Waliokwama
Wafungwa wa Kiafrika wa vita ya mbali
Lud Beverley, kuruta wa kijeshi kutoka Jamhuri ya Kongo, baadhi ya vidole vyake vimefungwa bandeji vingine vikiwa vimekatika.
Amekaa katika kitanda cha zahanati iliyopo katika gereza la wafungwa wa kivita magharibi mwa Ukraine.
Beverley ana miaka 28. Wakati wanahabari wa BBC wametembelea gereza hilo mwezi Machi alikuwa amekaa hapo kwa miezi mitatu. BBC ilikwenda kufatilia zaidi juu ya ongezeko la idadi ya wapiganaji wa Kiafrika katika vita kati ya Urusi na Ukraine.
Kwa mujibu wa hesabu za Ukraine, mmoja kati ya wafungwa nane wa kivita waliokamatwa na Ukraine mwaka jana anatoka Afrika. Ukraine inaamini takribani 10% ya wapiganaji zaidi ya 27,000 wa kigeni wa Urusi wanatoka Afrika.
"Tulipokuwa katika mapambano vitani, mikono yangu iliganda kwa baridi - na wakati nakamatwa sikuwa na glovu (soksi za mikono)", anasema Beverly akizungumza kwa Kirusi.
"Tulikuwa tunatembea, ilikuwa baridi sana"
"Vidole vilijeruhiwa baada ya kuganda," anasema.
Miaka saba iliyopita, alipelekwa Urusi kusoma katika chuo cha jeshi la majini, baadae alipata mwenza na mtoto pia. Lakini alipata shida ya kifedha, akaanza kuuza dawa za kulevya, hatimaye akifungwa katika jela ya Urusi. Vita ilipoanza, aliambiwa kuchagua aidha kubaki jela au kujiunga na jeshi na kwenda kupigana.
"Badala ya kutumikia kifungo, nikaamua kutumikia Urusi, na kwasababu hiyo wakanituma kupigana vitani" alisema Beverley.
Ukraine hukaribisha wanahabari kutembelea gereza la wafungwa Alhamis ya mwisho ya kila mwezi. Hii ni sehemu ya jitihada yao ya kuonyesha ulimwengu kwamba wanawatunza vizuri wafungwa wa kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Maofisa hawakutuambia idadi kamili ya wafungwa inaowashikilia, walisema tu kwamba kuna wafungwa kutoka nchi 15 za Afrika.
Beverley alisema hana malalamiko yoyote juu ya anavyotunzwa hapo gerezani; matabibu ni wakarimu na maisha ya gerezani hapo ni kama kuwa jeshini tu - panachosha kwa kutokuwa na chakufanya.
Wafungwa wa kivita wa Kiafrica wakiwa gerezani nchini Ukraine, 26 Novemba 2025. Getty Images
Katika mahojiano, Beverley alikuwa na majuto, akiomba nchi na familia yake wamsamehe kwa ushiriki wake katika vita. Zaidi ya yote anataka vita iishe tu.
“Pande zote mbili zimepata hasara kubwa - ya watu na vitu - nilikuwepo huko, ni kubaya sana.”
Lud Beverly
Mfungwa wa kivita, Ukraine
Wafungwa wa kivita
Wafungwa wote wa vita (PoWs) waliokubali kuzungumza nasi walikuwa na njia tofauti zilizowapeleka kwenye mzozo huu. Wengi wao walisema wanataka kurejea Urusi ili kuhakikisha wanachukua fedha walizoahidiwa waliposaini mikataba. Hakuna aliyesema anataka kurejea vitani katika mapigano.
Tulipowasili ndani ya gereza, harufu ya kupendeza ya supu ilitukaribisha, huku wafungwa waliovaa sare za buluu ya bahari wakijipanga kwa utulivu kwenye foleni ya chakula cha mchana.
Baadaye, wafungwa waliulizwa kama wako tayari kuzungumza na wanahabari waliotembelea gereza hilo. Baadhi ya Waafrika walikuwa wamekusanyika nyuma ya bweni; baadhi wamejitenga pembeni, wengine wachangamfu wanataniana na kucheka, na wengine wanakwepa kabisa hata kuwaangalia wanahabari, hawataki kuhojiwa.
Mwanaume mmoja akajitokeza mbele mara tu anaposikia kwamba kuna wanahabari kutoka BBC. Alijitambulisha kwa jina la Richard Kanu kutoka Freetown, mji mkuu wa Sierra Leone.
Anasema kuzungumza na vyombo vya habari ni njia ya kuwahakikishia familia yake - na hasa watoto wake watatu - kwamba bado yuko hai na ana afya njema.
Kanu - mwenye umri wa miaka 43 - amekuwa katika gereza hili kwa mwaka mmoja, na amekuwa mikononi mwa Ukraine kwa takribani miaka miwili tangu alipokamatwa.
Kama Beverley, naye pia alikuwa mwanajeshi nchi kwao - lakini anasema hakufikiria kwamba alipokubali kazi ya ulinzi wa kawaida huko Urusi angejikuta mstari wa mbele wa vita.
Alikuwa ametumikia Jeshi la Sierra Leone kwa miaka 17, akilipwa kama dola 100 tu kwa mwezi. Migogoro ya kibinafsi ndani ya kikosi chake ilimfanya kuondoka, na akiwa na hamu kubwa ya kupata kipato zaidi, alianza kutafuta njia ya kwenda Ulaya kupitia viza za utalii.
"Binti yangu anataka kuwa daktari. Nilitaka niweze kugharamia masomo yake ya chuo kikuu ili aweze kutimiza ndoto zake,” ananiambia.
Kila nchi aliyoomba viza ilimnyima isipokuwa Urusi. Alipowasili huko mwaka 2024, aliwasiliana na wakala wa ajira na hakuamini bahati yake alipoahidiwa malipo ya dola 15,000 kusaini mkataba wa mwaka mmoja, pamoja na mshahara wa dola 2,000 kwa mwezi, licha ya kutofahamu hata neno moja la Kirusi. Baadaye alipelekwa katika mji wa Rostov-on-Don kusini mwa Urusi, takriban kilomita 200 kutoka mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.
Nilipowasili Rostov, nilijikuta ndani ya kambi ya kijeshi,” anasema, akieleza kwamba hapo ndipo mtu mmoja alipomwambia kuwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja na jeshi la Urusi. Anasema alishtuka sana kusikia hivyo, lakini baadaye alijipa moyo baada ya kufahamishwa kwamba mkataba huo ungemwezesha kupata uraia wa Urusi.
"Baada ya mwaka mmoja, ningepata nyaraka za Urusi pamoja na fedha zangu. Ningekuwa na fursa ya kuileta familia yangu Urusi, na kuishi maisha ya kawaida huko,” anasema.
Lakini anasema hali kwenye mstari wa mbele wa mapigano ilikuwa hatari kupita kiasi kutokana na maendeleo ya teknolojia za kivita zinazotumiwa na pande zote mbili kama vile matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones). Kwa baadhi ya wafungwa, athari za walichopitia vitani bado zinaonekana wazi kabisa.
Katika bweni jingine, mfungwa kutoka Kenya Evans Kibet mwanzoni anakataa kuzungumza nasi. Lakini anaposalimiwa kwa Kiswahili ghafla analegeza msimamo wake.
Lakini mwonekano wa Kibet unaanza kubadilika mara anaposikia jinsi familia nyingi nyumbani zilivyo na wasiwasi kuhusu taarifa za watu walioshawishiwa kwenda Urusi kupitia mawakala wa ajira wasio waaminifu, walioahidiwa kazi za kiraia zenye mishahara mizuri, lakini baadaye wakajikuta wakipigana katika vita vya Urusi.
Ripoti za kijasusi za Ukraine zinaonyesha kuwa Wakenya ndio kundi kubwa zaidi la Waafrika waliojiunga na jeshi la Urusi, wakifuatiwa na raia wa Misri, Cameroon, Ghana na Uganda.
Uwanja wa vita si jambo la mchezo. Watu wanakufa kila upande, kila wakati, na hakuna anayejali kabisa,” anasema Kibet, mwenye umri wa miaka 36.
Anaeleza jinsi mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yanavyoacha miili ya watu ikiwa imetapakaa kila mahali.
Wanajeshi wanasonga mbele, wakiwa hawawezi au hawataki kurudi nyuma kuwasaidia wenzao waliojeruhiwa
Anawaelekeza wanahabari wa BBC kumtafuta Mkenya mwenzake aliyekuwa katika bweni lingine, akisema huenda yeye akawa tayari kuzungumza zaidi na kurekodiwa.
Na kweli, Willy Macharia anakuwa tayari kuzungumza nasi kabla ya kuelekea kupata chakula cha mchana; “Chakula kipo cha kutosha hapa. Naweza kula baadaye,” anasema.
Namtambua kama kijana - ana umri wa miaka 23 - ambaye video zake zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii akiwatahadharisha vijana wa Kenya wasijiunge na vita hivyo.
Nilipomuuliza kuhusu hilo, anadai kwamba alilazimishwa kurekodi video hizo na maafisa wa Ukraine.
Baadaye nilimuuliza Petro Yatsenko, msemaji wa Ukraine juu ya masuala ya Wafungwa wa Vita, kuhusu madai hayo, lakini aliyakanusha.
Macharia anasema alikaa kwenye mstari wa mbele wa mapigano kwa miezi mitatu - baada ya kujiunga na jeshi la Urusi kwa kuvutiwa na ahadi za mshahara mzuri pamoja na fursa ya kuendelea na masomo. Hata hivyo, anakuwa mwangalifu anapoulizwa kueleza kwa kina jinsi alivyoajiriwa. “Nilikuwa napigana upande wa Urusi, hivyo kuwa hapa Ukraine kunamaanisha niko mikononi mwa adui,” anasema.
Ili kupoteza muda hapo gerezani, kama wafungwa wengine, yeye hufanya kazi ndogo ndogo zinazomwingizia fedha za kutumia katika kioski kidogo kinachouza vitu vidogo vidogo kama vile sabuni na sukari.
Pia anajifunza lugha ya Kiukreni katika maktaba ya gereza, akisema anataka kuelewa vizuri zaidi wanachokizungumza maofisa wa gereza hilo. Kijana huyo anatamani sana kuachiliwa huru na ana matumaini kwamba jina lake litaonekana hivi karibuni kwenye orodha ya wafungwa watakaobadilishana kati ya Urusi na Ukraine, ili aweze kurejea Urusi.
Lakini Yatsenko, msemaji wa Ukraine juu ya masuala ya Wafungwa wa Vita, haoni uwezekano mkubwa wa kubadilishana wafungwa hao. Anasema hadi sasa Ghana ndiyo nchi pekee ya Afrika iliyoonyesha nia ya kuwarejesha raia wake wanaoshikiliwa kama wafungwa wa vita, huku wawakilishi wa nchi hiyo wakitembelea gereza hilo huku mazungumzo yakiendelea.
“Kwa sasa, Waafrika hawajajumuishwa katika mabadilishano haya ya wafungwa. Wanataka kubadilishwa na kurejeshwa Urusi kwa sababu wanataka kupata fedha walizoahidiwa. Lakini hadi sasa hatujaona hatua yoyote kutoka upande wa Urusi ya kuwarejesha,” anasema.”
Petro Yatsenko
Msemaji wa Ukraine, Masuala ya Wafungwa wa Vita
Pia nilimhoji Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Andrii Sybiha, ambaye anaona Waafrika waliojiunga na jeshi la Urusi kuwa waathirika wa kile alichokiita “shughuli haramu za Urusi na propaganda zake.”
“Wakati mwingine walialikwa kwenda kusoma nchini Urusi, lakini ghafla wanajikuta kwenye uwanja wa vita,” aliniambia.
Waziri huyo alisema kuwa raia wa kigeni wanaweza pia kujiunga na jeshi la Ukraine kupigana vitani. Hata hivyo, alisisitiza kwamba tofauti na Urusi, mchakato wa kujiunga na jeshi la Ukraine ni wa kisheria, wa hiari na wa wazi. Alisema hakuwa na takwimu wala taarifa rasmi juu ya idadi ya raia wa kigeni waliopo katika jeshi hilo.
Lakini ukweli ni kwamba wafungwa wa vita kutoka Afrika tuliokutana nao wanatamani kurejea Urusi — na huenda hilo lisitokee hadi vita hivi vitakapofikia mwisho.
Kwa Beverley, suala si fedha pekee. Binti yake anaishi Urusi, na anasema kama angerudishwa moja kwa moja Congo, asingekuwa na uwezo wa kurejea tena Urusi.
Kanu yeye ana uhakika kwamba hana nafasi ya kuwa na maisha bora nchini kwao Sierra Leone; “Nilisaini mkataba na Urusi, na ninataka kurejea Urusi. Maisha ya Urusi ni bora kuliko maisha yangu nchini Sierra Leone,” anasema.
Baada ya kuondoka Ukraine, tulielekea Freetown kukutana na Elsie, binti wa Kanu mwenye umri wa miaka 19.
Akiwa amesimama nje ya nyumba yao — makazi yaliyochakaa, yaliyojengwa kwa mabati na vipande vya vyuma chakavu katika vilima vya mtaa wa Tengbeh - anasema amemkumbuka sana baba yake, lakini anakubaliana naye kwamba anapaswa kuvumilia na kutafuta namna ya kurejea Urusi.
“Kurejea Sierra Leone hakutatatua matatizo yaliyomfanya aondoke hapo awali. Nadhani ana nafasi nzuri zaidi ya kufanikiwa akiwa Urusi - nafasi bora ya kupata kipato, kujijenga kimaisha, na kubadilisha maisha yetu sote.”
Elsie Kanu, 19
Waliorejea
Si wengi wanaofanikiwa kurejea nyumbani. Lakini Duncan Chege, raia wa Kenya, alifanikiwa. Alitoroka kutoka hospitalini alikokuwa amelazwa baada ya kujifanya kuwa na matatizo ya afya ya akili alipokuwa akihudumu katika hospitali ya kijeshi ya Urusi.
Chege yeye alishawishika na ahadi ya kupata kipato bora. Baada ya kushindwa kupata kazi Dubai kutokana na matatizo ya viza, wakala wake wa ajira alimshauri kujaribu bahati yake Urusi, ambako alipata viza ndani ya wiki moja tu.
Picha kwa hisani ya Duncan Chege
Ili kugharamia safari hiyo, mama yake alikopa fedha kutoka kwa majirani na ndugu, akalipia ada ya wakala pamoja na tiketi ya kwenda tu nchini urusi.
Duncan Chege
Hata hivyo, mustakabali wa wafungwa hawa wa vita kutoka Afrika bado haujulikani.
CREDITS
Mwandishi: Sammy Awami, Akiripoti kutoka Ukraine magharibi
Muandaaji na mpiga picha: Hassan Lali
Msanifu: Millie Wachira
Mbunifu ukarasa wa mbele: Mayowa Alabi
Michoro: George Wafula
Picha: Ukraine (Getty Images), Sierra Leone (Sammy Awami) and Kenya (Hassan Ali)
Mhariri: Lucy Fleming and Victor Oluoch
Muandaaji na mhariri wa video: Kathy Harcombe
Mhariri wa ukurusa: Dorothy Otieno
Wahusika wengine: Shalom Olatunji, Brian Osweta, Njoroge Muigai, Boaz Ochieng
Tarehe ya kuchapishwa: 4 Juni 2026

