Trump azomewa alipohudhuria mchezo wa mpira wa kikapu, NBA

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Donald Trump amezomewa wakati wa mechi ya mpira wa kikapu mjini New York, akiwa Rais wa Marekani aliyeko madarakani wa kwanza kuhudhuria Fainali za NBA.
Vishindo vya kuzomewa vilisikika baada ya mashabiki waliokuwa na tiketi kulazimika kusubiri kwa saa kadhaa kwenye mistari mirefu zaidi nje ya Madison Square Garden kutokana na hatua kali za kiusalama zilizoambatana na uwepo wa rais.
Trump alihudhuria mechi kati ya New York Knicks na San Antonio Spurs katika mchezo wa tatu wa mfululizo wa fainali za NBA za michezo saba. Knicks walikuwa wameshinda michezo miwili ya kwanza.
Meya wa New York Zohran Mamdani na kundi la watu maarufu pia walihudhuria mchezo huo.
Tukio la kuzomea lilizuka Jumatatu jioni wakati kamera ilipomuonesha Trump kwenye skrini kubwa ndani ya uwanja, akiwa anatoa saluti wakati mwimbaji akiimba wimbo wa taifa.
Rais huyo alihudhuria mchezo huo akiwa na mjukuu wake Kai Trump na mmiliki wa New York Knicks, James Dolan, pamoja na baadhi ya maafisa wa utawala wake wakiwemo Waziri wa Uchukuzi Sean Duffy, Waziri wa Mambo ya Ndani Doug Burgum, mkuu wa EPA Lee Zeldin, na mjumbe maalum Steve Witkoff.
Rais huyo wa chama cha Republican, ambaye alizaliwa katika eneo la Queens mjini New York City, amekuwa na uhusiano mgumu na mji wake wa asili ambao kwa kiasi kikubwa unaunga mkono chama cha Democratic.














