Bodi ya Dawa Kenya yaonya dhidi ya matumizi ya cetirizine kukaza au kukausha uke
Bodi ya Dawa na Sumu Kenya (PPB) imewaonya Wakenya dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya vidonge vya cetirizine kwa lengo la kukaza au kukausha uke, ikisema tabia hiyo inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii inaweza kusababisha madhara ya kiafya.
Katika tahadhari yake ya usalama, bodi hiyo imekanusha madai yanayoashiria kuwa cetirizine, dawa inayotumika kupunguza dalili za mzio, inaweza kutumiwa kwa madhumuni yanayohusiana na uke.
Bodi hiyo imesema hakuna ushahidi wa kisayansi uliothibitishwa unaounga mkono madai hayo na kusisitiza kuwa cetirizine haijaidhinishwa kutumiwa ukeni.
Cetirizine ni dawa ya kumeza inayotumika kutibu hali mbalimbali za mzio, zikiwemo mzio wa njia ya pua, hali inayosababisha vipele vinavyowasha kwenye ngozi. Dawa hiyo inapaswa kumezwa tu kwa kufuata kipimo kilichopendekezwa na maelekezo ya mtaalamu wa afya.
Bodi hiyo imeonya kuwa kuingiza vidonge vya cetirizine ukeni kunaweza kusababisha muwasho, hisia ya kuungua, maumivu na usumbufu.
Imewataka wananchi kutoweka ukeni cetirizine au dawa nyingine yoyote iliyotengenezwa kwa ajili ya kumezwa. Pia imeonya dhidi ya kutegemea madai yasiyothibitishwa yanayosambazwa mitandaoni kuhusu afya ya uzazi na afya ya tendo la ndoa.
Aidha, imewashauri watumiaji wa dawa hiyo kutozidisha kipimo kilichopendekezwa na kuitumia kwa madhumuni yaliyoidhinishwa pekee, kwa njia iliyoelekezwa na wataalamu wa afya.
Watu wanaokabiliwa na ukavu wa uke au changamoto nyingine zinazohusiana na afya ya uzazi na tendo la ndoa wameshauriwa kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya wenye sifa badala ya kujaribu njia za matibabu ambazo hazijaidhinishwa.
Bodi hiyo pia imewataka wananchi kuripoti madhara yanayoshukiwa kusababishwa na dawa pamoja na changamoto nyingine za usalama wa dawa kupitia mifumo yake ya kuripoti matukio hayo.
Taarifa hiyo ya tahadhari imesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Dawa na Sumu, Dkt Ahmed I. Mohamed, Novemba 4, 2026.
Onyo hilo limetolewa wakati ambapo kuna wasiwasi unaoongezeka kuhusu taarifa potofu za kiafya zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hususan madai yanayohamasisha matumizi ya dawa kwa madhumuni ambayo hayajaidhinishwa katika afya ya uzazi na maeneo nyeti ya mwili.
Soma Pia: