Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Afganistan: Je, kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani kutaifanya al-Qaeda kurejea tena?
Kutokana na agizo la Rais wa Marekani Joe Biden, wanajeshi wa Marekani waliosalia Afghanistan wameondoka kwa haraka. Hatua ambayo imetoa mwanya kwa kundi la Taliban kushamiri. Hivi karibuni, walishambulia tena miji na kukalia vituo vya jeshi, huku ikisemekana kuwa jeshi la Afghanistan lisilo na nguvu ama lilijisalimisha au lilitoroka.
Wafuatiliaji wa mambo wanaamini kuwa ugaidi wa kimataifa unarejea.
Mchambuzi wa masuala ya usalama na ugaidi Dkt. Sajan Goher ameiambia BBC kuwa: "Kujiondoa kwa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan kunafanya serikali ya nchi hiyo kushindwa kuzuia kuepusha kurejea kwa Taliban."
Hali hiyo pia inatoa fursa kwa al-Qaeda kujenga tena mtandao wake, huku baadhi wakiamini mtandao huo "unaweza kufikia kiasi cha kuwa na uwezo wa kutekeleza mashambulizi kote duniani." Wakuu wa mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi wana wasiwasi lakini je madai yao yana msingi wowote?
Taliban wamesambaa zaidi
Kuna mambo mawili ya msingi: Kwanza, Taliban - wanamgambo wenye msimamo mkali walio tawala Afghanistan kutoka mwaka 1996 hadi mwaka 2001 wanarejea kwa namna fulani.
Sasa hivi, wanadai kuwa hawana nia kuchukua mji mkuu kwa lazima lakini tayari wamekuwa wenye ushawishi mkubwa katika maeneo mengi nchini humo na bado hawajaachana na nia yao ya kufanya nchi hiyo kuwa ya Kiislamu chini ya uongozi wao mkali.
Pili, al-Qaeda na vikosi vingine vya kigaidi katika eneo hilo kama tawi la Khorosan la Dola la Kiislamu la Iraq na Syria (ISIS) maarufu kama "Islamic State Khorasan Branch" vitakuwa ni vyenye kutafuta kufaidika kutokana na hatua ya wanajeshi wa Marekani, hivyo basi kuwapa nafasi ya kutawala maeneo mengi.
Nchi hii ina milima mingi na emabonde, kwa hiyo, kuna maeneo mengi ya kujificha kwa makundi ya kigaidi.
Lakini kabla ya hapo, Shirika la Usalama wa Taifa la Afghanistan, lilifanikiwa kudhibiti kwa kiasi fulani vitisho kupitia ushirikiano wa karibu na wanajeshi wa Marekani na vikosi vingine maalum.
Mipango ya mashambulizi na milipuko bado inatokea lakini si mashambulizi yote yaliyopangwa yanafanikiwa kwa sababu wanaoshughulika na uchunguzi wa taarifa au kunasa mawasiliano ya simu wanawezesha wanajeshi wa nchi za Magharibi na vikosi maalum vya Afghanistan kutekeleza kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Huendeleza shughuli zao kutoka kambi ya Afghanistan na kawaida wanaweza kujibu shambulizi ndani ya sekunde chache. Wanachukua helikopta hadi eneo la tukio usiku wa manane na kukabiliana na adui bila yeye kujua.
Hivyo kuondoka kwa wanajeshi hao ni pigo kwa serikali ya Afghanistan katika kudhibiti Taliban lakini pia kuwadhibiti magaid wa kimataifa.
Tishio kwa Uingereza
Taliban iliwahi kuweka wazi kwamba watachukulia wanajeshi wowote wa nchi za Magharibi waliosalia Afghanistan wenye jukumu la kulinda uwanja wa ndege wa Kabul na ubalozi wa Marekani kama ukiukaji wa mkataba wa Doha. Miongoni mwao ni Marekani kuahidi kuondoa wanajeshi wote wa Marekani kabla ya Septemba 11.
Pia waliahidi kushambulia wanajeshi wengine. Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson atakuwa mwenyekiti wa mkutano wa Baraza la Usalama wa Taifa kujadiliana kuhusu usaidizi wa kijeshi wa Uingereza unaostahili kufika mwisho na upi unaostahili kuendelea.
Alex Younger, aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la kijasusi la Uingereza (MI6) amezungumza na shirika la habari la Sky News na kusema: "Ikiwa wanajeshi wa Magharibi wataondoka Afghanistan, tishio la ugaidi Uingereza litaongezeka."
Hali hiyo inaliacha taifa hilo katika njia panda: Kuacha huduma ya kikosi maalum cha jeshi la anga au wafanyakazi wengine maalum wa jeshi bila ya jeshi la Marekani au usaidizi wa ulinzi wa anga, hivi karibuni au siku za baadaye kundi la Taliban litajitokeza tena.
Ikiwa watu watahamishwa kwa ombi la Taliban, wanajeshi wa nchi za Magharibi hawataweza tena kuchukua hatua kwa haraka kuchunguza au kukabiliana na vitendo vya ugaidi.
Ishara mbaya
Kiongozi wa kundi la al-Qaeda Osama bin Laden ambaye alihamisha kundi hilo kutoka Sudan hadi Afghanistan mwaka 1996 hadi 2001, na hapo Taliban ikatoa hifadhi kwa Osama.
Saudi Arabia ilikuwa moja ya nchi tatu pekee duniani ambazo zilitambua utawala wa Taliban nchini Afghanistan. Mkurugenzi wa shirika la kijasusi la Saudia Mwana Turki al-Faisal akatumwa nchini humo kama mjumbe kushawishi Taliban iweze kukumkabidhi, bin Laden.
Kundi la Taliban lilikataa maombi hayo wakisema huyo ni mgeni wao ambaye watamlinda kwa gharama yoyte.
Baada ya maelfu ya watu wakauawa na kujeruhiwa vibaya katika mashambulizi ya Septemba 11, yaliopangwa na kuratibiwa kutoka kambi ya al-Qaeda nchini Afghanistan, Taliban pia ilikataa kumkabidhi Bin Laden kwa Marekani.
Uamuzi huo wa Taliban uliilazimu Marekani na washirika wake kuivamia kijeshi Afghanistan miaka 20 ilopita.
Hata hivyo, Jenerali Sir Nick Carter, Mkuu wa Jeshi la Uingereza, ambaye ameongoza vikosi kadhaa nchini Afghanistan anaamini kwamba uongozi wa Taliban huenda umejifunza kutokana na makosa waliyofanya awali.
Anaamini kuwa lazima Taliban wawe na matumaini ya kugawana au kuchukua madaraka, lakini safari hii hawatataka kuwa wasiowezekana kimataifa.
Changamoto ni kwamba: Wanachama wa Taliban walioshiriki mazungumzo ya amani hivi karibuni wataendelea kujitenga na jitihada za kuleta amani na kutumia njia hiyo kama mabadilishano na jumuiya ya kimataifa ili iwakubali.
Lakini katika nchi yenye usimamizi dhaifu kama vile Afghanistan, hata Taliban wakiingia madarakani hakutakuwa na uhakika kwamba kundi la al-Qaeda litachukua udhibiti ambako kunaweza kulisaidia kuwa na matawi yao kwengineko kwa urahisi kabisa katika maeneo ya vijijini.