Kutoka pomboo hadi tembo: Wanyama wanaopenda kulewa

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Iwe ni vilevi vinavyotengenezwa kiasili porini au vile vilivyotengenezwa na binadamu, baadhi ya wanyama hupenda kutafuta vitu vinavyowasaidia kulewa au kubadilisha hali ya fahamu zao.

Kwa mamia ya miaka, kumekuwa na simulizi kutoka sehemu mbalimbali duniani kuhusu wanyama wanaopenda kulewa kwa kutumia kemikali zinazozalishwa kiasili porini. Baadhi hula matunda yaliyovundika kwa wingi, huku wengine wakijipatia chakula katika mashamba ya mipapai inayozalisha kasumba.

Imekuwa vigumu kubaini ni kwa kiasi gani ushahidi huu wa simulizi ni wa kweli na ni kwa kiasi gani tunawahusisha wanyama na tabia zetu sisi binadamu. Hata hivyo, ushahidi na tafiti zaidi zimeanza kujitokeza, zikionyesha kwamba katika baadhi ya matukio, ni kweli kuna wanyama wanaopenda kulewa.

1. Pomboo

Licha ya samaki aina ya pufferfish kuwa miongoni mwa viumbe wenye sumu kali zaidi baharini, pomboo wachanga wameonekana wakicheza naye kwa kumrushiana na kumchokoza ili amwachie kiasi kidogo cha sumu inayoshambulia mfumo wa fahamu.

Sumu hiyo inaweza kuua, lakini kwa kiwango kidogo inaweza kuwa na athari za kulevya. Picha za video za BBC zinaonyesha pomboo wakionekana kufurahia hali hiyo na hata kumrushiana samaki huyo kutoka mmoja hadi mwingine ndani ya kundi lao.

Baada ya kupata athari wanazotafuta, pomboo hao humwachia pufferfish, ambaye hujivimbua na kuogelea zake.

2. Wallaby

Tasmania (jimbo la kisiwa lililopo nchini Australia) huzalisha takribani nusu ya kasumba yote inayolimwa kihalali duniani. Kasumba hiyo hutumika kutengeneza mofini na dawa nyingine za kutuliza maumivu.

Mara kwa mara, wallaby wenye shingo nyekundu huvamia mashamba hayo na kula vichwa vya mipapai. Wakulima wameripoti kuwakuta wallaby wakiwa wamechanganyikiwa, wakionekana kulewa na kutangatanga mashambani.

3. Sokwe

Sokwe wa porini wamepigwa picha wakila na kugawana matunda yenye pombe.

Katika utafiti uliofanyika mwaka 2025, timu ya watafiti ikiongozwa na Chuo Kikuu cha Exeter iliweka kamera katika Hifadhi ya Taifa ya Cantanhez nchini Guinea-Bissau, Afrika Magharibi. Kamera hizo ziliwanasa sokwe wakigawana matunda yaliyovundika ya mti wa mkate wa Afrika, ambayo yamethibitishwa kuwa na ethanoli, aina ya pombe.

Kamera zilizowashwa na mwendo zilirekodi sokwe wakigawana matunda hayo katika matukio 10 tofauti.

Ingawa kiwango cha pombe katika matunda hayo kilikuwa kidogo kwa kiasi, kiwango cha juu kilikuwa sawa na asilimia 0.61 ya pombe kwa ujazo (ABV).

Watafiti wanapendekeza kwamba huenda haya ni matokeo machache tu yanayoonekana, huku hali halisi ikiwa kubwa zaidi. Kwa kuwa matunda ni sehemu kubwa ya chakula cha sokwe, hata kiwango kidogo cha pombe kinaweza kukusanyika mwilini na kusababisha unywaji wa kiasi kikubwa zaidi ya kinavyodhaniwa.

Lakini si wanyama wa maeneo ya kitropiki pekee wanaoonyesha tabia hiyo.

4. Swala wa kaskazini (Reindeer)

5. Nyuki

Utafiti unaonyesha kwamba, kama binadamu, nyuki pia huvutiwa na kafeini. Tofauti na sisi, hata hivyo, hawahitaji kutumia pesa kununua kahawa kila asubuhi.

Nyuki hupata kafeini kwa kunywa nekta ya maua fulani, kama yale ya mimea ya kahawa na jamii ya michungwa. Kafeini hiyo huimarisha kumbukumbu zao kuhusu mimea husika, na kuwafanya warudi kwenye aina hizo za maua mara kwa mara wanapokusanya nekta na kusaidia uchavushaji.

Katika jaribio lililotumia nekta yenye kafeini, ilibainika pia kwamba kafeini iliwafanya nyuki kucheza dansi mara nyingi zaidi.

Nyuki walikuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya dansi yao maarufu ya waggle dance - miondoko wanayotumia kuwasiliana na wenzao kuhusu mahali chanzo cha nekta kilipo.

6. Nyani aina ya Vervet

Katika visiwa vya Karibiani vya St. Kitts, Nevis na Barbados, nyani aina ya vervet wamejifunza kuiba pombe kwenye baa na kutoka kwa watalii wasiotambua kinachoendelea.

Nyani hao wamefanyiwa tafiti ili kusaidia kuelewa tabia za binadamu kuhusu unywaji wa pombe.

Jambo la kuvutia ni kwamba sehemu fulani ya makundi hayo ya nyani hupendelea kunywa pombe kidogo sana au kutokunywa kabisa. Asilimia ya nyani wenye tabia hiyo inafanana na ile inayopatikana katika idadi ya watu wanaopendelea kutokunywa pombe au kunywa kiasi kidogo.

7. Kasuku aina ya Lorikeet

Mwanzoni mwa msimu wa mvua kaskazini mwa Australia, makumi ya kasuku aina ya red-collared lorikeet wanaoonekana kulewa hukusanywa katika mitaa ya jiji la Darwin.

Daktari wa mifugo Stephen Cutter, anayefanya kazi katika Hospitali ya Wanyama ya Ark, anasema ndege hao hushindwa kuruka na hupata ugumu wa kupanda au kujisawazisha wanapokuwa kwenye matawi au sehemu wanazotua.

Inaaminika kwamba ndege hao hula maua ya mti wa Schotia brachypetala, ulioletwa kutoka Afrika Kusini na unaojulikana katika eneo hilo kama "mti wa kasuku walevi".

Maua ya mti huo yana nekta nyingi kiasi kwamba huanza kuvundika kabla ndege hawajaila. Matokeo yake ni kwamba kasuku hao humeza kiasi kikubwa cha pombe wanapokula nekta hiyo.

8. Paa aina ya Elk

Kusini mwa Uswidi, elk mmoja aliripotiwa kula matufaha yaliyokuwa yakivundika na kukwama miguu yake mirefu ya mbele alipokuwa akijaribu kufikia matunda yaliyokuwa juu zaidi.

Ilibidi wazima moto wamwokoe mnyama huyo kwa kumkata sehemu iliyokuwa imemtega. Inasemekana alikuwa katika hali ya kulewa au kuchanganyikiwa sana.

Matunda yoyote yenye sukari ya kutosha yanaweza kuvundika kiasili.

Hata hivyo, bado hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba kiasi cha pombe kinachozalishwa na matunda hayo kinaweza kumlewesha mnyama mkubwa kama elk.

9. Tembo

Tembo wa Afrika Kusini wamepigwa picha wakionekana kulewa baada ya kula matunda ya mti wa marula yaliyovundika. Hata hivyo, kama ilivyo kwa baadhi ya wanyama wengine, huenda wasile matunda ya kutosha kupata athari za ulevi.

Nadharia nyingine inapendekeza kwamba huenda tembo hao wanakula mabuu ya wadudu aina ya mende yaliyomo kwenye magome ya miti ya marula. Mabuu hayo yanaweza kuwa na sumu zinazoshambulia mfumo wa fahamu.

Kwa mujibu wa nadharia hiyo, kula mabuu hayo pamoja na matunda ya marula kunaweza kusababisha hali inayofanana na ulevi kwa tembo hao.

Ingawa ushahidi hutofautiana kati ya spishi moja na nyingine, tafiti zinaonyesha kwamba si binadamu pekee wanaovutiwa na kemikali zinazoweza kubadilisha hali ya fahamu. Katika mazingira mbalimbali duniani, baadhi ya wanyama wameonekana kutafuta vitu vinavyoweza kusababisha athari zinazofanana na ulevi.