Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mambo 5 ambayo huenda huyajui kumhusu Erling Haaland
Mara ya mwisho kwa Norway kushiriki Kombe la Dunia ilikuwa mwaka wa 1998, wakati ambapo Erling Haaland alikuwa bado hajazaliwa.
Lakini leo, timu hiyo ya nchi za Nordic, ikiongozwa na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, imefuzu kwa robo-fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuiondoa Brazil—timu iliyotwaa ubingwa mara tano—kwa msaada wa mabao mawili kutoka kwake.
Kwa hakika, mchezaji huyo mwenye kimo cha mita 1.94, anayeitwa "Android," anawania tuzo ya mfungaji bora wa michuano hiyo akiwa na mabao saba, idadi sawa na ile ya nyota wa Argentina Lionel Messi na nyota wa Ufaransa Kylian Mbappé.
"Sijui, nadhani kufunga mabao ndiyo taaluma yangu... ndivyo ilivyo tu," Haaland alisema huku akicheka siku chache zilizopita baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Senegal.
Norway tayari imeweka historia kwa kufuzu hatua ya robo-fainali kwa mara ya kwanza, lakini inaweza kufikia mafanikio makubwa zaidi iwapo itaifunga Uingereza siku ya Jumamosi na kutinga nusu-fainali.
Na matumaini ya Norway kwa mara nyingine tena yatategemea sana mabega ya Haaland, ambaye tunakuletea mambo matano kumhusu ambayo huenda hukuyafahamu.
1. Alizaliwa England
Haaland alizaliwa mwaka wa 2000 katika jiji la Leeds nchini Uingereza, ambapo baba yake, raia wa Norway Alf-Inge Haaland—mchezaji wa timu ya taifa aliyeshiriki Kombe la Dunia la mwaka 1994 nchini Marekani—aliichezea klabu ya Leeds United.
Hata hivyo, alipokuwa na umri wa miaka minne tu, familia hiyo ilirejea katika mji wao wa asili wa Bryne kusini mwa Norway, ambapo Haaland akiwa bado mdogo alianza kucheza soka (pamoja na michezo mingine, kama vile kuruka na kuendesha baiskeli).
"Nilimwona Erling kwa mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka mitano, alipojiunga na mazoezi ya ndani na kundi lililomzidi mwaka mmoja," kocha Alf Ingve Berntsen aliambia Goal.
"Miguso yake miwili ya kwanza ilisababisha mabao. Alikuwa mzuri sana tangu mwanzo, ingawa hakuwa ameichezea klabu hiyo hapo awali."
"Alikuwa mfupi kidogo kuliko wapinzani wake kwa sababu alikuwa mdogo kwa mwaka mmoja. Lakini hata kama mpinzani wake alikuwa mrefu zaidi, bado alifunga mabao. Alipokuwa na umri wa miaka 11 au 12, tulijua angefika mbali. Hata hivyo tulijua alikuwa na kile kilichohitajika kuwa mchezaji wa kimataifa wa vijana."
Akiwa na umri wa miaka 15, tayari alikuwa akiichezea klabu ya kawaida ya Bryne FK, ambayo imepanda daraja kati ya ligi ya pili na ya kwanza ya nchi yake katika historia yake yote.
Lakini uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao ulimfanya asaini kwa klabu nyingine ya Norway, Molde FK, inayoongozwa na mshambuliaji maarufu Ole Gunnar Solskjaer, ambaye anachukuliwa kuwa mmoja wa washauri wa Haaland.
Ilikuwa wakati wa kipindi chake katika klabu ya Red Bull Salzburg ya Austria ambapo mshambuliaji huyo alianza kuvutia umakini wa kimataifa na kisha akajiimarisha katika klabu ya Ujerumani ya Borussia Dortmund.
Leo ndiye mchezaji nyota wa Manchester City nchini Uingereza.
2. Ni mashine ya kufunga mabao katika timu ya taifa
Katika Kombe hili la Dunia, Haaland habebi tu matarajio ya taifa zima, bali pia matarajio ya wachezaji wote wa zamani ambao hawakufanikiwa kutimiza ndoto zao za kucheza katika Kombe la Dunia.
Mbali na kufuzu kwa mashindano mfululizo mwaka 1994 na 1998, Norway imekuwa ikikosa kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa kwa muda mrefu, huku mara ya mwisho kushiriki mashindano makubwa ikiwa ni michuano ya Euro ya mwaka 2000.
Lakini sasa wana nyota wao, ambaye umaarufu wake umekua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.
Akiwa na timu yake ya taifa, mshambuliaji huyo wa Manchester City amefunga bao katika kila moja ya mechi zake 14 rasmi zilizopita akiichezea Norway, na kufikisha jumla ya mabao 27 katika kipindi hicho.
Kwa jumla, amefunga mabao 62 katika mechi 54 za kimataifa, ikiwa ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 71.
3. Mlo wa kushangaza wa Haaland
Akiwa nje ya uwanja, Haaland ametumia mitandao ya kijamii kuonyesha maisha yake, ikiwemo mahitaji yake maalum ya lishe.
Mshambuliaji huyo kijana hutumia takriban kalori 6,000 kwa siku. Lishe yake inajumuisha vyanzo visivyo vya kawaida vya protini, kuanzia moyo na ini la ng'ombe hadi asali mbichi na maziwa.
"Ninafanya kila niwezalo ili kuwa toleo bora zaidi la nafsi yangu," mchezaji huyo kijana alisema katika mojawapo ya video zake.
Pia ana tabia madhubuti sana, ikiwemo kuzima vifaa vyote wakati wa usiku na kulala kwa angalau saa 10.
Lakini hili si jambo geni. Kwa kweli, tangu alipokuwa Red Bull Salzburg nchini Austria, wachezaji wenzake walimtazama kwa mshangao kutokana na jinsi alivyojijali kwa umakini mkubwa akiwa na umri mdogo kiasi hicho.
"Yeye ni mtaalamu wa kiwango cha juu. Wakati sisi tunacheza karata kwenye safari, yeye huwa anasoma makala za kisayansi kuhusu jinsi ya kuboresha usingizi au lishe yake. Daima hutafuta maelezo madogo kabisa anayoweza kuyaboresha ili kupiga hatua zaidi," mwenzake wa zamani, Maximilian Wober, aliambia DAZN.
4. Fahari ya kuwa Braut
Kwa kuwa alizaliwa Leeds, Haaland angeweza kuichezea Uingereza na kufikia viwango vya juu kabisa vya soka barani Ulaya na duniani, lakini hilo halikuwahi kuwa chaguo kwake.
"Licha ya hadhi yake kama nyota wa kimataifa, Haaland bado ni yuleyule," mwandishi wa habari za michezo wa Norway, Andreas Korssund, aliambia BBC Sport.
"Anajua vyema anakotoka na mara kwa mara hutembelea mji wake mdogo wa asili huko Rogaland. Anajivunia sana asili yake na huwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari vya Norway anapoiwakilisha nchi yake."
Amehamasishwa na historia ya Waviking ya Norway na anajivunia sana kuwakilisha nchi yake.
Ni uhusiano huo na asili yake ndio uliomfanya pia kuweka jina lake kamili la ukoo, Braut Haaland, mgongoni mwa jezi yake ya timu ya taifa.
Braut ni jina la ukoo la mama yake kabla ya kuolewa, na kuliunganisha na jina la baba yake ni desturi ya Norway.
"Haaland ana maana kubwa sana kwa Norway," anasema Korssund. "Amekuwa nyota mkubwa wa kipekee katika mchezo maarufu zaidi duniani. Kwa taifa lenye watu zaidi ya milioni 5.5 tu kutoa mmoja wa wachezaji bora wa soka duniani, ni jambo la ajabu na la kuvutia sana."
5. Haiba isiyo ya Kinorwey
Akiwa na kimo cha kuvutia cha mita 1.95 na nywele ndefu za rangi ya dhahabu, Haaland amekuwa mmoja wa wachezaji wanaotambulika zaidi katika ulimwengu wa soka.
Haiba yake ilianza kung'aa alipokuwa Manchester City, na ucheshi wake—ambao wakati mwingine huwa na mtindo wa Kiingereza—umemfanya apendwe sana na mashabiki.
Akaunti yake ya YouTube, ambapo huchapisha video zinazoonyesha "siku moja katika maisha ya Haaland," ina wafuasi milioni 1.6. Pia atashiriki katika filamu ya katuni iitwayo *ViQueens*, akitoa sauti yake kwa mhusika wa jamii ya Viking ambaye, bila shaka, anaitwa Haaland.
"Nadhani Erling, kwa namna fulani, si Mnorwey wa kawaida," alisema mwandishi wa habari wa Norway, Lars Sivertsen. "Ana kujiamini na anaweza kuwa na utani wa aina yake. Anajua thamani yake, anajua uwezo wake, na anajiamini sana."
"Skandinavia ina utamaduni unaosisitiza unyenyekevu, na Erling angeweza hata kulalamika kama angekaa benchi. Hivyo, nadhani anaonekana kama mtu wa tofauti kidogo kwa Wanorwe... Hilo linamfanya kuwa shujaa wa kuvutia kwetu."
Umaarufu wake unaambatana na mambo yanayohusiana na kuwa nyota mkubwa: mauzo ya jezi, kuongezeka kwa hamasa kuhusu Kombe la Dunia, na kuhamasisha vijana.
"Sasa yuko katika daraja tofauti kabisa la umaarufu ukilinganisha na kile tulichozoea kuona kwa mashujaa wetu wa michezo," alisema Sivertsen. "Lakini nadhani ukilitazama taifa zima, kuna hisia kubwa ya fahari kwamba mchezaji mwenye uwezo na mafanikio kama yake anatoka nchini mwetu."
Taarifa kutoka kwa Jess Anderson na Adwaidh Rajan, BBC Sport.