hapa:

  6. Dunia iko katika hatari ya kuongezeka kwa maambukizi ya VVU - UNAIDS

    Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na UKIMWI limesema dunia iko katika hatari ya kushuhudia kuongezeka tena kwa janga la maambukizi ya VVU baada ya ufadhili wa kimataifa kupunguzwa kwa karibu asilimia 20 mwaka uliopita.

    Katika ripoti iliyotolewa kuadhimisha ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa UKIMWI nchini Brazil, UNAIDS ilisema ufadhili ulipungua hadi takriban dola bilioni saba za Marekani, kiwango cha chini zaidi katika karibu miongo miwili.

    "Ni ripoti inayoonyesha mambo mawili, kwanza ni kuhusu maendeleo ya kisayansi na pili ni onyo kwamba kuondolewa kwa misaada inaleta kukosekana kwa usawa kunakoathiri haki za binadamu. Na kuweka maisha katika miongo kadhaa hatarini," amesema Winifred Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS.

    Byanyima ameongeza kuwa kwa sasa matwakwa ya kisiasa ndio yanayoamua namna ya kupambana na virusi vya UKIMWI na si masuala ya kisayansi

    "Swali sio tena kama tunaweza kumaliza UKIMWI, bali ni je, tunachagua kumaliza Ukimwi. Harakati za kupambana na ukimwi kwa sasa hazikumbwi na changamoto za kisayansi bali zinakabiliwa na kukosekana kwa usawa kutokana na msukumo wa kisiasa. Kama tunatokomeza ukimwi haitaamuliwa maabara, basi ni matwaka ya kisiasa," amesema Byanyima.

    Marekani ilikuwa ikichangia takriban robo tatu ya ufadhili wa kimataifa wa mapambano dhidi ya VVU kabla ya Rais Trump kurejea madarakani mnamo Januari 2025.

  7. Moto wa nyika: Macron asema Ufaransa inakabiliwa na hali mbaya zaidi tangu Vita vya Pili vya Dunia

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameahidi kutumia kila rasilimali iliyopo kupambana na moto mkubwa wa nyika unaoendelea nchini humo akisema janga hilo ni mbaya zaidi kuwahi kuikumba Ufaransa tangu Vita vya Pili vya Dunia.

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameonya kuwa hali itaendelea kuwa ngumu zaidi alipokuwa akitembelea kituo cha operesheni za kuzima moto katika eneo la Gironde, ambalo limeathiriwa vibaya na moto huo uliosababisha mioto mikubwa isiyoweza kudhibitiwa.

    Akizungumza na vikosi vya zimamoto na wahudumu wa dharura, Macron alisema:

    "Tunakabiliwa na hali ngumu zaidi kuwahi kushuhudiwa, hali ambayo haijawahi kutokea tangu Vita vya Pili vya Dunia."

    Aliongeza kuwa msimu wa moto wa nyika, ambao kwa kawaida hufikia kilele mwezi Agosti, bado haujaanza kikamilifu.

    Rais Macron ameonya kuwa viwango vya joto vinatarajiwa kupanda tena, akisisitiza kuwa cha msingi kwa sasa ni kuokoa maisha.

    Wakati huo huo, wazima moto nchini Uhispania wamekuwa wakipambana kudhibiti baadhi ya moto mbaya zaidi wa nyika katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo huku kukiwa na onyo la wimbi kubwa la joto linaloongezeka ambalo linaweza kuzorotesha zaidi hali hiyo.

    Viwango vya joto katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo vinatarajiwa kuwa ya juu zaidi.

    Waziri Mkuu, Pedro Sanchez, ameonya kuwa ni wakati mgumu kwa nchi yake huku akitoa wito kwa vyama vya kisiasa kuweka kipaumbele katika kuunda mkataba wa kitaifa wa dharura wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

    Soma Zaidi:

  8. Johnson & Johnson yajitolea kulipa hadi $5.5bn kumaliza kesi za poda ya watoto

    Kampuni ya Johnson & Johnson (J&J) imejitolea kulipa hadi dola bilioni 5.5 (pauni bilioni 4.14) ili kumaliza maelfu ya kesi zinazodai poda yake ya watoto pamoja na bidhaa nyingine zenye madini ya talcum husababisha saratani ya ovari au kifuko cha mayai.

    Makubaliano hayo makubwa yanakusudia kumaliza mzozo wa kisheria uliodumu kwa miaka kadhaa na kuendelea kuigharimu kampuni hiyo kubwa ya huduma za afya nchini Marekani.

    J&J imeendelea kusisitiza kuwa bidhaa zake zenye talcum hazisababishi saratani, na tayari imebadilisha viambato vya poda yake ya watoto inayotumiwa na watu wengi.

    Makamu wa Rais wa masuala ya kesi za kisheria wa kampuni hiyo, Erik Haas, alisema Jumatatu kuwa madai hayo "hayana msingi", na kwamba J&J imeamua kufikia makubaliano ili kutatua kabisa suala hilo.

    Kampuni hiyo imesema makubaliano hayo yatahusisha takriban kesi 69,000, ambazo ni sehemu kubwa ya madai yaliyosalia yanayohusiana na bidhaa za talcum. J&J imeeleza kuwa italipa hadi dola bilioni 3 mwaka ujao, na kusitarajiwe malipo mengine kabla ya mwaka 2028.

    J&J pia imesema pendekezo hilo litalazimika kukubaliwa na kampuni za mawakili zinazowawakilisha asilimia 95 ya walalamishi wa kesi za saratani ya ovari katika mahakama za majimbo na za shirikisho, kabla ya makubaliano hayo kukamilika.

    Katika taarifa yake, Haas alisema kampuni ina imani kuwa ingeibuka mshindi endapo kesi hizo zingeendelea mahakamani, kama ilivyofanikiwa katika kesi nyingi ambazo tayari zimeamuliwa.

    Aliongeza kuwa makubaliano hayo yataiwezesha kampuni kuhitimisha suala hilo na kuelekeza nguvu zake katika jukumu lake la kutengeneza dawa na vifaa vya tiba vinavyookoa maisha.

    Soma Zaidi:

  9. Mazungumzo ya vita vya Iran yanaendelea huku mashambulizi yakisitishwa - Trump

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa kuna "mazungumzo ya kirafiki yanayoendelea" kuhusu mzozo wa Iran, baada ya pande zinazopigana kutoshambuliana kwa siku ya tatu mfululizo.

    Akiwa ndani ya ndege ya Air Force One siku ya Jumatatu, Trump alieleza matumaini yake kwamba vita hivyo vinaweza kufikia mwisho. Aliwaambia waandishi wa habari: "Ninaamini kuna uwezekano mkubwa jambo fulani likatokea."

    Alionyesha matumaini kwamba vita vinaweza kumalizika Jumatatu, akiwaambia waandishi wa habari ndani ya ndege ya Air Force One: "Nafikiri kuna fursa nzuri ya kutokea kwa jambo fulani."

    Hata hivyo, alionya kuwa iwapo mazungumzo hayo hayatakuwa na mafanikio, Washington "itarejea kufanya kile tulichokuwa tukifanya" kabla ya kusitishwa kwa mashambulizi.

    Kwa upande wake, Tehran imekanusha kuwa kuna mazungumzo yoyote ya moja kwa moja yanayoendelea.

    Trump alisema aliamua kusitisha mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran siku ya Ijumaa baada ya nchi zinazosaidia kupatanisha pande hizo kumwomba kutoa fursa nyingine kwa mazungumzo.

    Iran pia imesitisha mashambulizi yake.

    Hatua hiyo inafuatia karibu wiki mbili za mashambulizi ya kila siku ya Marekani na ya kulipizana kisasi kati ya pande hizo, hali iliyovuruga kwa kiasi kikubwa makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa mnamo mwezi Juni.

    Wakati huo, jeshi la Marekani lilisema mashambulizi yake yalilenga kupunguza uwezo wa Iran wa kuhatarisha usafirishaji wa meli za kibiashara katika Mlango Bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu duniani ya usafirishaji wa mafuta.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Hujambo Msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara tarehe ni 28/07/2026.