Israel imesema imefanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya magharibi na katikati ya Iran.
“Dakika chache zilizopita, Jeshi la Anga la Israel lilishambulia maeneo ya kijeshi yanayomilikiwa na utawala wa kigaidi wa Iran katika maeneo ya magharibi na katikati ya Iran,” Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kupitia Telegram.
Hakukuwa na maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu idadi ya walioumia au waliouawa, wala maeneo halisi yaliyolengwa katika mashambulizi.
Katika hatua nyingine, Televisheni ya taifa ya Iran sasa inaripoti milipuko katika miji mitatu baada ya Israel kusema jeshi lake la anga limefanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi katikati na magharibi mwa Iran.
“Milipuko kadhaa imeonekana kusikika Tehran, Tabriz na Isfahan,” televisheni ya taifa imeandika kupitia Telegram.
Milipuko pia imeripotiwa kusikika karibu na mji wa kati wa Karaj.
Taarifa hizi zinakuja wakati hali ya tahadhari ikiendelea kuongezeka kutokana na mfululizo wa mashambulizi kati ya Israel na Iran, huku maelezo zaidi yakitarajiwa kutolewa.