Mwanasesere Natasha afufua mjadala wa dhulma mitandaoni, ni ubaguzi au burudani?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Msongo wa mawazo umegeuka kuwa moja ya matatizo makubwa zaidi yanayowakabili watu katika karne ya 21.

Ili kukabiliana na msongo wa mawazo wa muda mrefu, baadhi ya watu hukandamiza mipira ya povu, huchezea pete maalumu za kutuliza mawazo au hukamua vitu vya jeli laini.

Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa mtandao nchini China wamekuwa wakitoa hasira na mfadhaiko wao kwa kuchezea wanasesere wanaojulikana kama Natasha Dolls.

Jambo linalozua wasiwasi mkubwa ni kwamba kwa kiasi kikubwa huwalenga wanasesere wenye ngozi nyeusi.

Mwanasesere mtoto mweusi anayejulikana kama Natasha Doll ameibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, huku wakosoaji wakisema maudhui hayo yana sura ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Waafrika.

Lakini kwanza 'Natasha Doll' ni mwanasesere wa aina gani?

Natasha Doll ni mwanasesere wa mpira anayevutika, anayeweza kubanwa, kuvutwa na kukunjwa bila kuharibika kirahisi. Anauzwa kama kifaa cha kupunguza msongo wa mawazo na burudani hasa nchini China.

Kwa nini kimezua utata?

Mjadala uliongezeka baada ya video kusambaa zikionyesha watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China wakikifanyia vitendo vya ukatili mwanasesere huyo huku wakicheka na kufurahia.

Katika baadhi ya video, watumiaji waliulizwa kwa nini mwanasesere huyo alitengenezwa kwa sura ya mtoto mweusi badala ya mtoto wa rangi nyingine. Mmoja wao alidai kuwa watu wangehisi huruma zaidi kama kingekuwa na sura ya mtoto mweupe.

Kauli hiyo ilizua ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu na watumiaji wa mitandao ya kijamii waliodai kuwa inaonyesha mtazamo wa kuwapunguzia utu watu weusi.

"Kwa nini ni wanasesere wenye ngozi nyeusi hasa wanaofanyiwa ukatili wa kiwango hiki? Haitoshi kwamba sura zao zinakumbusha taswira za kibaguzi na vikaragosi vilivyotumiwa zamani kuhalalisha ukandamizaji wa kimfumo dhidi ya watu weusi," alisema mtayarishaji wa maudhui Tanaïssa Dee katika video aliyochapisha kwenye TikTok siku ya Ijumaa.

Na sasa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini China wanachapisha video zinazowaonyesha wakifanya vitendo vinavyofanana dhidi ya watoto halisi Weusi wakidhulumiwa huku wahusika wakionekana kufurahia hali hiyo.

Kwa kisingizio cha "kukabiliana na msongo wa mawazo", baadhi ya watumiaji huwapiga wanasesere hao, huwamwagia maji ya moto, huwakanyaga bila huruma na hata kuwakatakata vipande vipande.

Wengine hujiburudisha kwa kupaka vipodozi vya kuwafanya waonekane wenye ngozi nyepesi au kwa kuwabinya na kuwabana hadi kuwa bapa kama chapati.

"Ni mwanasesere tu"

Mwanasesere huyo huonekana kama mtoto mchanga mdogo aliyevalishwa nepi ya rangi. Tofauti na wanasesere wa kauri ambao huvunjika kwa urahisi, wanasesere hawa wameundwa kustahimili kushikwa au kushughulikiwa kwa ukali bila kuharibika.

Hubadilika umbo wanapobinywa kwa nguvu au kutikiswa kwa makusudi, lakini muda mfupi baadaye hurudi katika umbo lao la awali.

Baadhi ya watumiaji wa mitandao wametofautiana na kile kinachodaiwa ni udhalilishaji wa rangi.

Kwa mitazamo yao wanahisi kuwa ni mwanaserere na haifai kuchukuliwa kama binadamu halisi.

Madai haya si mapya kabisa

Mwaka 2022, BBC ilichapisha makala maalum yanayojulikana kama 'Racism for sale'.

Kwa mujibu wa makala hayo uchunguzi ulibaini kuwa raia mmoja wa China Lu Ke aliyekuwa akiishi Malawi alikuwa akiwarekodi watoto wa kijijini wakitamka maneno ya Kichina ambayo hawakuyafahamu, lakini yalikuwa yakibaguzi wa rangi.

Mwana mtindo huyo alidaiwa kuuza video hizo mtandaoni kwa watazamaji nchini China.

Kwa mujibu wa ripota wa bbc aliyefanya uchunguzi huo, Video moja ilikuwa ikiuzwa kwa dola 70 lakini alikana kurekodi video hizo.

Lu Ke alikanusha kutengeneza video zenye maudhui ya kudhalilisha au ya kibaguzi.

Alisema lengo la video zake lilikuwa kueneza utamaduni wa China kwa jamii za wenyeji.

Katika moja ya video zilizoonekana na BBC, kundi la watoto wadogo linaonekana likitamka kwa Kichina maneno yanayosema: "Mimi ni mnyama mweusi, nina akili ndogo," bila kufahamu maana ya kauli hiyo.

Akiwa amerekodiwa kwa siri na mwandishi wa habari aliyejifanya mnunuzi mtarajiwa, Lu Ke kwanza alikubali kuwa alihusika katika kutengeneza video hiyo, lakini baadaye akakanusha madai hayo.

Mamlaka za Malawi hazikumuachilia zilimfunga mwaka mmoja na kuwafidia watoto waliohusishwa na video hizo.

Kwa nini maudhui haya hayaonekani sana nje ya China?

Kutokana na mfumo wa udhibiti wa mtandao nchini China, unaojulikana kama "Great Firewall", majukwaa mengi ya kimataifa ya mitandao ya kijamii hayapatikani kwa urahisi. Badala yake, watumiaji hutegemea programu za ndani kama RedNote na WeChat.

Hali hiyo ina maana kwamba sehemu kubwa ya maudhui yanayochapishwa kwenye majukwaa hayo hubaki ndani ya China na kulengwa mahsusi kwa hadhira ya ndani pamoja na matakwa yao.

Madai yanayotolewa na wakosoaji ni kwamba kuna soko linalowezesha na kuhamasisha maudhui yanayowaonyesha watoto weusi wa Afrika wakifanyiwa vitendo vya udhalilishaji kwa ajili ya burudani.

Kuna machapisho ambayo BBC Swahili imeyaona kwa mtandao wa Tiktok yakionesha mwanasesere huyo wa rangi nyeusi akifanyiwa maudhui ambayo ni ya kudhalilisha.

Hata hivyo, akaunti hizo bado hazijafutwa.

China inasemaje?

Fang Zengquan, ambaye ni Katibu wa Chama katika Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Beijing Normal University na mkurugenzi wa Kituo cha Uelewa wa Mtandaoni kwa Watoto, amesema mkakati wa kuuza mwanasesere huyo unatia wasiwasi mkubwa.

Kwa mujibu wake, kuhusisha moja kwa moja mwanasesere anayefanana na mtoto mchanga na njia ya kupunguza msongo wa mawazo kunaweza kuwahamasisha watumiaji, hasa vijana, kupata burudani au kuridhika kwa kumbinya, kumshughulikia kwa ukali au kumharibu mwanasesere huyo.

Fang ameonya kuwa kuendelea kuhusisha taswira ya watoto wachanga na vitendo vya ukatili au uharibifu kunaweza kupunguza hisia za huruma na ya kuwalinda watoto halisi.

Aliongeza kuwa katika hali mbaya zaidi, hali hiyo inaweza kuchochea mielekeo ya fujo au ukatili dhidi ya viumbe hai bila mtu kutambua.

Kwa nini mjadala huu ni muhimu kwa Afrika?

Kulingana na baadhi ya watengenezaji maudhui wa mitandaoni haswa wa kiafrika, wamehoji kuhusu namna Waafrika wanavyowakilishwa kwenye mitandao ya kijamii, ubaguzi wa rangi katika mazingira ya kidijitali, na wajibu wa serikali za Afrika katika kulinda hadhi ya raia wao.

Ili kukabiliana na kuhalalishwa kwa ubaguzi wa rangi na maudhui yanayochochea chuki mtandaoni, mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yamechukua msimamo mkali.

Human Rights Watch limesema:

"Serikali ya China inapaswa kutambua na kulaani ubaguzi dhidi ya watu weusi unaoendelea kusambaa kwenye mtandao nchini humo, na kuchukua hatua za kuhimiza uvumilivu pamoja na kupambana na chuki na ubaguzi."