Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yakubali pendekezo la usitishaji mapigano la siku 10

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amethibitisha kuwa Tehran imekubali pendekezo la wapatanishi la kusitisha mapigano kwa siku 10, lakini haitatoa maelezo yake kwa sasa.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Viongozi wa dunia wampongeza Burnham kwa kuwa Waziri Mkuu

    Viongozi kadhaa wa dunia wamemtumia salamu za pongezi Andy Burnham baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.

    Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema anatarajia kushirikiana naye kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili za Mfereji wa Kiingereza.

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema anatumaini nchi hizo mbili zitaimarisha zaidi uhusiano wao kwa manufaa ya raia wao, huku pia akitaka uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Uingereza upewe msukumo mpya.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amemtakia Burnham mafanikio katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili Uingereza na kusisitiza kuwa Ukraine iko tayari kushirikiana naye kwa njia zote zinazowezekana.

    Dakika chache baada ya kutoa hotuba ya kwanza kama Waziri Mkuu wa Uingereza Andy Burnham amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump kwa njia ya simu.

    Hta hivyo, haijabainika masuala walioyazungumzia.

  2. Qalibaf: Marekani yajiandaa kwa vita vikubwa huku ikizungumzia diplomasia

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ameishutumu Marekani kwa kudai kuwa inataka kumaliza vita huku ikiendelea kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Qalibaf, ambaye pia ni mmoja wa viongozi wakuu wa mazungumzo ya Iran na Marekani, aliandika kwenye mtandao wa X:

    "Marekani inaendelea kupeleka vifaa vipya vya kijeshi katika eneo hili huku ikidai inataka kusitisha vita. Wamedhani uwezo wetu wa kijasusi ni mdogo kuliko wao. Sasa tunaelewa kikamilifu mbinu hizi za Marekani na tumejiandaa ipasavyo. Vitendo ndivyo vinavyopaswa kuthibitisha kauli, si kuvipinga."

    Kauli zake zimekuja wakati vyombo kadhaa vya habari vya Marekani vikiripoti kuwa Washington inaongeza nguvu zake za kijeshi katika eneo hilo, hatua inayotafsiriwa kama maandalizi ya uwezekano wa vita vikubwa zaidi na Iran.

    The New York Times, likinukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutajwa majina, liliripoti kuwa Marekani inapeleka ndege zaidi za kivita aina ya F 16, F 35 pamoja na ndege za kujaza mafuta angani katika Mashariki ya Kati.

    Kwa upande wake, The Washington Post limemnukuu afisa mmoja wa Marekani akisema Washington inajiandaa kwa uwezekano wa vita kupanuka dhidi ya Iran.

    Afisa huyo, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, alisema operesheni za Marekani zinaweza kukabiliwa na vikwazo kutokana na kupungua kwa mifumo ya ulinzi wa anga, akiba ya silaha za masafa marefu, pamoja na changamoto za kupeleka wanajeshi na ndege zaidi katika eneo hilo.

    "Tunakabiliwa na upungufu unaotishia kuathiri usalama wa operesheni zetu, na sidhani kama Ikulu ya White House inalielewa kikamilifu suala hili," alisema.

    Haya yanajiri wakati Iran na Marekani zikiendelea kushambuliana, huku pande zote mbili pia zikionyesha utayari wa kutafuta suluhu kupitia njia ya diplomasia.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baqaei, amethibitisha kuwa Tehran imepokea mapendekezo kutoka kwa nchi zinazopatanisha ili kupunguza mvutano, lakini hakufichua maudhui yake.

    Amesema mbali na hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Iran, juhudi za kidiplomasia pia zinaendelea.

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Washington iko tayari kufikia suluhu ya kidiplomasia, lakini akasisitiza kuwa mabadiliko hayo yatategemea pia mwelekeo wa Iran.

    Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran anatarajiwa kuzuru Pakistan, nchi inayotajwa kuwa mmoja wa wapatanishi wakuu katika juhudi za kupunguza mvutano kati ya Tehran na Washington.

    Unaweza kusoma;

  3. Wahouthi watangaza mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia

    Wahouthi wa Yemen wametangaza kuanza kutekeleza mzingiro wa baharini dhidi ya Saudi Arabia, wakisema hatua hiyo inaanza kutumika mara moja.

    Katika taarifa yao, Wahouthi wamesema mzingiro huo unatekelezwa kwa msingi wa sera ya "kulipiza kisasi."

    Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi wa Yemen, Yahya Saree, ameionya Saudi Arabia dhidi ya kuongeza mvutano, akisema Wahouthi wako tayari kwa hatua zote zitakazoweza kujitokeza.

    Mvutano kati ya pande hizo umeongezeka baada ya Saudi Arabia kudaiwa kuzuia ndege ya Iran kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa.

    Mvutano huo umeongezeka baada ya Saudi Arabia kuzuia ndege ya shirika la Mahan Air la Iran kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sanaa.

    Mnamo Julai 4, ndege ya Mahan Air iliondoka Tehran kuelekea Sanaa lakini ilirejea Iran saa chache baadaye. Huo ulikuwa safari ya kwanza ya moja kwa moja kati ya Tehran na Sanaa katika kipindi cha miaka 11.

    Safari hiyo ilifanyika saa chache baada ya kutangazwa kusainiwa kwa makubaliano ya usafiri wa anga kati ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Yemen na shirika la Mahan Air.

    Ndege ya pili kutoka Tehran ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Hodeidah wiki iliyopita, baada ya njia za kutua katika uwanja wa ndege wa Sanaa kuharibiwa kwa mabomu, kabla ya kurejea Tehran saa chache baadaye.

    Serikali ya Yemen yenye makao yake Aden, inayoungwa mkono na Saudi Arabia, imeeleza kuwa safari za Mahan Air kwenda Sanaa zinakiuka anga yake.

    Kwa upande wake, Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran wanasema mzingiro wa anga dhidi ya Sanaa ni kinyume cha sheria.

    Wahouthi, wanaojiita Ansar Allah, wanadhibiti sehemu kubwa ya magharibi mwa Yemen, ikiwemo mji mkuu Sanaa, bandari muhimu ya Hodeidah na sehemu kubwa ya pwani ya Bahari ya Shamu. Serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabia inadhibiti mji wa Aden na maeneo mengine ya kusini.

    Baada ya miaka kadhaa ya vita, Wahouthi na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia walikubaliana kusitisha mapigano. Hata hivyo, Wahouthi wanasema makubaliano hayo yalivunjwa kufuatia shambulio dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Sanaa.

    Soma Zaidi;

  4. Khalil al Hayyah ateuliwa kiongozi mpya wa Hamas

    Hamas imemtangaza Khalil al Hayyah, aliyekuwa mkuu wa timu yake ya mazungumzo, kuwa kiongozi mpya wa kundi hilo.

    Ni mtu wa kwanza kuteuliwa kushika wadhifa huo tangu Yahya Sinwar auawe na majeshi ya Israel huko Gaza miaka miwili iliyopita.

    Kwa mujibu wa Hamas, uchaguzi wa ndani ulifanyika Gaza, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel pamoja na maeneo mengine ambako wanachama wa kundi hilo walikuwepo.

    Viongozi wengi wa ngazi za juu wa Hamas waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel yaliyofuatia vita vilivyozuka baada ya mashambulizi ya Hamas.

    Khalil al Hayyah alizaliwa mwaka 1960 katika Ukingo wa Magharibi na amekuwa mwanachama wa Hamas tangu kuanzishwa kwa kundi hilo mwaka 1987.

  5. New York Times: Makumi ya wanajeshi wa Marekani wajeruhiwa katika shambulio la Iran Jordan

    Gazeti la New York Times, likimnukuu afisa mmoja wa Marekani, limesema makumi ya wanajeshi wa Marekani walijeruhiwa na helikopta kadhaa kuharibika katika mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Jordan wiki iliyopita.

    Kwa mujibu wa gazeti hilo, likinukuu vyanzo vya kijeshi, mashambulizi mengine matatu kama hayo yalitangulia shambulio la Ijumaa lililosababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Marekani.

    Afisa huyo wa Jeshi la Marekani, aliyezungumza bila kutajwa jina, alisema Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani haikulazimika kutangaza taarifa kuhusu wanajeshi waliojeruhiwa iwapo walirejea kazini kwa haraka.

    Afisa mwingine mwandamizi wa jeshi aliliambia New York Times kuwa, "Kwa nini Wizara ya Ulinzi ya Marekani itoe taarifa zinazoweza kuisaidia Iran kulenga kwa usahihi zaidi mashambulizi yake ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Jordan na kambi nyingine za Marekani Mashariki ya Kati, ambako maelfu ya wanajeshi wa Marekani wamewekwa?"

    Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani, zaidi ya wanajeshi 400 wa Marekani wamejeruhiwa tangu mapigano kati ya Marekani na Iran yaanze.

    Wakati huo huo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran lilitoa taarifa likiwashukuru "wananchi wa Jordan" kwa kile lilichodai kuwa ni kutoa taarifa sahihi kuhusu maeneo 20 ya ulinzi yanayotumiwa na vikosi vya Marekani.

    Unaweza kusoma;

  6. Burnham: Tutarejesha utulivu wa Uingereza na kuwasilisha mpango wa miaka 10

    Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Andy Burnham, amesema uteuzi wake ni "wakati wa kutafakari na kujenga azma mpya", akiahidi kuleta mwelekeo mpya wa uongozi na kuirejesha nchi katika utulivu.

    Akihutubia taifa kwa mara ya kwanza kutoka Downing Street, Burnham amesema kizazi chake cha wanasiasa kinapaswa "kuongeza kiwango cha utendaji" ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili Uingereza.

    Amesema wananchi wengi wamechoshwa na siasa, na serikali yake italazimika kurejesha imani yao kwa vitendo.

    Burnham ameahidi kuhamisha baadhi ya mamlaka kutoka Westminster na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali nchini ili jamii zipate uwezo mkubwa wa kufanya maamuzi yanayowahusu.

    Aidha, amesema serikali yake itajenga uchumi mpya kwa kurejesha baadhi ya huduma muhimu chini ya usimamizi wa umma ili ziwe nafuu kwa wananchi, huku ikiahidi kufufua sekta ya viwanda na kuunga mkono uzalishaji wa ndani.

    Waziri Mkuu huyo amesema baadaye mwaka huu atawasilisha mpango wa maendeleo wa miaka 10 utakaoeleza dira ya Uingereza kwa muongo ujao.

    Ameongeza kuwa kuanzia kesho serikali yake itaanza kutangaza hatua za kupunguza makali ya gharama ya maisha pamoja na kueleza jinsi hatua hizo zitakavyofadhiliwa.

    "Nawasikia. Hatujafanya vizuri vya kutosha na tunapaswa kufanya vizuri zaidi. Tutafanya hivyo," amesema.

    Burnham amesema serikali yake itatumia kipindi hiki kama mwanzo wa mabadiliko makubwa ya kisiasa, akiahidi siasa za ushirikiano na utatuzi wa matatizo badala ya siasa za kushambuliana.

    Pia amekosoa baadhi ya sera za miaka ya 1980, zikiwemo ubinafsishaji na kuporomoka kwa sekta ya viwanda, akisema maeneo mengi ya nchi bado hayajapona kutokana na athari zake.

  7. Andy Burnham ateuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza

    Andy Burnham amekuwa rasmi Waziri Mkuu wa 59 wa Uingereza baada ya Mfalme Charles III kumwalika kuunda serikali katika mkutano wa faragha uliofanyika Ikulu ya Buckingham.

    Ikulu ya Buckingham imesema katika taarifa yake:

    "Mfalme alimpokea kwa mazungumzo Mbunge Andrew Burnham na kumwomba kuunda serikali mpya. Burnham alikubali ombi hilo la Mfalme kwa kumbusu mkono na akateuliwa rasmi kuwa Waziri Mkuu na Mkuu wa Kwanza wa Hazina."

    Kumbusu mkono Mfalme ni sehemu ya mila ya kifalme ya Uingereza inayomaanisha kukubali rasmi uteuzi wa Mfalme.

    Taarifa hiyo ya ikulu pia imesema kuwa Marie France van Heel alipokelewa na Mfalme wakati wa hafla hiyo.

    Andy Burnham ameondoka Ikulu ya Buckingham na sasa anaelekea katika makazi rasmi ya Waziri Mkuu, Downing Street.

    Atakapowasili, atatoa hotuba yake ya kwanza akiwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

    Moja ya majukumu yake ya kwanza yatakuwa kutangaza baraza lake jipya la mawaziri, litakaloongoza serikali mpya.

    Soma Zaidi:

  8. Keir Starmer ajiuzulu rasmi uwaziri mkuu wa Uingereza

    Keir Starmer amejiuzulu rasmi wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza baada ya kukutana na Mfalme Charles III katika Ikulu ya Buckingham.

    Picha zilizotolewa zimewaonyesha Starmer na Mfalme Charles wakipeana mikono ndani ya Chumba cha Chakula cha Wachina katika ikulu hiyo, ambako Starmer aliwasilisha rasmi barua yake ya kujiuzulu.

    Katika taarifa, Ikulu ya Buckingham imesema:

    "Sir Keir Starmer MB alikuwa na mazungumzo na Mfalme leo asubuhi na kuwasilisha kujiuzulu kwake kama Waziri Mkuu na Mkuu wa Kwanza wa Hazina, jambo ambalo Mfalme alilikubali."

    Taarifa hiyo pia imeongeza kuwa mkewe Starmer alipokelewa na Mfalme wakati wa mkutano huo.

    Kujiuzulu kwa Keir Starmer kunamaanisha sasa kuna mawaziri wakuu tisa wa zamani wa Uingereza walio hai, idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya nchi hiyo.

    Mawaziri hao wakuu wa zamani ni John Major, Tony Blair, Gordon Brown, David Cameron, Theresa May, Boris Johnson, Liz Truss, Rishi Sunak na Keir Starmer.

    Wote wanatarajiwa kuhudhuria kwa pamoja maadhimisho ya Remembrance Sunday yatakayofanyika katika Mnara wa Cenotaph, Whitehall.

    John Major, mwenye umri wa miaka 83, ndiye mzee zaidi miongoni mwao, huku Rishi Sunak akiwa mwenye umri mdogo zaidi wa miaka 46.

  9. Iran yapokea mapendekezo ya kupunguza mvutano na Marekani

    Iran imethibitisha kupokea mapendekezo kutoka kwa wapatanishi mbalimbali yanayolenga kupunguza mvutano kati yake na Marekani.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baqai, amesema Tehran itaendelea na juhudi za kidiplomasia huku ikiendeleza pia hatua zake za kijeshi.

    Akizungumza katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari Jumatatu, Baqai alijibu swali kuhusu mapendekezo mapya ya upatanishi, yakiwemo ya Qatar yanayodaiwa kupendekeza usitishaji wa mapigano kwa siku 10 kati ya Iran na Marekani.

    Swali hilo pia lilihusu ziara ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, nchini Qatar.

    Akijibu, Baqai alisema ni wazi kwamba wapatanishi wanafanya juhudi za kuzuia hali ya mvutano isizidi kuongezeka.

    "Wakati huo huo, Iran haitasita kufanya kila iwezalo kukomesha kile ilichokiita uhalifu wa Marekani," alisema.

    Aliongeza kuwa wakati vikosi vya jeshi la Iran vinaendelea kujibu kwa nguvu mashambulizi ya Marekani, mfumo wa kidiplomasia wa nchi hiyo pia unaendelea kufanya kazi kikamilifu.

    Baqai alithibitisha kuwa Tehran imepokea mapendekezo yaliyowasilishwa na wapatanishi, lakini akasema si wakati muafaka kuweka hadharani maudhui yake.

    Unaweza kusoma;

  10. Mamlaka za Iran zathibitisha mtu mmoja kufariki katika mashambulizi ya Marekani

    Maafisa wa Iran wamesema mtu mmoja amethibitishwa kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Marekani yaliyofanyika Jumatatu.

    Idara ya Usimamizi wa Dharura katika jimbo la Azerbaijan Mashariki imesema mtu mmoja aliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mashambulizi ya Marekani kaskazini magharibi mwa Iran.

    Kwa mujibu wa idara hiyo, shambulio lililolenga eneo la kijeshi kusini magharibi mwa mji wa Tabriz lilitokea majira ya saa 8:35 usiku kuamkia Jumatatu.

    Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Majanga katika jimbo la Azerbaijan Magharibi, Hamid Safri, amesema eneo karibu na wilaya ya Silwana, mjini Urmia, lililengwa na kombora Jumatatu asubuhi.

    Vyombo vya habari vya Iran vimemnukuu Safri akisema watu kadhaa walijeruhiwa katika shambulio hilo.

    Kwa upande mwingine, gavana wa jimbo la Bushehr, Mohammad Mozaffari, amesema mji wa Bushehr umeshambuliwa mara mbili katika saa za hivi karibuni.

    Hata hivyo, amesema hadi sasa hakuna vifo wala majeruhi walioripotiwa kutokana na mashambulizi hayo.

    Mashambulizi hayo yalifanyika saa chache baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani kutangaza kukamilika kwa awamu ya tisa ya operesheni zake dhidi ya Iran.

    Maelezo zaidi kuhusu mashambulizi hayo bado hayajatolewa.

    Unaweza kusoma;

  11. Misri na Eritrea zashutumu nchi zinazojaribu kudhibiti bahari Shamu kinyume na sheria

    Misri na Eritrea zimesisitiza kuwa usalama na utawala wa Bahari ya Shamu ni jukumu la nchi zinazopakana na bahari hiyo pekee.

    Mataifa hayo pia yamesema kuwa jaribio lolote la nchi zisizo za mwambao wa Bahari ya Shamu kutaka "kuidhibiti isivyo halali" ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

    Kwa mujibu wa gazeti la Misri la Al Ahram, msimamo huo wa pamoja ulitangazwa baada ya mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, na mwenzake wa Eritrea, Osman Saleh.

    Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zililaani juhudi zozote za mataifa yasiyopakana na Bahari ya Shamu za kujihusisha au kujipa nafasi ya kusimamia usalama wa eneo hilo.

    Mawaziri hao pia walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi zao na kuratibu misimamo kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja.

    Waziri Abdelatty alisisitiza kuwa Misri itaendelea kuipa Eritrea "uungwaji mkono kamili" katika juhudi zake za kulinda mamlaka ya nchi, umoja wa taifa na mipaka yake.

    Aidha, pande hizo zilisema ziara ya hivi karibuni ya Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki, nchini Misri ilikuwa na mafanikio makubwa na imeweka msingi wa kuimarisha zaidi uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kimkakati kati ya mataifa hayo.

    Mwezi Mei mwaka huu, Misri na Eritrea zilisaini makubaliano kuhusu usafiri wa baharini na uunganishaji wa bandari, yakisisitiza tena msimamo wao kwamba masuala yanayohusu Bahari ya Shamu yanapaswa kuamuliwa na kushughulikiwa na nchi zinazopakana na bahari hiyo pekee.

    Pia Unaweza kusoma:

  12. Kocha wa Argentina abubujikwa na machozi baada ya Argentina kupoteza fainali ya Kombe la Dunia

    Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, alitoka kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa analia alipokuwa akizungumzia mustakabali wake baada ya Argentina kufungwa na Uhispania katika fainali ya Kombe la Dunia Jumatano usiku.

    Scaloni, mwenye umri wa miaka 48, alikuwa akiwania kuwa kocha wa pili katika historia kutwaa Kombe la Dunia mara mbili mfululizo, baada ya kuiongoza Argentina kutwaa taji hilo nchini Qatar mwaka 2022.

    Hata hivyo, bao la Ferran Torres mwanzoni mwa muda wa nyongeza lilizima matumaini ya Argentina, huku Uhispania ikitwaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili katika historia yake.

    Mkataba wa Scaloni unatarajiwa kumalizika mwezi Desemba mwaka huu. Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake, alishindwa kuficha hisia zake na kujibu kwa sauti ya huzuni huku akibubujikwa na machozi.

    "Nitazungumza na rais wa shirikisho. Nina wazo kuhusu ninachotaka kufanya. Nitamaliza mkataba wangu, lakini bado nilikuwa na mambo mengi niliyotaka kufanikisha. Sijui kama kuna jambo kubwa zaidi kama hili ambalo linaweza kufikiwa tena. Tunahitaji kulijadili kwa utulivu," alisema.

    Aliendelea kusema:

    "Ninamshukuru nahodha wa timu kwa kunipa nafasi ya kufika hapa nilipo leo. Hapa ndipo kila mmoja anatamani kuwa. Hadi dakika ya mwisho tulijitahidi kwa kila namna, kama wachezaji na kama benchi la ufundi. Nafikiri nahitaji muda wa kutafakari kwa makini."

    Akiwa anatokwa na machozi, Scaloni aliongeza:

    "Nivumilieni. Sijui kama ninaweza kuendelea."

    "Hapa ni mahali pazuri sana. Ni sehemu ambayo kila kocha huota kufika. Mimi na wenzangu hatukuwahi kufikiria kwamba tungefikia kiwango hiki."

    "Ili kuendelea unahitaji mambo mengi, hasa utulivu wa akili, nguvu mpya na uwezo wa kujenga timu kama hii. Hilo si jambo rahisi kulifanya tena."

    Baada ya kauli hizo, Scaloni alisimama, akaomba radhi na kuondoka ukumbini akiwa analia.

    "Ni huzuni kubwa. Naomba mniwie radhi," alisema.

    Unaweza kusoma;

  13. Ukraine yaishambulia Moscow kwa zaidi ya droni 400 baada ya mashambulizi ya Urusi

    Meya wa Moscow amesema zaidi ya ndege zisizo na rubani 400 zimedunguliwa katika eneo la Moscow tangu Jumatano jioni.

    Shirika la habari la Interfax limemnukuu Sergei Sobyanin akisema:

    "Kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 11:00 alfajiri ya leo, zaidi ya droni 400 ziliingia katika anga la eneo la Moscow."

    "Takriban zote zilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga kabla hazijafika zilipokuwa zikielekea. Droni 85 zilidunguliwa zilipokuwa zinakaribia jiji la Moscow."

    Sobyanin amesema vikosi vya uokoaji vinaendelea kufanya kazi katika maeneo ambako mabaki ya droni hizo yameanguka.

    Katika miezi ya hivi karibuni, Kyiv imeongeza mashambulizi dhidi ya maeneo ya Urusi, ikisema ni kulipiza kisasi kwa kampeni ya Urusi ya mashambulizi ya mabomu nchini Ukraine ambayo imeendelea kwa miaka minne.

    Wakati huo huo, shirika la habari la TASS limeripoti kuwa watu sita, wakiwemo raia watatu wa kigeni, wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha yaliyosababishwa na milipuko ya mabomu. Hata hivyo, haijabainika iwapo majeraha hayo yanahusiana na mashambulizi ya droni.

    Haya yanajiri baada ya Urusi kuushambulia mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, kwa makombora ya masafa mafupi ya balistiki usiku wa kuamkia Jumapili.

    Waandishi wa AFP waliokuwa Kyiv walisema walishuhudia makombora yakipiga majengo ya makazi.

    Mkazi mmoja wa Kyiv aliliambia shirika la AFP:

    "Makombora yaliendelea kuanguka mfululizo, na milipuko yake ilikuwa mikubwa sana."

    "Nilidhani huo ulikuwa mwisho wangu."

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameelezea shambulio hilo kuwa "moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya makombora ya balistiki dhidi ya Kyiv", akisema zaidi ya makombora 40 yalirushwa kuelekea mji huo mkuu, yakiwemo makombora 25 ya balistiki.

    Urusi pia imeendeleza mashambulizi yake katika maeneo ya Zaporizhzhia, Kharkiv, Dnipropetrovsk na Odesa.

    Soma Zaidi:

  14. Feri iliyokuwa imebeba abiria na wahudumu 133 yazama katika pwani ya Guyana

    Maafisa wa Guyana wamesema watu 67 wameokolewa baada ya feri iliyokuwa imebeba abiria 116 na wafanyakazi 17 kuzama katika pwani ya nchi hiyo.

    Watoto 15 ni miongoni mwa waliookolewa baada ya feri ya MV Barima kupinduka muda mfupi baada ya kuondoka katika mji mkuu, Georgetown, siku ya Jumamosi. Hata hivyo, watu kadhaa bado hawajulikani walipo.

    Waziri wa Ujenzi wa Umma, Juan Edghill, alisema kuwa kituo cha uokoaji kilipokea taarifa ya dharura saa 11:01 jioni kwa saa za eneo hilo (03:01 GMT Jumapili), jambo lililosababisha kuanzishwa kwa operesheni ya utafutaji na uokoaji iliyohusisha vikosi vya serikali pamoja na boti zinazomilikiwa na watu binafsi.

    "Tuna matumaini kwamba tutawapata watu wote waliokuwa ndani ya feri hiyo," Edghill aliwaambia waandishi wa habari huku shughuli za utafutaji zikiendelea Jumapili mchana.

    Waziri Mkuu Mark Phillips alisema waliookolewa ni pamoja na wanaume 41, wanawake 11 na watoto 15. Aliongeza kuwa nahodha wa feri hiyo pia ameokolewa.

    Nahodha huyo amerudi katika eneo la ajali kusaidia operesheni ya uokoaji, ambayo imeimarishwa kwa kiwango kikubwa, huku eneo la utafutaji likipanuliwa zaidi ya mara mbili.

    Phillips alisema feri hiyo haikuwa imezidisha idadi ya abiria inayoruhusiwa wakati wa ajali, na kwamba ilikuwa na leseni ya kubeba zaidi ya abiria 300.

    Aliongeza kuwa majina ya watu waliokuwa ndani ya feri hiyo yatatangazwa baada ya operesheni ya uokoaji na uchunguzi wa afya kukamilika.

  15. Trump asema mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran yalifanywa kwa heshima ya wanajeshi waliouawa

    Rais Donald Trump amesema mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani yameiathiri Iran "kwa kiwango kikubwa sana", akiongeza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa "kwa heshima" ya wanajeshi watatu wa Marekani waliouawa katika siku za hivi karibuni, wawili nchini Jordan na mmoja nchini Iraq.

    Mapema alfajiri ya Jumatatu, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imeanzisha "wimbi jipya" la mashambulizi kwa usiku wa tisa mfululizo, huku milipuko ikisikika katika maeneo mbalimbali nchini Iran.

    Marekani ilisema imelenga maeneo ya kijeshi na mitandao ya mawasiliano ili "kuendelea kupunguza" uwezo wa Tehran wa kufanya mashambulizi dhidi ya meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz.

    Kwa upande wake, Iran ilisema imejibu kwa "shambulio la kushtukiza" nchini Syria na kulenga ndege za kijeshi za Marekani katika uwanja wa ndege wa Aqaba nchini Jordan.

    Kwingineko katika eneo hilo, jeshi la Kuwait lilisema lilifanikiwa kuzidungua ndege zisizo na rubani za Iran.

    Kuhusu mashambulizi ya Marekani, shirika la habari la Tasnim, ambalo lina uhusiano wa karibu na serikali ya Iran, liliripoti kuwa miji kadhaa ilishambuliwa, ikiwemo Tabriz, Chabahar, Konarak, Bandar Mahshahr na Bandar Imam Khomeini.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran pia viliripoti kuwa meli mbili za kubeba mafuta zililipuka zilipokuwa zikijaribu kuvuka Mlango wa Hormuz.

    Jeshi la Iran (IRGC) lilidai kuwa meli hizo zilikuwa zinapitia njia iliyotajwa kuwa "isiyo salama na yenye hatari" katika sehemu ya kusini ya Mlango wa Hormuz, na kwamba zililipuka na kusimama. Hata hivyo, CENTCOM ilipinga madai hayo.

    Unaweza kusoma;

  16. Jeshi la Iran latangaza kufanya shambulio dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Kuwait

    Jeshi la Iran (IRGC) limetangaza kuwa siku ya Jumatatu lilishambulia maeneo ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait, yakiwemo "mfumo wa rada wa tahadhari ya mapema."

    Katika taarifa yake, IRGC ilidai kuwa mfumo huo "uliharibiwa kabisa."

    Jeshi hilo pia lilisema kuwa katika shambulio la ndege zisizo na rubani, rada hiyo ya Marekani iliharibiwa kikamilifu.

    Aidha, lilidai kuwa katika shambulio jingine lililenga ghala la kuhifadhi vifaa na vipuri vya ndege pamoja na hanga la ndege zisizo na rubani aina ya MQ-9 katika kambi ya kijeshi ya Ali Al-Salem.

    IRGC ilisema mashambulizi hayo yalifanyika kujibu mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani dhidi ya Iran.

    Awali, Marekani ilikuwa imetangaza kutekeleza duru ya tisa mfululizo ya mashambulizi dhidi ya Iran.

    Unaweza kusoma;

  17. Vipimo vya kubaini chanzo cha mlipuko wa ugonjwa wa kuhara Marekani vilitoa matokeo ya uongo, maafisa wa afya wasema

    Vipimo vya sampuli ya mboga mboga za lettuce aina ya iceberg vilivyodhaniwa kuwa na kimelea kilichosababisha mlipuko mkubwa wa ugonjwa wa kuhara nchini Marekani vimebainika kutoa matokeo ya uongo, maafisa wamesema.

    Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) ilitangaza siku ya Jumamosi kuwa sampuli kutoka kwa msambazaji wa chakula Taylor Farms, ambaye husambaza bidhaa kwa mgahawa wa Taco Bell, ilikuwa imeonesha uwepo wa kimelea cha Cyclospora.

    Hata hivyo, FDA ilisema siku ya Jumapili kuwa ilifanya ukaguzi upya wa sampuli hiyo na kubaini kuwa matokeo yale yalikuwa ya uongo. Mamlaka hiyo ilimjulisha Taylor Farms kuhusu hitilafu hiyo na kuongeza kuwa inaendelea kushirikiana na kampuni hiyo kuhakikisha bidhaa zinazohusishwa na mlipuko huo zimeondolewa sokoni.

    Taarifa hiyo ya hivi karibuni ina maana kuwa chanzo halisi cha kimelea hicho bado hakijafahamika.

    Hakuna kifo kilichoripotiwa kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Cyclosporiasis, lakini takribani watu 94 wamelazwa hospitalini.

    Taylor Farms ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa imeamua kwa hiari kuondoa sokoni nchini Marekani mboga ya lettuce zote aina ya iceberg zilizotoka katikati mwa Mexico, na pia ilitoa orodha ya bidhaa zilizoathirika.

    Siku iliyofuata, FDA ilisema sampuli iliyopatikana na matokeo chanya ilitokana na bidhaa ambayo haikuwa sehemu ya bidhaa zilizoondolewa sokoni na Taylor Farms katika tangazo lake la Ijumaa.

    Tofauti kati ya urejeshaji wa bidhaa na uondoaji wa hiari wa bidhaa sokoni ni kwamba urejeshaji wa bidhaa hulazimisha kampuni kuwafahamisha wateja na kukusanya bidhaa zilizoathirika kutoka sokoni, hivyo huwa hatua pana zaidi na yenye gharama kubwa kuliko uondoaji wa hiari.

  18. Mbappe ashinda kiatu cha dhahabu kwa kuwa mfungaji wa magoli mengi

    Mshambuliaji wa Ufaransa, Kylian Mbappe, ameandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Kombe la Dunia mara mbili, baada ya kumaliza akiwa mfungaji bora wa mashindano ya mwaka 2026.

    Mbappe alifunga mabao 10 katika mechi nane, akimzidi Lionel Messi katika mbio kali za ufungaji bora.

    Baada ya kufunga mabao manane na kushinda Kiatu cha Dhahabu katika Kombe la Dunia la Qatar 2022, Mbappe sasa ameshinda tuzo hiyo katika Kombe la Dunia mfululizo.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 pia amekuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 10 katika Kombe la Dunia tangu Gerd Muller wa Ujerumani Magharibi alipofanya hivyo mwaka 1970.

    Ni Just Fontaine wa Ufaransa aliyefunga mabao 13 mwaka 1958 na Sandor Kocsis wa Hungary aliyefunga mabao 11 mwaka 1954 pekee waliowahi kufunga mabao mengi zaidi katika mashindano.

    Mbappe pia sasa ndiye kinara wa mabao wa muda wote katika historia ya Kombe la Dunia kwa wanaume akiwa na mabao 22, bao moja zaidi ya Lionel Messi.

    Mabingwa wa dunia, Hispania, walitwaa tuzo nyingine nyingi za mashindano hayo, huku nahodha wao Rodri akishinda Mpira wa Dhahabu kama mchezaji bora wa mashindano.

    Mbappe alimzidi Messi kwa mabao baada ya kufunga mara mbili katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu siku ya Jumamosi. Hata hivyo, mabao hayo hayakuizuia Ufaransa kupoteza kwa mabao 6-4 dhidi ya England na kumaliza katika nafasi ya nne.

    Akizungumza baada ya mechi hiyo mjini Miami, Mbappe alisema:

    "Unapofunga mabao mengi kiasi hiki katika Kombe la Dunia, bila shaka unafikia kiwango cha juu kabisa."

    "Lakini ningependelea kutokuwa mfungaji bora kama tungefanikiwa kucheza fainali. Hii ni nzuri kwa historia yangu nitakapostaafu, lakini kwa sasa hicho si kitu ninachokifikiria zaidi."

    Mbappe pia alifunga mabao mawili dhidi ya Senegal na Iraq katika hatua ya makundi, pamoja na bao dhidi ya Sweden katika hatua ya 32 bora.

    Baadaye alifunga dhidi ya Paraguay katika hatua ya 16 bora, likiwemo bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 70, kabla ya kufunga tena dhidi ya Morocco katika robo fainali.

    Lionel Messi alikuwa na nafasi ya kumpita Mbappe kwa mabao kama angefunga hat-trick katika fainali ya Kombe la Dunia.

    Hata hivyo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 alishindwa kufunga katika mchezo wa fainali uliofanyika New Jersey, ambapo Argentina ilifungwa mabao 1-0 na Hispania. Messi alimaliza mashindano hayo akiwa amefunga mabao manane katika mechi nane.

    Kiungo wa England Jude Bellingham na mshambuliaji wa Norway Erling Haaland walifunga mabao saba kila mmoja, huku mshambuliaji wa Ufaransa Ousmane Dembele na nahodha wa England Harry Kane wakifunga mabao sita kila mmoja.

  19. Mwanajeshi wa Marekani auawa, mmoja ajeruhiwa baada ya shambulio la Iran nchini Iraq

    Jeshi la Marekani limesema mwanajeshi mmoja amefariki baada ya shambulio la Iran kaskazini mwa Iraq siku ya Jumamosi, siku moja baada ya shambulio dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Jordan kuwaua wanajeshi wawili wa Marekani na mwingine akiwa hajulikani aliko.

    Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema mwanajeshi huyo alifariki wakati wa "mlipuko uliodhibitiwa wa kifaa cha mlipuko ambacho hakikulipuka" kutoka kwa ndege isiyo na rubani ya Iran iliyokuwa imeangushwa. Tukio hilo pia lilimjeruhi mwanajeshi mwingine.

    Katika taarifa yake, Centcom ilisema imepata "mabaki ya mwili ambayo bado hayajatambuliwa" baada ya kufanya upekuzi katika eneo la shambulio la Ijumaa nchini Jordan. "Mchakato wa kuyachunguza mabaki hayo ili kuthibitisha utambulisho unaendelea," iliongeza.

    Tukio hili linajiri wakati Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana kwa siku ya nane mfululizo katika mzozo unaozidi kuongezeka.

    Pande zote mbili zimetuhumiana kushambulia miundombinu muhimu katika siku za hivi karibuni. Wakati huo huo, Washington imerejesha vizuizi vyake dhidi ya bandari za Iran, huku Tehran ikitangaza kufungwa kwa Mlango bahari wa Hormuz na kuwalenga washirika wa Marekani katika eneo hilo, baada ya makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano kuvunjika chini ya mwezi mmoja tangu yaanze.

    Jeshi la Marekani lilisema mashambulizi yake ya hivi karibuni yalilenga "kupunguza uwezo wa Iran wa kutishia usafiri wa meli za kibiashara" katika Mlango wa Hormuz, na "kuwaadhibu kwa haraka" wanajeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC), ambao liliwatuhumu kuhusika na shambulio la Jordan.

    Video zilizothibitishwa kutoka ndani ya kituo cha kijeshi nchini Jordan zilionesha takribani milipuko miwili na mlipuko mkubwa.

    Idadi ya vifo vya Wamarekani katika mzozo huu sasa imefikia 17, baada ya rubani mmoja wa Jeshi la Wanamaji la Marekani aliyekuwa ametoweka mapema mwezi huu kutangazwa kuwa amefariki.

    Unaweza kusoma;

  20. Hispania mabingwa Kombe la Dunia 2026

    Hispania ilistahili kushinda fainali ya Kombe la Dunia baada ya ushindi mwembamba dhidi ya Argentina iliyobaki na wachezaji 10, huku bao la Ferran Torres katika muda wa nyongeza likivunja upinzani wao.

    Mabingwa wa Ulaya walitengeneza nafasi bora zaidi dhidi ya mabingwa watetezi wa dunia, ambao kwa kiasi kikubwa walitegemea mbinu za kuchelewesha mchezo na kuharibu kasi ya wapinzzani.

    Enzo Fernandez alitolewa kwa kadi nyekundu muda mfupi kabla ya mchezo kuingia katika muda wa nyongeza.

    Torres alikuwa shujaa wa Hispania alipoupokea mpira wa kichwa kutoka kwa mchezaji aliyeingia akitokea benchi, Nico Williams, na kumshinda mlinda lango wa Argentina Emiliano Martinez kwa shuti kali la karibu katika dakika ya 106.

    Mchezo huo uligeuka kuwa pambano la nguvu na tahadhari badala ya soka la kuvutia. Wakati huo huo, mbali na uwanja, fainali hiyo ilikuwa ya kipekee kwa shamrashamra na uwepo wa mastaa mbalimbali.

    Rais Donald Trump aliwasili New Jersey kwa msafara wa helikopta kabla ya mchezo kuanza, huku Shakira, Madonna na Justin Bieber wakitumbuiza katika onesho la kwanza kabisa la mapumziko ya kipindi cha kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, na kufanya mapumziko hayo yadumu kwa dakika 27.

    Katika mchezo uliokuwa na makosa mengi na kusimamishwa mara kwa mara, Hispania ilionekana kuwa bora zaidi, huku Lamine Yamal na Mikel Oyarzabal wakimlazimisha Emiliano Martinez kuokoa mipira muhimu katika kipindi cha kwanza.

    Wachezaji wa Hispania walimlalamikia mara kwa mara mwamuzi Slavko Vincic kwa kuwa mpole katika kutoa adhabu, hasa baada ya Alexis Mac Allister kumchezea vibaya Dani Olmo. Kadi ya kwanza ya njano ilitolewa dakika ya 40 baada ya Lisandro Martinez kumuangusha Oyarzabal, ingawa mlinzi huyo wa Manchester United alitolewa baadaye kutokana na majeraha.

    Mchezo ulizidi kuwa mkali katika dakika za nyongeza za muda wa kawaida, ambapo Enzo Fernandez, ambaye tayari alikuwa ameonywa kwa kadi ya njano, alipata kadi ya pili ya njano kwa kumchezea vibaya beki wa Hispania Pau Cubarsi na hivyo kutolewa nje.

    Mlinda lango wa Argentina Emiliano Martinez aliendelea kuwa tegemeo la timu yake alipookoa kwa ustadi mkubwa mpira wa adhabu wa Lamine Yamal katika sekunde za mwisho za muda wa kawaida. Pia aliokoa kichwa cha Nico Williams katika muda wa nyongeza, lakini baadaye Williams alifunga bao ambalo lilikataliwa kutokana na Mikel Merino kumfanyia madhambi Nicolas Otamendi wakati wa kutengeneza shambulizi.

    Argentina ilikuwa imeonesha uwezo mkubwa kwa kugeuza matokeo dhidi ya Misri na England katika hatua za mtoano, lakini haikuweza kufanya hivyo tena dhidi ya Hispania.

    Kwa ushindi huo, Hispania ilitwaa Kombe la Dunia la wanaume kwa mara ya pili katika historia yake.

    Aidha, ushindi huo uliifanya Hispania kuwa taifa la kwanza kabisa katika historia kushikilia ubingwa wa Kombe la Dunia la wanaume na wanawake kwa wakati mmoja.

    Unaweza kusoma;