Ifahamu droni ya baharini iliyotumiwa na Marekani kuwaokoa wanajeshi wake

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Jeshi la Marekani linasema lilitumia chombo cha majini kisicho na muelekezi kuwaokoa wafanyakazi wawili kutoka kwa helikopta ya Jeshi la Marekani iliyoanguka katika pwani ya Oman mapema wiki hii.

Hiki ni mara ya kwanza ambapo chombo kisicho na muelekezi kimetumika kutekeleza shughuli ya uokoaji.

Kwa mujibu wa Rais Donald Trump, helikopta ya Apache ilidunguliwa na Iran karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz, njia kuu ya majini ambayo imefungwa tangu kuanza kwa vita vya Iran.

Wanajeshi hao wawili "waliokolewa ndani ya takriban saa mbili na wako katika hali nzuri," Kamandi kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) iliripoti.

BBC Verify imechanganua taarifa zilizopo kuhusu chombo hiki kisicho na muelekezi na jinsi operesheni hiyo ya uokoaji ilivyofanyika.

Droni ya majini ya Marekani ikoje?

Centcom imethibitisha kuwa Corsair, chombo cha majini kisicho na muelekezi iliyotengenezwa na kampuni ya droni ya wanamaji ya Texas, ilitumika katika uokoaji.

Ina urefu wa mita 7.3, uwezo wa kubeba mzigo wa takriban kilo 450 na inaweza kusafiri kwa zaidi ya knots 35 (kama kilomita 65 kwa saa), kulingana na tovuti ya kampuni hiyo.

"Corsair inakaribia ukubwa wa mashua ya wavuvi. Imeundwa kubeba mizigo na pengine ina nafasi ya watu watatu hadi wanne," anasema Bryan Clark, mtaalamu wa ndege zisizo na rubani katika Taasisi ya Hudson.

Clark anaongeza kuwa chombo hicho kina kamera ya digrii 360, mfumo wa rada ya urambazaji wa masafa marefu, na sensa ya redio ya kielektroniki ya kunasa mawasiliano kwa lengo la kijasusi.

"Corsair imekuwa ikifanya kazi kwa miaka michache sasa. Jeshi la Wanamaji la Marekani lina takriban droni 50 za majini za aina hiyo," asema Dk. Stacie Pettyjohn, mtaalamu wa masuala ya kijeshi ya Marekani katika Kituo Kipya cha Usalama cha Marekani.

Anafafanua kuwa, "kwa ujumla chombo hiki hutumika kwa ajili ya uchunguzi wa vilipuzi vya majini au kazi za ufuatiliaji, lakini Jeshi la Wanamaji linaendelea kufanya majaribio ya utenda kazi wake katika mlango wa bahari ili kutathmini uwezo wake."

Droni hiyo ya baharini inaendeshwa na Task Force 59, kitengo cha kwanza cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kinachojitolea kwa mifumo isiyo na rubani, iliyoundwa mnamo 2021.

Marekani ilianza kuipeleka Mashariki ya Kati mwezi Machi, kama sehemu ya mpango wa Pentagon wa kupanua matumizi ya ndege zisizo na rubani.

Mwaka jana, Jeshi la Wanamaji lilimpa mtengenezaji wa Corsair mkataba wa uzalishaji wa dola milioni 392 milioni kwa vyombo vyake huru.

Shughuli ya uakoaji ilifanyika vipi?

Ingawa droni hiyo ya majini inaweza kuendeshwa bila muelekezi, wataalam hao wawili walioshauriwa na BBC Verify walionyesha kuwa huenda shughulizingine zilifanywa na wanadamu wakati wa uokoaji.

"Katika operesheni hii, kuna uwezekano mkubwa ilidhibitiwa kwa mbali na mtu anayetumia temoti, ili kuhakikisha kuwa inafika eneo halisi la wafanyakazi," Clark alisema.

"Ingeelekezwa kwenye eneo linalojulikana la watu walioharibikiwa na meli, ambao wangeabiri, kama vile wangepanda mashua kwenye bahari kuu," aliongeza.

Corsair ilitumika kwa shughuli hiyo kutokana na "ukaribu na uwezo wake," alisema Kapteni Tim Hawkins, Msemaji wa Centcom, baada ya uokozi.

"Chombo hicho kisichoelekezwa na mtu ilitumika badala ya kutuma meli au helikopta ambayo watu waliomo ndani huenda waka shambuliwa," alisema Dr. Pettyjohn.

Alisema kuwa, "ingawa uokoaji sio lengo kuu ya chombo hiki, ilionekana wazi kuwa muhimu kwa shughuli hatari kama hii."

Wanajeshi wa Marekani waliokolewa mwendo wa saa 3:30 asubuhi siku ya Jumanne (saa za huko) na kupelekwa sehemu nyingine baharini, kulingana na Kapteni Hawkins.

"Baadaye, walipandishwa kwenye helikopta ili kuondolewa katika eneo hilo," aliongeza.

Je, droni za baharini hutumiwa wapi kwingine duniani?

Utumiaji wa droni za baharini umeongezeka katika vita kati ya Urusi na Ukraine kama ilivyowahi kuripotiwa na BBC Verify.

Ukraine imepakia vilipuzi kwenye chombo hicho na kushambulia meli za kijeshi za Urusi, lakini hakuna rekodi yoyote inayoonyesha kutumika kwa shughuli za uokoaji.

"Boti nyingi zinazotumiwa na Ukraine ni ndogo, inakaribia ukubwa wa jet ski, na hazina uwezo wa kubeba mtu," Clark anasema.

Waasi wa Houthi nchini Yemen pia wameendesha boti zinazofahamika kama ndege zisizo na rubani (au kamikazes), na Iran imetumia meli zisizo na rubani katika mzozo wa sasa kushambulia meli zinazojaribu kuvuka Mlango-Bahari wa Hormuz.

"Wahouthi na Wairan tayari walikuwa na ndege zisizo na rubani za baharini, lakini Waukraine waliipeleka teknolojia hii katika ngazi nyingine na kuonyesha kile ambacho nchi nyingine zinaweza kufanya," anasema Dk. Pettyjohn.

"Utengenezaji wa droni za baharini za Marekani kwa ulitokana na vita vya Ukraine na ubunifu unaoonekana huko," anasema.