Uganda yamteua Otunnu kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
Serikali ya Uganda imemteua Balozi Olara Otunnu kuwania wadhifa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ikimtanguliza mwanasiasa na kiongozi mashuhuri ambaye miongo kadhaa ya utumishi wake katika diplomasia ya kimataifa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Julai 26, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda ilitangaza kuwa imewasilisha ombi la kugombea nafasi ya juu katika Umoja wa Mataifa, huku mchakato wa kumtafuta mrithi wa António Guterres—ambaye muhula wake wa pili unafikia tamati tarehe 31 Desemba 2026—ukianza.
Serikali ilimwelezea Otunnu kama kiongozi wa taifa anayeheshimika na mtumishi wa kimataifa mwenye uzoefu wa zaidi ya miongo minne katika nyanja za diplomasia ya kimataifa, serikali, taaluma na asasi za kiraia, ikisema kuwa historia yake pana ya uongozi inamfanya kuwa mtu mwafaka kuongoza Umoja wa Mataifa katika kipindi muhimu cha masuala ya dunia.
''Ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, Balozi Olum aliwahi kuhudumu kama Naibu Katibu Mkuu na Mwakilishi Maalum wa kwanza wa masuala ya watoto na migogoro ya kivita kati ya mwaka 1998 hadi 2005,'' ilisema taarifa hiyo.
Balozi Otunnu pia aliwahi kuhudumu kama Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, pamoja na kuwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja huo; katika kipindi hicho, alianzisha mfumo wa upigaji kura wa awali (straw ballot) kwa ajili ya kumchagua Katibu Mkuu—utaratibu unaojulikana tangu wakati huo kama "Mfumo wa Otunnu" na ambao umekuwa ukiongoza uchaguzi wa aina hiyo tangu mwaka 1981.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huteuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pendekezo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kufuatia mchakato wa uteuzi wa ushindani unaohusisha nchi zote wanachama.