Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Dawa mpya na ghali za Ugonjwa wa Alzheimer hazitaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wagonjwa-Utafiti
- Author, James Gallagher
- Nafasi, Health and science correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Uchambuzi muhimu umehitimisha kuwa dawa zinazodaiwa kuwa "mapinduzi" kwa Ugonjwa wa Alzheimer huenda hazitawanufaisha wagonjwa.
Watafiti walisema matokeo ya dawa hizo yako "chini sana" ya kiwango kinachohitajika kuleta mabadiliko ya maana katika maisha ya wagonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
Hata hivyo, ripoti hiyo imezua upinzani mkali kutoka kwa wanasayansi wengine mashuhuri, ambao wanaielezea kuwa ina mapungufu makubwa ya msingi.
Kwa sasa, mfumo wa afya wa Uingereza (NHS) haulipii dawa hizi, na dozi ya matibabu ya miezi 18 inaweza kugharimu takriban pauni 90,000 kwa mtu binafsi. Gharama hii ni kubwa mno kwa watu wengi, hivyo hata kama mtu ana uwezo wa kifedha, bado swali linabaki: je, zinafaa kweli kulipiwa?
Dawa hizi hufanya kazi kwa kushambulia mabonge ya protini yanayonata yanayoitwa beta amyloid, ambayo hukusanyika kwenye nafasi kati ya seli za ubongo kwa watu wenye ugonjwa wa Alzheimer.
Kutofikia viwango
Kingamwili (antibodies), zinazofanana na zile ambazo mwili hutengeneza kupambana na virusi au bakteria, zimetengenezwa mahsusi ili kutambua protini ya amyloid na kuiondoa kwenye ubongo.
Kwa miaka mingi, mbinu hii haikufanikiwa. Hata hivyo, majaribio ya dawa mbili za hivi karibuni, Donanemab na Lecanemab, yalionesha kuwa zinaweza kupunguza kasi ya kushuka kwa uwezo wa kufikiri.
Hii ilikuwa hatua muhimu sana, kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza kwa dawa yoyote kuonesha uwezo wa kupunguza kasi ya uharibifu wa ubongo unaosababishwa na Ugonjwa wa Alzheimer.
Cochrane Collaboration, ambayo hufanya uchambuzi wa kina na wa kujitegemea wa data za kitabibu, ilichunguza tafiti 17 zilizohusisha washiriki 20,342 kuhusu dawa zinazolenga kuondoa amyloid kwenye ubongo.
Kwa ujumla, walihitimisha kuwa mbinu hiyo kweli hupunguza kasi ya ugonjwa wa Alzheimer, lakini si kwa kiwango cha kutosha kuleta mabadiliko ya maana katika maisha ya wagonjwa.
Wakati huo huo, dawa hizo zina hatari ya madhara kama:
Uvimbe wa ubongo
Kutokwa na damu kwenye ubongo
Aidha, zinahitaji kutolewa mara kwa mara (kila wiki mbili hadi nne) na kwa gharama kubwa sana.
Mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo, Profesa Edo Richard, ambaye ni profesa wa magonjwa ya mfumo wa fahamu, Radboud University Medical Centre nchini Uholanzi, huwakaribisha wagonjwa wa dementia katika kliniki yake.
Alipoulizwa huwaambia nini wagonjwa wake, alisema:
"Ninawaambia kuwa huenda msipate faida kubwa kutokana na dawa hizi, na pia ni mzigo kwenu na kwa familia zenu."
Aliongeza:
"Nafikiri ni muhimu sana kuwa waaminifu kwa wagonjwa wetu kuhusu wanachoweza kutarajia. Mimi huwa makini kuepuka kuwapa watu matumaini yasiyo ya kweli."
Pia alisema kuwa mbinu nyingine za kutibu Ugonjwa wa Alzheimer wa kupoteza kumbukumbu, uvimbe (inflammation) kwenye ubongo, vinapaswa kuchunguzwa zaidi.
Matokeo ya ripoti hiyo pia yameungwa mkono na wakosoaji wa muda mrefu wa dawa hizi.
Profesa Robert Howard wa University College London (UCL) alisema kuwa ni "bahati mbaya na si haki" kwa familia zilizoathiriwa na dementia kuona dawa hizi zikipigiwa debe kwa namna ambayo "haiungwi mkono na ushahidi thabiti wa kisayansi na imeongeza matumaini yasiyo ya kweli."
Hata hivyo, namna uchambuzi huu ulivyofanywa imezua mjadala mkali.
Timu ya watafiti inasema kuwa dawa zote walizochunguza zinafanya kazi ya kuondoa amyloid kwenye ubongo, hivyo uchambuzi wao unaonesha kama mbinu hiyo inafanya kazi au la.
Lakini wataalamu wengine wanasema kuwa tofauti za jinsi kila dawa inavyofanya kazi ni muhimu, na si haki kuweka pamoja dawa za zamani za majaribio na zile mpya ambazo tayari zimeonesha mafanikio fulani.
Profesa Bart De Strooper kutoka taasisi ya utafiti ya UK Dementia ya Chuo cha London alisema kuwa mapitio hayo "hayafafanui ushahidi, bali yanautia ukungu," na akaongeza kuwa "kasoro ya uchambuzi huu ni ya msingi kabisa."
Alisema:
"Programu nyingi za awali zilishindwa, lakini kingamwili mpya zimeonesha faida ndogo lakini ya kweli kwa wagonjwa."
Dkt. Richard Oakley kutoka shirika kuu la hisani nchini Uingereza linalojihusisha na ugonjwa wa Alzheimer alisema:
"Ni muhimu sana kutafsiri mapitio haya kwa umakini na kuepuka kuyapuuza kabisa miongo ya tafiti za kisayansi zilizokuwa za ubunifu."
Kwa sasa, njia pekee ya kupata dawa hizi nchini Uingereza ni kwa kuzilipia binafsi, jambo linalozifanya zisiweze kufikiwa na watu wengi.
National Institute for Health and Care Excellence (NICE), ambayo huamua dawa zipi zitafadhiliwa na NHS, ilizikataa hapo awali, lakini sasa inapitia upya ushahidi huo ili pia kuzingatia mzigo unaobebwa.