Israel yatangaza kumuua kamanda wa Hamas baada ya shambulizi la anga Gaza
Shirika la usalama la Israel, Shin Bet, pamoja na jeshi la nchi hiyo, vilisema katika taarifa ya pamoja kuwa majengo aliyokuwa akijificha Mohamed Odeh yalilengwa baada ya miezi kadhaa ya ufuatiliaji wa kijasusi kuhusu harakati zake.
Muhtasari
- Kenya yafanya mazungumzo na Marekani kuhusu ugonjwa wa Ebola
- Iran imesema pendekezo la Marekani, huenda likachangia Mlango bahari wa Hormuz kufunguliwa
- Raia wa Ghana warejea nyumbani kutoka Afrika Kusini, baada ya maandamano ya kupinga wahamiaji
- DRC: Mamlaka zasema kudhibiti virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo huenda ikachukua miezi sita
- Trump aongeza idadi ya wakimbizi wanaoingia Marekani, ili kuwaruhusu wazungu wa Afrika Kusini kuingia nchini humo
- Israel yatangaza kumuua kamanda wa Hamas baada ya shambulizi la anga Gaza
- Marekani kuweka kituo cha karantini Kenya kwa raia wake walioambukizwa Ebola DRC
- Waislamu kote duniani wanaadhimisha sherehe za Eid al-Adha
- Kiongozi mwingine wa timu ya taifa ya Iran ajiondoa kuelekea Kombe la Dunia
- Iran yasema dola bilioni 12 za fedha zilizozuiliwa bado zipo Qatar
- Nasa yazindua hatua zinazofuata za kujenga kituo cha kudumu mwezini
- Makumi ya watu wauawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon
Moja kwa moja
Kenya yafanya mazungumzo na Marekani kuhusu ugonjwa wa Ebola

Chanzo cha picha, Aden Duale
Maelezo ya picha, Waziri wa Afya wa Kenya, Aden Duale Kenya imesema iko tayari kufanya kazi na washirika wa kimataifa katika kuimarisha usalama wa afya duniani, huku wakiendeleza mazungumzo na serikali ya Marekani pamoja na wadau wengine wa kimataifa kuhusu maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.
Katika taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari, Waziri wa Afya, Aden Duale,amesema serikali ya Kenya inafanya mazungumzo yanayolenga kuboresha mifumo ya pamoja ya kukabiliana na Ebola na vitisho vingine vipya vya afya vitakavyoibuka.
“Kenya inakaribisha ushirikiano unaoimarisha usalama wa afya duniani na kuendeleza dhamira yetu ya pamoja ya kulinda maisha.”
Awali gazeti la New York Times, liliripoti kuwa serikali ya Donald Trump, inapanga kuwapeleka raia wa Marekani walioambukizwa virusi vya Ebola nchini Kenya kwa uangalizi na matibabu, hata hivyo, taarifa ya Wizara ya Afya ya Kenya haijatoa maelezo ya kutosha kuhusu kituo hicho kinachopendekezwa cha karantini kwa raia wa Marekani.
“Mipango yoyote kuhusu ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya itaongozwa na sheria za kitaifa za Kenya, kanuni za afya ya umma, viwango vya usalama wa kibayolojia pamoja na wajibu wa serikali wa kulinda afya na ustawi wa wananchi wa Kenya,” alisema Waziri wa Afya Aden Duale katika taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari.
Pia unaweza kusoma:
Iran imesema pendekezo la Marekani, huenda likachangia Mlango bahari wa Hormuz kufunguliwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Televisheni ya serikali ya Iran imesema Tehran imepokea hati isiyo rasmi ya makubaliano ya kumaliza vita kati yao na Marekani.
Kulingana na hati hiyo, Iran inafaa kurejesha viwango vya usafiri kupitia Mlango bahari wa Hormuz hadi viwango vya kawaida chini ya mwezi mmoja, huku Marekani ikitarajiwa kuondoa majeshi yake karibu na Iran pamoja na kiziuzi cha baharini katika mlango bahari wa Hormuz.
Pia unaweza kusoma:
Raia wa Ghana warejea nyumbani kutoka Afrika Kusini, baada ya maandamano ya kupinga wahamiaji

Chanzo cha picha, Reuters
Raia wa Ghana wanaoishi Afrika Kusini, mapema leo wamekuwa wakipanga foleni katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa OR Tambo, mjini Johannesburg, kurejea nchini Ghana, kufuatia wimbi la maandamano ya kupinga wahamiaji nchini Afrika Kusini.
Watu 300, wakiwemo wanawake na watoto ni miongoni mwa wale wanaorejea nchini Ghana kwa hiari yao, kutokana na ukosefu wa usalama kwa kulengwa na wale wanaopinga wahamiaji.
Mamlaka za Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana na mamlaka za Ghana kuandaa orodha ya takriban watu 800 ambao wameonyesha nia ya kutaka kuondoka nchini humo.
Mchakato huu wa kuwarejesha raia wa Ghana nyumbani kwao, umetokana na wimbi la maandamano la kupinga wahamiaji, na kuwatuhumu kwa kuongeza viwango vya uhalifu na kuchukua nafasi zao za ajira.
Pia unaweza kusoma:
DRC: Mamlaka zasema kudhibiti virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo huenda ikachukua miezi sita

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka za afya za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),zinasema kuwa takriban watu 1000 wameonyesha dalili ya kuwa na ugonjwa wa Ebola, ila visa 105 pekee ndivyo vimethibitishwa na maabara, kufikia sasa.
Mlipuko wa ugonjwa huo unaendelea kuzua wasiwasi huku idadi ya vifo ikiripotiwa kufika 223.
Mamlaka za afya sasa zinawatafuta watu waliokutana au kutangamana na wanaougua ugonjwa wa Ebola kwa uangalizi zaidi.
Mlipuko wa Ebola umeripotiwa katika wilaya ya Ituri, Kivu kusini na Kivu kaskazini.
Pia unaweza kusoma:
Trump aongeza idadi wakimbizi wanaoingia Marekani, ili kuwaruhusu wazungu wa Afrika Kusini kuingia nchini humo

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump, ameongeza kiwango cha idadi ya wakimbizi wanaoruhusiwa kuingia nchini humo, na kufikia watu 10,000 mwaka huu, ili kuruhusu wazungu ambao ni raia wa Afrika Kusini kuingia Marekani.
Wazungu wa Afrika Kusini, wanaojulikana kama Afrikaner, wanasemekana kukabiliwa na ubaguzi wa rangi unaochochewa kisiasa.
Trump, alikuwa amesitisha mpango wa kuruhusu wakimbizi kuingia nchini humo mwezi Januari mwaka wa 2025 alipoingia madarakani, lakini baadaye akaanzisha mpango wa kuwaleta wazungu wa Afrika Kusini nchini humo.
Serikali ya Afrika Kusini imekanushaa tuhuma za kuwanyanyasa na kuwabagaua kirangi wazungu hao.
Israel yatangaza kumuua kamanda wa Hamas baada ya shambulizi la anga Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Israel imesema imemuua Mohamed Odeh, Kamanda wa tawi la kijeshi la Hamas, katika shambulizi lililotekelezwa Gaza Jumanne, siku chache baada ya mtangulizi wake kuuawa katika shambulizi jingine kama hilo.
Kwa mujibu wa madaktari na mashuhuda wa eneo hilo, angalau Wapalestina watatu waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi kubwa lililolenga jengo la makazi katika moja ya masoko yenye shughuli nyingi zaidi mjini Gaza.
Shirika la usalama la Israel, Shin Bet, pamoja na jeshi la nchi hiyo, vilisema katika taarifa ya pamoja kuwa majengo aliyokuwa akijificha Odeh yalilengwa baada ya miezi kadhaa ya ufuatiliaji wa kijasusi kuhusu mienendo yake.
Shambulizi hilo ni miongoni mwa mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Gaza licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas kuendelea kuwepo.
Mashambulizi hayo yalipiga ghorofa tatu za juu za jengo la al Kayali katikati mwa mji wa Gaza, wakati eneo hilo lilikuwa na shughuli nyingi za wananchi waliokuwa wakifanya manunuzi ya sikukuu ya Eid al Adha.
Jeshi la Israel (IDF) na Shin Bet yamesema:
“Katika operesheni ya pamoja dhidi ya gaidi Mohamed Odeh, majengo kadhaa katikati mwa Gaza yaliyokuwa maficho yake yalilengwa baada ya miezi ya ufuatiliaji wa kiintelijensia dhidi yake na washirika wake.”
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa nyumba ya karibu inayomilikiwa na mwanachama wa Hamas aliyeshiriki mashambulizi ya Oktoba 7 pia ililengwa.
Vikosi vya uokoaji vilifika haraka eneo la tukio lakini vilikumbana na ugumu wa kufikia ghorofa za juu kutokana na uharibifu mkubwa na msongamano wa watu.
Mashuhuda walisema makombora angalau matano yalilipiga jengo hilo karibu kwa wakati mmoja kutoka pande tofauti.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ilisema Mohamed Odeh alikuwa miongoni mwa watu waliopanga mashambulizi ya Oktoba 7 mwaka 2023.
Taarifa hiyo iliongeza:
“Odeh alikuwa anahusika na mauaji, utekaji na kujeruhiwa kwa raia wengi wa Israel pamoja na wanajeshi wa IDF.”
Soma zaidi:
Marekani kuweka kituo cha karantini Kenya kwa raia wake walioambukizwa Ebola DRC

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Marekani inatarajiwa kupeleka maafisa wa afya ya umma nchini Kenya ili kusimamia kituo kinachoweza kutumika kwa karantini, kufuatia mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kituo hicho, ambacho hadi Jumanne Mei 26, 2026 kilikuwa bado kinasubiri idhini ya serikali ya Kenya, kinalenga kuwahifadhi raia wa Marekani waliotangamana na walioambukizwa na virusi hivyo au walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa, pamoja na wale watakaothibitishwa kuwa wameambukizwa.
Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya maafisa wa Huduma ya Afya ya Umma ya Marekani, kitengo kilicho chini ya Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu, tayari wamepata taarifa za kujiandaa kupelekwa nchini Kenya.
Hatua hiyo inakuja wakati mamlaka za afya zikikabiliana na mlipuko unaosambaa kwa kasi wa aina adimu ya Ebola katika DRC na Uganda.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko huo wa aina ya Bundibugyo kuwa dharura ya afya ya kimataifa, likibainisha kuwa ni mojawapo ya milipuko mikubwa zaidi ya ugonjwa huo kuwahi kurekodiwa.
Ebola ni ugonjwa hatari na mara nyingi husababisha vifo, unaoambukizwa kupitia mgusano wa moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.
Waislamu kote duniani wanaadhimisha sherehe za Eid al-Adha

Chanzo cha picha, Getty Images
Waislam kote duniani wanasherehekea sherehe za Idd al-Adha, zinazofanyika wakati wa Hija inayofanyika kila mwaka mjini Mecca.
Sherehe hiyo ambayo pia hufahamika kama sherehe ya kutoa kafara, ni moja kati ya sherehe kubwa za kiislam.
Ni kumbu kumbu ya kujitolea kwa utashi kwa Abraham kumtoa kafara mwanae kwa Mungu na wakati wa sherehe hii waislam hutoa kafara wanyama.

Chanzo cha picha, EPA
Maelezo ya picha, Wanawake wakihudhuria ibada katika jimbo la Bandeh Aceh, Indonesia 
Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Katika soko la wanyama la Ashmun cattle nchini Misri, wafanyabiashara wakiuza wanyama kwa ajili ya kafara kabla ya sherehe za Eid al Adha Kiongozi mwingine wa timu ya taifa ya Iran ajiondoa kuelekea Kombe la Dunia

Chanzo cha picha, IRNA
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirikisho la Soka la Iran, Ali Khatir, ametangaza kujiondoa katika msafara wa timu ya taifa ya wanaume ya Iran kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia. Amekuwa mtu wa tatu kutoka uongozi wa shirikisho hilo kujiondoa katika safari hiyo.
Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, liliripoti Jumanne kwamba Khatir alimwandikia barua rais wa shirikisho hilo, Mehdi Taj, akieleza kuwa kutokana na majukumu mengi aliyonayo na kutokuwapo kwa ulazima wa kushiriki katika mashindano hayo, hataandamana na msafara wa timu.
Awali, wajumbe wengine wa bodi hiyo, Heydar Baharvand na Mohammad Rahman Salari, pia walikuwa wamejiondoa katika msafara huo.
Hatua hiyo inakuja wakati bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu maombi ya visa vya kuingia Marekani na Canada kwa wanachama wa msafara wa Iran. Hata hivyo, Mexico, ambayo ni mmoja wa wenyeji wa Kombe la Dunia, imekubali kuwa mwenyeji wa kambi ya maandalizi ya timu ya taifa ya Iran.
Wakati huo huo, nahodha wa Iran, Alireza Jahanbakhsh, pamoja na mshambuliaji mpya mwenye asili ya Iran, Denis Dargahi, wamejiunga na kambi ya timu nchini Uturuki ili kukamilisha kikosi kinachoendelea na maandalizi.
Iran inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Gambia siku ya Ijumaa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano hiyo.
Iran yasema dola bilioni 12 za fedha zilizozuiliwa bado zipo Qatar baada ya mpango wa kuzihamisha kuzuiwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera ya Kigeni ya Bunge la Iran, Ahmad Bakhshish Ardestani, amezungumzia fedha za Iran zilizozuiliwa nje ya nchi.
Amesema kuna tofauti kuhusu kiasi cha fedha hizo, ambapo Iran inadai ni dola bilioni 25, wakati Marekani inasema ni takribani dola bilioni 12 zilizoko Qatar.
Mbunge huyo amesema kuwa siku chache zilizopita kulikuwa na mpango wa kuingiza fedha hizo Iran kupitia Urusi, lakini Marekani ilizuia mpango huo. Kwa sasa, anasema kiasi hicho cha takribani dola bilioni 12 bado kipo Qatar.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, ujumbe wa Iran ulioongozwa na Mohammad Baqer Qalibaf ulifanya ziara Qatar kujadili mali za Iran zilizozuiliwa kutokana na vikwazo vya Marekani.
Hakuna taarifa rasmi kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo, lakini vyombo vya habari viliripoti kuwa kulikuwa na maelewano fulani yaliyofikiwa.
Nasa yazindua hatua zinazofuata za kujenga kituo cha kudumu mwezini

Chanzo cha picha, Getty Images
Nasa imetoa maelezo ya vifaa inayopania kupeleka anga za juu ikiwa ni pamoja na roboti, ndege zisizo na rubani na magari ambayo kama sehemu ya mipango ya Marekani ya kujenga kituo cha anga mwezini.
Kampuni ya anga ya juu ya mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos ya Blue Origin ni mojawapo ya makampuni kadhaa yaliyochaguliwa kujuunda mashine hizo.
Marekani inataka kuwarejesha Wamarekani kwenye Mwezi kabla ya Rais Donald Trump kuondoka madarakani mwaka 2029.
Lakini Nasa inashindana na China kurudisha wanadamu mwezini, kumaanisha shirika hilo la anga liko chini ya shinikizo la kushinda mbio mpya za anga.
China inaendelea mbele na mipango yake ya kuwapeleka wanadamu Mwezini ifikapo 2030.
Siku ya Jumatatu ilizindua chombo chake cha anga za juu cha Shenzhou-23, na kutuma wafanyakazi wa wanaanga kwenye kituo cha anga za juu cha Tiangong nchini humo.
Mnamo Machi, Nasa ilitangaza mpango wa dola bilioni 20 wa kujenga kituo cha kudumu itakayoendeshwa na nguvu ya nyuklia na nishati ya jua kwenye ncha ya kusini ya Mwezi ifikapo 2032.
Msimamizi wa Nasa Jared Isaacman alisema Jumanne kwamba matangazo hayo yanamaanisha Marekani "haitaachana tena na harakati zake mwezini".
Soma zaidi:
Makumi ya watu wauawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Makumi ya watu wameuawa katika wimbi kubwa la mashambulizi ya Israel kusini na mashariki mwa Lebanon, baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuapa kuongeza hatua za kijeshi dhidi ya Hezbollah.
Takriban watu 31 wameuawa katika wimbi la hivi punde la mashambulizi, wakiwemo watoto kadhaa, wizara ya afya ya Lebanon ilisema.
Jeshi la Israel limesema lilipiga zaidi ya maeneo 100 ya miundombinu ya Hezbollah na wapiganaji wake katika siku ambayo ilikuwa ni moja ya usiku mzito zaidi wa mashambulizi ya mabomu tangu usitishaji vita uliosimamiwa na Marekani uanze kutekelezwa katikati ya mwezi Aprili.
Haya yanajiri baada ya Netanyahu kusema Jumatatu kwamba ametoa maagizo ya "kushinikiza juhudi zaidi" katika kulenga Hezbollah.
Akizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri la usalama siku ya Jumanne, alisema Israel "inazidisha operesheni nchini Lebanon".
"IDF [Vikosi vya Ulinzi vya Israel] vinashirikiana na vikosi vikubwa ardhini na kuchukua eneo kubwa," alisema, akiongeza kuwa "wanaimarisha eneo la usalama" kulinda jamii za kaskazini mwa Israel kutokana na mashambulizi ya Hezbollah.
Usitishaji wa mapigano umekuwa ukikiukwa mara kwa mara na pande zote mbili, na hatua hiyo inatishia kusambaratisha mazungumzo tata yanayoendelea ili kumaliza vita kati ya Marekani, Israel na Iran.
Mashambulio ya anga ya Israel yameendelea kila siku, hasa kusini mwa Lebanon, wakati Hezbollah imekuwa ikirusha maroketi na ndege zisizo na rubani kulenga jamii za kaskazini mwa Israel na wanajeshi wa Israel wanaokalia maeneo ya kusini mwa Lebanon.
Soma pia:
Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.
