Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini watu hudanganya katika mahusiano?
Mahusiano ya wapendanao hujengwa kwa uaminifu na uwazi. Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba kila mtu anatamani amani na uaminifu, uongo umekuwa moja ya changamoto kubwa inayosambaratisha mamilioni ya mahusiano duniani kote.
Mke humdanganya mume, mume humdaganya mke, wachumba hudanganyana, na hata wale ambao wako katika mahusiano yasiyo ya ndoa, nao ni wahanga wa uongo katika mapenzi.
Wataalamu wa mahusiano kama Esther Perel kutoka Ubelgji na mwandishi wa kitabu cha Mating in Captivity, wanaamini udanganyifu katika uhusiano kwa kawaida ni dalili ya tatizo kubwa ndani ya uhusiano huo.
Uongo katika mahusiano si jambo la bahati mbaya; ni tabia inayochochewa na sababu mbalimbali za kisaikolojia, kijamii, na mazingira. Makala hii inachambua sababu kuu zinazowafanya watu wadanganye wenza wao.
Kukwepa migogoro
Sababu kubwa inayowafanya watu wengi waseme uongo ni uoga. Watu wengi hawana uwezo au ujasiri wa kukabiliana na matokeo ya kusema ukweli.
Uongo huu unajumuisha kuepuka ugomvi. Mtu anaweza kudanganya kuhusu mahali alipo au fedha alizotumia ili tu kuepuka mzozo au hasira ya mwenza wake.
Pia uongo hutumika ili kulinda amani ya muda mfupi. Wasema uongo wanajidanganya kwamba uongo mdogo unalinda amani ya wakati ule, bila kujua wanatengeneza bomu la wakati ujao.
Kuficha uchepukaji
Uongo unaohusiana na uchepuka ndio unaoumiza zaidi. Mara nyingi, usaliti wa kimapenzi huenda pamoja na msururu wa uongo. Mtu anapochepuka, analazimika kutengeneza mtandao wa uongo (kuhusu muda, marafiki, na safari za kikazi) ili kulinda siri yake.
Hapa, uongo hautumiki tu kulinda uhusiano uliopo, bali unatumika kama ngao ya kuzuia aibu na kupoteza heshima kutoka kwa mwenza wako.
Kupungua kwa mapenzi
Mahusiano yanapokosa mawasiliano ya dhati na ya wazi, uongo hupata nafasi ya kushamiri. Ikiwa mmoja anahisi hasikilizwi au hapewi kile anachohitaji (kihisia au kimwili), anaweza kuanza kutafuta vitu hivyo nje ya ndoa na kudanganya ili kufunika pengo hilo.
Kushindwa kueleza hisia halisi za kutoridhika, iwe kimwili au kihisia, humfanya mtu aishi maisha ya maigizo mbele ya mwenza wake.
Kutafuta kukubalika
Wakati mwingine watu hudanganya ili waonekane wao ni bora zaidi. Hii hutokea sana mwanzoni mwa mahusiano au pale mtu anapokuwa na changamoto za kiuchumi na kijamii.
Mtu anaweza kudanganya kuhusu kazi yake, kipato chake, au historia ya maisha yake ili amvutie mwenza wake au aonekane wa hadhi ya juu.
Kukosa kujiamini (low self-esteem) humfanya mtu aamini kuwa ukweli kuhusu maisha yake hauvitii, hivyo anahitaji kuyapamba kwa uongo ili apendwe.
Mazoea na tabia
Kuna kundi la watu ambao uongo kwao ni tabia yao ya kila siku. Watu hawa hudanganya hata katika mambo madogo yasiyokuwa na ulazima wowote wa kudanganya.
Tabia hii inaweza kuwa imetokana na malezi ya utotoni, ambapo walijifunza kuwa uongo ndiyo njia pekee ya kujilinda au kupata walichotaka kutoka kwa wazazi au walezi. Kisha huitumia katika maisha yao ya mahusiano
Athari za uongo
Dkt. Ellyn Bader, mwanasaikolojia na mwanzilishi wa Taasisi ya Wanandoa, iliopo Marekani, anasema, “kadiri unavyosema uongo, ndivyo nguvu ya kuendelea na mahusiano inavyozidi kupungua.”
Madhara ya uongo katika mahusiano ni makubwa na mara nyingi hayarekebishiki. Uongo unapogundulika, unaharibu uaminifu kitu ambacho kikishapotea ni vigumu sana kukirudisha, kama kioo kilichovunjika.
Hata kama uhusiano utaendelea, mara nyingi hubaki na kovu la mashaka, chuki ndani ya nafsi, na ukosefu wa amani na hata kuchunguzana.
Ili kujenga uhusiano imara, ni vyema wenza kujenga utamaduni wa kuongea ukweli, hata kama ukweli huo unaumiza. Mahusiano yenye afya hayajengwi kwa kutokuwa na matatizo, bali yanajengwa kwa uwezo wa kukabili matatizo hayo kwa uaminifu, uwazi, na ukomavu wa kiakili.