Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Dalili ndogo 5 ambazo watu wengi huzipuuzia, lakini zinaweza kuashiria ugonjwa mkubwa
Kila mtu ana mtazamo tofauti kuhusu afya yake. Wapo wanaomwona daktari mara tu wanapoanza kuhisi dalili ndogo, huku wengine wakisubiri hadi hali iwe mbaya zaidi. Lakini wataalamu wa afya wanaonya kuwa baadhi ya dalili zinazoonekana kuwa za kawaida zinaweza kuwa ishara ya ugonjwa unaohitaji matibabu ya haraka.
Kuanzia kucha kubadilika rangi, midomo kuwa ya bluu, kupungua uzito bila sababu
hadi kukoroma kupita kiasi ni dalili ambazo hupaswi kuzipuuza.
Mabadiliko yoyote mapya yanayodumu, hata kama yanaonekana madogo, yanapaswa kufuatiliwa.
Baadhi ya magonjwa makubwa, ikiwemo saratani, yanaweza kutokutoa dalili za wazi katika hatua za mwanzo. Vivyo hivyo, maambukizi kama VVU au homa ya ini yanaweza kuendelea kwa muda bila dalili zinazoonekana.
Dalili na ishara ni tofauti
Katika tiba, ishara ni jambo linaloweza kuonekana au kupimwa na watu wengine, kama vile upele, homa au kiwango cha juu cha sukari kwenye damu.
Dalili, kwa upande mwingine, ni hali anayohisi mgonjwa pekee, kama maumivu, kizunguzungu au mlio masikioni. Dalili hizi mara nyingi huwa ishara ya awali kwamba kuna jambo lisilo la kawaida mwilini.
Hizi ni baadhi ya dalili ambazo hazipaswi kupuuzwa.
1. Kupungua uzito bila sababu
Kupungua uzito bila kubadili lishe au kufanya mazoezi zaidi kunaweza kuwa ishara ya ugonjwa mkubwa.
Madaktari wanashauri kwamba kupungua kwa zaidi ya asilimia tano ya uzito wa mwili bila sababu ya wazi kunapaswa kuchunguzwa.
Hali hiyo inaweza kuhusishwa na kisukari, tezi kufanya kazi kupita kiasi, saratani, magonjwa ya moyo au magonjwa ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.
2. Maumivu au shinikizo kifuani
Maumivu ya kifua, hasa yanayosambaa kuelekea taya, shingo, bega au mgongo wa juu, yanaweza kuwa dalili ya mshtuko wa moyo.
Hii ni hali ya dharura inayohitaji matibabu ya haraka.
3. Kucha kubadilika rangi
Ni muhimu kuzingatia mabadiliko ya rangi, kwenye kucha zako na vipengele vingine vinavyotumika kama tahadhari kwa magonjwa mengi. Hii inapotokea, inashauriwa kutafuta daktari wa ngozi ili kutathmini kwa kina na kufanya vipimo kama vile vya damu na zinginezo ambazo daktari anaweza kuamua.
Kucha zinazogeuka kuwa za njano, bluu, nyeupe au kuwa na mistari isiyo ya kawaida zinaweza kuashiria matatizo ya mapafu, moyo, ini, figo au upungufu wa virutubisho. Mabadiliko yanayoendelea yanapaswa kuchunguzwa na daktari.
4. Midomo kuwa ya bluu
Midomo au ngozi kuwa ya bluu inaweza kuwa ishara kwamba mwili haupati oksijeni ya kutosha.
Hali hii inaweza kusababishwa na matatizo ya moyo au mapafu na inahitaji matibabu ya haraka.
5. Kutokwa jasho usiku
Ingawa kutokwa na jasho mara kwa mara usiku kunaweza kusiwe sababu ya wasiwasi, matukio ya mara kwa mara yanaweza kuashiria shida ya kiafya.
Kutokwa jasho jingi usiku bila sababu ya mazingira ya joto kunaweza kuashiria maambukizi, mabadiliko ya homoni au magonjwa makubwa kama kifua kikuu na baadhi ya aina za saratani. Ikiwa hali hii inaendelea, ni muhimu kupata uchunguzi wa kitabibu.
Jifunze kuusikiliza mwili wako
Wataalamu wa afya wanashauri kujenga tabia ya kufuatilia mabadiliko yoyote mapya mwilini.
Ukiwa na dalili inayodumu au inayozidi kuwa mbaya, andika ilianza lini, jinsi inavyobadilika na dalili nyingine zinazoambatana nayo, kisha wasiliana na daktari.
Kugundua ugonjwa mapema huongeza nafasi ya matibabu kufanikiwa na husaidia kuepuka madhara makubwa. Mwili wako unapokutumia ishara, usizipuuzie.